Jul 11, 2020
Je, Unahitaji Kufanya Biashara Na Hujui Ni Biashara Ipi Ya Kufanya? Soma Hapa Kujua Ni Biashara Ipi Ya Kuifanya Sasa?
Wapo
watu ambao mara nyingi hujiuliza ni biashara gani wafanye katika maisha yao
ambayo itaweza kuwaingizia pesa nyingi ya kutosha. Ni wazo ambalo hutokea
kutokana na pengine kuona kila biashara wanayoitazama kwa wakati huo kama hailipi. Hali hiyo
husababisha mkanganyiko mkubwa wa mawazo ambao husababisha wabaki njia panda.
Kama
imeshawahi kukutokea hali kama hii kwa namna moja au nyingine makala hi ni
muhimu sana kwako kuisoma. Kwa kusoma makala hii inakuonyesha kwa uwazi orodha
za biashara ambazo unatakiwa uzifanye ukiwa katika mazingira uliyopo. Karibu
kila biashara ipo hapo, kazi ni kwako kuchagua mojawapo unayoipenda na
kuifanya, acha kulalamika tena kuwa huelewi nini cha kufanya.
Twende
kwa pamoja kuzijua biashara hizo ambazo unauwezo wa kuzifanya na kukufikisha
kwenye mafanikio makubwa:-
1. Kutengeneza na kuuza chaki.
Hii
ni moja ya biashara nzuri unayoweza kuifanya na soko lake liko juu. Unaweza
ukanunua mashine yako za kutengeneza chaki na kisha ukaanza kuzisambaza kwenye
stationary au mashuleni. Uzuri wake
mashine hizi za kutengenezea chaki gharama yake pia sio kubwa sana ni ya
kawaida tu ambayo hata wewe unaweza kuimudu. Hii inaweza ikawa ni sehemu
mojawapo ya kuingizia kipato chako.
2. Kufungua duka la kuuza asali.
Uzuri
wa bidhaa hii muda mwingi soko lake lipo juu. Ni biashara ambayo unaweza
ukaifanya kwa kuagizia asali kutoka kwa wakulima kama nilivyo mimi na kisha
kuanza kuiuza moja kwa moja katika vipimo vinavyotakiwa.
Kama
huwezi kufungua duka hili unaweza ukafanya mbadala wake ukaenda kutengeneza
mizinga wewe mwenyewe na kuwafuga. Pia hii ni biashara ambayo ni nzuri kwako
kukuingizia kipato kikubwa kwa urahisi.
3. Kuanzisha biashara ya kuuza
vyakula katika matamasha mbalimbali.
Hapa
siyo lazima uwe na Hotel au Mgahawa ndiyo uanzishe biashara ya namna hii.
Kikubwa unahakikisha unakuwa makini na sherehe katika eneo ulilopo. Kama ni
kuweka mawakala watakao kusaidia kukujulisha kuwa eneo fulani kuna sherehe ya
aina fulani na siku fulani itakuwa nzuri zaidi kwako kuchangamkia tenda hizo
mapema.
4. Kujenga nyumba za kulala wageni.
Kama
mtaji wako unaruhusu hii ni moja kati ya biashara nzuri kuifanya. Ni biashara
ambayo hahitaji kukimbizana sana ukishamaliza kujenga, zaidi unatakiwa kuweka
mfumo sahihi wa kusimamia na kuanza kuingiza pesa. Na kwa bahati nzuri kwa
Tanzania yapo maeneo mengi ambayo yanauhitaji mkubwa wa huduma hii. Ni Biashara
nzuri kuifanya hata kama umri umeenda, kwa sababu haihitaji mkimbizano mkubwa.
5. Kutengeneza matoroli/mikokoteni na
kuikodisha.
Katika
hili hapa unatakiwa kutengeneza kwa
idadi unayoitaka na unamwachia kijana ambaye anaikodisha huku ukiendelea na
majukumu mengine. Unaweza ukaiona ni biashara ndogo lakini fuatilia kwa
waliowekeza nguvu na mawazo yao hapo wakwambie kile wanachokipata utashangaa.
6. Kuazisha huduma ya AIRTEL MONEY,
MPESA, TIGOPESA, EZYPESA.
Hakuna
ubishi hii ni moja ya huduma ambayo imezagaa kila eneo na watu wengi wanaihitaji.
Kikubwa ni juhudi yako na kuzingatia eneo uliloweka biashara yako liwe hasa la
mzunguko mkubwa zaidi kukuwezesha kufanya biashara hii vizuri.
7. Kupamba maharusi na kumbi za harusi/sherehe.
Pia
unaweza ukajiingiza hapa na kushughulika na kupamba tu maharusi. Kama hujui
sana ni kitu cha kujifunza pia, kisha unachangamkia sherehe zinazojitokeza
mjini.
8. Kuanzisha kilimo cha kisasa.
Wengi
wanaposikia kilimo kichwa kinakataa. Lakini ikiwa utawekeza kwenye kilimo cha
kisasa na cha kitaalamu ambacho unategemea kumwagilia zaidi, uwe na uhakika
unatoka. Yapo mazao mengi unaweza ukalima lakini mojawapo ni kitunguu. Inaweza
ikawa ni njia rahisi ya kufikia mafanikio yako
kuliko unavyofikiri.
9. Mashine za kusaga na kukoboa
nafaka.
Pia
unaweza ukajitengenezea kipato chako na kuwa kikubwa na cha uhakika kwa kufunga
mashine hizi. Kila siku watu wanahitaji kula hivyo ukifunga mashine hizi ni rahisi
sana kupata wateja wa kuwauzia unga na kupata
faida. Na uzuri mahindi ya kusaga yanapatikana maeneo mengi kwa wingi
kama kule Kibaigwa (Dodoma), Gairo(Morogoro), Kiteto(Manyara) na maeneo mengine
mengi kama Iringa na mbeya.
10. Yadi kwa ajili ya kupaki magari.
Kitu
unachotakiwa hapa ni kununua kiwanja na kukigeuza kuwa yadi ambapo magari
yanakuwa yanapaki iwe kwa kulala au kwa muda. Kila gari linalokuwa linapaki
linakuwa linatozwa kiasi fulani cha pesa ambacho kinakuwa ndiyo hiyo huduma
unayoitoa.
Zipo
aina nyingi sana za biashara ambazo unaweza ukazifanya na kukuingizia kipato. Katika
Orodha ya kipande cha makala hii kinachoendelea zimebaki biashara zaidi 110
ambazo sijaziweka hapa kutokana na ufinyu wa nafasi. Kuzijua zinazoendelea na
ufafanuzi wake unaweza ukaniandikia
email kwenda diramafanikio@gmail.com
nitakutumia mara moja.
ILA
KAMA YOTE HAYO UTASHINDWA KUPATA LA KUFANYA WEWE UTAKUWA UMESHAPOTEA, ENDELEA
NA UTARATIBU WAKO WA KUILAUMU SERIKALI.
Tunakutakia
ushindi katika safari yako ya mfanikio, ila kumbuka daima tupo pamoja mpako
maisha yako yaimarike.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Jul 10, 2020
Siri Kubwa Ya Kufanya Mabadiliko Kwa Kitu Chochote.
Kwa muda sasa, nimekuwa nikijifunza mambo
mengi yanayohusiana hasa na mabadiliko ya tabia anayoweza kufanya binadamu hadi
kufikia mafanikio makubwa. Kutokana na umuhimu wa hili pia nimekuwa nikiwafundisha
wengine kuweza kumudu kubadili tabia zao mbaya zinazoweza kuwazuia kufikia
mafanikio makubwa na kujijengea tabia bora za mafanikio katika maisha yao.
Pamoja na harakati zote hizo nzuri, lakini
ugumu umekuwa ukijitokeza kwa wengi kushindwa kubadili tabia zile mbaya hasa
zinazowasumbua kila siku. Tabia hizi mbaya ninazozizungumzia zinaweza zikawa
matumizi mabaya ya pesa, ulevi, uasherati, uvivu, kutokujiwekea akiba, malengo
na nyinginezo nyingi ambazo kwa vyovyote vile ni kikwazo kikubwa katika kufikia
mafanikio makubwa.
Hata hivyo kutokana na kujifunza nilikuja
kubaini kwamba tabia zote hizo mbaya kila mmoja wetu anauwezo wa kuzitawala. Inaweza ikawa ngumu kidogo kueleweka kwako
lakini uwezo huu wa kuzitawala unakuja kwako, ikiwa tu utatambua siri kubwa iliyofichika
katika mabadiliko yoyote unayohitaji katika maisha yako. Kwa kujua siri hii
utaweza kubadili chochote unachokitaka katika maisha yako.
Kumbuka kila kitu duniani kina uwezo wa
kubadilika. Kama mabadiliko yalikuwepo na yataendelea kuwepo. Amini maisha yako
pia yanauwezo wa kubadilika na kuwa mazuri, hata kama kwa sasa upo kwenye hali
ngumu kiasi gani. Kitu pengine ambacho unajiuliza utawazaje kuzitawala tabia
zako zinazokutesa na kukusumbua kwa sasa?
Kama una tatatizo kubwa la kutokujiwekea
malengo na kuyatimiza, hapa pia ni lazima uwajibike kuhakikisha malengo yako yanatimia
kwa gharama yoyote ile. Malengo yako yataweza kutimia kwa kuyafatilia kila siku
hatua kwa hatua. Kitendo cha wewe kufuatilia malengo yako hatua kwa hatua mpaka
kutimia hiyo yote inaonyesha ni kwa jinsi gani uko makini na kile
unachokifanya.
Kwa hiyo mpaka hapo unaona kuwa siri kubwa
ya kufanya mabadiliko yoyote katika maisha yako ipo kwenye kuwa makini na kile
kitu unachotaka kukibadili. Wengi wanashindwa kufikia malengo yao na kutofanikiwa
kutokana na kutokuwa makini katika hili. Kwa tafsiri nyingine unapokuwa makini
inamaanisha nguvu zote za uzingativu unakuwa unazielekeza hapo.
Unaweza ukaanza sasa kubadili maisha yako na kuwa na maisha ya tofauti kwa kuwa makini
kwa yale mambo ambayo hutaki yawe katika maisha yako. Hii itakusaidia kumudu
kufikia ndoto zako ulizojiwekea. Bila shaka unajua ama umeshawahi kusikiwa
kwamba watu wote makini mara nyingi kufanikiwa kwao ni rahisi. Na huo ndio
ukweli.
Kwa kadri utakavyozidi kuongeza umakini kwa
jambo ambalo hulitaki liwe sehemu ya maisha yako ndivyo utakavyojikuta unamudu
kulitawala kwa sehemu kubwa tabia zako na hatimaye kufanikiwa. Hii ni siri
muhimu kuijua na inanguvu ya kubadilisha maisha yako na chochote kile
kinachokusumbua.
Tunakutakia safari njema katika kufikia
mafanikio makubwa.
Kwa elimu na maarifa bora ya kuboresha
maisha yako, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI
NGWANGWALU,
0687449428
Jul 9, 2020
Kama Hujui, Ndoa Imara Ni Tamu Kuliko Fedha.
Karibu
tena mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Karibu tena katika
siku nyingine ya kuweza kujifunza yale yote yaliyomuhimu kuweza kuboresha
maisha yetu. Katika makala yetu tutaangalia umuhimu wa kuwa na ndoa bora ambayo
inaweza ikatusaidia kufikia mafanikio makubwa. Kumbuka, unapokuwa katika
migogoro mingi ya kifamilia itakuwa ni ngumu kwako kufanikiwa kutokana na
vurugu za hapa na pale kila siku.
Je,
wewe binafsi unaamini katika kuoa au kuolewa, kwamba ni muhimu sana kwa maisha
ya binadamu? Kama huamini sana katika jambo hilo, huenda inabidi uanze kuamini.
Kwa nini?
Tafiti
za karibuni kuhusiana na furaha maishani, zinaonyesha kwamba, watu waliolewa au
waliooa wameonesha kuwa na furaha zaidi kuliko wale wasiooa au kuolewa, bila
kujali kipato.
Wale
watu wenye kipato kizuri na ambao wameoa au kuolewa wamebainikia kuwa na furaha
kwa asilimia kubwa zaidi. Wale watu ambao wameolewa au kuoa, bila kujali kipato
chao, wanaripotiwa kuwa na furaha kuliko wale wasiooa au kuolewa, ambao ni
matajiri.
Watu
sita kati ya kumi ambao wameoa au kuolewa, wanadaiwa kuwa na ridhiko la namna
maisha yao yanavyoenda, ukilinganisha na wanne kati kati ya kila kumi ambao
hawajaoa au kuolewa.
Inaonyesha
kwamba, kuna uhusiano kati ya fedha, ndoa na furaha na ridhiko kwenye maisha ya
watu. Watafiti wengi hivi sasa wanakiri kwamba, ndoa ina thamani na maana zaidi
kuliko fedha, linapokuja suala la furaha au ridhiko la maisha kwa binadamu.
Mtu
mwenye ndoa ya furaha, anakuwa na ridhiko na furaha kubwa maishani, bila kujali
pato lake. Yule ambaye hayuko kwenye ndoa, bila kujali pato lake, kiwango chake
cha furaha huwa ni cha chini sana. Kama unafikiri natania waulize wenye ndoa
ambazo zina usalama ndani yake watakwambia ukweli wa hili zaidi.
Nimesema
ndoa ya furaha kwa sababu, mtu aliye kwenye ndoa ngumu, kiwango chake cha
furaha kinakuwa chini kuliko kile cha mtu ambaye hayuko kwenye ndoa, bila
kujali vipato vyao.
Tafiti
zinaonyesha pia kwamba, karibu watu sita kati ya kila kumi walio kwenye ndoa za
furaha, ambao wanapato la chini hufurahia maisha yao na wanaridhiko kubwa
zaidi. Ni watu watano kati ya kumi tu ya wale wenye pato kubwa, ambao hawako kwenye
ndoa, wanaofurahia maisha.
Hata
hivyo, wale walio kwenye ndoa, ambapo pia wanakipato kikubwa, wameonekana kuwa
na furaha zaidi. Ni saba kati kati ya kumi kati ya watu hao, ambao wamebainika
kuwa na furaha na kuridhishwa na maisha wanayoishi.
Kuna
wimbo ambao nimewahi kuusikia ukisema, kwamba, watu wanashangaa wanandoa fulani
maskini, kwani kila siku wanawaona wanandoa hao wakitabasamu, pamoja na ‘njaa’
waliyonayo. Ni kweli, walio kwenye ndoa imara, wanajisikia vizuri bila kujali
kama wanafedha au hawana.
Wasio
kwenye ndoa au wenye ndoa ngumu, hata
kama wanamamilioni ya fedha vipi, maisha yao ni mzigo mzito sana. Kwa nje
wanaweza kuonekana kama ni watu walioridhika, wakati kwa ndani wanamashaka
makubwa na maumivu yasiyosemekana.
Ndio
maana baadhi ya wanauchumi wanasema, watu waliokwenye ndoa imara ni rahisi sana
kwao kupata pesa. Urahisi huu unaletwa na ule ukweli kuwa, watu hawa wanafuraha
na wameridhishwa na maisha yao, kiasi kwamba huyaona mambo kwa upana wake.
Pamoja
na kwamba, watu wengine kwenye ndoa, huwa wanaamini kwamba, wakipata fedha
ndipo watakapokuwa na furaha katika ndoa zao, hali ni kinyume.
Ndoa
isiyo imara haiwezi kubadilishwa na kuwa imara kwa kupatikana kwa fedha, zaidi
italeta matatizo mengine. Lakini ndoa imara ni nzuri na tamu kuliko kuwa na
fedha.
Kwa
makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza kila siku na kuboresha maisha yako.
Pia usiache kuwashirikisha wengine kuweza kujifunza kupitia mtandao huu.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0687449428.
Jul 8, 2020
UTAISHI MAISHA GANI BAADA YA UONGOZI,MAISHA YA MBABE YAHAYA ADBULY JAMMEH BAADA YA KUONDOLEWA MADARAKANI KWA NGUVU ZA KIJESHI
Watu walikuwa wamesimama Baada ya maisha marefu ya shida na mateso hatimaye watu wa Gambia mapema January 2017 walipata kushudia kitu ambacho pengine hawakukitegemea katika maisha yao kwamba yangetokea ,ilikuwa ni siku ambayo wanagambia walikuwa wanafungua ukurasa mpya wa maisha yao na hii ni baada ya kuishi maisha ya Utumwa kwa mda wa miaka 22 chini ya utawala wa Yahaya Jameh (54) ilikuwa ni siku ya furaha na majonzi kwa wengine pia.
Waandamanaji wakina mama, vijana kwa wazee walikuwa wamejazana uwanja wa ndenge wa taifa la Gambia na wengi walikuwa wanalia na kukubujikwa na machozi wengine walikuwa wanatabasamu kuashiria yamekwisha maana waliokuwa wanayashuhudia waliona kama ndoto kwao ,wengi wa wandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyosomeka "GO AND FEEL THE PAIN "ulikuwa ni Ujumbe wao wa mwisho wakimaanisha Nenda na wewe ukaonje utamu wa jiwe .
TAZAMA SIMULIZI NZIMA KATIKA CHANNEL YETU YA YOUTUBE VIDEO IPO HAPO CHINI.
USIACHE KU LIKE, SUBSCRIBE NA KUSHARE
Mpoki Buyah kaminah
Contacts:0762155025
Contacts:0624027362
Email:mpokibuya@gmail.com
Jul 7, 2020
Hii Ndiyo Silaha Kubwa Ya Mjasiriamali Katika Kufikia Mafanikio Makubwa.
Wahenga walisema:
“Maisha ni kuona mbele.” Huu ni usemi unaompa mjasiriamali matumaini ya kusonga
mbele pasipo kutumia muda mwingi kuwaza yale aliyokwishafanya.
Katika maisha ya kila
siku kwenye ujasiriamali, wajasiriamali wanakumbana na changamoto nyingi.
Changamoto hizi wakati mwingine huwasaidia kuona mbele na hatimaye kuwa watu
wenye mafanikio.
Kwa mfano, kama mtu
anajishughulisha na ujasiriamali halafu akawa anasumbuliwa na mamlaka
zinazohusika na urasimishaji wa biashara kwa sababu za kutorasimisha shughuli
zake, akiamua kurasimisha biashara yake atafanya shughuli zake bila
kubughudhiwa.
Mwisho wa siku atakua
kibiashara, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi yake kwa kulipa kodi na kuajiri
watu. Kwa mjasiriamali wa aina hii hatakuwa na muda tena wa kuanza kuwaza yale
yaliyotokea bali atakuwa anaiona dunia yenye matumaini kesho yake.
Atakuwa anafikiria
zaidi juu ya siku za baadaye. Atakuwa na malengo ya kuhakikisha anaibadili
dunia na wala siyo kusubiri dunia imbadilishe. Ni kwa sababu, akisubiri dunia
imbadili, atakuwa miongoni mwa watu wanaosubiri kutupwa kwenye shimo la sahau.
Hii ina maana kuwa,
mjasiriamali hatakiwi kukumbuka changamoto za jana kwa lengo la kumpa huzuni na
machungu yatakayomsababisha ashindwe kupiga hatua. Bali anatakiwa kuchukulia
changamoto hizo kama somo, ambalo litamwezesha kufika anakoelekea pasipo kurudi
katika hali yake ya jana, ambayo siyo taswira nzuri katika kichwa chake.
Kama nilivyowahi
kusema katika makala zangu za mwaka jana, mwanzo ni mgumu. Leo narudia tena
kusema kuwa mwanzo ni mgumu. Mwanzo wa shughuli za ujasiriamali, wakati
mwingine utaona kama hakuna anayekujali.
Unaweza kuhangaika
siku nzima na hata zaidi ya miezi kadhaa pasipo kupata kile ulichokusudia. Wakati
mwingine unaweza kuwa unatafuta msaada fulani ili kukamilisha kile
ulichokianzisha ukaambulia patupu! Unaweza kuchekwa na baadhi ya watu, wakiwamo
wale uliowategemea kuwa wangekuunga mkono. Pia, unaweza kukutana na upinzani
mkubwa kutoka kwa wajasiriamali wenzako, hata kwa wivu wake kana kwamba
unapigana vita.
Hata hivyo, ukiamua
kuona mbele utavuka vikwazo hivi vyote na kupata kile ulichokusudia. Kuona
mbele ni pamoja na kuwa na dira au mweleko wa wapi unataka kuwa. Mjasiriamali
mwenye dira huwa hakati tamaa na haogopi vita kutoka kwa wenzake au kwa baadhi
ya watu. Ni mtu mwenye kuangalia ni njia zipi azitumie kufika pale anapotaka
kufika.
Ikumbukwe kuwa
ushindi huja kwa mtu mwenye kupambana kwa malengo ya kuiona kesho yenye nuru ya
mafanikio.
Ushindi hupatikana na
kujifunza kila hatua na njia anayoipita mjasiriamali ili kufika kwa mafanikio
pale anapopata. Ili kufanikisha hili, mbali ya kuwa na maono, mjasiriamali
anatakiwa kuwa mvumilivu na mwenye kuthubutu.
Uvumilivu na uthubutu
ni miongoni mwa vitu muhimu sana kwa mjasiriamali. Ni vitu vinavyochangia suala
zima la utekelezaji wa dira ya mjasiriamali, ambayo siku zote huwa ni kuona
mbele. Kwa hiyo utakuja kutambua kuwa uvumilivu na uthubutu ndiyo silaha ya
mjasiriamali kufikia kwenye mafanikio.
Watu wengi
wameshindwa kufika popote kwa sababu ya kukosa uthubutu na uvumilivu wa kufanya
yale wanayofikiria.
Kwa mjasiriamali
anayethubutu na kuvumilia, ataiona kesho yake yenye neema na ambayo
itamfaidisha yeye, jamii yake na Taifa kwa ujumla kwani mwendapole hajikwai,
akijikwaa hataanguka wala kushindwa kuendelea na safari yake.
Makala hii imeandikwa na Chiraka Muhura
wa Gazeti la Mwanachi.
Jul 6, 2020
Misingi 6 Muhimu Ya Kujiwekea, Ili Kujenga Mafanikio Ya Kudumu.
Ili
uweze kufanikiwa, ni lazima kujiwekea misingi imara ya kimafanikio itakayokuwa
ikukuongoza kila siku. Bila kuijua misingi hii mapema sitashangaa kuona maisha
yako yakibaki kuwa yaleyale bila ya kubadilika sana. Kwa kujiwekea misingi hii,
inauwezo wa kufanya maisha yako kubadilika kwa sehemu kubwa sana.
Kama
misingi hiyo ipo, ni nini kinachokuzuia wewe kufanikiwa sasa? Bila shaka
hakuna. Unachohitajika kukifanya ni kutumia misingi hiyo mpaka kufanikiwa.
Uwezo na nguvu za kubadilisha maisha yako kwa kadri unavyotaka unao. Kwa kuijua
misingi hii, kwako itakuwa chachu ya kukusaidia kuweza kusonga mbele na kujijengea
maisha ya mafanikio makubwa:-
Je,
misingi hiyo ni ipi?
Hii
Ndiyo Misingi 6 Muhimu Ya Kujiwekea, Ili Kujenga Mafanikio Ya Kudumu.
1. Kaa mbali na watu hasi.
Kama
vile ambavyo ilivyo kompyuta inaweza ikaharibiwa na virusi na kuharibika
kabisa, hata wewe maisha yako yanaweza kuharibiwa vivyohivyo lakini ikiwa una
watu hawa hasi wengi wanaokuzunguka. Unapokuwa na watu hasi inakuwa ni rahisi
sana kwako kuweza kuua mipango na malengo mazuri uliyojiwekea.
Ninajua
watu hawa wanaweza wakawa ni rafiki zako au ndugu kabisa, lakini hiyo haina
namna tena kwako, zaidi ya kuachana nao. Ikiwa utaendelea kung’ang’ania kuwa na
watu hawa hasi utarudishwa nyuma sana katika maisha yako. Ili kuokoa maisha
yako ni lazima kukaa mbali nao na kutafuta marafiki chanya watakaokupa hamasa
ya kufanikiwa zaidi. Kukaa mbali na watu hasi ni msingi mzuri kwako unaotakiwa
kuujua.
2. Wekeza kila siku katika maisha
yako.
Huu
ni msingi muhimu sana kujiwekea ili kuwa na mafanikio ya viwango vya juu. Kama
katika maisha yako unawekeza kila siku, tambua baada ya muda kidogo kuanzia
sasa utakuwa mbali sana kimafanikio. Pengine unaweza ukaanza kusema ‘oooh mimi sasa sina pesa, sina mtaji hili
halinihusu nitawekeza vipi sasa hapa?’
Sikiliza,
hauhitaji kuwa na pesa ili kuwekeza. Anza na kuwekeza kwanza kwenye akili yako
kwa kujifunza kupitia vitabu au semina mbalimbali. Maisha yako yatakuwa ya thamani
sana kila utakavyozidi kufanya uwekezaji huu. Maarifa utakayoyapata huko kwani
yataweza kukusaidia kuwekeza katika maeneo mengine na kufanikiwa zaidi pale
utakapopata mtaji unaouhitaji.
3. Kuwa wewe kama wewe.
Kuna
wakati wengi wetu huwa ni watu wa kutaka maisha ya kuwapendezesha wengine.
Nikiwa na maana kutaka kuishi maisha kama wengine wanavyoishi. Hiki ni kitu
hatari sana kwako kwa sababu unakuwa unaishi kwa kufuata bendera ama wengine
wanavyoishi na kujikuta unakuwa mtu wa kupoteza mwelekeo.
Ili
uweze kuishi kwa mafanikio ni vizuri ukajijengea msingi wa kuishi maisha yako
ukiwa wewe kama wewe. Kwa kuishi wewe kama wewe itakulazimisha kutambua unataka nini kwenye haya maisha, ni lini
utafikia mipango yako uliyojiwekea na unataka kitu gani kikusaidie kufikia
malengo yako. Huo ndiyo msingi muhimu pia kuujua kwa ajili ya mafanikio yako ya
leo na kesho.
4. Jiwekee mipaka katika maisha yako.
Ishi
maisha yako kwa kujiwekea mipaka. Usije ukaruhusu kila mtu kuingilia maisha
yako kwa jinsi anavyotaka hata awe ndugu wa karibu kiasi gani. Bila shaka
umeshawahi kuona watu ambao maisha yao yanaharibiwa kutokana na kuingiliwa na watu
walio karibu nao. Na hii yote imekuwa ikitokea kutokana na wahusika kushindwa
kujiwekea mipaka iliyoimara katika maisha yao.
Mipaka
hii unatakiwa ujiwekee katika maeneo mabalimbali kama vile katika muda, kazi
zako za kawaida na wakati mwingine kwenye biashara zako unazozifanya. Kwa
kufanya hivyo watu wako wa karibu watakuwa hawako huru sana kuingilia yale
maeneo uliyojiwekea mipaka maana wakifanya hivyo watajua utakuwa mkali au
hutakubali kiurahisi. Hiyo itakusaidia kukujengea msingi mwingine imara wa
mafanikio yako.
5. Kuwa king’ang’anizi wa mafanikio.
Kwenye
maisha yako kitu ambacho hutakiwi kukiruhusu ni kushindwa kiurahisi. Kama ikitokea
umeshindwa katika jambo kwa namna moja
au nyingne, jaribu kutafuta njia ya kulifanya jambo hilo kwa namna ya tofauti
mpaka kufanikiwa. Unapokuwa king’anga’nizi wa mafanikio huo utakuwa msingi bora
kwako unaojitengenezea wa kufikia mafaniko makubwa.
Maisha
ni kusonga mbele. Ng’ang’ania mafanikio yako mpaka uyaone hata kwa gharama
yoyote ile. Usiruhusu kitu kikakukatisha tamaa. Kama unafikira za nyuma
unazoziweza kwa kudhani kuwa ulikosea eneo fulani ni bora ukaachana nazo fikra
hizo kwa sasa, kwa sababu hazitakusaidi kitu chochote zaidi ya kukwamisha wewe.
Yaliyopita yamepita, songa mbele.
6. Jijengee ukomavu wa fikra.
Ili
uweze kufanikiwa inatakiwa ifike mahali fikra zako ziwe zimekomaa na kuweza
kutambua kila hali inayojitokeza katika maisha na jinsi ya kuweza kukabiliana
nayo. Kwa mfano, inapotokea kushindwa au ukakosea katika jambo fulani
unakabiliana vipi na kushindwa huko bila kuumia au kujiona hufai na kisha
kuendelea mbele.
Hakuna
kingine zaidi ya wewe kuwa na ukomavu fulani wa fikra utakao kuwezesha kusonga
mbele. Ukomavu huu ni rahisi kuupata, utaupata tu ikiwa wewe ni mtu wa
kujifunza mambo mbalimbali ya kimafanikio kama unavyofanya sasa hivi. Bila
kufanya hivyo hutaweza kuhimili mawimbi mengi ya maisha yanayojitokeza kwa
upande wako.
Kumbuka
hii ni sehemu ya misingi ambayo unaweza ukajiwekea kama nguzo ya mafanikio
yako. Lakini, kwa kutumia kijitabu chako kidogo cha kujifunzia unaweza
ukaongeza misingi mingine ambayo unaona kwako inafaa kukuongoza katika safari
ya mafanikio. Bila kujiwekea misingi binafsi, utayumbishwa sana katika maisha
kwa mambo mengi na itakuwa ngumu kufanikiwa.
Tunakutakia
kila la kheri katika safari ya mafanikio, endelea kuwashirikisha wengine
kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku kwa kujifunza na
kuhamasika zaidi.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
04 80 35,
Jul 5, 2020
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuachana Na Tabia Ya Kujihukumu.
Kuna
wakati katika maisha yako unaweza ukajiona umekosea hili ama lile na lile na
kuhisi umeharibu maisha yako kabisa. Kukosea kwa mambo hayo ambayo unaona
kabisa ulitakiwa kuyafanya kiusahihi lakini yamekuwa sivyo ndivyo, hali hii hupelekea
kuumia moyo na kujihukumu kila wakati.
Ni
hali ambayo huwa inatukuta wengi wetu nakujiona ni wakosefu kutokana na
kuhukumiwa huko. Hali hii inapotokea kwa muda huwa siyo tatizo kubwa sana
lakini inapozidi hapa ndipo ambapo inakulazimu kutafuta tiba ya kukutoa huko
kwenye kujihukumu.
Inawezekana
ukawa ni miongoni mwa watu ambao huwa wanajihukumu sana ama ulishaona watu wako
wakaribu wakiwa hivyo. Kama ni hivyo unatakiwa kuchukua hatua zitakazo kufanya
uachane na kujihukumu huko ambako kunakupotezea furaha.
Fuatana
nasi katika makala hii kujua hatua muhimu unazotakiwa kuchukua ili kuachana na
tabia ya kujihukumu:-
1.
Acha kujilinganisha na wengine.
Kama
una tabia ya kujilinganisha na wengine sana ni lazima utakuwa mtu wa kujihukumu
ndani yako iwe kwa vibaya au vizuri. Ikiwa itatokea wale unaojilingisha nao
wakawa wamekuzidi kimaisha kwa sehemu kubwa ni lazima utajihukumu vibaya na
kujiona wewe pengine hufai na si chochote katika maisha yako.
Watu
wengi ambao huwa wanatabia hii ya kujilinganisha na wengine, ni watu ambao huwa
wanajihukumu sana tena kwa vibaya. Kwa kadri wanavyozidi kujihukumu badala ya
kuboresha maisha yao ndivyo hujikuta wanaya bomoa zaidi. Na hiyo huwa inatokea
kwa sababu huwa wanashindwa kuchukua hatua na kubaki kujihukumu.
Ili
uweze kutoka hapo na kuweza kuishi maisha ya furaha na yasiyo ya majuto
unalazimika wewe binafsi kuachana na tabia ya kutokujihukumu tena. Unatakiwa
kuishi wewe kama wewe kwa kukimbia mbio zako mwenyewe na siyo kuiga maisha ya
watu ambayo yanaweza yakakuumiza na kukutesa siku zote.
2. Jiamini wewe kama wewe
ulivyo.
Unapokuwa
unajiamini wewe binafsi kuwa unaweza inakuwa siyo rahisi sana kwako kuweza
kujihukumu bila sababu. Ni lazima utambue kuwa una uwezo mkubwa ndani yako
usioweza kuzuiliwa na kitu chochote. Hivyo, ni muhimu kuutumia uwezo huo
ulionao ndani yako kuweza kukufanikisha.
Jifunze
kuchukua hatua mathubuti ambazo zitakupelekea wewe uweze kujiamini. Kama kuna
kitu huna iwe maarifa au chochote kile weka utaratibu wa kujifunza au kupata
kitu hicho. Kwa kuwa na maarifa hayo hiyo itakuwa ni chachu kwako mojawapo ya
kuweza kukufanya ujiamini na hutoweza tena kujihukumu ndani yako.
Ukijaribu
kuchunguza kidogo, utaelewa kwamba watu wengi ambao huwa hawajimini mara nyingi
ni watu ambao ni wa kujihukumu sana kwa mabaya na kutilia shaka uwezo wao
mkubwa walionao. Ili uweze kuachana na kujihukumu nguzo mojawapo muhimu kwako
ni kujiamini.
SOMA;
Haya Ndiyo Mambo Mawili Usipokuwa Nayo Makini Yatakutesa Na Kukusumbua Sana Katika Maisha Yako.
3. Chukua hatua.
Badala
ya kukaa na kuzidi kujihukumu chukua hatua za kuweza kukutoa hapo ulipo.
Unaweza ukachukua hatua za kuachana na maneno ya wanaokuona huwezi, umeshindwa
na pengine hutafanikiwa, hayo yote yanayokufanya uanze kujihukumu. Kama
utaendelea kujihukumu tu, itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kufanikiwa.
Kwa
kufuata hatua hizo tatu muhimu yaani kujiamini, kuacha kujilinganisha na
wengine na kuchuua hatua ni njia muhimu sana ya kukusaidia kuondokana na
kujihukumu.
Kwa
makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza
kila siku na kuboresha maisha yako.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Jul 4, 2020
Watu Watano Hatari Ambao Hutakiwi Kufanya Nao Biashara.
Ili
uweze kufanikiwa katika biashara unayoifanya ni muhimu kufanya biashara na watu
sahihi ambao wanaweza kukusaidia hata wewe kuweza kusonga mbele. Watu hawa
wanaweza wakawa ni wateja wako ama timu nzima inayokuzunguka na kukusaidia
kukua katika biashara yako unayoifanya.
Inapotokea
ukajikuta ukawa na ‘timu’ au watu
unayofanya nayo biashara ikawa siyo sahihi sana kwako hapo ndipo matatizo na
kushindwa mara nyingi huweza kuanza kujitokeza. Watu hawa ndiyo ambao
tutawajadili katika makala hii, wale wanaoweza kutukwamisha na kutufanya
tushindwe kufikia ndoto zetu tulizojiwekea.
Ni
watu ambao tunawajua na tunashirikiana nao mara kwa mara katika shughuli
tunazozifanya kila wakati za kibiashara. Kitu cha msingi na cha kujiuliza ni
watu gani hasa ambao unatakiwa kuwaepuka na ambao wanaweza wakawa ni hatari kwa
maendeleo ya biashara yako leo na kesho?
Hawa
Ndiyo Watu Watano Hatari Ambao Hutakiwi Kufanya Nao Biashara.
1.
Watu wanaokubali kila kitu.
Hawa
ni watu ambao kila kitu wanachoambiwa huwa ni wepesi wa kukubali. Mara nyingi
ni watu ambao hawana misimamo na wakati wowote wanaweza kuyumbishwa. Unapokuwa
na watu kama hawa katika timu yako ya biashara inakuwa ni rahisi hata kwako
wewe kuweza kukuangusha wakati wowote bila kutegemea.
Inapotokea
kidogo tu wakapewa ushawishi na mtu mwingine pia ni rahisi kwao kuweza kukubali
kwa sababu hiyo ndiyo asili yao. Kama unataka kufanya kazi au biashara yako
vizuri ikafanikiwa zaidi, hakikisha unafanya kazi na watu wenye misimamo imara
ambayo haiyumbishwi hovyo. Ikiwa utafanya kazi na watu hawa ‘Yes Man’ ipo siku watakukwamisha tu.
SOMA; Sababu 10 Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.
2. Watu wanaochochea maneno.
Ni
mara nyingi sana hawa ni watu ambao huwa tunao katika kazi zetu na pengine
katika timu zetu za biashara. Hawa ni watu ambao mara nyingi hujifanya ni watu
wa kupeleka sana habari kwa bosi wakati mwingine habari hizo wanazozipeleka
zinaweza kuwa hata siyo za kweli kwa namna moja au nyingine ilimradi tu
wazifikishe.
Unapokuwa
na watu wa namna hii hata kama ni wawili katika bishara yako hicho ni kitu cha
hatari kwako. Watu hawa wanakuwa wanauwezo mkubwa wa kuweza kuiharibu ama
kuibomoa ‘Staff’ yako kwa jinsi
wanavyoweza. Watu hawa wakati mwingine hufahamika kama wambea ambao kila mara
hutaka kujifanya wako karibu na bosi, hivyo ni muhimu kuwaepuka sana katika
kazi zetu na biashara kwa ujumla.
3. Watu wanaojua kila kitu.
Ni
watu ambao huwa hawapo tayari kuelekezwa kitu kutokana na wao kujifanya wanajua
kila kitu. Kama katika biashara yako una watu wa namna hii iwe wateja au
wafanyakazi wako ama wafanyakazi wenzako hii itakupa tabu na shida kubwa sana
katika suala zima la utendaji wa kazi.
Kwa
maana kila utakachotaka kumwambia mtu wa namna hii, hata kama kuna sehemu
amekosea utashindwa kwa sababu yeye anajua kila kila kitu. Najua bila shaka kwa
namna moja au nyingine umewahi kukutana na watu wa namna hii katika eneo ulipo
na unajua vizuri usumbufu wa watu hawa kuwa ni mkubwa.
SOMA;
Mambo 12 Ya Kuzingatia Kama Unataka Kujiajiri.
4. Watu wanaobadilika badilika.
Katika
biashara yoyote unayoifanya, moja ya watu hatari wa kuwaepuka ni watu hawa
wanaobadilika badilika kila wakati. Watu hawa mara nyingi huweza kubadilika
zaidi kutokana na mambo mengi waliyonayo ndani mwao. Kitu kimojawapo
kinachoweza kuwapelekea wao kubadilika zaidi ni tamaa walizonazo na kutokuwa
waaminifu.
Unapoamua
kufanya biashara na watu wa namna hii inakuwa siyo rahisi kwako kuweza
kufanikiwa. Hii ni kwa sababu dakika na muda wowote ule ni rahisi sana kwao
kuweza kukugeuka na inakuwa ni rahisi kuweza kukupa hasara ambayo hukutegemea.
Dawa pekee ya kuweza kukwepa matatizo hayo ni kuwaepuka watu hawa kwa namna
yoyote ile unayoweza.
5. Watu wanaolalamika sana.
Unapokuwa
unafanya biashara na watu wa namna hii watakufanya ujihisi au uone kuwa wewe
unakosea katika kila kitu. Hawa ni watu wenye tabia ya kulalamikia mambo mengi
sana ikiwa ni pamoja na huduma, pengine kwa kuona kwao mbovu au wananyonywa kwa
namna moja au nyingine lakini ilimradi tu walalamike.
Ni
watu ambao kiuhalisia ukiwa nao pamoja katika eneo la biashara ni rahisi sana
kuweza kukuvunja hata moyo. Upo wakati utafika ambao unaweza ukahisi kweli kwa
wanayolalamikia inaweza ikawa ni kweli kumbe hakuna hata ukweli wa kitu hicho
hata kidogo kama wao wanavyodai iko hivyo.
Kumbuka,
kama nilivyosema mwanzo unapokuwa na watu hawa inakuwa ni vigumu kwako kuweza
kufanikiwa katika eneo la biashara unallolifanyia hata ufanyaje. Lakini kwa
kifupi, hao ndiyo watu ambao tunao katika maeneo yetu ya kazi na ni muhimu
kuwaepuka ili kuweza kufanikiwa zaidi.
Tunakutakia
kila la kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika
zaidi. Pia hakikisha unawashirikisha wengine waendelee kujifunza kupitia
mtandao huu.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
04 80 35,
Jul 3, 2020
Ni Ipi Imani Yako Kuhusu Mipango Uliyonayo?
Watu waliowengi ni kawaida kusikia
wakisema jipe IMANI Mungu atakusaidia ufanikiwe au bora imani tu!
utafanikiwa.
Pengine hali hii inatokana na
msukumo ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa viongozi wa dini, ambao mara zote
wamesisitiza waumini wao kuwa na IMANI; lakini..pasipo
kuwambia, ni jinsi gani ya kuwa na hiyo IMANI.
Huwezi kuwa na IMANI hivihivi
kutokea hewani tu! ni lazima IMANI yako ijengeke kutoka kwenye msingi fulani.
Kwa mfano msingi wa IMANI juu ya
kupata PESA au MAFANIKIO ni kuanza KUTAMANI kitu fulani, halafu unapanga MPANGO
wa jinsi ya kupata hicho kitu unachokitamani.
Kutokana na MPANGO, utatengeneza
mchakato wa utekelezaji (mpango kazi) na hapa utatambua majukumu yako ya
kufanya kila siku.
MPANGO ambao umejiwekea utaratibu wa
kuupitia kila siku, utakujengea IMANI kwamba siku moja utafanikiwa kupata hicho
unachotamani, kwasababu mpango utakuonyesha njia inayokwenda kufikia kile
unachokitaka.
IMANI yako iliyojengwa katika msingi
huu, inakufanya uweze kuwapuuza wakatisha tamaa wote ambao wamejaa sana mitaani
kwetu.
Kwa hiyo, tunajifunza kwamba ni
lazima tupange MIPANGO ya kupata PESA au kile tunachotamani kuwanacho. Japokuwa
kuna imani kwamba mipango yote inapangwa na MUNGU, hivyo wasiojua ukweli huu
hawaoni haja ya kupanga MIPANGO. Watu wengi wanadai kwamba wao
wanaishi kwa IMANI na wanaichukulia siku kama ilivyokuja. Hii inamaanisha kwamba
watu hawa huwa hawapangi siku yao, mwezi na hata mwaka.
Mungu wetu amekwishatupatia akili ya
kutambua baya na zuri na pia tumepewa zawadi ya uwezo wa kupiga picha ya akili,
ili kusudi tuweze kushiriki kwenye mchakato wa uumbaji na kutengeneza vitu mbalimbali
kupitia MIPANGO.
Kwa kifupi ni kwamba, unahitaji
MPANGO kuamini katika IMANI na ukweli ni kwamba:
“yeyote
asiyekuwa na MPANGO wa kupata pesa hana IMANI ya kupata PESA”.
Unahitaji Mpango kazi wa kuamini
kuwa utapata siku moja kile unachotamani kukipata. Kumbuka kuwa IMANI ya kweli
inayojionyesha katika vitu viwili; yaani MPANGO na MATARAJIO.
IMANI siku zote, inatanguliwa na
mawazo ya kitu Fulani (KUTAMANI), na baadae MPANGO KAZI (utekelezaji), ambao
unakufanya upate kutambua majukumu ya kutimiza kila siku.
Utekelezaji wa majukumu yako ya kila
siku unakupa MATARAJIO ya kufanikiwa. Matarajio ndiyo yanakujengea IMANI ya
kwamba utafanikiwa siku moja.
Kwahiyo, MPANGO kwa maandishi juu ya
kupata PESA au mafanikio yoyote, ndiyo inaonyesha matendo makuu ya kwamba
UNAAMINI utapata pesa au mafanikio.
Jul 2, 2020
Ukifanyia Kazi Mambo Haya Mara Kwa Mara, Yatakufikisha Kwenye Ndoto Zako.
Kila mtu anatamani kuzifikia
ndoto za maisha yake ya mafanikio. Kwa sababu hiyo kila mtu huchukua hatua
anazoziona yeye zinamfaa ili kutimiza malengo hayo. Je, ni wangapi wanajua kuwa
huwa wanachukua hatua sahihi au la.?
Katika makala haya, ni lengo
langu ni kukumbusha wewe, mambo ya msingi na kama utayazingatia mambo haya
yatakusaidia wewe kuweza kukufikisjha kwenye ndoto zako za mafanikio. Je mambo
hayo ni yapi?
1. Andika malengo
yako.
Najua malengo yako unayajua vizuri tu, lakini kuna sababu muhimu
sana kwa wewe kuyaandika malengo yako tena. Chukua kalamu na karatasi, na andika
vitu vyote unavyotaka kuvifikia kwenye maisha yako.
Fikiria juu ya kitu ambacho unataka kufanya au unahitaji
kukifanya. Inaweza kuwa kitu chochote kama malengo ya afya au malengo ya
biashara yako. Orodhesha vitu vingi iwezekanavyo, lakini viwe vile unavyotaka
kuvifanikisha.
2. Weka vipaumbele
vya malengo yako.
Ndio, najua umeandika malengo mengi, lakini ukweli ni
kwamba huwezi kuyatimiza yote. Ili uweze kuyafikia malengo hayo, yagawawe kwa kuzingatia vipaumbele. Unapaswa kujua,
malengo yapi uanze nayo na yapi uyaache.
Kwa kuweka vipaumbele itakupa nguvu wewe, ya kuweza
kuyafikia malengo yako kwa urahisi. Na ukishaweka vipaumbele, usibabaishwe na
malengo mengine yatakayotokea hapa katikati, vipaumbele vyako vinatosha,
vitekeleze kwanza.
3. Vunja vunja
malengo yako.
Vunja kila lengo kuwa dogo ambapo unajua unaweza kutimiza
kwa urahisi. Hakikisha pia unajipa muda wa wewe kutekeleza malengo yako kulingana
na wakati uliokadiriwa wa mradi huo uliojiwekea.
Kwa mfano, ikiwa lengo lako ni kusoma kitabu.
Usijilazimishe kusoma kurasa mia moja, kwa mara moja, soma kurasa chache na
zielewe. Fikiri kama unataka kujifunza kuogelea, je! Ungeingia ndani ya bahari
au ungeanza kwanza kujifunza katika dimbwi?
4. Amua kuwajibika.
Lengo kuu ni kuishi maisha bora ya kufikia malengo yetu na
kufanya hivyo lazima tuchukue hatua moja kwa wakati mmoja na kwa hiyo
tunahitaji msimamo thabiti. Je! Unahakikisha vipi malengo yako yanatimia?
Hapa hakuna ujanja, unatakiwa kuwajibika. Fanya kila
linalowezekana kwa wewe kuamua kuwajibika ili kuhakikisha malengo yako
yanatimia. Ukikubali kuwajibika nakupa uhakika unaweza kufanikiwa na kufika
mbali kimafanikio.
Fanyia kazi mambo hayo na hakikisha unachukua hatua kuona
ndoto zako zinatimia.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kumbuka, ufalme hauji kwa maneno bali unakuja kwa vitendo,...chukua hatua.
Nikutakie kila la kheri,
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA NDOTO ZAKO ZITUMIE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
Mawasiliano, Whats app; 0713048035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)