Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Saturday, June 6, 2015

Mambo 12 Ya Kuzingatia Kama Unataka Kujiajiri.

No comments :
Ulishawahi kufikiria kujiajiri wewe mwenyewe katika maisha yako? Hili ni swali ambalo litakuwa linakuja kwako kila utakapokuwa unalalamika kukosa kazi uliyoisomea. Kila mmoja wetu amezaliwa na uwezo huu wa kujiajiri, ingawa wengi wetu huwa siyo rahisi kutambua uwezo huo na kujikuta ni watu wa kukimbilia kazi za wengine.

Ikumbukwe kuwa tumezaliwa na shauku, kiu, kufanya mambo ya hatari, uvumbuzi, akili na vitu vingine vingi ambavyo huonyesha wazi kuwa mtu hawezi kufundishwa ujasiliamali bali uko ndani yake kiasili, kinachohitajika ni yeye tu kujiweka katika mazingira ya kuruhusu akili yake kutatua tatizo lililojitokeza sehemu husika.

Kwa kadiri jinsi mtu anavyoifikirisha akili yake katika kutaka kujiajiri, ndivyo anavyapata majibu na mafanikio zaidi. Kwa nini uteseke kwa kujiajiri wakati uwezo wakujiajiri unao na unaweza kufanikiwa sana. Hapa katika makala hii utajifunza mfululizo wa mambo unayotakiwa kuyazingatia kama kweli una nia ya kujiajiri na kuiamsha hamasa ya ujasiriamali iliyo ndani yako:-

1. Jenga nidhamu:
Unapotaka kuwa mjasiriamali ni lazima utengeneze nidhamu yako ya kazi.
Kabla hujaanza kuingia katika hatua ya kujiajiri ili uepuke hatari ya kupoteza kila kitu jiulize kama una nidhamu ya kutosha kuingia katika hiyo shughuli. Huwezi ukawa mjasiriamali ambaye hauheshimu hata muda wako wa kazi. Hii itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa. Kujenga nidhamu, hili ndilo jambo la kwanza la kuzingatia kama unataka kujiajiri.2. Tambua jamii inahitaji nini.

Kama unataka kuwa mjasiriamali ni lazima uwe na uwezo wa kuchemsha akili yako katika kuyasoma mazingira uliyopo yanahitaji kitu gani na wewe ili uje na utatuzi wake. Lenga eneo moja ambalo unaona kweli lina uhitaji na unaweza ukaja na utatuzi wake. Toa huduma ile muhimu ambayo jamii yako inaihitaji na siyo kinyume chake. Kwa kufanya hivyo utakuwa unajitengenezea sifa halisi ambayo mjasiriamali wa kweli anatakiwa kuwa nayo.

3. Tengeneza lengo
Kutengeneza lengo la biashara ni hatua muhimu katika hatua za kuwa mjasiriamali. Lengo hili uliweke katika maandishi na litakusaidia katika kuwashawishi watu kukusaidia mtaji. Mara utakapokuwa umeandika lengo la biashara unayotaka kufanya usiweke maandishi hayo kabatini, anza kuyatafutia njia ya kuwa kitu halisi kutokana na hayo maandishi.Na pia lengo hili litakusaidia wewe usiyumbe na kutoka katika mstari wa lengo ulilojiwekea na litakuwa ni muongozo wako.


4. Jiunge na wajasiriamali.
Ikiwa unataka kuwa mjasiliamali ni muhimu kutafuta eneo ambalo wajasiriamali wengi wanakutana kujadiliana.Katika mazingira kama haya utakuwa kama yai linaloatamiwa na kuku ili lije kutoa kifaranga. Wengi wao huwa wamepitia magumu kufika walipofika na hivyo wakiwa wanasimulia habari zao watakufanya ujiamini kuwa na wewe unaweza.

5.Hojiana na wajasiriamali waliokutangulia.
Kama unataka kuwa mjasiriamali utapata faida kubwa sana kuzungumza na watu ambao tayari wanafanya ujasiriamali. Ukiwa na bahati kumpata mwenye moyo wa dhati wa ujasiliamali hatokuficha kitu ili kukusaidia ufikie ndoto yako. Kwani kiasili mjasiriamali huwa anajitoa kuisadia jamii yake na hana haja ya kuwa mchoyo wa maarifa.


6. Tengeneza marafiki.
Yeyote anayetaka kuwa mjasiriamali ni lazima atengeneze marafiki wengi wenye mtazamo  chanya kama yeye. Usiwe na marafiki ambao unatofautiana nao mtazamo, watakuwa wanakukatisha tamaa kwani kwao hilo wazo wanaona haliwezekani na watakwambia huwezi. Kauli kama hizo zitakukatisha tamaa na ukizingatia wazo lolote mwanzo huwa gumu na haliwezekani mpaka uanze kulifanyia kazi. Ndio ule msemo wa ukitembea na mwizi na wewe utakuwa mwizi unaingia hapa.

7. Tengeneza wazo rahisi kutekelezeka.
Kama unataka kuwa mjasiliamali ni vyema ukawa umechagua eneo moja maalumu la kulitafutia ufumbuzi na ambalo rahisi kutekelezeka na pia kuwa makini na hilo jambo unalotaka kulifanyia kazi uwe na uzoefu nalo japo kidogo, kwani huwezi kutibu ugonjwa usijua hata unakaa wapi.


8. Fanya bidii kuliko wengine.
Hapa lazima utambue kuwa kila mtu anaweza kuwa mjasiriamali, lakini tofauti huja katika bidii wanayoweka katika shughuli waliyochagua. Kama umejitolea kuwa mjasiriamali ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa bidii kuliko mtu yeyote yule.

9. Tafuta mshauri.
Ukitaka kuwa mjasiriamali ni vizuri ukawa na mtu anayekuongoza kwa mawazo kwani si kila wakati utakuwa unawazo sahihi. Si kwamba yeye ndio awe anakutengenezea wazo bali anaweza akawa anapitia wazo lako na kukushauri kama uboreshe au kuna vitu uondoe. Ikiwa utampata mshauri mzuri itakusaidia kupunguza hatari ya kuumia mapema. Kuwa makini na mtu utakayemchagua, uwe unamuamini na awe hana ushindani na wewe.


10. Hakikisha unafurahia:
Hapa ni lazima ujue, kama unataka kuwa mjasiriamali mzuri na utakayefanikiwa ni lazima ufanye kitu unachokipenda. Unapokuwa unafanya kitu unachokipenda unajitengenezea mazingira ya kuwa na furaha muda mwingi.

11. Fanyia kazi hatari unayoifahamu.
Sifa ya mjasiriamali wa kweli, ni yule asiyeingia kichwa kichwa kutaka kutatua tatizo pasipo kupiga hesabu za kutosha za hatari iliyopo. Mjasiriamali, kweli huwa anachukua hatari za jamii na kujibebesha yeye lakini anapaswa achukue hatari ambayo hesabu zake anazifahamu.


12. Hudhuria semina na makongamano
Wewe kama unataka kuwa mjasiriamali ni lazima utenge muda wako kuhudhuria semina mbali mbali, zinazohusiana na shughuli unazotaka kuja kufanya. Unapohudhuria maeneo kama hayo itakusaidia kutengeneza mtandao na watu wengine na hata kukutana na watu wanaoweza kukusaidia kufika unapotaka.

Kwa wale wote wenye mawazo ya kutaka kujiajiri, hizo ni baadhi ya hatua ambazo unaweza kuzitumia katika kufikia ndoto yako. Unaweza kuvitumia vidokezo hivyo kukusaidia kutimiza ndoto zako.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio ya kibiashara iwe ya ushindi kwako, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

MAKALA HII IMEANDIKWA NA FRANK VICTOR WA LISHA UBONGO.


.


No comments :

Post a Comment