Nov 2, 2018
Ukilenga Kutafuta Pesa Ya Kula Utapata Lakini…
Kila mmoja anajitahidi kutafuta pesa popote anakojua. Habari njema ni kwamba kila anayetafuta pesa hii ya KULA anapata. Lakini..
pamoja na kuipata, wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ni ndogo
na kwamba inatosha kula tu! Wengi wanatamani kupata pesa nyingi zaidi ya hiyo
wanayoipata kwasasa. Kwaujumla, wengi wanashangaa ni kwanini hawapati pesa ya
kutosha kuweza kufanya mambo makubwa zaidi ya KULA na kulipa ADA za
watoto.
Sababu mojawapo ya kushindwa kupata pesa ya kutosha ni malengo
mahususi tunayojiwekea kabla ya kutafuta pesa. Watu wengi wakiamka asubuhi,
malengo yao makubwa kabisa ni kutafuta pesa ya KULA, ADA na kujenga NYUMBA ya
makazi. Wengine akijikakamua kidogo analenga kununua GARI la kutembelea.
Malengo ya watu yanabainishwa kwenye maongezi yao ya kawaida. Pindi
ukiwasikiliza watu, utasikia wakiambizana kuwa “mimi natafuta pesa ya
kula basi! Wengine utawasikia wakisema “natafuta pesa kwaajili
ya watoto”wengine wamekwenda mbali na kusema kuwa wanatafuta pesa, “ili
watoto wao angalau waweze kwenda choo” Ni wazi kuwa maongezi ya namna
hii, yanakupa jibu la moja kwa moja kuwa watu wengi wana malengo ya kutafuta
kiasi kinachotosha KULA, kulipa KARO na kujenga NYUMBA ya makazi basi! kwamba
zaidi ya hapo ni bahati tu.
Ukweli ni kwamba, pesa ya KULA siku zote huwa ni ndogo japokuwa
inapatikana kila ikitafutwa. Pamoja na kupatikana kila siku, tatizo lake ni
moja; kwamba, ikishapatikana muhusika anakuwa tayari ana njaa na hivyo kuitumia
mara moja. Ikishaisha muhusika uenda kutafuta tena, na huo ndio unakuwa mzunguko
na mtindo mzima wa maisha ya kila siku.
Kujiwekea malengo ya kutafuta pesa ya KULA na ADA siyo jambo
baya! Ubaya unakuja pale utakapofanya suala la kutafuta pesa ya KULA kama lengo
lako kuu. Mara nyingi watu waliofanikiwa wanatushauri kuyaweka malengo ya KULA
na ADA ndani ya malengo makubwa zaidi (Utajiri). Tunahimizwa kuachana na
utamaduni wa kuweka KULA na ADA kama malengo makuu katika maisha, kwasababu,
kwa kufanya hivyo tutazidi kupoteza muda mwingi na matokeo yake hututakaa
tupate muda wa kufanya mambo makubwa.
Kwa mfano: “Ikiwa wewe unaishi DAR-ES-SALAAM
na lengo lako kuu ni kwenda KARAGWE, maana yake, inabidi ujipange kutafuta
jinsi ya kupata pesa itakayokuwezesha kufika KARAGWE. Pesa ya kufika KARAGWE
ikishapatikana, maana yake ni kwamba sehemu zote za njiani kabla ya kufika
mwisho wa safari yako kwa vyovyote vile, utafika sehemu zote za njiani japo
hilo halikuwa lengo lako kuu. Sehemu za njiani ambazo kwa vyovyote vile lazima
upite ni pamoja na Morogoro, Dodoma, singida, Tabora, Kahama n.k. Sehemu zote
hizi utaweza kufika kwa kutumia nauli ile ile ya DAR-ES-SALAAM hadi
KARAGWE”
Mfano huo hapo juu, unatufundisha kwamba tunahitaji kuweka
juhudi na maarifa yetu kwenye vitu vikubwa kama vile miradi ya maendeleo (majumba
ya kupangisha, kilimo biashara, viwanda, biashara kubwa n.k). Tukiwekeza
akiri zetu kwenye mambo kama hayo ni wazi kwamba pesa ya KULA na ADA za watoto
zitapatikana humo humo ndani ya miradi hiyo. Kitu cha msingi hapa ni
kuhakikisha tunajizuia kufanya kazi ya kutafuta pesa ya KULA na ADA kama
malengo yetu makuu. Tusifanye KULA na ADA kuwa mwisho wa safari yetu BALI suala
la pesa ya kula na ADA liwe ni sehemu za njiani kuelekea Kwenye ndoto kubwa
(Utajiri).
Wito wangu kwako msomaji ni wewe kuiambia akili yako na nafsi
yako mwisho wa safari yako, yaani safari ya kuelekea kwenye maisha unayotamani
kuishi. Naamini ukiweza kuiambia ukweli akili na nafsi yako, basi ujue hapo
utakuwa umefikia hatua ya kutafuta pesa nyingi zaidi ya hiyo ya KULA na kulipa
ADA. Ili linawezekana, limewezekana kwangu, limewezekana kwa wengine na hakuna
sababu yoyote ya kutowezekana kwako.
Endelea kukuza uelewa wako juu ya namna ya kupata pesa zaidi ya
ile ya KULA na kulipa ADA za watoto. Fanya hiyo kila mara kwa kutembelea
mtandao wako wa DIRA YA MAFANIKIO.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
shukran
ReplyDeletekwa pamoja tutafika.