Mar 28, 2015
Hii Ndiyo Sababu Inayowafanya wengi Wawe Na Kisirani Asubuhi.
Mara nyingi imeshawahi
kukutokea wewe binafsi ama kuona kwa watu wengine mara wanapoamka asubuhi huwa
ni watu wa kisirani sana tofauti na muda mwingine. Umeshawahi kujiuliza nini
chanzo au sababu yake hasa? Kwa nini asubuhi mtu anapotoka usingizini, kisirani
kinaweza kuzuka kirahisi zaidi kuliko wakati mwingine? Huenda jibu hulifahamu.
Lakini, wataalamu wasiolala, wakichunguza matukio ya kila siku ya maisha ya
binadamu wana majibu.
Kwa kawaida, mtu anapokuwa
ameamka kutoka usingizini, akili yake inakuwa ina mawenge na kushindwa kufikiri
vizuri. Inahitaji muda kidogo, ili mtu ambaye ametoka usingizini karibuni,
kuweza kumudu kufikiri vizuri kwa utaratibu ule wa kawaida. Inaelezwa kwamba,
uwezo wa kufanya uamuzi wa hekima unajengwa baada ya mtu aliyetoka usingizini,
kupata muda wa kutafakari kwanza.
Kama mtu anatakiwa kufanya
uamuzi wa haraka, mara baada ya kushtuka au kuamka kutoka usingizini, inaweza
kumwia vigumu sana. Mara nyingi, akili ya mtu ambaye ndiyo ametoka usingizini
muda huohuo, inakuwa na aina ya ukungu unaomzuia kufikiri vizuri na kwa haraka.
Inaelezwa kwamba, akili ya
mtu ambaye ndio kwanza ametoka usingizini, inakuwa na ukungu kuliko ile ya mtu
aliyekosa usingizi kwa saa 26. Hii inakuonesha ni kwa kiwango gani, mtu
anapotoka usingizini, anakuwa na hali mbaya katika kufikiri.
Hata hivyo, wataalamu
walioshughulikia kujua ukweli unaohusiana na kisirani cha asubuhi kwamba,
huchukua kiasi cha dakika kumi hadi ukungu kuondoka akilini, ambapo mtu anaweza
kuanza kufikiri vizuri. Lakini hata hivyo, imebainika kwamba, kwa watu wengine
huchukua hadi saa mbili tangu kuamka, kabla ukungu wa akili haujatoka.
Utafiti huo bado unaendelea
katika kutaka kujua muda hasa ambao akili inachukua kujirudisha katika hali ya
kawaida baada ya mtu kuamka. Lakini pia kuangalia athari za watu kama madaktari
ambao huamshwa usingizini kwenda kufanya uamuzi mkubwa unaohusu maisha ya mtu.
Je, hali hii haiwezi kuwafanya madaktari kufanya makosa ya wazi yanayoweza kusababisha
maafa kwa wagonjwa?
Ni juu yako sasa kujua namna
ya kuwasiliana na mtu ambaye ndiyo kwanza ametoka usingizini. Kama kuna jambo
linaweza kusubiri angalau kwa dakika ishirini baada ya mtu kuamka, ndiyo
likasemwa, ni hekima kwa mtu kufanya hivyo. Kuchokoza hisia za mtu ambaye ndiyo
kwanza ametoka usingizini kunaweza kuzaa kisirani ambacho vinginevyo
kisingeweza kuzuka.
Kwa watu wanaojua jambo
hili, huwa hawazungumzi jambo lolote wanapokuwa wametoka usingizini, labda kama
ni muhimu sana. Wako wale ambao pia, wanapokuwa na jambo mbalo ni muhimu
hawaambii wahusika wahusika, kama ndiyo kwanza wametoka usingizini. Husubiri
‘wachangamke’ kama inavyofahamika.
Unapolazimisha kuzungumza na
mtu ambaye katoka usingizi muda sio mrefu kinachotokea mara nyingi ukijibiwa
vibaya au usipojliwa usishangae pia hii
ndio huwa hali inayotokea. Na ndio ukweli wenyewe akili inakuwa bado ina
maluweluwe. Kwa mujibu wa wataalamu hawa wanadai kuwa mara nyingi unpotoka
usingizini hiki ndio huwa kipindi ambacho akili yako yako haifanyi kazi vizuri
sana, kwa sababu inakuwa haijachanga sana.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu
na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035
- dirayamafanikio@gmail.com,
Mar 26, 2015
Kiri Kosa, Jifunze, Jipe Nafasi Ya Kuanza Upya.
Katika safari ya maisha, ni jambo la kawaida kabisa kukutana na vikwazo vinavyoweza kukatisha tamaa. Ukubwa wa vikwazo au changamoto hizo, zinaweza kukusababishia ukaiona dunia kama imegeuka, au wakati mwingine ukatamani ipasuke uingie ndani yake.
Yapo mambo mengi yanayoweza
kukufanya ufikirie hivyo. Huenda yakawa ni makosa ya kibinadamu, matatizo,
changamoto, kukatishwa tamaa na baadhi ya watu au kujiponza mwenyewe kutokana
na hili au lile. Lakini ukikaa chini, ukatafakari utatambua kuwa hakuna binadamu
asiyeteleza kwa kufanya makosa au kupitia changamoto kwenye safari ya maisha.
Hivyo wakati mwingine
unapaswa kuelewa kuwa kwa kila linalokupata, bado unayo nafasi ya kufungua
ukurasa mpya. Kupatwa na mitihani katika maisha, mara nyingi ni darasa mojawapo
tunalotakiwa kuliangalia kwa umakini ili kupata somo au fundisho lililo ndani
yake.
Ikiwa mtihani huo umekuja
kutokana na kosa ulilofanya, ni vyema kukubali kama umekosea na kisha kujipa
nafasi ya kusonga mbele. Tunaelewa kuwa maisha ya kila mmoja wetu kwa namna
moja au nyingine yanaendeshwa na misimamo mbalimbali. Kuna wale wanaoamini kuwa
wao hawawezi kufanya jambo Fulani na
wakati mwingine kuamini kuwa hawawezi kukosea kabisa.
Ni sawa lakini tukumbuke
kwamba hakuna binadamu aliyekamilika kwa kila mmoja wetu anaweza kuteleza na
kufanya kosa bila kukusudia . Hivyo basi kwa namna yoyote ile katika maisha
yetu kutenda makosa ni sehemu ya maisha. Ni vyema kujifunza kukubali kama
umekosea na kujirekebisha.
Pili, jifunze kutokana na
lile kosa. Si dhani kama leo ukikosea jambo Fulani unaweza kulirudia kosa kama
lile siku nyingine. Hata kama ikitokea labda kwa namna nyingine tena. Nakumbuka
wakati nikiwa mdogo baba yangu aliniletea zawadi kama pongezi ya kufanya vizuri
darasani.
Siku hiyo aliponiletea
tulikuwa tumekaa na kaka zangu. Alinikaribisha tukiwa pamoja ili iwe chachu kwa
wao kufanya vizuri pia. Au pengine kuwafanya waone wivu na wao waweze kufanya
vizuri wakiwa shuleni. Basi alinipa ile zawadi. Wakati wa kupokea nilifanya
kosa kwa kupokea na mkono wa kushoto. Kwa ukali aliniambia nirudishe ile zawadi
akaondoka nayo.
Baada ya kutafakari kwa muda
nikakumbuka kumbuka kuwa nilifanya kosa kupokea na mkono wa kushoto kitendo
ambacho alishawahi kutusisitizia kuwa siyo cha heshima. Lile lilikuwa funzo
kwangu kwani mpaka leo sikuwahi kufahamu ile zawadi ilikuwa ni ya aina gani,
kwani ilikuwa imefungwa.
Baada ya kutokea kwa kadhia
ile na kuweza kugundua kosa langu, moja kwa moja nilienda kuomba msamaha kwa
baba. Tangu siku ile sikuwahi tena kumpa au kupokea kitu chochote na mkono wa
kushoto. Hata ikitokea hivyo kama nimejisahau lazima nitaomba radhi.
Ninachoamini mimi ni kwamba
kwa hali yoyote ile ni lazima tuyape nafasi maisha yaendelee. Hivyo hatuna haja
ya kuangalia nyuma pale tunapojikwaa, kwani utakachoambulia hapo ni maumivu
tena inawezekana ukaumia hapo kuliko awali.
Wapo waliofikia kufanya
maamuzi ya ajabu baada ya kukutwa na mtihani au kufanya makosa katika jamii.
Wengine hata waliweza kutengwa kutokana na makosa yao. Lakini kushindwa kwao
kukubali makosa waliyotenda, kulizaa matatizo mengine. Kwani utakuta ili
kuondoa aibu iliyo mbele yao, waliamua kukimbia miji yao na hivyo kwenda kuanza
maisha sehemu nyingine.
Suluhisho pekee la jambo
kama hili ni kuomba msamaha na kujipanga upya. Usikubali kukata tamaa kwa
kuanguka mara moja, hata ukianguka mara tatu bado unayo nafasi ya kusimama na
kuanza upya na kufanya vizuri hata pengine kuliko mwanzo. Kitu kikubwa jiamini
kisha chukua jukumu la kusonga mbele kwa kujiamini zaidi, utabadili maisha yako
na utafanikiwa.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili
ya kujifunza na kuboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Suzan Mwillo wa Gazeti la Mwananchi.
- Mawasiliano suzanmwillo@gmail.com
Mar 24, 2015
Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
Ni jambo ambalo mara nyingi huwa linafahamika na liko wazi kuwa, ili kuweza kufanikiwa na kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa ni lazima suala la kufanya kazi kwa ubunifu, juhudi kubwa na maarifa pamoja na kuwa king’ang’anizi kwenye mipango na malengo yako huwa linahusika kwa sehemu kubwa sana. Hutaweza na huwezi kuwa mjasiriamali mkubwa na kufikia mafanikio makubwa kama utakuwa huzingatii mambo hayo.
Pamoja na kufanya kazi kwa
ubunifu, juhudi kubwa na maarifa, kuwa ni nguzo muhimu sana kwako wewe
mjasiriamali ili kuweza kufikia mafanikio makubwa, lakini pia huwa kuna kitu
cha ziada ambacho ni lazima ukifanye na kukifuata ili kuweza kuona mafanikio
hayo unayoyataka. Kitu hiki ni wewe kuweza kujua hatua muhimu za kufuata ili
kuweza kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa.
kwa kadri unavyozidi kujua
hatua hizi zinakuwa zinakupa nguvu na hamasa kubwa ya kuendelea kung’ang’ania
na kushikilia ndoto zako mapaka kuona zinatimia. Hizi ni hatua muhimu sana
kwako na kwa kila mjasiriamali mwenye nia na kiu ya kutaka kufanikiwa na kufika
mbali hasa katika safari ya kibiashara na maisha kwa ujumla. Je, unajua ni
hatua zipi unazotakiwa kuzifuata ili kuwa majsiriamali mwenye mafanikio?
Hizi
Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
1.
Fanya kile unachokipenda kwa moyo wote.
Watu wengi huwa wana kawaida
ya kufanya mambo yale ambayo hawayapendi sana katika maisha yao. Hii huwa
inatokea au wanafanya hivyo kwa lengo hasa la kuingiza kipato. Kutokana na kufanya mambo kwa kutopenda iwe
kazi au biashara hii mara nyingi husababisha kutokuwa na mafanikio
makubwa kwa kile wanachofanya.
Mafanikio huwa hayawezi
kupatikana kwa sababu unapokuwa unafanya kazi ambayo huipendi kikubwa
kinachokutokea utajikuta unakuwa ni mtu wa kulalamika sana na pia unakuwa
unakosa ubunifu kitu ambacho ni hatari na
kitakufanya ushindwe moja kwa moja kwa kile unachokifanya. Kama unataka
kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, chagua kitu kimoja unachokipenda na
kifanye kwa moyo wote, mafanikio makubwa utayaona.
2.
Anza kwa kidogo.
Ni ushauri ambao pengine
umewahi kuusikia mara nyingi kwa namna
moja ama nyingine, lakini na mimi napenda kukumbushia leo kwa kile unachotaka
kukifanya kwenye biashara yako hiyo anza kwa hatua ndogo kwanza. Unapokuwa
unaanza kwa kidogo inakuwa inakusaidia wewe kuweza kupima kama utaweza kwenda
kwa hatua nyingine zaidi.
Acha kuogopa wala kukatishwa
tamaa na kitu chochote katika maisha yako kwa kuhofu kuwa pengine hayo malengo
yako hayawezi kutimia. Kila kitu kinawezekana na hakuna kitu kinachoshindikana
kwako hata kidogo. Anza kutekeleza malengo yako kidogo kidogo hata kama ni
makubwa vipi, lakini tambua kuwa ni lazima uyafikie.
3.
Jifunze kutoka kwa wengine.
Hautaweza kufanikiwa kama
utakuwa tu unaendesha biashara yako wewe mwenyewe na kushindwa kujifunza kutoka
kwa wengine. Unapojifunza kutoka kwa wengine inakuwa inakusaidia kukupa wewe
kuweza kutambua mapungufu uliyonayo ambayo yanaweza kukukwamisha na kukusaidia
kuweza kusonga mbele zaidi.
Hata hivyo unaweza pia
ukajifunza mikakati na mbinu za ujasiriamali zaidi kwa kujisomea kutoka kwa
wajasiriamali wengine wakubwa kupitia vitabu ambapo nako huko utapata
maarifa bora yatakayokutoa hapo ulipo.
Kama una nia na shauku kubwa kweli ya kutaka kufanikiwa na kuwa mjasiriamali
mwenye mafanikio makubwa ni lazima ukubali kujifunza kutoka kwa wengine kila
siku.
4.
Chukua hatua mapema.
Kusoma sana hakutakusaidia
kitu hata kama utasoma vipi hiyo itakuwa ni sawa na kazi bure kama tu utakuwa
huchukui hatua kwa vitendo kufanyia kazi kile kidogo unachojifunza. Kuwa mtu wa
vitendo ni hatua muhimu sana kwako wewe ya kukuwezesha kufikia mafanikio
makubwa katika safari yako ya ujasiriamali na biashara.
Watu wengi wenye mafanikio
makubwa siku zote huwa ni watu wa vitendo tu. Ndani ya maisha yao huwa
yametawaliwa na vitendo na huwa ni watu ambao hawajui kitu kinachoitwa
kuahirisha mipango waliyojiwekea. Jifunze kuchukua mapema katika kila kitu
unachokifanya katika maisha yako, hiyo itakusaidia kufika mbali sana katika
maisha yako.
5.
Kuwa na mipango imara.
Kila kitu unachokijua wewe
chenye mafanikio makubwa hapa duniani, huwa kinaanza na mipango tena mipango
iliyoimara. Hata biashara yako inahitaji kuwa na mipango mathubuti na imara ili
iweze kufanikiwa zaidi na kukuletea matunda unayoyataka. Kinyume cha hapo
utabaki ukilaumu tu kuwa mambo magumu kama wengine wanavyofanya.
Jifunze kujiwekea mikakati
na mipango endelevu kwa biashara yako. Hakikisha mipango utakayojiwekea iweze
kukusaidia kuisimamisha biashara yako na kuwa imara zaidi kwa miaka mingi
zaidi. Chukua muda wa kutafakari na kujiuliza baada ya miaka miwili, mitatu au
mitano kuanzia leo utakuwa umefika wapi kibiashara? Kuwa na mipango imara ni
nguzo muhimu ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyahitaji.
6.
Tengeneza ‘timu’ imara itakayokusaidia.
Mara nyingi huwa hakuna
jeshi la mtu mmoja au mafanikio makubwa yatakayoonekana kwa mtu mmoja pekee. Kuna
wakati katika maisha yetu huwa tunalazimika kutafuta watu watakaotusaidia
katika biashara zetu hilo ni lazima. Hii huwa ni muhimu sana kwa sababu sio
kila kitu tutaweza kukifanya sisi wenyewe tunahitaji wasaidizi ambayo ndiyo
timu yenyewe.
Katika zoezi zima la zima la
kujenga timu hakikisha unatafuta watu ambao watakusaidia kupigania kile
unachotaka kitimie katika maisha yako. Nikiwa na maana kuwa timu yako inatakiwa
kuwa msaada na kuweza kufanya kazi na wewe bega kwa bega mpaka malengo yako
uliyojiwekea yanatimia yanatimia. Kuwa na timu imara ni kitu muhimu sana katika
safari yako ya ujasiriamali.
7.
Acha kufikiria kuwa umechelewa.
Unaweza ukawa unakwama au
kushindwa kuendelea mbele kama inavyotakiwa iwe katika biashara yako, kutokana
na mawazo ambayo unayo ya kuhisi kwamba pengine umechelewa kwa kile unachotaka
kukifanya. Kwa mawazo haya yamekuwa yakikupelekea wewe kushindwa kufanya
mabadiliko makubwa yako katika biashara.
Kitu usichokijua hakuna kitu
kinachoitwa kuchelewa katika maisha yako. Wapo watu ambao mwanzoni walijihisi
na kujiona wamechelewa katika maisha yao, lakini walipokuja kugundua ukweli huu
walikuja kufanya mabadiliko makubwa sana. Kisikuzuie kitu chochote kufikia
ndoto zako. Unaweza ukawa na maisha yoyote unayotaka ukiamua.
8.
Kuwa na mitazamo chanya.
Hiki ni kitu muhimu sana
kukufikisha katika ngazi ya juu ya mafanikio na hatimaye kuwa tajiri kama
utaamua kuwa na mitazamo chanya. Unapokuwa na mitazamo chanya inakuwa inakusaidia
kukupa hamasa na nguvu ya kuona mambo yako yanawezekana hata katika maeneo
ambayo kweli yanakuwa yanachangamoto.
Ikumbukwe kuwa watu wengi
huwa wanakosa kufikia mafanikio makubwa kibiashara kutokana na kuwa watu wa
hasi sana katika maisha yao. Hali hii huwa inawapelekea wao kushindwa
kukabiliana na changamoto hata zile ndogo ambazo walikuwa wanauwezo wa
kuzivuka. Kuwa na mawazo chanya ni muhimu sana kwa mafanikio yako.
Kwa kumalizia, ukumbuke kuwa kiu ya mafanikio yako
unayoitaka uitimize itafanikiwa tu endapo, utakuwa mtu wa kujifunza na kuchukua
hatua muhimu zitakazoweza kubadili maisha yako. Chukua hatua leo na acha
kusubiri kesho au kesho kutwa utakuwa umechelewa sana na hautabadili kitu. Hizo
ndizo hatua muhimu za kufuata ili kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com.
Mar 21, 2015
Sifa 15 Ambazo Matajiri Wa Kweli Huwa Nazo.
Ni ukweli uliowazi kwamba
ili uweze kuwa tajiri wa kweli katika maisha yako huwa kuna sifa zake muhimu
ambazo zinamfanya tajiri huyu wa kweli aweze kutofautiana na tajiri Yule ambaye
anaweza kuwa ametumia njia za mkato ama ujanjaujanja fulani ambao huweza hata
kuwaumiza wengine kihisia au kimwili ilimradi tu kuweza kufikia utajiri huo
anaoutaka. Sifa hizi ndizo huwa zinaleta upekee na kuwafanya matajiri wa kweli
kuwa muhimu sana duniani.
Sifa za matajiri wa kweli
ambazo tunazizungumzia katika makala hii, ni za wale matajiri ambao wameamua kupigania maisha yao kutoka
chini kabisa mpaka kufanikiwa, ni wale ambao wameamua kutumia nguvu ya kuamua
na kuvikabili vikwazo mpaka kufanikiwa.
Swali ambalo unaweza ukawa umeshaanza kujiuliza ni sifa zipi ambazo matajiri wa
kweli huwa nazo, ambazo hata wewe unaweza kuzitumia katika maisha yako na
kukuwezesha kuwa tajiri?
Hizi
Ndizo Sifa Ambazo Matajiri Wa Kweli Huwa Nazo.
1.
Wamenuia.
Watu wenye mafanikio
wanakuwa wamenuia kufanikiwa. Wanachapa kazi na kila mara wanajifunza mambo
mapya. Wanafanya kila jambo ambalo litawawezesha angalau kufanikisha ndoto zao.
Ndani ya nafsi zao wanakuwa na shauku kubwa ya kufanikiwa hali ambayo
inapelekea wafanye kila linalowezekana hadi waweze kufanikisha hizo ndoto zao.
2.
Wamedhamiria.
Ukiwa una dhamira kubwa,
utasababisha mambo yako mengi, kusonga mbele. Watu wenye mafanikio huwa wepesi
sana kujua mambo gani ni ya kuyafatilia na mambo gani ya kuyapuuza. Kwa mambo
waliyodhamiria huamua kufanya kazi kwa nguvu kubwa hadi kufanikiwa katika
malengo yao.
3.
Hujitoa mhanga
Mara nyingi watu wenye
mafanikio hujitoa mhanga lakini zaidi zaidi ni majasiri . Wako tayari kuwekeza
na kufanya maamuzi yanayoonekana kuwa ya
HATARI kwa watu wa kawaida. Katika suala zima la kujitoa mhanga huwa hawaogopi
kitu na hawajali nani atasema nini? Wanachoangalia ni matokeo ya mbele
yatakayowasaidia.
4.
Hawakati tamaa.
Hawana msamiati wa “kukata
tamaa” kwenye kufikiri zao na hata kuzungumza kwao au hata kwenye hisia zao. Hakuna
kitu kama hicho kwenye ubongo wa mtu mpenda mafanikio. Wanaendelea kusonga
mbele hata kukiwa na vikwazo lukuki. Wanachojua ni kufanya kazi mpaka kuweza
kutimiza kile wanachokihitaji katika maisha yao.
5.Wabunifu.
Kila mtu anapenda kufanya
maamuzi ya ubunifu katika maisha yake kwa kiasi fulani. Lakini watu wenye
mafanikio wamegundua kwamba kuzama kwenye mafanikio huku ukiwa ndani mwako una
ubunifu ni kitu muhimu sana katika kupata mafanikio unayoyahitaji. Kwa hiyo
watu wote wenye mafanikio, wamezama sana kwenye ubunifu ili kupata matokeo
wanayoyataka.
6.
Ni wenye ndoto.
Ili kuweza kuishi maisha
yenye maana, binadamu hana budi kuishi maisha yenye ndoto katika mipango na
malengo muhimu aliyojiwekea. Watu wengi wenye mafanikio, kwa kawaida wanakuwa
wametumia muda mwingi wakifikiria ni aina gani ya ndoto waitimize katika maisha
yao. Wanapokuwa wameipata huweza kuifanyia kazi kwa nguvu zote mpaka kuweza
kufanikiwa kwa kile hasa ambacho wanakuwa wamelenga katika maisha yao.
7.
Hupenda kujifunza.
Wat wenye mafanikio mara
nyingi huwa wana sifa ambayo huwa ni ya pekee ambayo huwa inawatofautisha
kabisa na watu ambao hawana mafanikio. Sifa hii muhimu ambayo huweza kuwa nayo
ni sifa ya kupenda kujisomea. Watu wenye mafanikio mara nyingi huwa ni watu wa
kujifunza siku zote na huwa hawaachi. Kutokana na kujifunza huku kupitia vitabu
na semina mbalimbali hujikuta wana maarifa mengi sana ambayo huweza kuwasaidia
na kuwafanikisha kwa kiasi kikubwa kusonga mbele.
8.
Wana uwezo wa kubadilika.
Watu wapenda mafanikio
huenda kufuatana na upepo. Kuwa king’ang’azi, bila kusoma hali za nyakati za
upepo na maisha yanaendaje kwa wakati huo kuna wakati kunaweza kukupeleka
kuzimu. Watu wenye mafanikio wanaweza kubadili mwelekeo muda wowote ule hata
bila kutarajia, hii ni moja ya sifa muhimu ambayo hata wewe unatakiwa uwe nayo.
9.
Hawaogopi kutoa maamuzi.
Wahenga walisema, uwe
mwepesi kutoa maamuzi na nenda polepole katika kubadili maamuzi. Watu wenye
mafanikio ndivyo walivyo. Wanafanya maamuzi ya haraka na kuangalia mbele zaidi
katika maisha. Kuwa mtu wa kigugumizi sana huweza kupunguza nguvu ama mwendo wa
kuelekea kwenye mafanikio yako.
10.
Watulivu.
Ni ukweli usiopingika
mafanikio huchukua muda kuweza kuyajenga. Matajiri huwa sio watu wa kupenda
mafanikio ya haraka kama unavyofikiri bali huwa ni watu wa kujiwekea mipango na
malengo hadi kufanikisha kile wanachokihitaji. Huwa ni watu ambao sio wa
kulazimisha mambo katika maeneo ambayo hayawezekani hasa katika njia za mkato huwa hawaamini hilo. Huwa ni watu wa
subira kuhakikisha mambo yanaenda katika uhalisia wake.
11.
Wanajifahamu.
Ili kuwa mtu mwenye
mafanikio huna budi kujijua uwezo wako ulionao na hata mapungufu uliyonayo ili
kama ni kujirekebisha uweze kujirekebisha na kuweza kusonga mbele. Watu wenye
mafanikio mara nyingi hujijua undani mwao, wanataka nini na kitu hicho
wakitakacho watakipataje. Wanajua viwango vyao na hawavipunguzi zaidi ya
kuviboresha.
12.
Wawazi.
Watu wenye mafanikio mara
nyingi huwa wawazi katika mambo yao. Kile wanachoongea ndio huwa wanamaanisha
na sio tofauti na hapo. Huwa hawaoko tayari kuuma maneno, kama jambo
haliwezekani watakwambia haliwezekani tu. Lakini zaidi ya hapo watu hawa huwa
wako tayari kupokea habari zozote ambazo zinaweza kusababisha kufanikisha ndoto
zao zifanikiwe bila kinyongo.
13.
Ni watu wa kawaida.
Watu matajiri ni watu wenye
furaha sana katika maisha yao na huwa hawana makuu hata kidogo. Huwa ni watu
ambao wapo karibu sana na familia zao na kupata muda wa kuburudika. Ni watu
ambao unaweza kupishana nao mara kwa mara kadhaa kutwa usijue kwamba wanauwezo
mkubwa ndani mwao. Ni watu wanaojua kujichanganya kirahisi na hawauoni utajiri
wao kama kitu cha ajabu sana, hivyo hujikuta ni watu wa kujali sana wengine.
14.
Watu wa kiroho.
Hawa mara nyingi huwa ni
watu wenye mambo ya kiroho. Wanaamini kwamba maisha yao sio tu maumbile ya nje
bali hata mambo ya ndani mwao. Wanaamini kuongozwa na roho. Kumbuka sizungumzii
dini hapa, bali nazungumza maisha yaliyo juu ya uhitaji na utashi wa mwili,
hisia na akili.
15.
Ni watu pia wa kuburudika.
Kuishi maisha mazuri haina
maana kuwa kwamba ni kazi..kazi..kazi.. haina maana hiyo hata kidogo. Matajiri
wa kweli na wenye furaha mioyoni mwao huwa ni watu wenye furaha na ni watu
wanaopata muda wa kupumzika, wakifurahia upande wa pili wa maisha yao.
Kwa kuishi maisha ya kuwa na
sifa muhimu ambazo matajiri wa kweli wanazo ni njia bora kabisa
itakayokufikisha kwenye mafanikio ya kweli ambayo dunia inayahitaji. Hizo ndizo
sifa ambazo matajri wa kweli huwa nazo na kuweza kuzitumia katika maisha yao ya
kila siku.
Kwa pamoja tunaweza
kuyafikia mafanikio makubwa tuyoyahitaji katika maisha yetu, endelea kutembelea
DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maaarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA
SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Mar 19, 2015
Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.
Kuna wakati katika maisha
yako unaweza ukajikuta ama unatamani sana uwe katika ngazi fulani ya mafanikio,
lakini ni kitu ambacho huwa hakitokei kwako. Wakati mwingine umekuwa
ukidhamiria na kuamini kwamba, lazima itakuwa, lakini huwa haiwi kama unavyofikiria.
Pamoja na juhudi nyingi ambazo umekuwa ukizifanya, zimekuwa ni kama kazi bure
kwani mara nyingi umekuwa ukishindwa kupata hasa kile unachokihitaji katika
maisha yako ambacho ni mafanikio.
Pengine umekuwa ukijitahidi
hata kufanya sala au tahajudi(Meditation) ili kuweza kubadili mwelekeo na
kuweza hata kufanikisha kile unachokihaji, lakini wapi mafanikio hayo umekuwa
huyaoni. Ni kitu ambacho kumekuwa kikikuchanganya na kushindwa kuelewa unakosea
wapi hasa na ufanye nini? Hali hii imekuwa kuna wakati inataka kukuvunja nguvu
na kukufanya uamini kuwa, suala la kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako
ni kitu ambacho hakiwezekani.
Katika hali ya kushangaza
umekuwa ukiona wengine wakijaribu kuomba mara moja na kuweza kufanikisha jambo
lile, wakati kwako inakuwa ni vigumu sana, ingawa kama ni kudhamiria, na
kuamini kwamba itakuwa ni kulekule na pengine zaidi kwa hilo linaloshindikana.
Hali ama matokeo kama hayo yamekuwa yakikutisha tamaa na kukupelekea wewe
kutaka kuamini kuwa una kitu kama mkosi au laana fulani hivi inayokuzuia
ushindwe kufanikiwa, kitu ambacho sio kweli hata kidogo.
Bila shaka kwa namna moja au
nyingine unaweza ukawa umewahi kukutana na hali hii katika maisha yako ambayo
pengine imekuwa ikikuumiza kichwa na kushindwa kuelewa kabisa ni kitu gani
kinachopelekea wewe usiweze kupata matokeo mazuri kwa kile unachokihitaji
katika maisha yako?
Ingawa ukweli ni kwamba,
kuamini kwamba inawezekana na kudhamiria kumudu, huweza kuzaa au kutozaa
matunda kwa sababu moja tu kubwa. Huwa
kunakuwa na kusigishana au kupingana kati ya kile ambacho mtu anachoamini na
kile ambacho anadhamiria au kupania kiwe katika maisha yake na hiki huwa ndicho
kitu kinachokufanya usipate kile unachokihitaji katika maisha yako.
Kama mtu kwa mfano, anadhamiria au anapania kwamba,
anataka kuona uhusiano wake na mke wake au mume wake unakwenda vizuri, huku
akiwa anaamini kwamba, wanawake hawaaminiki, au wanaume ni wakorofi, uhusiano
huo hauwezi kuwa mzuri, hata kama amepania na kusali vipi kwake uhusiano mzuri
hauwezi kutokea. Unajua ni kwa nini?
Iko hivi, mara nyingi kupania
au kuamini kwetu kwamba, inawezekana na kutaka kwetu jambo liwe kama
tunavyotaka, sala zetu na maombi yetu, vyote hivi huwa vinafanyiwa kazi na
mawazo yetu ya kina. Sasa, kama kuna kitu kingine ambacho ni kinyume na kile
tunachotaka au kupania kiwe, ni wazi tunakuwa tunayachanganya mawazo ya kina na
inakuwa ni vigumu sana kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.
Kama kweli tunataka uhusiano
wetu uwe mzuri na tunaamini kwamba, inawezekana, lakini huko kwenye mawazo yetu
ya kina tunaamini kwamba, wanawake ni dhaifu, hatutaweza kupata tunachotaka kwa
sababu, mawazo yanakuwa yanapokea
taarifa au imani mbili zenye kukinzana au kupingana.
Kwa kuamini kwamba, wanawake
ni dhaifu, lile wazo la kwamba inawezekana kuwa na uhusiano mzuri na bora sana
litatupwa nje na kufanyiwa kazi lile lililokuwa hapo awali. Ni hadi ile imani
kwamba, wanawake ni dhaifu iondolewe, ndipo ambapo kudhamiria au maombi
yatafanya kazi.
Utakuta mtu anasali kila
siku na kuamini kwamba, atafanikiwa katika jambo fulani, lakini anakuwa ana
imani kwamba, rangi yake itamponza kwa sababu, anashindana na watu wenye rangi
nyingine. ‘Wenzetu wale wanajua namna
mambo haya yanavyofanywa’, atawaza. Kwa hiyo, dhamira na sala yake
vitatupwa nje na hili la ‘wenzetu’, ndilo litakalofanyiwa kazi.
Imani zetu, ambazo
tuliwekewa kwenye mawazo yetu siku za nyuma kwenye malezi au mazingira
tulimokulia, zinakwenda kwa kina kirefu hivyo zina nguvu zaidi. Tunapoleta imai
mpya zenye kukinzana na zile za zamani, hizi mpya ni lazima zitupwe nje au
tuseme haziwezi kufanyiwa kazi kabisa kwenye mawazo yetu ya kina na kujikuta
hatuwezi kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.
Hebu jaribu leo kufikiria
ama kutengeneza orodha ya mambo ambayo umekuwa ukiyaomba au ukitaka
uyafanikishe katika maisha yako na umekuwa ukiamini kwamba yanawezekana na
umekuwa ukifanya kwa kupania, lakini bado hayakubali. Kama utayapitia vizuri na
kurudi nyuma, utabaini kwamba, huenda kile ulicholishwa utotoni kuhusu
kutowezekana kwa mambo hayo, bado kina nguvu kubwa kwenye mawazo yako ya kina.
Ili sasa uweze kumudu kupata
kile unachokihitaji katika maisha yako ni muhimu sana kwako, kusafisha kwanza
mawazo yako kuhusu yale mabaya yaliyowekwa humo kuhusiana na jambo ambalo
unataka kufanikiwa kwalo. Kila kitu utaweza kukifanikisha katika maisha yako
kama hakuna kukinzana ndani yako. Kumbuka na tambua kuwa kukinzana ndani mwako
ndicho kitu kinachopelekea ushindwe kupata kile unachokihitaji katika maisha
yako.
Ansante kwa kutembelea mtandao
huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kwa ajili ya
kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048035,
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com.
Mar 17, 2015
Kama Unatafuta kitu Hiki Katika Maisha Yako, Utateseka sana.
Hebu fikiria, jaribu
kufikiria, halafu karibia kuamini au amini kabisa kwamba, una vitu vifuatavyo.
Una magari ya kifahari kumi, nyumba za kifahari mbili kila mkoa kwa mikoa yote
Tanzania, mashamba ya ekari elfu moja kila mkoa na fedha zipatazo shilingi
bilioni kumi benki. Hebu fikiria.
Najua unaweza kujenga
taswira, kama tunavyofanya wakati tunapoota ndoto za alinacha, hadi kufanya
hali ionekane kuwa ni kweli. Hebu fikiria tena kwamba, kwa sababu ya mali hizo
umekuwa maarufu katika nchi za afrika mashariki na kati. Hebu fikiria kwamba, unaandikwa
na kutajwa magazetini, redioni na kwenye televisheni.
Jione kwenye hizo fikra zako
kwamba, hayo ndiyo maisha yako, tajiri na maarufu. Halafu endelea kufikiria
kuhusu maisha yako. watu wanakujua, wanakuogopa, wanakushangaa na
kukunyenyekea. Kila unapoenda unajua watu wanakutazama na kutamani wangekuwa
kama wewe labda.
Endelea kufikiria kwamba,
umekuwa tajiri na maarufu tangu mwaka 1990 hadi leo. Hebu jaribu kufikiri kwa
makini zaidi, baada ya kusifiwa, kuogopwa, kunyenyekewa na kufahamika kila kona
, halafu kingefuata kitu gani? Ni kitu gani ungekuwa umekipata? Sawa, umesifiwa
na kufahamika na ukajisikia vizuri. Halafu inakuwaje baada ya kujisikia vizuri
kwa muda wote huo?
Katika kufikiri kwako,
unadhani bado utaendelea kujali kusifiwa na kunyenyekewa? Hapana, haiwezekani.
Baada ya muda fulani wa kusifiwa na kunyenyekewa, utagundua kwamba, hakuna
chochote ndani ya sifa hizo na kunyenyekewa huko. Kwanini? Kwa sababu, wewe siyo kusifiwa na kunyenyekewa, wewe ni
wewe hiki ndicho kitu hasa nataka ukijue vizuri hapa.
Lakini, hata kama utaendelea
kusifiwa na kujisikia vizuri, halafu itakuwa ni kitu gani? Hebu fikiria kwamba,
kila asubuhi ukiamka, magazeti yamendika kuhusu wewe kwa sifa zote, hata bei ya
viatu vyako, televisheni zinakuonesha
ukipanda gari lako la kifahari na kwenda uendako na redio zinazungumzia
juu ya fedha na utajiri wako sana tu. Hebu fikiria, unadhani itakusaidia kitu
gani hiyo?
Mwisho wa sifa hizo ni upi
hasa? Unaposifiwa ni wapi panajisikia vizuri, ni sehemu gani ya mwili inapata furaha au starehe? Lakini,
gharama ya kulinda sifa na kunyenyekewa huko unaijua? Huwezi kuijua kwa sababu
hujaingia kwenye sifa na kunyenyekewa na watu. Ukiingia na wale ambao tayari
wameshaingia, wanataka kutoka, hawataki tena ‘balaa’ hilo.
Mcheza soka maarufu wa siku
za nyuma kidogo, David beckam aliwahi kusema, maisha yake ni upuuzi mtupu kwa
sababu ya umaarufu, Diana aliwahi kujuta kufahamika kwake. Unapotafuta
mafanikio kaa chini ujiulize kweli unataka mafanikio hayo makubwa hasa au
unatafuta sifa tu ili watu wakujue?
Halafu jiulize tena
wakishakujua nini kinatokea? Tunawajua akina Bush, Tunawajua akina Neymer, hata
pia tunawajua akina Tyson. Halafu kuwajua kwetu kunawapa kitu gani, kinatokea
kitu gani? Wanaendelea kuwa watu walewale, wanaendelea kuwa binadamu na kama
sisi, miili yao itapotea hivi pindi.
Kuna profesa mmoja kwa jina
alipata kufahamika kama Yunus, ambaye ni raia wa Bangladesh. Huyu alikuwa ana Benki
ambayo iliweza kukopesha na kubadili hali za maisha ya familia karibu millioni
tatu(siyo watu, ni familia) nchini humo.
Lakini, pamoja na uwezo huo
aliokuwa nao yeye alipata kuishi kwenye nyumba ya kawaida tena ya kupanga. Hiyo
yote inaonyesha profesa huyu alikuwa hataki sifa wala kunyenyekewa na kuandikwa
kila mahali kwenye magazeti hilo lilikuwa sio lake, kikubwa alichokuwa
akitafuta ni mafanikio katika maisha yake na ambayo yatasaidia na wengine.
Tuna watu katika jamii yetu
tunayoishi, huwa ni watu wa kupenda sifa sana kiasi cha kujiita waheshimiwa. Si
ajabu huwezi kuwashangaa watu hawa wakilewa sana kwa lengo la kutaka kuonyesha
jeuri ya pesa kiasi cha kwamba mpaka kuweza kusahau nyumbani kwao.
Inadaiwa kwamba kwa watu
kama hawa, ili akupe stahili yako, hata kama ni madaraka kazini, lazima
umnyenyekee. Kama ametoka ndani, ni lazima uhakikishe unamkimbilia, kupokea
mkoba na kujidai hata kama kumfuta vumbi kidogo kwenye suti hata kama haina
vumbi.
Halafu unajiuliza, ni ya
nini yote hiyo? Ni huyuhuyu ambaye anakunywa pombe hadi anasaidiwa kuingia
garini? Kwanini anywe kiasi hicho? Pesa na umaarufu aliodhani utampa nafuu,
vimeshindwa kufanya kazi hiyo. Sasa ina maana gani, utajiri na umaarufu?
Labda utajiri kama ule wa
Profesa Yunus ndiyo utajiri tunaoutaka. Utajiri unaoangukia mikononi mwa watu
waliokamilika, kimwili, kihisia, kiakili na kiroho. Huu utajiri mwingine ni
visu vyenye kuwachanja walionao na kuwakatia wanaozunguka. Umaarufu tunaoutaka,
hauna kitu kwa sababu, hata kama ungekuwa maarufu vipi, polepole umaarufu
utafifia na maisha yako ya mwili hayazidi miaka 120.
Sasa kusifiwa kwa miaka 120
tu, kuna maana gani, kunakusadia kitu gani, wakati hata dini yako haikwambii
kuwa itaishi milele. Umebaini kwamba, hukuja duniani kutafuta sifa na umaarufu,
bali umekuja kuishi ili ufurahie maisha yako. Mara nyingi tunamtaja Bill Gates
kila siku unafikiri anajali hilo? Unafikri anajali kutajwa huko, ambao ni mtihani
mgumu kuliko kutafuta mali na utajiri alionao.
Ndiyo maana unaweza kukuta
mtu amenunua kagari na kujenga kajumba, halafu anamtukana na kumdharau kila
mtu. Anakwenda kwa wanamziki wamtaje jina lake kwenye nyimbo zao, anakwenda
kwenye televisheni kujidai anasaidia watoto yatima. Anatafuta sifa na kutaka
watu wamjue. Halafu wakishamjua ndiyo iwe nini?
Akiishiwa, anajifungia
ndani, anachanganyikiwa, anajenga uadui na kila mtu, anadai amelogwa. Anakuwa anababaika
kwa sababu amepoteza kile alichodhani ndicho yeye, mali na umaarufu. Hajui kwamba,
yeye yupo kama binadamu na ni kamili
bila chochote. Ni lini binadamu atainua macho na kuuona ukweli? Inaniuma
sana.
Kutafuta kujulikana ni
kutafuta kuinuliwa kutoka pale ambapo mtu anaamini yupo(Chini) ili ajisikievizuri.
Mtu ambaye anajua yupo anapostahili hana haja ya kutaka ainuliwe kutoka hapo
nakupelekwa mahali ambapo atahisi kustahili.
Kutaka sifa ni kutaka
kuondolewa kwenye tope, kwenye uchafu, pasipo faa na kuwekwa mahali pengine. Kwa
hiyo mpenda sifa, ni mnyonge kuliko mtu mwingine yeyote.
Wengi huwa hatujui kwamba,
sisi ni sisi na hatuwezi kuwa kitu kingine, tupande ndege, tununue merikebu, tujulikane
hadi uvunguni, tuimbwe na maredio na kuoneshwa na matelevisheni kutwa kucha,
bado ni sisi tu. Thamani yetu inaendelea kuwa ileile.
Huko ndani mwetu kunaendelea
kuwa kulekule. Ni kama kiti, hata ukikiwekea marembo gani, ukaweka miguu
mitatu, ukakitandika na dhahabu na lulu, kazi yake ni ileile ya kukaliwa,
haibadiliki. Ikishabadilika, kinakuwa siyo kiti tena.
Nasi hata tuwe vipi,
ubinadamu wetu hauwezi kubadilika, uko palepale. Msingi wa binadamu
haubadilishwi na chochote, kama ambavyo dhima ya kiti haibadilishwi na namna
kilivyotengenezwa. Kila mtu anapaswa kujua kuwa, amekuja duniani kuishi kama
yeye.
Kama ni furaha atajipa
mwenyewe, kama ni kero atajipa mwenyewe, kama ni kujishusha atafanya hivyo
mwenyewe, hali kadhalika kujipandisha. Lakini, hata kama itakuwa vipi, anabaki
kuwa binadamu.
Kama nilivyoanza awali mwa makala
haya. Nakuomba ujaribu kufikiri tena kwamba, tayari una kila kitu
kinachokuhangaisha hivi sasa. Fedha kibao, magari, majumba, umaarufu, mke au
mume mzuri kuliko wote duniani, watoto wenye akili kuliko wote. Halafu kitafuata
kitu gani?
Nataka ujiulize baada ya
hayo yote kutimia, ni kitu gani kitafuata? Kama umefikiri vizuri, utagundua
kwamba, ni upuuzi mtupu mbele. Utagundua kuwa hukuhitaji hivyo vyote hivyo,
bali ulihitaji ulivyohitaji wewe kuvihitaji.
Hivyo vingine siyo wewe
uliyevihitaji. Ni nani sasa anayekusumbua na kuhangaika na kubabaika na maisha
kuvitafuta hivyo? Nakuachia swali hilo.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu
na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com
Mar 12, 2015
Iheshimu Leo Isije Kukugharimu Kesho.
Hivi umewahi kufanya kitu
fulani halafu miaka ikapita ukajiuliza kama ni wewe umefanya hilo jambo, mimi
nimewahi. Kuna wakati katika maisha unaweza ukajikuta umefanya jambo fulani
halafu baadaye ukaja kujuta, ukajiona ni mjinga au hata limbukeni. Wakati
mwingine linaweza likawa fundisho kwako kiasi cha kwamba hata mtu akushawishi
vipi huwezi kurudi kufanya jambo hilo tena.
Hata hivyo tikirudi nyuma
huenda wakati unafanya hayo mambo ulikuwa unashauriwa, hivyo ukajikuta ukawa
sikio la kufa lisilosikia dawa. Au huenda hukupata nafasi ya mtu kukwambia
unachofanya siyo na kwamba kitakuja kukugharimu maishani. Tuachane na sisi
ambao tumepitia huko, tukajifunza na tukamwomba Mungu hiyo historia isije
kujirudia tena katika maisha yetu.
Leo, naongea na wale
wenzangu na mimi ambao tunaingalia leo. Kesho ni kama hatuijui vile au kama
haitakuwapo kutokana na mambo tunayoyafanya. Wengine husema ‘kesho itajijua’.
Kama ingekuwa hivyo basi tusingekuwa tunaihangaikia kesho.
Inafahamika wazi kuwa kila
mtu ana uhuru wa kufanya kile anachokisikia, lakini ukweli unabaki palepale
kwamba hata uhuru wa mtu binafsi una mipaka yake. Huwezi kufanya kila kitu bila
kuzingatia mambo muhimu hasa ya kimaadili.
Unajua kwa sisi vijana kuna
mambo mengi tunayafanya kwa sababu ndio wakati wake, ujana si maji ya moto
bwana. Ni kweli wala siyo uongo lakini wengi wetu tunafanya kwa kufuata mkumbo.
Kuiga sijui fulani kafanya hivi na mimi nifanye, mwingine kaenda huku na wewe
huyo kama kumbikumbi vile. Sasa unavyofanya hivyo unajua mwenzako kwa nini
anafanya?
Wengi hasa wasichana wanaona
fahari kumuiga fulani kafanya hivi ama vile. Kapate kile yeye atafanya kile
akiwezacho hata kama kitamgharimu maisha yake lakini bora tu awe kama fulani.
Kumbuka kuna kesho katika maisha yako, Yule unayemuiga hufahamu alivyojipanga
hadi akafanya yale unayoyaona. Mambo mengine ni siri ya mtu. Sasa wewe unaingia
kichwa kichwa utaumia.
Mwingine anaweza kuona
rafiki yake, kachora tattoo na yeye huyo. Hivi unafahamu kwamba unaweza kukatisha
ndoto za kuwa na mafanikio kuliko uliyonayo kwa sababu ya kufuata mkumbo? Kuna
vitu tunaweza kuviona ni vya kawaida lakini kuna watu hadi leo wakikumbuka
jinsi vilivyowagharimu katika maisha yao inakuwa inauma. Kuwa mtu na msimamo
wako, maisha yako ni yako. Mwisho wa siku utakuja kusimama wewe kama wewe
kwenye mambo yako ya msingi.
Nakumbuka kuna jamaa mmoja
alipata nafasi ya kazi serikalini lakini alikuwa amechora tattoo. Kila siku
akawa mtu wa kuvaa mashati yenye mikono mirefu, hata kukiwa na joto la aina
gani hata mikono hawezi kukunja.
Alipoona watu wanamuuliza
sana na kuna baadhi ya watu walianza kuhisi kwamba kuna kitu anaficha,
alilazimika kwenda india kufanyiwa upasuaji. Huko alichomwa sindano ile ngozi
ya juu iliyokuwa imechorwa ikaamuka halafu ikakatwa. Baada ya hapo aliuguza
kidonda na kurejea akiwa na kovu. Hadi leo anakovu kwenye mikono. Sasa shida
zote za nini? Iheshimu leo, isije ikakugharimu kesho.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
kupata elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
- Makala hii imeandikwa na Suzan mwillo wa Gazeti La Mwananchi.
- Mawasiliano suzanmwillo@yahoo.com
Mar 10, 2015
Hivi Ndivyo Kufikiri Kimazoea Kunavyoweza Kuharibu Maisha Yako.
Kuna wakati katika maisha
yetu huwa tunajikuta ni watu wa kutenda mambo yetu kwa mazoea zaidi na kudhani
tupo sahihi, wakati tupo kwenye makosa matupu ambayo huwa yanatuumiza, badala
ya kutusaidia kama tunavyofikiri. Makosa haya huwa tunayafanya kutokana na
matendo ama mienendo ambayo tunakuwa nayo binafsi katika maisha yetu ya kila
siku bila kujijua sisi wenyewe kuwa tunakosea.
Makosa haya mara nyingi huwa
yanatokana na kufikiri kimazoea. Kufikiri huku kimazoea kwa kawaida huwa ni
jambo baya sana ambalo huweza kuathiri
maisha yetu. Tunapoamua kufikiri kimazoea maana yake huwa tunalazimika kufikiria
kwa mujibu wa kile tulichofundishwa utotoni katika malezi au mazingira
tulimokulia, bila kujiuliza wala kuchukua hatua zozote muhimu zenye uwezo wa
kuleta mabadiliko tofauti kwetu.
Hebu fikiria kuhusu
kulalamika au kunung’unika. Watu wengi huwa hawajui kwamba, tunaponung’unika
tunasema au kujiambia kwamba hili tatizo ambalo tunalinung’unikia hatuwezi
kulikabili au kulitatua, bali kuna wengine wanaoweza kulitatua. Kulalamika, iwe
tunajua au hatujui, lakini kuna maana ya sisi walalamikaji kukosa uwezo,
kushindwa kumudu, hivyo kutegemea wengine kumudu au kufanya kwa niaba yetu.
Kwa kulalamika, tunaamini
kwamba, kwa hizo kelele zetu tunawachochea wengine ambao tunaowaamini kwamba wana uwezo wa
kukabiliana na yale matatizo yanayotukabili kwa wakati huo. Badala ya
kulalamika, tunatakiwa kupeleka nguvu zetu zote kwenye suluhu ya tatizo.
Kulalamika kuna maana kwamba, nguvu zetu tumezipeleka kwenye kuamini kwamba
tatizo ambalo linatukabili hatuliwezi na hatuoni suluhu yoyote.
Hebu fikiria juu ya kulaumu
kwako. Hii ni tabia ambayo wote tunaiona ni sahihi kabisa kwa sababu ya mazoea
tu. Tunapolaumu, bila kujua tunaiambia dunia pamoja na sisi wenyewe kwamba,
hatuna nguvu, bali kuna wenye nguvu zaidi kuliko sisi ambao wameshindwa
kutuwezesha au kutugawia. Fikiria tena tokea umeanza kulaumu katika maisha yako
ni kati kikubwa ambacho umevuna, zaidi ya kuharibu maisha yako?
Kwa kulaumu, tunatupa nguvu
na uwezo uwezo wetu wa kubaki watupu. Kwa kuwa kila binadamu anapaswa
kuwajibika kwa maisha yake, kulaumu tuna maana kwamba tumeshindwa wajibu wetu.
Tunaamua kwa kusudi kabisa kuwa wahanga wa maisha yetu, uamuzi ambao
haupendezi. Badala ya kulaumu sana, jifunze kukaa chini na kuchukua hatua
ambazo zitakusaidia kuelekea kwenye kubadili maisha yako.
Kuna kujilaumu au kujikosoa,
tabia ambayo pia ni ya kimazoea. Kumbuka, kile kinachoenda ndani, kwenye
kufikiri kwetu, ndicho chenye kujionesha nje. Kwa kuwa maisha hutupatia kile
tunachokihitaji, kwa kujilaumu au kujikosoa, tunachopata ni maumivu ya jambo
tunalojilaumu kwalo. Tunapojiambia kwamba, sisi ni wajinga kwa sababu
tumeshindwa biashara fulani, ni lazima
tutakuwa wajinga kweli, kwani hicho ndicho tunachokitaka.
Badala ya kujikosoa
tunapofanya jambo kinyume na matarajio yetu na tunakuta tunataka kujilaumu,
inabidi tuchukue kalamu na karatasi na kuandika yale yote ambayo ni mazuri kwa
upande wetu. Tunayo mazuri mengi, kila mtu ana mazuri mengi. Hivyo, hatuna haja
ya kujikosoa kwa mabaya yetu, kwani hayo siyo tunayoyahitaji. Unachohitaji wewe
ni kuachana na kujikosoa sana na kusonga mbele.
Kila tunapojikosoa,
tunapaswa kujua kwamba, tunazuia nguvu nyingi chanya kuweza kutufikia na
kutusaidia tunakotaka kwenda. Hii ni kwa sababu tunayaambia mawazo ya kina
kwamba, hatustahili kupata mema au mazuri. Kumbuka, maishani huwa tunakipata
kile tunachokitaka au kukitarajia. Kama utakuwa tu wewe ni wa kujikosoa sana,
itakuwa ni sawa na kujiambia hutaki mafanikio makubwa maishani mwako.
Kunakuwakosoa wengine
kimazoea. Kwa mazoea, tabia hii huwa tunaiona kuwa ni ya kawaida sana na haina
madhara kwetu. Huwa tuaamini kwamba, tuna haki ya kukosoa wengine na jambo hilo
haliwezi kutudhuru. Kwa kuwahukumu wengine vibaya au kuwakosoa , tunatengeneza
vurugu na ukosefu wa amani kwenye mfumo wetu wa kufikiri na ufahamu. Hii ni kwa
sababu, tunaupeleka uzingativu wetu kwenye jambo ambalo hatulitaki.
Kijicho ni tabia ambayo
wengi tunadhani au kuamini kwamba, ni lazima tuwe nayo. Lakini kijicho ni
dalili ya mtu kuamini kwamba yeye hawezi kama huyo anayemwonea kijicho na
hatakuja kuweza. Kuwa na kijicho ni moja ya tabia ya kimazoea ambayo huwa
inauwezo mkubwa wa kuharibu maisha yetu wenyewe bila kujijua.
Jaribu kufikiria au kutazama
ule uzoefu mzuri kuhusu maisha na siyo usioutaka. Jaribu kuangalia yale tu
unayoyapenda kwa watu kuhusu watu wengine.
Kisha jenga tabia nzuri ambazo zitakusadia katika maisha yako na achana
na kufikiri kimazoea ambako hakuwezi kukusidia kitu zaidi ya kukupa maumivu tu.
Hivyo ndivyo kufikiri kimazoea kunavyoweza kuharibu maisha yako.
Nakutakia mafanikio mema,
ansante kwa kutembelea matandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea
kwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri yanayoendelea hapa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)