Feb 13, 2015
Kama Unaendeshwa Na Kitu Hiki, Maisha Yako Ni Magumu Sana.
Mtu mwenye hisia nyingi
ambaye anaongozwa na hisia, ni yule ambaye huweza kuathiriwa au kutikiswa kwa
urahisi zaidi na hisia. Ni jambo zuri kujijua sisi wenyewe na haiba zetu na
hata kutambua hisia zetu. Ninapozungumzia hisia nikiwa na maana ya hali kama
kuwa na furaha, huzuni, chuki na hata wakati mwingine kijicho hizo ni baadhi tu
ya hisia.
Baadhi ya watu ni wenye
kuongozwa sana na hisia wakati ambapo wengine hawako hivyo na kwa kuutambua ukweli huu tutaweza kuzuia na
kuepuka kuumiza vichwa vyetu na hata kupata maumivu mengine katika maisha yetu.
Hata kama hatumo katika kundi la wale wenye hisia nyingi, bado kila mmoja wetu
anazo hisia na yuko katika hatari ya kuongozwa na hisia hizo.
Tunaweza kuamka mapema sana
asubuhi siku moja, huku tukiwa tumejazwa na hisia za huzuni na kwa siku hiyo
nzima tukaongozwa na kufuata hisia hizo. Siku inayofuata tunaweza tukaamka pia
tukiwa tumechukia, huku tukihisi au kutaka kuona kila mmoja wetu pale nyumbani kwetu
aondoke machoni petu, hivyo tukajikuta tukaishia kufanya vituko vya ajabu tu.
Wakati mwingine tunaweza
kuamka na hisia za kujisikitikia sisi wenyewe na kujuta sana na hata kuamua
kukaa kwenye kona tukiugulia kwa siku nzima huku tukiwa tumeshika tama. Na
kujiuliza maswali mengi ambayo hayana majibu na huku tukiwa hatutaki kabisa
kuongea na mtu. Na inapotekea mtu akatuongelesha tunakuwa wakali sana kiasi cha
kwamba tunaweza kumjibu vibaya kama sio sisi tuliozoeleka.
Hivyo basi, iwapo tutaamua
kuziachia hisia zetu zifanye vile zinavyotaka, basi ni wazi kabisa hisia hizi
zitachochea matatizo ambayo yatasababisha tutoke nje ya makusudio yetu mema na
kutupeleka kwenye makusudio au matakwa ya kutuangusha. Hapa ndipo pale
tunapoanza kusema, ‘ilikuwa ni ibilisi tu’. Ndio maana katika maisha yako, kama
bado ni mtumwa na unaendelea kuendeshwa na hisia zako, maisha yako ni magumu
sana. Ni magumu kwa sababu kila wakati utakuwa unaishi maisha yanayokuumiza
wewe tu.
Nimetumia miaka mingi ya
maisha yangu katika kufuata vile nilivyokuwa nikijihisi. Kama niliamka asubuhi
nikiwa mwenye huzuni, basi nilihuzunika siku nzima. Kwa wakati huo sikuweza
kujua kwamba, ningeweza kuzizuia hisia za aina hiyo. Sasa nimetambua kwamba,
ninaweza kupambana kikamilifu na hisia zote mbaya na zilizo hasi ambazo
zinatamani kuniongoza siku nzima.
Ni lazima tujifunze kuwa wenye
tahadhari kuhusiana na hisia zetu mwenyewe na kuweza kuelewa jinsi
tutakavyoweza kuziongoza na kuzisimamia kwa usahihi na uhakika zaidi. Njia mojawapo
ya kufanya hivyo, ni kuzijua aina tofauti za haiba au tabia na kujua namna
zinavyoitikia kwa njia tofauti, hali au mazingira yanayofanana.
Nimejifunza kwamba,
ninapoamka asubuhi nikiwa na kisirani, sipaswi kuendelea kukilea kisirani
hicho. Ninapaswa badala yake kuamua kuwa mimi, kuamua kuwa na mkabala tofauti
wa kimaisha kwa siku hiyo. Ni mimi ninayepaswa kusema ninataka nijisikie vipi,
siyo mazingira au hali inayonizunguka.
Ninapojikuta nimenyong’onyea,
ni lazima nijiulize haraka kama ni lazima ninyong’onyee. Ni wazi wazi kwamba,
huwa ninapata jibu la hapana. Kwa hiyo, kuanzia hapo hutafuta sababu ya kunyong’onyea
kwangu. Nikishaipata hutafuta sababu iliyo kinyume na hiyo, ambapo hunisaidia
kuondokewa na kunyong’onyea huko sana.
Nakutakia maisha mema yawe
ya furaha kwako, endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na
kuhamasika kila siku, karibu sana.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035/dirayamafanikio@gmail.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.