May 29, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuishi Na Watu Wasumbufu Ulionao Kazini Kwako.
Ajira au kazi katika ujumla
wake huwakusanya pamoja watu wa tabia, haiba na mikabala mbalimbali ya
kimaisha. Tabia na haiba hizi tofauti wakati mwingine huweza kusababisha
misuguano , majuto na hata sononi. Kuna wakati bosi ni mkorofi na watumishi
wengine wanakuwa wamekaa kisharishari tu.
Hali kama hizi ndizo
huwafanya baadhi ya watumishi kusubiri likizo kwa hamu kubwa sana. Kwa kwenda likizo hujisahaulisha na vurugu
hizi. Lakini wengine huamua kubadili ama kuacha kazi kabisa. Hatua hizo mbili
zinaweza kuwa ni za muda mfupi tu. likizo hatimaye huisha na mtu hurejea kazini
au kule anakoenda baada ya kuacha sehemu ya awali, anaweza kupambana na kero
kubwa na nyingi zaidi.
Nijuavyo mimi, kuna mambo
ambayo mtu akiyafanya, vurugu na tafrani hizi za makazini haziwezi kumdhuru,
bila kuhama au kwenda likizo.
Mambo haya akiyafanya
atahisi amani ya nafsi, utulivu wa mawazo na kufurahia kazi au kufurahia maisha
hata nje ya eneo la kazi. Haya ni mambo ambayo katika hatua za awali, mtu
anaweza asifanikiwe, hata baada ya kufanya. Lakini kwa kujizoeza tena na tena
atapatwa na mshangao kugundua yanafanya kazi.
Kama watu wa kazini kwako au
pengine popote wanazungumza kwa kufoka au mkabala wa kukosa adabu na upendo,
unaweza kujikuta unawaiga. Kama ni kufoka nawe utafoka, kama ni kutukana nawe
utatukana na kama ni ubishi utabishana pia. Hii husaidia kuongeza tatizo na
kuchokoza na kuchochea hisia.
Badala ya kufanya hivyo,
unashauriwa kuwa mtulivu, uzungumze na kutenda kwa amani na upendo. Kwa kufanya
hivyo, bila ya wao kujua, watajikuta wakiiga tabia zako. Bila kujali nafasi
yako kazini, utaona wengine wakikutazama kama dira, kwa mfano na kama mwanga.
Kila siku kabla hujafika au
kuingia kwenye eneo lako la kazi, jitahidi kusema kwa kurudia maneno haya ‘mawazo ni yenye utulivu mkubwa kwa siku
nzima ya leo. Namwaga utulivu ambao umenizunguka. Nazungumza kwa amani, utiifu
na tabasamu. Nachagua kutenda kwa amani na upendo.’ Yaseme haya ukiwa
umedhamiria na hisia zako zikiamini hivyo.
Jaribu kusalimia kila
unayekutana naye hapo kazini. Kila unapojihisi kuwa umekerwa, vuta pumzi kwa
upole na kwa kina kiasi mara tatu hivi, kabla hujaamua au kusema lolote.
Unapaswa kutambua pia maneno
unayoyasema au kuyaandika. Hii ina maana kwamba, kabla hujaandika au kusema
jambo, uwe unajiuliza kwanza. Kila linalotoka mdomoni mwako au mkononi
mwako(Kuandika) liwe limepata kibali chako baada ya kulitafakari na kuona
halitasababisha madhara kwako au kwa wengine.
Usizungumze kwa sauti ya juu
sana au ya chini sana wala usikubai kuchotwa na mtu anayefoka, nawe ukaanza
kufoka. Wacha anayefoka afoke huku ukijua wazi kwamba, anajiumiza bure, huku
wewe ukiwa huna haja ya kujiumiza. Kumbuka kwamba, kufoka ni kujitetea kwa
sauti kuliko mantiki. Usikubali kuwa dhaifu wa kiwango hicho.
Jaribu kutafuta muda, tuseme
wakati wa mapumziko la mchana. Tafuta mahali palipotulia, kaa hapo na kujaribu
kupeleka mawazo yako kwenye eneo lenye mandhari inayopendeza. Yapeleke hapo,
yakae kwa muda wa kutosha. Kama siyo mandhari, basi kumbuka tukio lolote huko
nyuma ambalo liliwahi kukufurahisha sana. Liweke mawazoni mwako kwa muda wa
kutosha.
Jaribu kuweka mawazo yako
yote kwenye kile unachokifanya kwa wakati huo. Hii itakuwezesha kutokuingiza
mawazo yenye kukera kwenye mfumo wako wa kufikiri.
Badala ya kupoteza muda na nguvu
kwa kujiuliza sababu za watu kufanya mambo fulani dhidi yako au kuhusu tabia
usizozipenda kwa baadhi ya watu, ni botra kuweka nguvu na mawazo yako kwenye
namna utakavyoweza kuboresha vitendo vyako.
Kabla hujazungumza na mtu
anayekukera au unayemwogopa ama pengine usiyempenda, pumua polepole kwa kina,
ukivuta pumzi ndani na kuzitoa nje, kiasi cha mara tatu na tengeneza picha
kwenye mawazo yako, ukijiona kuwa mnazungumza kwa amani na upendo na mtu huyo.
Kwa kufanya haya na baadhi
yake utamudu kukabiliana na watu na mazingira ambayo hayakuridhishi kazini
kwako au hata nyumbani na kwenye mkusanyiko wa watu ambao unapaswa kuwa nao.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza
zaidi kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.