Aug 18, 2017
KITABU; The Time Management (Matumizi Mazuri Ya Muda).
Katika
kitabu hiki cha THE TIME MANAGEMENT,
mwandishi Brian Tracy anaonyesha
umuhimu wa kuwa na matumizi mazuri ya muda ili kujihakikishia furaha na
mafanikio ya kudumu kwa yale tunayoyafanya.
Mwandishi
anaweka wazi bila ya kujijengea tabia ya kuwa na matumizi mazuri ya muda, basi
maisha yako yatakuwa yanapotea sana pasipo kujua kwa nini iko hivyo. Hivyo
anasihi kutumia muda vizuri kwa manufaa yetu ya leo na kesho.
Yapo
mengi ya kujifunza kutoka kwenye kitabu hiki, lakini hebu tuangazie haya
machache kwa kifupi na tujifunze pamoja.
1. Pamoja
na kwamba kwa siku, juma, mwezi na hata mwaka una mambo mengi kufanya, lakini jifunze kuchagua mambo matatu
ya muhimu ambayo utayafanya kwa siku, wiki, mwezi na hata mwaka mzima. Mambo
hayo matatu ndiyo yawe muhimu na kuyawekea vipaumbele vya hali ya juu sana.
2. Washindi
katika maisha siku zote wanatumia muda wao vizuri, wale wanaoshindwa katika
maisha siku zote wanatumia muda wao hovyo. Ili kuthibitisha hili, angalia watu
wenye mafanikio wanatumia muda wao vipi na washindwaji wanatumia muda wao vipi.
3. Kama
unataka kuwa na matumizi mazuri ya muda ni muhimu kujua matumizi mazuri ya muda
wako yanakwenda wapi na yana maana gani kwako.
Hapa
ina maanisha unakuwa unachagua aina ya maisha ambayo unatakiwa uyaishi
kulingana na matumizi ya muda wao.
Wengine
matumizi mazuri ya muda wao ni kufanya kazi kwa juhudi sana kutwa nzima na
wakati wa usiku ni kulala usingizi mzito.
Wengine
matumizi mazuri ya muda wao yapo kwenye kukaa na familia zao pamoja na
kufurahia maisha.
Wengine
matumizi ya muda wao ni kuongea na watu makini ambao wana msaada mkubwa wa
maisha.
Inabidi
ujue namna ya kuchagua mambo ya kufanya hasa pale unapokuwa na muda ambao
umeupata. Ukishindwa kufanya hivyo utapoteza sana muda wako.
4. Kila
siku ieleweke kwamba yapo majukumu ambayo yanatakiwa kutekelezwa. Linapokuja
swala la majukumu, kuna majukumu makubwa ya aina tatu;-
Majukumu muhimu na ya lazima,
hapa kwa mfano kuongea na wateja, kutekeleza kazi uliyojiwekea kwa siku au
kulipia ‘bill’ inayotakwa kukatwa.
Majukumu muhimu lakini sio ya lazima, katika majukumu haya
inaweza ikawa ni kusoma masomo mapya kwa baadae au kununua nguo.
Kuna mjukumu ambayo siyo ya muhimu na
sio ya lazima, majukumu haya inaweza ikawa kama kuangalia
sinema, kutembea tembea hata kuongea soga zisizo za msingi.
Tatizo
la watu wengi linakuja wanapoteza muda sana kwenye majukumu ambayo siyo ya
muhimu kwao na pia sio ya lazima.
Ili
kufanikiwa unahitajika sana kufanya majukumu ambayo ni ya muhimu kwako na pia
ya lazima kwenye maisha yako.
5.
Kati ya kitu kibaya katika safari ya mafanikio ni kuahirisha mambo.kuahirisha
mambo hiyo ni sawa na kujiibia muda wako wewe mwenyewe au kuahirisha mambo
naweza nikasema hiyo ni sawa kuamua na kupoteza maisha yako mwenyewe.
Tofauti
inayojitokeza kati ya waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa ni kwamba,
waliofanikiwa wanairisha mambo kwenye yale mambo ambayo sio ya msingi, lakini
wasiofanikiwa wanaairisha mambo yale ya msingi sana kwao.
6. Ili
kufanya kazi zako kwa ufanisi, jifunze kugawa muda wako angalau kwa dakika 90
za kufanya kazi kwa uhakika. Ukifanya chini ya hapo unajidanganya na
unajipotezea muda wako wingi bure.
7.
Ili kuokoa muda wako, kama umeamua kufanya kazi fulani, ifanye na kuweka akili
zako zote hapo. Maongezi ya simu au chochote kile kisiingilie kazi ambayo
umeamua kuifanya kwa manufaa. Kama ni simu ongea maneno machache sana na ya
faida.
8. Ili
kuokoa muda wako, tenga muda wa kusoma e-mail zako, hakuna ambaye atakufa kama
akituma e-mail akashindwa kusubiri angalau kwa siku moja. Jiwekee utaratibu wa
kusoma e-mail hata kama ni kila saa kumi jioni. Kama kuna dharura, mtu huyo
apige.
9.
Ili kuokoa muda wako, jiwekee pia utaratibu wa kupokea simu na kuingia kwenye
mitandao ya kijamii. Unaweza ukawa unaingia kila baada ya masaa 4 au zaidi ili
kuokoa muda, hususani mitandao kama whats app, na mitandao mingine ya simu.
10.
Ili kuokoa muda wako, usipokee simu zako hovyo, ‘usi-chat’ kwa meseji hovyo, usiongee kwenye simu muda mrefu sana,
ongea agenda muhimu za kuweza kukusaidia. Matumizi ya hovyo ya simu ni upotevu
wa muda.
11.
Wekeza angalau saa moja kila siku kwa kusoma, ikiwa utawekeza angalau saa moja
kwa kusoma, basi baada ya miaka mitano utakuwa upo juu sana kimafanikio na
utakuwa ni miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa sana kwa wakati wako.
12.
Moja ya matumizi mazuri ya muda ni kulala mapema na kuamka mapema kwa kufanya
mambo yako kwa ufasaha. Unapolala mapema unapata muda wa kupumzisha mwili wako
sana, na hali ambayo inakupelekea uamke ukiwa na hamasa mpya.
Chukua
hatua kufanyia kazi haya muhimu uliyojifunza hapa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.