Aug 31, 2016
Kama Unajiambia Na Kufikiri Hivi Kila Wakati, Huwezi Tena Kufanikiwa.
Mara nyingi katika maisha yetu kama tuna kawaida ya kujiambia
maneno au kauli za aina fulani, ni lazima tutajihisi kwa namna ile
tunavyojiambia sisi mwenyewe. Kumbuka kujiambia huku huwa tunafanya kati yetu
binafsi kila siku na kila wakati vichwani mwetu ambapo mazungumzo huwa
yanaendelea huko, ambayo mara nyingi ni siri zetu.
Kama ikatokea tuna kawaida ya kujiambia maneno au kauli za aina
fulani, ni lazima tutajihisi kwa namna tunavyojiambia. Hivyo, wakati mwingine
kujiamini au kutokujiamini kwetu ni matokeo ya yale yanayoenda vichwani mwetu,
yaani tunajiambia nini kuhusu sisi wenyewe. Kwa kujiambia kwa namna fulani,
hisia, hali na mazingira yetu yatakuwa hivyohivyo.
Naomba nikufundishe jambo moja ambalo ni muhimu sana kwako
kulijua. Kama kweli unataka kujiamini, ni lazima uanze kujichunguza namna au
jinsi unavojiambia wewe mwenyewe. Kujichunguza huku maana yake ni kutambua,
kufahamu na kujua kwamba, huwa kuna mazungumzo ambayo unayaendesha kichwani
mwako kuhusu wewe mwenyewe.
Kumbuka kwamba, kile ambacho huwa tunajiambia, yaani yale
mazungumzo tunayoyafanya vichwani mwetu, ambapo mara nyingi ni kujilaumu,
kujishusha, kujikatisha tamaa na mengine ya aina hiyo, yanakuwa yana nguvu sana
kwetu. Kwa nini? Ni kwa sababu, tunapojiambia mambo hayo inakuwa sawa kabisa na
tunavyowaambia watu wengine.
Kasi ya kuzungumza, lafudhi na hata sauti tunayoitengeneza huko
kichwani, havina tofauti sana na wakati tunapokuwa tunamwambia mtu mwingine kwa
sauti tu ya kawaida ya mdomo. Ndiyo maana yanakuwa yana nguvu ya kutuathiri.
Inakuwa ni kama kweli kabisa, ingawa ni ukweli kwamba hayo yote tunakuwa
tumeyazungumzia vichwani mwetu.
Hivyo, tunapojiambia huko kichwani, ‘mimi ni bwege tu siwezi kufanikiwa’ au ‘mtu mbaya kama mimi nani atanipenda!’ ama ‘nitakufa
maskini tu, si nimetoka familia maskini hata hivyo’, ni wazi hayo
yatakufanya ujitoe thamani na kutokujiamini. Yanakuwa ni maneno ya kukuumiza
wewe ni sawa kabisa na kama vile unaambiwa na watu wengine.
Mbaya zaidi pia ni kwa sababu ni sisi wenyewe, tunaojiambia mara
nyingi tena na tena na athari zinakuwa kubwa zaidi kwetu kutokana na msisitizo
tunaouweka bila hata kujua. Kama nilivyosema awali, unapaswa kujua kwamba
unafikiri. Ukishajua, itakuwa rahisi sana kwako kujiuliza kama yale unayojiambia
kuhusu wewe mwenyewe ndiyo unayotaka au hapana.
Kama siyo unayotaka, kwa kadri unavyojiambia ndiyo utakavyokuwa
unazidi kupata hisia usizozitaka. Kama ukianza kutambua kwamba huwa unafikiri,
itakuwa ni rahisi sana kwako kuweza kubaini kuwa, huwa unajiambia nini juu yako
mwenyewe ambacho kinaweza kukusaidia au kukuumiza na kuharibu maisha yako
kabisa.
Kama unataka kujiondoa na janga la kujitia katika kutokujiamini,
inabidi uchukue kalamu na karatasi, ujaribu kuandika kile usichokipenda ambacho
huwa unajiambia kuhusu wewe, mara kwa mara au kile unachojiambia katika mazingira
fulani. Kwa kujua kile unachojiambiwa mara kwa mara ambacho hukipendi,
itakusaidia kuwa makini nacho na pengine kukiepuka kabisa katika fikra
zako.
Kwa mfano, huwa inatokea ukajiambia, ‘achia hapo usije ukaadhirika
wewe’, au labda ‘usifanye tena si umeona ulivyoshindwa safari ile ‘, ama ‘ni
kawaida yangu kukosea nimezoea’ ama ‘siwezi kumudu kwa sababu ni bwege basi’.
Kumbuka kwamba, maneno hayo ni mabaya na kamwe hayawezi kukusaidia
kujiamini na kupata unachokihitaji. Ni maneno yenye nguvu sana ya kuweza
kuingiza hisia usizozitaka ndani kabisa ya mfumo wako wa kufikiri. Kumbuka,
siyo wakati huu, bali hata wakati mwingine, ukikutana na mazingira
yanayokufanya ujiambie hivyo, utajihisi hovyo hivyohivyo.
Kwa kuyaandika na kuyaelewa na kuelewa ni wakati gani na kwenye
mazingira gani huwa unajiambia maneno hayo, inaweza kuwa rahisi kwako kuanza
polepole kudhibiti mazungumzo hayo hayaendayo kichwani mwako. Ukifanya hivyo,
polepole, utaanza kujiamini.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.