Feb 19, 2015
Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.
Habari ya leo mpenzi msomaji
wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu ya kuwa umzima wa afya
na unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako ya kila siku. Ninakukaribisha
sana katika siku nyingine tena, ambapo tunakutana kujadili maisha, lengo likiwa
ni kuhakikisha tunapata maarifa bora yatakayoweza kutusaidia kuweza kuboresha
maisha yetu na kuwa ya kiwango cha juu kabisa cha mafanikio kama tunavyotaka
iwe.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia
hasa juu ya malengo na jinsi ambavyo tunaweza kufikia malengo tuliyojiwekea
bila kizuiliwa na kitu chochote. Mara nyingi wengi wetu kuna wakati huwa ni
watu wa kujiuliza, nitawezaje kufikia lengo hili ama lile katika maisha yangu.
Ni maswali ambayo huwa yanakuja pengine kutokana na mtu huyo kugundua kuwa kuna uwezekano wa
yeye kutotimiza malengo yake kwa sababu anazozijua yeye, ikiwa ni pamoja na
wasiwasi ama kushindwa kujiamini.
Wengine kutokana na wasiwasi
ama kushindwa kujiamini kama nilivyosema, hujikuta ni watu wa kuamini kuwa
labda wanaotimiza malengo ya aina fulani ni watu wenye vipaji, wamejaaliwa na
pia ni watu wenye bahati sana katika maisha yao, kitu ambacho sio kweli hata
kidogo. Kiukweli, unaouwezo mkubwa wa kutimiza malengo yoyote unayojiwekea
katika maisha yako, kama utaamua iwe hivyo kwako. Hakuna kitu ama mtu mwenye
uwezo wa kukuzuia wala huhitaji nguvu za ziada kufanikisha hilo.
Unaweza ukawa unaanza
kujiuliza nifanye nini au ni kipi cha kufanya ili niweze kutimiza malengo yangu
muhimu niliyojiwekea? Ni vizuri kujiuliza hivyo maana hiyo nayo ni hatua ya
kuonyesha kuwa una nia na mafanikio unayoyataka na wala hutanii. Kipo kitu
muhimu ambacho wewe unatakiwa ufanye ili kutimiza malengo yako, kitu hiki
nikufatilia na kufanyia kazi hatua hizi tano za kufikia malengo yako na si
vinginevyo. Ukifanya hivyo uwe na uhakika utafikia malengo
yako bila wasiwasi. Unajua hatua hizo ni zipi?
Hizi
Ndizo Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.
1.
Ni lazima uwe na hamasa ya kutaka kufanikiwa.
Hautaweza kufanikiwa kama
huna njaa na kiu kubwa ya mafanikio ndani mwako. Ili uweze kufanikiwa hasa kwa
malengo uliyojiwekea ni lazima uwe na hasira kubwa ya mafanikio. Ukiwa na
hasira hii, itakusaidia wewe kupita eneo lolote, hata katikati vizuizi ama
vikwazo ambavyo huwa tunakutana navyo katika safari ya mafanikio. Watu wengi
wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao walikuwa na hasira na malengo yao
waliyojiwekea.
2.
Anza kuchukua hatua mapema.
Kuongea sana juu ya mipango
na malengo mazuri uliyonayo hakutakusaidia kitu, zaidi ya kuchukua hatua muhimu
za kuelekea kwenye utekelezaji. Anza kuchukua hatua mapema za kutekeleza ndoto
zako hata kwa kidogo kidogo ipo siku utafika. Ni bora ukafanya kwa kidogo hiyo
itakusaidia sana tofauti na ambavyo ungekaa na kusubiri, hiyo ingekuwa
inakupotezea muda sana katika maisha yako.
3.
Unahitaji kujifunza zaidi.
Hii ni hatua muhimu pia ya
kufikia malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Ni muhimu kujifunza na
ukapata maarifa yanayoendana na malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Hiyo
itakusaidia kujua vitu vya msingi vinavyoendana na malengo uliyojiwekea. Kwa
mfano, kama malengo yako ni kuwa millionea baada ya miaka 20 kuanzia sasa ni
lazima uanze kujifunza kuishi maisha wanayoishi mamilionea kwa kujisomea kila
siku.
4.
Unahitaji kuwa na mitazamo chanya.
Mara nyingi kuna wakati huwa
tunashindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea kutokana na mitazamo tuliyonayo
juu ya malengo yetu. Kama unajiona huwezi kufikia malengo yako, huo ndio ukweli
hutaweza kuyafikia. Jenga mitazamo chanya ambayo itakusaidia kufikia malengo
muhimu uliyojiwekea. Achana na fikra ama imani za kuwa huwezi kufanikiwa kwa
sababu hii na hii, jiwekee mitazamo chanya na utaweza kufikia malengo yako.
5.
Jifunze kutokana na makosa.
Kuna wakati huwa tunafikia
mafanikio kwa yale tunayoyahitaji baada ya kukosea sana hiki na kile. Hautaweza
kufikia mafanikio au malengo yako kwa urahisi kama unavyofikiri, kuna wakati ni
lazima ukosee. Unapokosea huo ndio huwa wakati muhimu kwako wa kujifunza
kutokana na makosa uliyoyafanya. Acha
kusononeka wala kulia kama kuna sehemu umekosea, hiyo hatakusadia kitu. Badala
yake, chukua hatua muhimu ya kunyanyuka pale ulipoanguka, jifunze na kisha
songa mbele.
Mwisho, unaposhindwa kufikia
malengo yako kwa namna yoyote ile acha kulaumu vitu ambavyo viko nje ya wewe kuwa
ndiyo vimesababisha ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea. Mara nyingi sisi
wenyewe huwa ndio huwa vizuizi wa malengo yetu. Jifunze hatua hizo tano muhimu
zikusaidie kufikia malengo muhimu uliyojiwekea katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio. Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri
yanayoendelea humu.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.