google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Feb 9, 2015

Maisha Ni Vitendo Na Si Ndoto Pekee, Ndoto Ni Mwanzo Tu Wa Maisha…

No comments :
Kwa kawaida, binadamu ana mambo matatu muhimu ambayo anaweza kuyaendesha au yakamwendesha kichwani kwake, moja ni fikra zake au mtazamo (thoughts you think), mbili ni taswira anazozijenga kichwani kwake (image you visualize) na tatu ni vitendo vyake (the actions you take). Sisi binadamu tunawajibu wakuhakikisha tunaleta maendeleo katika maeneo tunayoishi kwa juhudi zetu binafsi. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu mwenyewe.

Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake. Mambo yote tunayoyaona duniani, ugunduzi, vitabu, miziki, filamu na kila kitu kilichopo duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha, vipaji, talanta na habari njema ya maisha yako. Kutokana na upekee ulionao duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe. Historia ya dunia inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na makubwa kuhusu uwezo wao.

Toka enzi za wajasiriamali tunaowasoma katika historia akina Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na hata kutojiamini kabisa. Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo mengi kwa kutumia vipawa vyao.

Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wameshawishiwa na mifumo ya dunia na maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama nakala. Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo wao wa kipekee na kutumia upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao.


Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako yatapata maana. Unacho kipaji ndani yako. Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani, Mungu aliumba mwanadamu mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.

Unaweza usiwe na uwezo kuanzisha biashara ya mgahawa au ya daladala lakini ukawa na uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo za kila aina hivyo ukawa mjasiriamali  katika kanda ya mziki iwapo una uwezo wa kuchekesha basi fanya ujasiriamali katika kipengele cha ucheshi kama jamaa wa futuhi. Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa duniani ili  kuifanya dunia itembee, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ing'are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa hatujayajua bado lakini yamo ndani yako. Aidha wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia iwe na mitandao tunayoiona sasa hivi.

Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na mengine. Bila kujionea aibu mwenyewe, na kujitafuta na kujiuliza kasoro zako ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza, tafuta kujua mazuri ya kwako huku ukitafuta kuongeza mengine.

Ukiona Kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope kujaribu, jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi. Sikiliza sauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani? Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?

Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. Vipo vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya. Lakini ni uamuzi wako kukubali kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa vile ninavyotaka maishani.

Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali kumalizwa, vumilia, jiamini, Jipende, jiendeleze, jikaze, jionyeshe, jitafute mwenyewe, jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na nguvu zozote mbele yako. Kumbuka kuwa dunia hii itaendelea kuendeshwa na hata kutengenezwa na binadamu wenye uelewa mpana wa nguvu iliyo ndani yao na si wababaishaji na wenye maisha ya maridadi.Wanadamu wote walioweza kufanikiwa.

Kuna wakati tumekuwa tukilaumu watu wasiohusika katika maisha yetu magumu, kuwa wanaharakati wa mambo yasiyotuhusu, kutoa maoni yasiyo na maoni na kuchambua timu za ulaya na kuelezea mchezaji fulani analipwa kiasi gani cha mshahara. Ni lini umewahi kaa nyumbani kwako au kwenu na ukatumia muda wako kuchambua vipaji vyako? Ambavyo ungevitumia katika maisha yako na jamii inayokuzunguka?Kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajijua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe.

Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki, nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio atakayotengeneza na mwenyewe. Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa, kila mwanadamu anao uwezo wa kufanikiwa. Na zaidi ni kuwa kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake, lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna vichangizi vya mafanikio / success ingredients.

Unachopaswa kutambua ni kuwa, hali ya maisha uliyonayo sasa si kipimo cha mafanikio yako ya baadaye, unaweza kuwa vyovyote kimafanikio kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha Kwa kujua vipaji na vichagizi hivyo ni kama vifuatavyo: Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha.

Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni, maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo. Ukitaka kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa duniani.

Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe, ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza. Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini. Kila mwanadamu anayo zawadi ndani yake, zawadi hii huja kama kitu anachokipenda na kukiweza. Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio. Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta mafanikio.

Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk. Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio. Maisha ni vitendo na si ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupanga peke yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo.

Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza na kujifunaza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha bila maarifa hayatembei. Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu.

Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuaji kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako unakua zaidi. Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa mjasiriamali wa kipekee na yale ayatakayo maishani, Dunia ina mengi ya kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli.

Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili. Siri kubwa ya watu wenye mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha, wapo tayari kuumia kwa kuchagua maisha wayatakayo. Chagua kipengele mojawapo cha kijasiriamali unachotaka kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua kufanikiwa.

·        MAKALA HII IMEANDIKWA NA MESHACK MAGANGA – IRINGA

·        MASALIANO - 0713486636

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.