May 16, 2016
Tabia Zinazoua Ndoto Na Mafanikio Ya Wengi.
Kimsingi,
tabia ni nguzo kubwa ya mafanikio katika maisha yako ikiwa lakini utazitumia
tabia hizo vizuri. Mafanikio yote uliyonayo na yale unayoyategemea kuyapata,
siku zote yanategemea sana tabia ulizonazo. Kwa maana hiyo, kabla hujaamua
kuibeba tabia ya aina fulani, ni vyema ukajiuliza kwanza kwa tabia hii itanisaidia
kunifanikisha au itanirudisha nyuma?
Maswali
hayo ni muhimu kujiuliza ili yakusaidie kuchagua tabia zinazokupa mafanikio.
Kwa sababu tunaambiwa mafanikio ni tabia. Kama mafanikio ni tabia usibishe na
wala hutakiwi kujiandaa kubisha, ni lazima kwako uwe na tabia za mafanikio ili
ufanikiwe. Ni tabia za mafanikio ambazo utakuwa unazitumia kila siku, ndizo
zitakazo kufanikisha na si vinginevyo.
Lakini,
hata hivyo katika hali ya kushangaza watu wengi bado wana tabia nyingi hasi
zinazowafanya wasifanikiwe. Kwa kifupi, ni watu wanaotumia sana tabia zisizo za
mafanikio kuendesha maisha yao. Kutokana na kuwa na tabia hizi kwa muda mrefu,
zimekuwa zikipelekea wao kuua ndoto na mafanikio yao kwa ujumla katika maisha.
Ni
tabia hizi hizi ambazo hata wewe unatakiwa kuzijua ama kuziepuka kabisa ili
usiweze kuua ndoto na mafanikio yako. Naamini una hamu ya kutaka kujua ni tabia
zipi ambazo ukiwa nazo huwezi kufanikiwa. Kwa sasa, tuliza akili yako na
fuatana nami katika makala haya kujua tabia zenye uwezo wa kuua ndoto na
mafanikio yako kabisa.
1)
Kuahirisha.
Kama
unataka kuokoa ndoto na mafanikio yako kwa ujumla, kuahirisha mambo ni tabia ya
kwanza ambayo unatakiwa kuachana nayo mara moja. Wengi wamekuwa ni watu wa
tabia hii ya kuahirisha mambo na kuona ni kitu cha kawaida.
Kwa
mfano, utakuta mtu anataka kuanzisha jambo fulani lakini katika hali ya
kushangaza analiacha jambo lile na kudai kwamba atalifanya muda mwingine.
Kuahirisha mambo kwa namna hiyo kunavyoendelea kwa muda ndivyo ambavyo hujikuta
ndoto na mafanikio ya wengi hufia hapo.
Acha kukata tamaa mapema. |
2)
Uvivu.
Huwezi
kufanikiwa katika maisha yako kama kazi zako unazifanya kwa uvivu. Kwa bahati
mbaya wengi wetu ni watu wa kufanya kazi kivivu na kutegemea kupata matokeo
makubwa kitu ambacho hakiwezekani. Ni watu wa kupenda starehe na kutaka kuona mafanikio
yanatokea kirahisi rahisi bila kujituma sana.
Ukweli
wa mambo ulivyo hakuna mafanikio rahisi. Hakuna mafanikio ya muujiza ya kulala
maskini na kuamka tajiri. Ili uweze kufanikiwa unatakiwa kujituma sana na kuacha
kila aina ya uvivu pembeni. Ila uking’ang’ania uvivu elewa kabisa unaua ndoto
na mafanikio yako na sahau kufanikiwa.
3)
Kukata tamaa mapema.
Hakuna
ubishi wowote, ikiwa una tabia ya kukata tamaa mapema ni wazi huwezi
kufanikiwa. Kutokufanikiwa kwako kutakuja si kwa sababu huna uwezo wa
kufanikiwa, bali ni kwa sababu unakuwa umeacha kile unachokifanya kabla ya
kufikia mwisho wa mafanikio yalipo.
Kwa
mfano, ili kuku aweze kutotoa kifaranga ni lazima aatamie kwa siku ishirini na
moja. Ikiwa kuku huyo ataatamia yai lake kwa siku ishirini na kuliacha, ni wazi
vifaranga wa kuku hao hawawezi kutoka kwa sababu siku za kuatamia hazijafika.
Halikadhalika na mafanikio yako hivyohivyo. Upo muda wa kufikia mafanikio yako.
Ukikata tamaa mapema kabla ya kufikia muda wako wa mafanikio, hautaweza
kufanikiwa.
4)
Visingizio.
Mara
nyingi zipo sababu nyingi sana ambazo
watu wanajiambia karibu kila siku kwa nini wanashindwa kufikia mafanikio ya
aina fulani. Kati ya sababu hizo ambazo zinatolewa ukiziangalia hakuna sababu
mbaya za wao kushindwa kufanikiwa, sababu zote ni nzuri na zinafaa. Lakini,
linapokuja suala la mafanikio kwa bahati mbaya sana huwa hakuna sababu.
Kwa
mfano, tuchukulie umepanga kufanya jambo fulani baada ya mwezi mmoja. Inapofika
ule mwezi ukashindwa kulifanya jambo hilo kutokana na sababu zako ambazo
unazijua, basi umeshindwa. Hakuna kutoa sababu. Hata kama sababu zako ukatoa
zikawa za kweli, haziwezi kusaidia kufanikisha jambo lako tena. Dunia haitaki
sababu zako, inachotaka ni matokeo ya kile unachokifanya. Ukikumbatia sana
visingizio hutaweza kufanikiwa.
5)
Mawazo hasi.
Tabia
kubwa ambayo watu wengi wanayo na inaua ndoto za wengi ni mawazo hasi. Mara
nyingi wengi wetu ni watu wa mawazo hasi sana. Mawazo haya hasi huwa yapo kwetu
sisi na hata kwa wale wanaotuzunguka. Ni kitu ambacho watu huwa wanakichulia
kwa kawaida iwe kwa kujua au kutokujua lakini kwa kifupi mawazo hasi yanaua ndoto
na mafanikio kwa ujumla.
Kwa
mfano, kama unaamini una mkosi, laana au unaona huna uwezo wa kufanikiwa,
tambua hayo ni moja ya mawazo hasi ambayo unayo na ni hatari sana kwa mafanikio
yako. Ili kufanikiwa ni vizuri ukajijengea tabia ya kuwa na mawazo chanya. Bila
kuwa na mawazo chanya ya kuamini kuna ushindi na mafanikio yapo, hakika huwezi
kufanikiwa hata ufanyaje.
6)
Matumizi mabaya ya pesa.
Ili
ndoto zako ziweze kutumia zinahitaji pesa. Bila kuwa na pesa malengo na mipango
yako haiwezi kutumia kwa uhakika kama unavyotaka. Sasa kama unapata pesa halafu
ukawa una matumizi mabovu, hiyo ni moja ya tabia ambayo inaua ndoto na
mafanikio yako kwa kiasi kikubwa.
Pesa
yoyote inayopatikana inatakiwa kutunzwa tena sana kwa ajili ya uwekezaji. Kwa
hiyo kabla hujatumia pesa yako ni vyema ukajiuliza mara mbilimbili, kwamba je,
fedha hii inakwenda kwa matumizi sahihi? Ukiwa na matumizi mabovu ya pesa hakuna
utakachokifanikisha kikubwa kwenye safari yako ya mafanikio.
7)
Kuridhika.
Kati
ya kitu ambacho hakifahamiki sana, lakini kinaua mafanikio makubwa ya wengi ni
kuridhika. Kama ndani yako una tabia ukipata mafanikio kidogo ndio umeridhika
basi elewa hutaweza kufanikiwa sana. Hautafanikiwa kwa sababu tena utakuwa
hauna kitu chenye nguvu au uwezo wa kukusukuma na kukutoa hapo ulipo.
Kama
unafikiria natania waangalie watu ambao baada ya kupata mafanikio kidogo
wakaridhika maisha yao yakoje. Bila shaka yoyote utagundua maisha yao yameshuka
si ya viwango vile vya kipindi kile. Kwa kawaida unaporidhika unakuwa unakosa
ubunifu na matokeo yake kujikuta siku hadi siku unakuwa unarudi nyuma badala ya
kufanikiwa.
8)
Ulevi kwenye mitandao ya kijamii.
Changamoto
kubwa inayowakabili vijana wa sasa ni matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Vijana wengi badala ya kutumia mitandao ya kijamii kwa faida huitumia kwa
hasara. Wengi hutumia mitandao hiyo kama ‘kuchati’
na kutuma picha ambazo hazina mbele wala nyuma.
Kama
unatumia mitandao ya kijamii kwa namna hii, ujue kabisa unaua mafanikio yako
bila wewe kujua. Hiyo yote kwa sababu unakuwa unapoteza muda na nguvu nyingi
kwa vitu ambavyo vilitakiwa kukusaidia. Kama unataka kufanikiwa badilisha
matumizi ya mitandao ya kijamii yawe kwa faida kwako.
Kwa
leo tutaishia hapa, lakini hizo ndizo tabia ambazo unatakiwa kuwa nazo makini
ili kuepuka kuua ndoto na mafanikio katika maisha yako.
Ni
wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,
Email;
dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.