Aug 31, 2017
Nguvu Ya Nidhamu Binafsi Katika Kufikia Malengo Yako.
Ili kufikia
mafanikio yako, kati ya kitu ambacho kinahitajika sana ni uwezo wa kujenga
nidhamu binafsi ambayo inaweza kukuongoza hadi kuweza kufikia malengo yako. Wapo
watu ambao wanakwama sana kutokana na kukosa nidhamu binafsi ambayo inatakiwa
iwaongeze katika kufikia malengo yao.
Hivyo
hapa unaona, nidhamu binafsi siku zote inasimama kama daraja la kuunganisha
pale ulipo na kule unakotaka kufika kutokana na malengo uliyojiwekea. Hiyo
ikiwa na maana kwamba, kama huna nidhamu binafsi huwezi kufikia malengo hayo,
maana utakuwa ni kama mtu ambaye anayebomoa daraja lako mwenyewe.
Kila
unapojiwekea malengo yako ya aina fulani na kisha ukaamua kuweka nidhamu
binafsi ya kuyafanyia kazi malengo hayo kila siku hata kama kwa kidogo sana,
uwe na uhakika ni lazima utafanikiwa. Kitachokufanikisha hapo ni nidhamu
binafsi uliyonayo, hasa ya kuweka juhudi kila siku ambapo umeamua kuiweka.
Unapojiwekea
nidhamu binafsi ya kitu chochote na kudhamiria kwamba hutafanya kitu hiki au
kitu kile mpaka malengo yako ya aina fulani yatimie, utakuwa upo kwenye
uwezekano mkubwa sana wa kutimiza malengo yako. Ila unapokuwa unakosa nidhamu
binafsi ni rahisi sana kuweza kushindwa.
Kuanzia
leo amua kuweka nidhamu kwenye kila eneo. Weka nidhamu kwenye eneo la pesa,
hakikisha pesa zako hazipotei hovyo. Weka nidhamu binafsi kwenye kazi yako. Weka
nidhamu kwenye matumizi ya muda wako, ili uutumie kwa faida. Kila eneo muhimu
liwekee nidhamu binafsi na utapata matokeo mazuri.
Hata
hivyo ukumbuke unapojiwekea nidhamu binafsi sio adhabu au unajitesa. Huwezi kufanikiwa
kama unaishi maisha kama unavyotaka wewe. Ipo misingi ambayo unatakiwa uifate ili
kufanikiwa ikiwa na pamoja na swala la kujiwekea nidhamu binafsi. Kufanikiwa kwako
kutakuwa lazima kama utafata nidhamu hii.
Ndio
maana usishangae kuona watu wengi wanashindwa katika maisha, hii sio kwa sababu
hawana uwezo au vipaji, yote hiyo ni kwa sababu ya kukosa nidhamu ndogo ndogo
ambazo zingeweza kuwaongza katika kufikia mafanikio yao. Ukijiwekea nidhamu
binafsi, tambua utafanikiwa tu, hakuna ubishi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 30, 2017
Hapa Ndipo Mafanikio Yako Makubwa Yanapoanzia.
Ni rahisi
kuwaza na kutafuta sana pale mafanikio yako makubwa yanapoanzia. Hata hivyo
pamoja na kuwaza huko kote bado wengi wanazunguka, hawajui sana mafanikio yao
makubwa yanaanzia wapi?
Leo kupitia
makala haya, nataka nikuonyeshe chanzo cha mafanikio yako makubwa yanaanzia wapi.
Ni ngumu sana kuweza kufanikiwa na kufika ngazi kubwa ya kimafanikio kama
huelewi vizuri mafanikio yako makubwa yanaanzia wapi.
Kwa kawaida,
mafanikio yako makubwa yanaanzia kwenye ile imani uliyonayo juu ya mafanikio
hayo makubwa unayoyataka. Hutaweza kufanikiwa sana zaidi ya ile imani
uliyonayo. Imani yako ndio kila kitu na dawa ya mafanikio yako makubwa.
Jenga imani sahihi ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. |
Unapokuwa
unaamini kwamba unaweza kufikia mafanikio yako fulani, unajikuta kutokana na
imani hiyo unaanza kuchukua hatua za kukufikisha kwenye kile unachokiona kwenye
akili yako. Imani yako inakuwa inakusukuma kufanya zaidi na zaidi hadi kufanikiwa.
Hapa
imani yako naweza nikasema inasimaama kama taa ya kuweza kukuongoza wapi uweze
kufika kimafanikio. Hiyo ikiwa na maana kama ukiwa na imani hafifu, imani
ambayo siyo kubwa huwezi pia kufanikiwa sana.
Kumbuka
ninachotaka hapa unielewe, nazungumzia imani yako kama dawa pekee ya kukufikisha
kwenye mafanikio yako. Na unielewe pia hapa sizungumziii tumaini, nazungumzia
imani yako.
Ipo tofauti
kubwa sana kwa mtu anayeishi kwa matumaini na mtu anayeishi kwa imani. Yule mtu
anayeishi kwa matumaini anaweza asichukue hatua yoyote lakini akajipa matumaini
atafanikiwa kitu ambacho sio kweli.
Ili kufikia
mafanikio uyatakayo, unatakiwa kuwa na imani sahihi ya mafanikio yako. Imani hii
tunaweza tukasema ni imani ya kumudu, imani ya kuamini kwamba unaweza kufanya
kitu fulani na kweli ukachukua hatua hata kuweza kufanikiwa kwenye kitu hicho
kwa uhakika.
Unapokuwa
na imani, unakua unaona mambo kwa utofauti, unakuwa unachukua hatua zako kwa
utofauti na inakuwa sio rahisi kwa mtu mwenye imani inayooendana na kuchukua
hatua kuweza kukata tamaa mapema. Wanaokata tamaa mapema ni wale wanaoishi kwa
matumaini sana.
Kipi
unachotakiwa kukifanya leo ili kujenga mafanikio yako, ni kwa wewe kujenga
imani ya mafanikio. Amini kwamba unaweza kuchukua hatua sahihi, usijaribu kuishi
kwenye matumani utakuwa unajitengenezea mazingira ya kushindwa.
Hakuna
mafanikio makubwa yanayoanzia nje ya imani uliyonayo. Utafika tu pale kwenye
mafanikio yako kutokana na imani inayokuongoza ndani mwako na sio vinginevyo.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Kila la kheri katika
kufikia mafanikio makubwa,
Ni wako rafiki
katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 29, 2017
Kama Unataka Kufikia Malengo Yako Kwa Uhakika, Fanya Mambo Haya.
Tambua kile unachokitaka,
hapa inabidi uelewe nini unachokitaka. Kama unataka kuongozeza uhuru wa kifedha
hilo pia unatakiwa kulijua. Unatakiwa kukijua kile unachokitaka kwa uwazi sana.
Andika malengo yako chini,
malengo yasiyondikwa ni kama moshi wa sigara wakati wowote ni rahisi kupotea.
Malengo ambayo yameandikwa yanakuwa ya muhimu kwenye akili na utendaji unakuwa
rahisi pia.
Weka tarehe ya mwisho kufikia malengo
yako, kama ni malengo makubwa weka tarehe ndogo ndogo za
kukamilisha malengo yako. Unapoweka tarehe hiyo akili yako inakuwa inafanya
kazi kwa nguvu sana kuhakikisha malengo yanatimia.
Andika orodha ya mambo yatakayokusaidia
kutimiza malengo yako, hapa andika watu, maarifa unayohitaji na
hata vizuizi ambavyo vinaweza kujitokeza na jinsi ya kuviepuka ili ufanikiwe.
Weka orodha ya vipaumbele vyako,
vipaumbele vinakusaidia kujua kipi cha muhimu na kipi ambacho sio cha muhimu
katika kutimiza ndoto zako. Hutaleta mchezo ukishawea vipaumbele vya malengo
yako.
Chukua hatua haraka sana,
usichelewe katika kuchukua hatua, kuahirisha mambo ni adui mkubwa sana wa ndoto
zako na unapoahirisha mambo kila wakati ni sawa na kujiibiwa mwenyewe kwenye
maisha yako.
Fanya kila siku kitu cha kukusogeza
kwenye malengo yako, hii ni hatua muhimu sana ambayo
inakuhakikishia mafanikio yako. Fanya kitu fulani katika siku saba za wiki,
fanya kitu kwa mwaka mzima, utafanikiwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 28, 2017
Utaendelea Kubaki Na Maisha Haya Mpaka Lini?
Kati
ya kitu ambacho unatakiwa ujiulize sana ni hali ya maisha yako uliyonayo sasa.
Je, maisha uliyonayo unayopenda au unaishi tu ilimradi siku ziende? Kama maisha
uliyonayo kwa sasa huyapendi, swali lingine la msingi, jiulize utaendelea kuwa
na maisha hayo mpaka lini?
Je,
kuna hatua ambazo unachukua? Je, kuna mikakati ambayo unaiweka ambayo
inaonyesha kweli umechoshwa na maisha hayo? Kuendelea kusema tu peke yake bila
kuchukua hatua yoyote ya msingi huko nikujichosha wewe menyewe. Unatakiwa uamue
mwisho wa ugumu wa maisha yako ni lini?
Hutaki
kuamua, basi kaa kimya usiendelee kulalamika au kupiga kelele zisizo za msingi,
tayari jibu ambalo tunakuwa nalo kichwani ni kwamba hayo maisha unayoyaishi
kuna namna unavyoyapenda, ndio maana hutaki kuchukua hatua sahihi zitakazoweza
kukusadia na kukutoa hapo ulipo.
Usitegemee kutakuwa na urahisi katika kutoka
hapo ulipo. Mabadiliko yoyote yahitaji nguvu tena nguvu kubwa ili kuweza
kubadilisha maisha yako na yakawa na tija. Lakini kama unataka kubadilisha
maisha yako halafu ukaendelea kufanya mambo yale yale, hakuna utakachoweza
kukibadili.
Kubali
kujikana kwa muda kubadilisha kila kitu kwenye maisha yako. Kubali kubadilisha
muda wa kufanya kazi, kubali kubadilisha marafiki na hata aina ya maisha
unayoyaishi, kinyume cha hapo utaendelea kubaki na maisha hayohayo na ugumu
uleule karibu kila siku.
Kila
kitu kinawezekana na pia unaweza kubadilisha maisha yako ukiamua kuweka juhudi
za lazima. Nini kinachoshindakana kwako? hutakiwi kuwa na maisha magumu wakati
wote. Ni wakati wa kubadilisha maisha yako na kuyafanya kuwa bora, hilo
litafanikiwa kwa kuchukua hatua na sio kwa kuishia kusoma makala haya tu.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 27, 2017
Sababu Mbili Zinazofanya Wengi Washindwe Katika Maisha.
Najua
unaelewa vizuri kwenye maisha kundi kubwa la watu wanaonekana wameshindwa
maisha au wameshindwa kufanikiwa kwa viwango vya juu ukilinganisha na kundi
dogo la watu ambalo ndilo limefanikiwa.
Kutokana
na matokeo hayo ya kundi kubwa la watu kushindwa katika maisha, kundi hili kihalisia, hujikuta likianza kumwaga sumu sana kwa wengine wanaotaka kwenda juu. Sumu hizi
zinaweza zikawa za maneno na kila namna ya kukatisha tamaa.
Kwa hiyo
inapotokea unapingwa sana kwa kile unachokifanya, hutakiwi kushangaa wala kuhoji
sana, ni kwa sababu unaishi na upo na jamii ambayo imeshindwa sana, sasa kitu
cha kujiuliza unafikiri watu hao watakwambia nini zaidi ya kukukatisha tamaa?
Ukiwa na sababu katika mafanikio, utashindwa tu. |
Ni ngumu
sana kuweza kukwepa kupingwa, kubezwa, na hata kudharauliwa kwamba huwezi kitu
ikiwa unaishi kwenye jamii kubwa inayokuzunguka ambayo mafanikio kwao ni
msamiati au ni kitu ambacho hakiwezekani.
Kitu
kingine ambacho ninatakiwa nikiulize wewe rafiki yangu, hivi umeshawahi
kujiuliza nini hasa chanzo au sababu inayopelekea kuona watu wengi wakiendelea
kubaki katika hali duni kwa muda mrefu sana? umeshawahi kujiuliza kwa nini hiyo iko
hivyo?
Kama
hujawahi kujiuliza kwa nini hiyo iko hivyo, leo nataka nikushirikishe sababu au
mambo mawili tu ambayo yanawafanya wengi washindwe sana kwenye maisha. Hata kama
wewe unafanya mambo hayo na utaendelea kuyafanya, hutakwepa kushindwa.
Jambo la kwanza, ni kuishi kwa kutoa
sababu sana/visingizio.
Wapo
watu ambao naweza nikasema maisha yao yote wameamua kuwa ni watu wakutoa
visingizio. Watu hawa ni wagumu sana kuchukua hatua ila wakiulizwa kwa nini
hawajafanya, wanasababu nzuri sana za kujitetea kwa nini hawajafanya hicho kinachotakiwa kufanyika.
Siku
hadi siku zinasonga, lakini utawakuta watu hawa wako pale pale, watakwambia
hawajawekeza kwa sababu wanasomesha, pia watakwambia hawajawekeza bado
wanajipanga na sababu nyingine kama hizo.
Kwa kawaida
ili kufanikiwa kila sababu unatakiwa uiweke pembeni, unatakiwa ubaki wewe kama
wewe. Kuendelea kuwa na sababu ni kitu ambacho kamwe hakitakuja kukusaidia
katika maisha yako zaidi kitakuangusha. Weka sababu pembeni,utimize ndoto zako.
Jambo la pili, kukosa nidhamu.
Mbali
na kuishi kwa kutoa visingizio sana, wapo watu ambao wanashindwa kwenye maisha
kwa sababu ya kukosa nidhamu. Watu hawa ukichunguza maisha yao karibu yote,
hawana nidhamu ya kila kitu.
Utakuta
wa ndio wanaongoza kwa kukosa nidhamu ya pesa, wao ndio wanaoongoza kwa kukosa
nidhamu ya muda na pia wanaongoza kukosa nidhamu ya kazi. Sasa watu wa namna
hii inakuwa ni ngumu au muujiza kwao kufanikiwa.
Kwa
kuhitimisha tunaona, mambo makubwa yanayowaangusha wengi kufikia mafanikio ni
kukosa nidhamu na kutoa visigizo sana. Ni jukumu lako yashughulikie mambo hayo
ili na wewe yasije yakakuangusha kwenye maisha yako.
Nikutakie
mafanikio mema na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza
maisha na mafanikio kila siku.
DAIMATUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 26, 2017
Kama Utafanya Mambo Haya, Utakumbukwa Wakati Wote Duniani.
Yupo
mtu mmoja ambaye katika wakati wake aliwahi kusema ‘haijalishi utaishi maisha ya kifahari na kitajiri kiasi gani, ila
utakumbukwa tu kwa jinsi ulivyogusa maisha ya watu na wala sio pesa zako’. Ukiangalia kauli hiyo, huo ndio ukweli.
Katika
maisha tunayoishi ni kweli vipo vitu ambavyo ukivifanya, ni rahisi kuacha alama
ambazo alama hizo zitakumbukwa na vizazi karibu vyote hata ukiwa umekufa. Ni
alama hizi hizi ambazo ingetakiwa kila mtu aziache.
Kitu
cha kujiuliza je, unaweza ukaacha alama za kukumbukwa na watu duniani, au siku
ukifa basi ndio historia imeishia hapo? Majibu unayo wewe, lakini najua kuna
watu ambao unawajua historia zao ni kubwa sana mpaka leo, ingawa wamekufa siku
nyingi.
Fanya mambo yatakayakufanya ukumbukwe wakati wote. |
Labda
nikuulize unafikiri walifanya nini watu hao? au unafikiri wanakumbukwa kwa
bahati mbaya. Kiuhalisia, yapo mambo ambayo walifanya ndio yanasababisha. Kwa
kufanya mambo hayo, hata wewe ukiwa nayo, ni lazima utaacha alama duniani.
Kupitia
makala haya ya leo, nataka tuangalie mambo ya msingi ambayo ukiyaendeleza kwa
usahihi na ukawa nayo basi elewa kabisa siku ukija kuiacha dunia hii
utakumbukwa kwa muda mrefu na hautayeyuka kama moshi.
Jambo
la kwanza, mchango ulionao.
Hauwezi
kukumbukwa au ukaacha alama duniani kama huna mchango mkubwa kwa jamii unayoishi.
Je, maisha yako unayoishi sasa yana mchango kwa wengine? Maisha yako yanaleta
unafuu kwa wengine? Je, unaishi kwa kusaidia wengine?
Unatakiwa
ukae na kujiuliza maswali mengi na kuangalia kila eneo je, una msaada kwa
wanaokuzunguka? Kugusa maisha ya wengine hata kama hauna pesa unaweza kufanya
hilo. Ukiweza kugusa maisha ya wengine, utaweza kukumbukwa sana duniani.
Kama
unafikiri natania, waangalie watu wote ambao wameacha historia kubwa duniani,
waligusa maisha ya watu, ukiangalia kuanzia wapigania uhuru waligusa maisha ya
watu wengi ndio maana nwanakumbukwa mpaka leo.
Lakini
leo hii ukiwa unataka kuishi kwa ubinafsi, ukabaki wewe kama wewe, nikwambie tu
siku ukitoka kwenye hii dunia ndio kwa heri, hauna alama au kumbukumbu ambayo
utakuwa umeiacha ya maana, utakufa wewe kama wewe.
Jambo
la pili, mahusiano.
Mbali
na mchango ulionao je, mahusiano na watu wako wa karibu yakoje? Je, una
mahusiano ya kubomoa au ya kujenga. Unapokuwa na mahusiano bora, elewa kabisa
unajenga msingi mmojawapo wa kuacha alama duniani.
Faida
ya kuwa na mahusiano bora inakusaidia wewe kuwa kiongozi bora wa maisha yako na
wengine pia. Hata kama hujachaguliwa kwa kura lakini jinsi unavyowaongoza watu
hiyo inatafsiriwa moja kwa moja wewe ni kiongozi kwa maisha ya watu.
Unataka
kujenga jina na unataka kuacha alama za uhakika duniani, anza kujenga
mahusiano bora na watu wengine. Jenga
mahusiano na watoto, jenga mahusiano na watu wazima, jenga mahusia na kila mtu,
utafanikiwa.
Jambo
la tatu, tabia.
Mbali
na mchango ulionao kwa wengine jambo lingine ambalo linaweza likakupelekea
ukaacha alama katika maisha yako ni tabia. Hapa kitu cha kuangalia tabia ulizonazo
ni zipi, je zinawafurahisha wengine au kila mtu anakereka na tabia zako?
Haiwezekani
ukawa na tabia mbaya na za hovyo halafu wakati huohuo ukawa ni mtu ambaye
unategemea ukaacha kumbukumbu kwa wengine. Unapokuwa na tabia njema kama za kusaidia
wengine ni wazi utakumbukwa.
Wengi
ambao tabia zao ni mbaya sana, huishia kukumbukwa kwa muda tu lakini baada ya
hapo husahaulika sana. Hivyo, unaona pia tabia ni moja ya kitu ambacho kinaweza
kikamfanya mtu akaacha alama duniani.
Kwa kuhitimisha,
ukiangalia kwa kina hayo ndiyo mambo ya msingi yanayopelekea moja kwa moja kwa
yeyote kuweza kuacha alama duniani ikiwa atayafanya. Ni jukumu letu sote kuweza
kufanyia kazi mambo haya ili tuwe na maisha ya msaada kwa wengine.
Nakutakia
mafanikio mema na endelea kutembelea DIRA
YA MAFANIKIO kujifunza kila siku maisha na mafanikio.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 25, 2017
Maumivu Haya…Yasiwe Sababu Ya Wewe Kushindwa Kabisa Kwenye Maisha Yako.
Kwenye
maisha kuna wakati unaweza ukawa na maumivu ya kushindwa, kuna wakati unaweza
ukawa una maumivu ya kupata hasara, kuna wakati unaweza ukawa una maumivu ya
kuachwa na mwenzi wako au hata maumivu ya kuumizwa na chochote.
Maumivu
kama haya yapo sana katika maisha yako
na yanapotokea maumivu ya namna hii ni rahisi kukuchanganya na kujiona kama vile
umepoteza kila kitu kwenye maisha yako na pia hata ukaona maisha hayana maana.
Kosa
kubwa ambalo hutakiwi kulifanya unapopatwa na maumivu haya ni kwa wewe
kusimamisha shughuli zingine zikasimama huku ukiwa umekaa ukisikilizia maumivu
hayo ambayo umekuwa umeumizwa.
Maumivu yako yasizuie ndoto zako. |
Kitu
unachotikiwa kuelewa maisha hayasimami, maisha yanaendelea kusonga mbele bila
kujali umeumizwa au hujaamizwa. Inapotokea umeumizwa na kitu, acha kusimama au
kuomba ‘poo’ endelea kupambana kwa
nguvu zote.
Ikiwa
itatokea ukakaa chini na kusubiria maumivu yapoe utakuwa ni mtu unayejichelewesha
mwenyewe. Najua ni kweli maumivu ya kuachwa au kupata hasara fulani kubwa
yanauma tena sana, lakini yasikufanye ukasimamisha shughuli zako.
Endelea
na shughuli zako hata kama huku unalia kwa kuugulia hayo maumivu lakini usonge
mbele. Ni bora ukawa unasonga mbele kidogo kidogo kuliko kusimama kabisa na
kusikilizia maumivu yako.
Ni kitu
kibaya sana kuamua kutulia kwa sababu ya maumivu yako. Inapotokea umeumizwa na
jambo fulani chukulia jambo hilo kama somo lakini kubali kung’ang’ania
kuendelea kumbana na hadi ufikie mafanikio yako.
Hapo
ulipo kaa chini angalia ni kipi kinachokuumiza, ni kipi ambacho kimekufanya
ukose tumaini kabisa, usichukulie kuumizwa huko wewe ndio basi huna kitu na
huwezi tena kufanikiwa, hapana haiko hivyo.
Unayo
fursa ya kufanya tena hicho kilichokuumiza na ukakifanya kwa mafanikio makubwa
kuliko ya hapo ulipo. Nafasi ya pili ya kurekebisha makosa yako unayo na ukaendelea
mbele zaidi.
Lakini
hiyo haitoshi hata nafasi ya tatu, nne na tano ya kujirekebisha unayo. Kwa nini
ujute na kuamua kukaa chini kabisa. Hebu shika mkono wangu na nyanyuka hapo
ulipo na ukafanye kile unachotakiwa kukifanya cha kukupa mafanikio.
Kama
nilivyosema maumivu yasiwe sababu ya wewe kushindwa kabisa. Chukulia maumivu
hayo kama changamoto. Na kisha amua kwa dhati kutekeleza ndoto zako bila kujali
ni nini au kitu gani kinatokea ndani mwako.
Kila
la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kutembelea
dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza maisha na mafanikio kila siku.
Ni wako
rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Aug 24, 2017
Misingi Mingine Ya Kuzingatia Wakati Unataka Kumjengea Mtoto Wako Nidhamu Ya Kweli.
Kumlea
mtoto katika nidhamu na maadili ni mojawapo ya jukumu kubwa sana kwa mzazi. Kila
mzazi anapenda kumwona mtoto wake akikua katika maadili mema yatakayomsaidia
katika maisha yake yote ya kesho.
Kutokana
na kiu hii ya kila mzazi kutaka kuona mtoto wake akikua katika maadili bora,
hapo sasa ndio kila mzazi huamua kutafuta njia au misingi bora ya kufuata
katika kumlea mtoto hadi kuleta mafanikio.
Najua
zipo njia nyingi au misingi bora ya kumlea mtoto hadi kuwa katika maadili bora.
Lakini leo nataka tuangalie misingi mingine ambayo unaweza kuifuta na kumlea mtoto
na kumjengea maadili bora kabisa.
Tunajifunza
misingi hii bora kwa sababu, usipojua njia bora mapema ya kumlea mwanao unaweza
kujikuta umekuwa kama polisi kwa mtoto wako na kupelekea mtoto hata kukukimbia bila
sababu na kuona nyumbani pa chungu.
Bila
ya kupoteza muda, hebu tuangazie dondoo kadhaa za kutusaidia mimi na wewe
kuweza kujenga msingi imara katika malezi ya watoto wetu.
Mlee mtoto wako katika njia njema impasayo. |
1.
Usimwekee mtoto sheria nyingi sana.
Itakuwa
ni kosa kwa mzazi kumwekea mtoto wako sheria nyingi sana kwa kufikiri kwamba
ndio unamjengea malezi bora. Kwa jinsi unavyomwekea sheria nyingi unamjengea
mtoto hofu na kujiona yupo kama jela kumbe yupo nyumbani.
Kama
ni sheria weka ila zisiwe nyingi. Hata hivyo unapoweka sheria hizo ambazo
unazitaka, mweleweshe mtoto vizuri aelewe ni nini anachotakiwa kufanya ili ajue
kabisa akivunja kuna adhabu fulani itafuata baada ya hapo.
2.
Toa zawadi na acha kuadhibu sana.
Najua
ukiwa kama mzazi kuna tabia ambazo unataka mtoto wako awe nazo. Tabia zile
ambazo unataka mtoto wako awe nazo jifunze kumpa hamasa kwa kumwahidi zawadi fulani
ili aziendeleze na ziwe tabia za kudumu.
Kwa
mfano, kama hutaki mtoto wako atembee tembee hovyo na umeamua iwe hivyo,
ikitokea akienda badala ya kumpa adhabu, anza kumwambia kwamba usipoenda labda
kutembea na kukaa hapa na kusoma nitakununulia hiki au kile, hiyo itamsaidia
pia.
3.
Kuwa mzazi kiongozi.
Mwongoze
mtoto wako katika kumwelekeza kujisomea, mwongoze katika mambo mbalimbali kama
michezo na mengineyo, kwa jinsi utakavyokuwa ukimwongoza katika mambo hayo,
mtoto wako ataelewa vizuri unataka nini na kufuata.
Ukiwa
mzazi kiongozi, hata ule msingi imara unaoutaka wa tabia, utajikuta zinajengeka
taratibu na hatimaye kuwa tabia zake za kudumu. Hakuna kinachoshindikana katika
malezi ila kikubwa tumia njia sahihi na sio za kumuumiza mtoto.
Nikutakie
ushindi katika malezi bora ya mtoto wako na endelea kutembelea
dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila siku juu ya maisha na mafanikio.
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 23, 2017
Matajiri Wote Duniani Wanaanza Na Kitu Hiki, Hadi Kufanikiwa Sana.
Kipo
kitu kimoja ambacho kila aliyefanikiwa anaanza nacho hadi kufikia ngazi kubwa
ya kimafanikio. Kitu hicho hata wewe unaweza ukawa nacho na ukikizingatia ni
lazima utafikia mafanikio makubwa na kutakuwa hakuna cha kukuzuia.
Kitu
hichi ndicho ambacho matajiri karibu wote duniani huwa wanaanza nacho na ndicho
kinapelekea wao kuweza kufanikiwa na kufika pale walipo leo. Hakuna mwenye
mafanikio makubwa sana ambaye hajaanza na kitu hicho.
Naona
umetega sikio lako kisawasawa kutaka kujua kitu hicho ni kitu gani ambacho nataka
kukiongelea hapa. Nakuomba usitie shaka, kitu ambacho nataka kukiongelea hapa ni
kuanzia pale ulipo na kile kidogo
ulicho.
Usishangae
sana, kama nilivyosema karibu matajiri wote waliopo duniani safari yao ilianza
na kidogo walichonacho au hawana kitu kabisa tena wengine wakitokea kwenye umaskini
na wingi wa madeni uliwaofunika.
Anzia pale ulipo hadi kufikia kilele cha mafanikio. |
Ukiangalilia
matajiri kama Bill Gates, Warren Baffet, Larry Ellison, Michael Dell na Paul
Allen wote hawa walianzia chini wakiwa na pesa kidogo, wakati mwingine hata
ilikuwa ikiwalazimu kuishi katika madeni.
Matajiri
hawa na wengineo, walipohojiwa nini siri ya mafanikio yao, wakati watu
walioanza nao pamoja wamewaacha pale pale, ni wazi walidai sio kwa sababu ya
akili au vipaji bali ni kujenga nidhamu binafsi na kuamua kufanya kazi kwa
juhudi kubwa kuliko mtu yoyote na tena kwa muda mrefu.
Kwa hiyo
unaona kwao kuanza chini sio kitu ambacho kinawaogopesha. Kuanza chini
wanachukulia kama changamoto tu ya kawaida ambayo mtu yeyote mwenye nidhamu na
kujituma anaweza akaanzia huko na kufanikiwa sana.
Kwa mantiki
hiyo, hata wewe unao uwezo wa kuanzia hapo ulipo na kufikia mafanikio makubwa
sana. Kitu gani unachokiogopa hadi ushindwe kuanzia chini? Unaogopa kuchekwa au
nini unachoogopa?
Tunaona
karibu historia ya watu wote duniani wenye mafanikio walianza chini. Sasa wewe
ambaye hutaki kuanzia chini eti unataka kuanzia juu nani kakwambia hivyo. Kila kitu
kiasili kinaanzia chini na hatimaye kufikia mafanikio makubwa sana tena ya
kutisha.
Ukiangalia
kuanzia mimea, viumbe hai ni vitu ambavyo vinaanzia chini na mwisho wa siku
kufikia mafanikio makubwa. Kwa hiyo, usijione kuna kitu ambacho utakosa sana
kama ukianzia chini, anza na ulichonacho weka nidhamu na juhudi utafanikiwa
sana.
Kuanzia
leo usiwe na shaka na kitu chochote. Anzia maisha yako pale ulipo. Ndio,
naamanisha hapo ulipo. Kila mtu anayeanzia chini anapata muda wa kujifunza na
kukua, hatimaye kujenga mizizi mikubwa ya mafanikio yake.
Usijisikie
vibaya au kujiona hufai kwa sababu unaanzia chini, anza na ulichonacho kutafuta
mafanikio yako, anza na nguvu zako, anza na vipaji ulivyonavyo upo wakati
utafika juu sana kimafanikio hadi utakuwa unajishangaa mwenyewe.
Ila kama
unatafuta maisha ya juu, halafu hutaki kuanzia chini, mafanikio yako yatakuwa magumu
sana kuweza kufikiwa. Ni asili ya
mafanikio kuanzia chini na kukua kidogo kidogo. Hata wanaorithi mali pia huweza
kufanikiwa sana kwa kuziendeleza.
Siri
ya mafanikio makubwa ni kuanza na kidogo na kukikuza hadi kuwa kikubwa. Kwa hiyo
hapo ulipo huna ulichokosa, anza leo kutafuta safari yako ya mafanikio
kiuhakika na ukifanya hivyo utafanikiwa na kuwa huru.
Tunakutakia
kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kutembelea
dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila siku.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 22, 2017
Hivi Ndivyo Utandawazi Na Teknolojia Vinavyofanya Kazi Katika Sayari Hii Ya Wasakatonge.
Ukuajaji wa utandawazi
pamoja na teknolojia kwa namna moja au nyingine umetusaidia kuweza kupima
kiwango cha maendeleo ya dunia na jamii kwa ujumla. Kiwango hicho cha maendeleo
kitokanacho na utandawazi kimekuwa kikipimwa siku hadi siku.
Utandawazi huo huo pamoja
na teknolojia umesadia kuweza kuipambanua dunia ya zamani na dunia ya sasa.
Kutoka na mabadiliko hayo ndipo tunapopata hadithi zama za kale za mawe, na
sasa tupo zama za tekolojia na ukuaji wa utandawazi.
Kiuhalisia ni kwamba
zama hizi za tekinolojia na ukuaji wa utandawazi zina faida lukuki sana hasa
kwa wale wenye kujua namna ambavyo wanaweza kuendana na zama hizi, lakini wengi
wate ambao hatuwezi kuendana na zama hizo, tumekuwa wakipata hasara tu.
Tunaweza tukajikita hata
kwa dakika chache kuwaza, hivi kwa mfano ugunduzi wa simu, kompyuta za kisasa
pamoja na ujio wa mitandao ya kijamii inakusaidia wewe na kwa kiwango gani? Au unaiona
ipo ipo tu.
Tumia teknolojia vizuri ikufanikishe. |
Bila shaka wengi hatujui
ni kwanamna gani vitu hivyo vitavyoweza kutusadia sisi kuweza kufika mbali
kimafanikio, wengi tunachukulia ujio wa teknolojia ni kama kuifurahisha tu
akili zetu.
Wakati mwingine
tunadhani ya kwamba ugunduzi wa mambo mbalimbali katika sayari hii ni kwa ajili
ya watu wachache tu, la hasha kila kitu ni kwa ajili ya watu wote madharani
wewe unayesoma makala haya. Hivyo kila kitu kilichopo zama hizi lazima ukiwazie
kinakupaje wewe fedha.
Kila kitu ambacho
unakiona katika ulimwengu huu wa utandawazi kina faida na hasara zake, ila
wengi wetu tumekuwa tunavitumia vitu hivyo kwa upande wa hasara zaidi huku
tukipumbazwa na kuona hasara hizo ndizo faida.
Kama upo katika katika
upande wa kuona hivyo, tafadhari nakuomba ufanye mapinduzi kwani dunia ya sasa
imebadilika sana, kile ambacho unakijua leo, upo uwezekano kitakuwa hakina thamani siku ya kesho.
Ukuaji wa wa utandawazi
ndio ambao umeleta maana hiyo. Hebu tujiulize kidogo na kuona maajabu ya teknolojia
jinsi ambavyo yanafanya hicho ambacho unakijua leo kinavyokuwa hakina thamani
siku ya kesho.
Hebu tujiulize wale
waliokuwa wanafanya kazi kwa kutumia ‘typwriter’
na leo utandawazi umeleta kompyuta, wale watu waliofanya kazi kwa ‘typwriter’ wanafanyakazi gani? Bila
shaka utagundua ya kwamba watu wa ‘typwritter’
watashindwa kuendana na kasi hii ya teknolojia.
Tuendelee kujihohoji
wale ambao walikuwa wanafanya kazi za uhasibu hapo awali, ambapo kazi hii kila
mtu akipeenda na leo hii karibu kila kampuni watu wanafanya miamala kwa kutumia
simu, hawa wahasibu wanafanyakazi gani? Bila shaka utagundua ya kwamba kazi
nyingi ambazo zilikuwa zinafanywa na watu mbalimbali kwa sasa zinapungua na kufanywa
na mashine.
Zipo kazi nyingi sana
ambazo leo zimerahisishwa sana, badala ya kufanywa na watu , zimekuwa
zikifanywa na mashine, kwa mtindo huu naendelea kuwaza kwa sauti hivi hicho
ambacho unakijua leo kesho kitakuwa na thamani tena? Bila shaka majibu unayo
mwenyewe.
Hivyo kwa kuwa
mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanyika katika sayari hii yanafanya mambo
makubwa kutokufanywa na wewe, unachotakiwa kufanya ni kujiongeza kwani zama
zimebadilika sana.
Hivyo jijengee mifereji
mingi ya kuweza kujua vitu vingi zaidi ya hicho ambacho unakijua sasa, kujua
vitu vingi kutakufanya uweze kujua namna ya kuweza kuishi kesho.
Maisha yanabadilika sana
hivyo ni heri kila wakati kuweza kuwa bora zaidi kwa kile ambacho unachokifanya
acha kung'ang'ana na mambo ya mwaka 47, kwani hayana tena thamani tena mbele ya
sayari hii, na hata kama yatakuwa na thamani kinachohitajika ni kuweza
kujifunza namna ya kukiboresha kitu hicho ili kuendana na kasi ya sayari hii.
Mpaka kufikia hapo sina
la ziada, tukutane siku nyingine.
Ndimi afisa mipango, Benson Chonya,
Aug 21, 2017
Hata Kama Mambo Kwako Ni Magumu…Bado Hujachelewa Kufikia Mafanikio Yako.
Kama
unafikiri umechelewa kufanya kile unachotakiwa kukifanya elewa hivi…
Mpaka
sasa kitabu kizuri bado hakijaandikwa…
Mpaka sasa nyimbo
nzuri kuliko zote duniani bado haijaimbwa,..
Mpaka sasa jengo zuri zaidi duniani bado mpaka dakika hii halijajengwa…
Mpaka sasa chakula
kizuri kuliko vyote bado hakijapikwa…
Mpaka sasa ugunduzi
mkubwa kuliko yote duniani bado haujafanyika unasubiriwa…
Mpaka sasa mashine
safi na ya kisasa bado haijagunduliwa…
Mpaka sasa mfanyabiashara
mkubwa kuliko wote duniani wa karne bado hajatokea…
Mpaka sasa mwandishi
bora wa vitabu kuliko wote na wakati wote bado hajaibuka…
Mpaka sasa mafanikio
yote makubwa yapo yanakusubiri wewe…
Narudia mpaka sasa mafanikio hayo makubwa yapo yanakusubiri wewe…
Huhitaji
kutilia shaka uwezo wako, tumia maarifa yako kutoa yaliyobora…
Hakuna
kinachoshindikana chini ya dunia, ikiwa utaamua…
Ndani
mwako una nafasi ya kutoa mafanikio yoyote ukiamua…
Kipi
kinachokuzuia, mafanikio makubwa wakati wote bado hayajatokea…
Je,
unataka kujiona unakata tamaa na kujiona tena basi…
Usijione
uko hivyo, unayo nafasi ya kubadilisha kila kitu kwenye maisha yako…
Unayo
mbegu ya mafanikio makubwa ndani mwako, itumie…
Wewe
ni bora na unaweza kuibadilisha dunia…
Usikubali
kufa kifo cha mende miguu juu kwa kufikiri huwezi…
Unaweza,
huo uwezo unao, na inawezekana…
Bado
hujachelewa hata kama mambo ni magumu...
Tumia muda wako vizuri...tumia nafasi uliyonayo vizuri...utafanikiwa...
Tunakutakia
kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila
siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 20, 2017
Acha Kuharibu Hatma Ya Maisha Yako Yote, Kwa Sababu Ya Kitu Hiki Tu.
Kwa kawaida
vipo vitu vingi vinavyopelekea maisha ya mtu kuharibika na kuwa ya kushindwa
kabisa. Vitu hivi kuna wanaovijua kwa uwazi na pia kuna ambao hawavijui au
hawana habari kwamba ndio chanzo cha kushindwa kwao.
Kama
nilivyokwambia vipo vitu vinavyopelekea
kushindwa kwa wengine katika maisha. Lakini leo kupitia makala haya, nataka
nikwambie kitu kimoja tu, ambaco kama utakibeba sana,utake usitake utashindwa
na kuharibu maisha yako yote.
Kitu
hicho sio kingine bali ni kukata tamaa mapema. Kama unakata tamaa mapema tambua
kabisa unakua umeamua kuharibu hatma ya maisha yako mwenyewe. Hakuna mtu aliyefanikiwa
mwenye sifa ya kukata tamaa mapema.
Watu
waliofanikiwa ni wabishi, wanakomaa na ndoto zao hadi kuweza kufanikiwa. Lakini
kama una ndoto yako, halafu kutokana na changamoto ukaamua kuachana na ndoto
hiyo, elewa kinachotokea sio tu unajiumiza sasa, bali pia unapoteza kesho yako
sana.
Usikate tamaa mapema. |
Kila
maamuzi unayoyachukua kwenye maisha yako, yanamuathiri mtu mmoja muhimu sana kwenye
maisha, ambaye ndiye wewe. Hata uamuzi wa kukata tamaa na kuacha ndoto zako
zisifike mwisho, pia ni uamuzi ambao ni hatari na unaharibu kesho yako.
Hatma
ya maisha yako ya kesho, inategemea sana maamuzi unayofanya leo. Inapotokea
ukafanya maamuzi ya kukata tamaa kwa kitu unachokifanya, elewa unajitengenezea
mazingira ya kuharibu sana maisha yako kesho.
Hivyo
kutokana na kukata tamaa mapema unajikuta unakuwa ni mtu wa kuanza jambo hili
leo, tena kesho unaanza lingine. Kwa maisha hayo unashangaa unapoteza muda na
pia unapoteza mafanikio yako ya kesho kwa sababu ya kukaa tamaa.
Kama
una wewe ni mtu wa kukata tamaa sana, ukumbuke katika maisha yako hakuna kitufe
cha kubonyeza kurudisha maisha yako yakarudi nyuma, maisha yanavyosonga mbele,
hayarudi nyuma hata kidogo.
Kikubwa
unachotakiwa kujua ni kwamba ili kufanikiwa unatakiwa kukomaa na kuvumilia kila
hali. Hakuna anayepitia mteremko wa maisha, kila mtu anachangamoto zake. Ukifanya
mchezo na ukaendeleza kukata tamaa hutafanikiwa.
Kama
unaona maisha ni magumu, elewa huo ugumu ndio unatakiwa kukomaa nao na
kuushinda. Hata hivyo ukiangalia nani aliyekupa ahadi kwamba maisha ni mepesi?
Changamoto kwenye maisha zipo toka enzi za mababu, kuwa mvumilivu ili
kufanikiwa.
Jaribu
kukaa chini na kujiuliza, kesho yako itakuwaje ikiwa kila kitu unakata tamaa
mapema? Nikwambie kitu rafiki yangu, usikubali hata kidogo kuharibu hatma yote
ya maisha yako kwa sababu ya kukata tamaa, nimesema kuwa mvumilivu utashinda.
Nakutakia
mafanikio mema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku kwa ajili ya kujifunza maisha na
mafanikio.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Aug 19, 2017
Kama Usiposhinda Kwenye Vitu Hivi, Sahau Mafanikio.
Kitu
ambacho natamani kila mtu angalau aelewe, ni kwamba huwezi kupata ushindi mkubwa
kama haujawahi kupata hata ushindi kidogo. Hiyo ikiwa na maana, ili uweze
kushinda makubwa lazima ushinde kwanza madogo.
Unapokuwa
unapata ushindi mdogo, ni rahisi kukupa hamasa, mzuka, nguvu na hata jeuri ya kuendelea
kufanya mambo mengine kwa uhakika ambapo utashangaa mambo hayo yanakupa
mafanikio hata bila kutarajia.
Hali
hii ndio tunayoiita nguvu au majabu ya mafanikio madogo madogo. Kuna nguvu sana
ya kufanikiwa kwa vitu vidogo vidogo na kuweza kukusaidia kufanikiwa. Kile unachokiona
ni kidogo kwako, lakini kina nguvu ya kuweza kukuvusha na kukupa mafanikio.
Ushindi mdogo, ni nguzo ya mafanikio makubwa. |
Unatakiwa
utulie na uelewe ili kuweza kutawala makubwa, kwanza unatakiwa kutawala mambo madogo.
Ili kutawala biashara kubwa unayoitaka, ni lazima na muhimu sana kwanza kutawala
biashara ndogo tena kwa mafanikio.
Mafanikio
makubwa yanakuja kutokana na nguvu ya
kufanikisha mambo madogo madogo. Sasa nguvu hii haiji kwa bahati mbaya bali ni kutokana
na ushindi mdogo unaoupata. Hivyo unaona ili uweze kuwa mshindi kwa chochote
kikubwa, ushindi mdogo ni muhimu sana.
Huhitaji
kujiuliza sana ushindi mdogo utaupata vipi wakati huna hata kitu cha kufanya. Sikiliza,
kuamka asubuhi na mapema yenyewe na kufanya majukumu uliyojiwekea na
ukafanikisha huo ni ushindi. Kusoma kitabu angalau kurasa 20 kwa siku pia huo
ni ushindi.
Au labda
nikueleze hivi haijalishi hapo ulipo una
kazi maalumu au huna, lakini kama unafanya vitu fulani hata kama ni vidogo sana
na ukavifanikisha huo ni ushindi pia ambao unatakiwa kuuzingatia.
Inawezekana
ukawa huoni maendeleo ya ushindi wako kwa sababu hufatilii, lakini hebu leo
anza kufatilia ushindi wako mdogo. Utashangaa unavyofatilia unazidi kupata
nguvu ya kufanya tena na tena.
Mafanikio
wakati mwingine yana kawaida ya kuja kwa ‘rekodi’
zake. Kwamba kutokana na umekuwa ukishinda hili na lile basi upo uwezekano na
hili hata kama linaonekana gumu sana, uwezo wa kulishinda unalo kwa sababu tu
ya ‘rekodi zako’ zinaonyesha hivyo.
Kuelewa
vizuri hapa angalia timu mbili za mpira kabla hazijaanza kucheza, kwanza
zinawekwa kumbukumbu za michezo waliyowahi kucheza na nani ameshinda mara
ngapi na kuna matarajio gani.
Kama
si hivyo hata mchezo wa ngumi uko hivyo hivyo zile ‘rekodi’ za nyuma zinaanza
kuwekwa kwanza kabla mchezo haujachezeka. ‘Rekodi’ hizo zinawekwa kuangalia
nani alikuwa mshindi kwenye mapambano mangapi na upo uwezekano wa nani leo
kushinda.
Mpaka
hapo, sina shaka sasa kwa sehemu unanielewa juu ya umuhimu wa kuweka kumbukumbu
juu ya ushindi wako mdogo anaoupata. Kumbuka, ushindi mdogo unaoupata unaweza kutumika
kama ngazi ya kukupeleka kwenye mafanikio ya juu.
Elewa
unaposhinda kwenye vitu vidogo, unapata nguvu ya kujiamini na kuamini alaa
kumbe inawezekana. Pia unapokosa ushindi mdogo ni ngumu sana kufanikiwa kwani
ndani mwako zinajengeka fikra za kuona kwamba huwezi kufanikiwa kwa kila kitu.
Nikutakie
siku njema, endelea kusheherekea ushindi mdogo unaoupata kwenye maisha yako
kila wakati, lakini elewa ushindi mkubwa unakusubiri na unakuja pia.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)