May 23, 2016
Mambo Ya Msingi Kuhusu Mafanikio Unayotakiwa Kuyajua.
Ili uweze
kufanikiwa kwa jambo lolote, ni lazima uwe na msingi imara wa jambo hilo kwanza.
Pasipo kuwa na misingi imara utasumbuka sana katika kufikia mafanikio kwa kile
unachokifanya. Lakini hiyo haitoshi unatakiwa pia kulielewa kwa mapana zaidi
jambo unalolifanya ili likufanikishe. Hata kwenye maisha yako binafsi, huwezi kufanikiwa
kama hujui mafanikio ni nini kwako au yanataka nini.
Wengi
kwa sababu ya kutokujua hili hujikuta wakisaka mafanikio kwa muda mrefu na
kuambulia patupu. Kama unataka kufanikiwa kweli, kuanzia leo anza safari yako
ya mafanikio kwa kuyapata mtazamo chanya wa kitofauti. Ni lazima ujue mambo ya
msingi yanayohusu mafanikio ili uweze kufaniwa na kuwa mtu wa tofauti. Acha kun’gang’ania
kukaa kwenye umaskini, toka hapo na uufuate utajiri.
Karibu
sana na twende pamoja kujifunza mambo ya msingi yanayohusu mafanikio.
Mafanikio
ni hatua.
Hakuna
ambaye amewahi kulala na kuamka asubuhi akiwa tajiri. Hakuna ambaye aliyeweka
juhudi kubwa kwa muda mfupi halafu akawa tajiri. Hakuna mafanikio ambayo
yanapatikana kwa muda mfupi. mafanikio yote unayoyajua wewe yanatengenezwa kwa
hatua. Ndio, mafanikio ni matokeo ya kupiga hatua kwa hatua kila siku.
Usitishike
na kuona mafanikio makubwa ya watu ukafikiri walianzia hapo walipo. Kama
unawaza hivyo, unajidanganya. Mafanikio yao yalijengwa kidogo kidogo, siku kwa
siku na hata miaka. Ikiwa unataka kufika huko waliko acha kukurupuka. Jipange
na anza kuelekea kwenye mafanikio yako hatua kwa hatua. Baada ya miaka michache
utakuwa mbali sana.
Mafanikio ni hatua kwa hatua, usikate tamaa. |
Mafanikio
ni kujitoa.
Siku
zote mafanikio ni kujitoa tena kwa moyo wote. Hakuna mafanikio ambayo unaweza
ukayapata kama haupo tayari kujitoa. Iwe unataka au hutaki ni lazima ujitoe na
kukubali kupoteza baadhi ya vitu ili uweze kufanikiwa. Upo wakati ambapo ni
lazima utapoteza marafiki, muda wako, pesa kwa ajili ya mafanikio.
Yanapotokea hayo yote usijali sana, kwani kumbuka kama nilivyosema mafanikio yanahitaji kujitoa. Kwa wale rafiki zangu ambao wanataka
mafanikio lakini wakati huo huo hawako tayari kupoteza baadhi ya vitu ili kufanikiwa,
huwa sio rahisi kwao kufanikiwa. Ili kufanikiwa unahitaji kujitoa mhanga kwa mambo mengi
sana ikiwemo pamoja na kuwa mgumu kwenye mambo yako. Bila kujitoa kikamilifu
mafanikio utayasikia kwa wengine.
Soma; Tabia Zinazoua Ndoto Na Mafanikio Ya Wengi.
Soma; Tabia Zinazoua Ndoto Na Mafanikio Ya Wengi.
Mafanikio
ni uchaguzi.
Kila
siku katika maisha yetu huwa tuna chaguzi nyingi ambazo tunazifanya. Kwa mfano
huwa ni watu wa kuchagua chakula tunachokula. Huwa ni watu wa kuchagua mavazi, njia
na mambo chungu nzima yanayofanana na hayo. Halikadhalika, na mafanikio
unayoyatafuta nayo ni uchaguzi. Ni lazima uchague kufanikiwa ili ufanikiwe bila
kufanya hivyo, hutafanikiwa.
Kwa
bahati mbaya wengi huwa hatuna uchaguzi na maisha ya kimafanikio tunayoyataka.
Kwa mfano nikuulize wewe, umeshawahi kujiuliza unataka kufanikiwa kwa viwango
vipi? Usitoe macho tu, ulishawahi kujiuliza hivyo? Kama huwa unajiambia nataka
tu kufanikiwa, lakini hujui kwa viwango vipi ni sawa na kama hujafanya uchaguzi
kabisa. Fanya uchaguzi sahihi wa kufanikiwa kwako na ujue unataka kufika wapi
na kwa muda upi?
Mafanikio
ni kuona fursa.
Ili
ufanikiwe ni lazima utumie kila aina ya fursa inayokuja mikononi mwako vizuri.
Lakini hiyo haitoshi, kama huna uwezo wa kuona fursa za kukusaidia kufanikiwa
pia hutaweza kufanikiwa. Ni muhimu sana kuzijua fursa ambazo unatakiwa uzitumie
ili kufanikiwa. Bila kufanya hivyo utahangaika sana kutafuta mafanikio bila
kuambulia kitu.
Watu
wanaopata mafanikio mazuri kwenye maisha yao, siku zote wanatumia fursa. Ni
jambo ambalo kwa sasa unatakiwa kulijua na kulizingatia vizuri sana kichwani
mwako kwamba mafanikio pia huwa yanakuja kwa kuona na kutumia fursa vizuri. Ikiwa utakuwa unaona na kutumia
fursa vizuri kila wakati, uwe na uhakika hakuna wa kukuzuia kufanikiwa.
Soma; Mambo 7 Ya Kujifunza Kutoka Kwa Bilionea Bill Gates.
Soma; Mambo 7 Ya Kujifunza Kutoka Kwa Bilionea Bill Gates.
Mafanikio
ni kutatua matatizo.
Katika
safari ya mafanikio wakati mwingine inakuwa ni safari yenye kila aina ya
vizuizi. Na wakati mwingine kutokana na vizuizi hivi hutufanya tuumie na hata
kulia. Sasa ili uweze kufanikiwa unapaswa kutambua pia mafanikio wakati mwingine
ni ule uwezo wa kutatua matatizo. Kwa kadri unavyotatua matatizo ndivyo ambavyo
unajikuta unazidi kufanikiwa.
Kama
unafikiri natania mafanikio sio kutatua fursa, kuanzia leo anza kutatatua
matatizo yaliyo katika kijiji chako au eneo unaloishi. Kwa kutatua matatizo hayo
utajikuta ukijipatia pesa kwa wingi sana. Hiyo yote inadhihirisha kwamba
mafanikio ni kutatua matatizo. Jifunze juu ya hili na tatua matatizo muhimu
kwenye jamii na hakika utafanikiwa.
Mafanikio
ni kufanya kazi kwa bidii.
Hakuna
ubishi wowote ili uweze kufanikiwa ni lazima ufanye kazi kwa bidii. Kama ulikuwa
huna mtazamo huu mwanzoni unalazimika kuwa nao na kujua kwamba mafanikio ni
kufanya kazi kwa bidii zote. Hakuna lelemama katika kutafuta mafanikio. Unatakiwa
kujituma sana tena sana kila siku ili ufanikiwe. Vinginevyo usipozingatia hili
hutaweza kufanikiwa.
Kwa
kuhitimisha makala hii, nifupishe kwa kusema mafanikio ni hatua, mafanikio ni
kujitoa, mafanikio ni uchaguzi, mafanikio ni fursa, mafanikio ni kutatua
matatizo ya jamii na mafanikio pia ni kufanya kazi kwa bidii. Kwa kujua mambo
haya yatakusaidia sana kujiwekea mtazamo tofauti juu ya mafanikio ambao utakupa
msukumo mkubwa wa kuweza kusonga mbele na kufanikiwa.
Ansante
kwa kuwa nami na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,
Email;
dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.