google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jun 25, 2015

Sababu 10 Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.

No comments :
Mara nyingi huwa inakadiriwa kuwa biashara nyingi mpya zinazoanzishwa, huwa zinajikuta  zinakufa kabla hazijafikia miaka mitano na chache huwa ndio zinazoendelea baada ya hapo. Kufa huku kwa biashara hizi huwa hakuji kwa bahati mbaya, bali huwa kunatokana na sababu kadhaa ambazo pengine huwa zinatokana na wajasiriamali wenyewe au nje ya wajasiriamali. Ni muhimu kujua sababu zinazopelekea biashara nyingi zife kabla hazijafikisha miaka mitano, ili kama upo kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ama upo kwenye biashara usije ukafanya makosa hayo na kujikuta umeua biashara yako.

Hizi Ndizo Sababu 10  Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.

1. Usimamizi mbovu.
Hili ndilo kosa kubwa huwa linafanyika kwa biashara nyingi na matokeo yake ni kuwa ni biashara za kawaida ambazo hazina mafanikio makubwa sana na mwisho wa siku kufa kabisa. Kunapokosekana usimamizi mzuri na wa kutosha, mara nyingi biashara huanza kujiendea kiholela ama kwa mazoea ya kawaida tu, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara. Ni muhimu kwa biashara ikawa na usimamizi mzuri na mipango iliyotulia ili iweze kuleta faida na mafanikio makubwa, vinginevyo itakufa.



2. Kukosekana kwa ung’ang’anizi.
Mara nyingi huwa inachukua muda mrefu kidogo kwa biashara mpya, kuweza kukuletea faida kama ulivyokuwa umepanga. Katika kipindi hiki huwa ni kipindi kigumu kwa wajasiriamali wengi, kwani ni kipindi ambacho biashara huwa inajiendesha kwa faida kidogo sana na uvumilivu wa hali ya juu huwa unahitajika. Hapa ndipo, biashara nyingi mpya huwa zinakufa ama kushindwa kuleta mafanikio makubwa, kutokana na kukosekana kwa ung’ang’anizi ambacho huwa ni kitu muhimu sana.


3. Kuweka biashara  katika eneo lisilo sahihi.
Hii ni moja ya sababu muhimu sana ambayo mara nyingi huwa inapelekea biashara nyingi mpya kufa. Unapoweka biashara yako katika eneo lisilo sahihi, mara nyingi kitakachotokea utaanza kukosa wateja na utajikuta unabaki kulaumu kuwa biashara hiyo hailipi au haifai kumbe eneo uliloweka ndilo sio sahihi. Ili kuepuka hili, ni muhimu sana kuiweka biashara yako katika eneo lililosahihi ambapo una uhakika unaweza kupata wateja, ambao watasaidia kuifanya biashara yako kuwa hai.

4. Biashara inakuwa haitatui matatizo mengi ya watu.
Lengo kuu la biashara sio kupata faida pekee, bali ni pamoja na kutatua matatizo ya watu. Kwa jinsi biashara inavyozidi kutatua matatizo mengi ya watu ndivyo inavyozidi kupata wateja wengi na faida kuwa kubwa zaidi. Hakuna biashara yoyote duniani ambayo imeendelea bila kutatua matatizo muhimu ya watu. Kama unataka kufanikiwa na kupiga hatua kwa biashara unayofanya,  ni lazima biashara yako itatue matatizo ya watu kwa sehemu kubwa.

5. Kushindwa kujifunza kutokana na makosa.
Ni ukweli usifiochika wajasiriamali walio wengi huwa ni watu wa kufanya makosa katika biashara zao. Lakini, pamoja na makosa hayo kitu pekee ambacho huwa kinawafanya wananyanyuka na kusonga mbele ni kile kitendo cha kuchukua hatua ya kujifunza na kujirekebisha kutokana na makosa hayo. Tatizo walilionalo wajasiriamali wapya, huwa ni wazito kujifunza kutokana na makosa na kujikuta ni watu wa kurudia makosa yale yale yanayopelekea kuua biashara zao.

6.Kukabiliwa na ushindani mkubwa.
Biashara nyingi mpya huwa zinashindwa kufanya vizuri sokoni kutokana na kukutana na ushindani wa hali ya juu. Kunapokuwa kuna ushindani wa kisoko, halafu wewe ukiwa kama mjasiriamali ukashindwa kusoma nyakati za jinsi gani unaweza kukabiliana hali hiyo, uwe na uhakika biashara yako haiwezi kufanikiwa sana, zaidi baada ya muda itaanza kupotea polepole na mwisho ni kufa kabisa.

7. Kutokuwa na mtaji wa kutosha.
Kutokuwa na mtaji wa kutosha katika biashara, hii pia huwa ni sababu mojawapo inayopelekea biashara nyingi mpya kufa mapema. Mtaji huwa unahusika sana hasa pale unapohitaji kuongeza pengine bidhaa ili kuweza kukabiliana na soko na wakati huohuo unakuwa hauna pesa ya kutosha. Inapotekea hali hii ya kukosa mtaji wa kutosha kwa biashara unayoifanya, hapo ndipo huwa mwanzo wa kushindwa kwenye ushindani na biashara huanzia kuyumbia hapo na baadae kupelekea kufa, kama jitahidi nyingine za ziada zisipofanyika.

8. Kunafanya biashara na watu ambao sio sahihi.
Ili biashara yako iweze kuleta mafanikio makubwa unayotaka, ni muhimu kwako kuwa na timu sahihi utakayoshirikiana nayo kukuletea mafanikio. Kwa kawaida huwa hakuna mafanikio makubwa ya mtu mmoja, ni vizuri ukashirikina na timu uliyonayo katika biashara yako ili kuleta mafanikio makubwa. Inapokosekana timu ya uhakika katika biashara, hii ndiyo huwa sababu mojawapo inayosabbisha biashara nyingi mpya kufa. 

9. Mipangilio mibaya ya bei.
Mara nyingi biashara nyingi zinazoanza huwa zinamipangilio sio mizuri ya bei kitu ambacho husababisha kuwachanganya wateja. Hili huwa linatokea pengine kutokana na kupanga bei ya bidhaa, pasipo kujali ama kuangalia ubora wa bidhaa husika, hali ambayo husababisha wateja kuingiwa na shaka na kuanza kuhama kidogo kidogo, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara kuweza kuendelea.

10. Kukosa ushauri mzuri wa Kibiashara.
Mjasiriamali unapokosa ushauri mzuri ambao ungewezakukusaidia kuifanya biashara yako ikawa hai, kinachotokea hapo ni kuua biashara. Biashara nyingi huwa zinakufa kwa sababu ya kupokea ushauri wa kila aina na kuufanyia kazi hata kwa watu ambao sio wazoefu sana wa biashara husika. Kama unataka biashara yako iweze kusonga mbele na kuleta matunda acha kupokea ushauri wa kila aina, vinginevyo utaua biashara yako.

Mwisho, zipo sababu nyingi zinazopolekea biashara nyingi mpya kutoweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa na kupelekea nyingi kuweza kufa hata kabla ya kufikisha miaka mitano. Kwa kuanzia, hizo ndizo baadhi ya sababu zinazofanya biashara nyingi kuweza kufa na kushindwa kusonga mbele kabisa. Ni muhimu kuweza kujifunza na kuchukua hatua zitakazotusaidia kuepuka makosa hayo na kuweza kufanikiwa.

Nakutakia ushindi katika biashara yako iwe ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa zaidi, yatakayoboresha maisha yako kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,




No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.