Jun 11, 2015
Kama Hujui, Akina Misifa Wote Hutafuta Kile Walichokosa Utotoni.
Na
Deogratius Gunju, Mbeya.
Kuna wakati nilipouwa
nikisomea ualimu siku za nyuma, nilikwenda kwenye shule moja ya sekondari
wakati wa kile tulichokiita field,
yaani mazoezi kwa vitendo. Nilipangiwa darasa ambalo kwa pale shule, mkondo huo
huwa darasa ni kwa wale wasio na uwezo kimasomo. Ilikuwa ni darasa la C.
Kwa kweli ile siku ya awali
tangu kuanza mafunzo ya ualimu wa diploma, ilitaka kunifanya nichukie Ualimu. Na chanzo ilikuwa ni mwanafunzi mmoja ambaye
kwa kweli aliniendesha.
Mwanafunzi huyu alikuwa ‘mjuaji’
sana, kwani kila nikifundisha, yeye alikuwa akizungumza au kujigeuza mara huku
mara kule . Awali nilijifanya sioni, lakini baadaye ilibidi nimuulize sababu ya
kufanya vile. Badala ya kujibu kwa adabu alibetua mdomo na kusema, ‘basi
yameisha, endelea.’
Hadi kumaliza kipindi cha
dakika 40 nilikuwa nimechoka, nilipotoka hapo darasani, nilikwenda kusoma
kuhusu saikolojia ya watoto zaidi. Nilikuja kugundua kuwa, mwanafunzi Yule alikuwa
akitafuta au kutafuta wengine wamjali, akitaka kukubaliwa na wengine, akitafutwa
kuonwa na wengine na uwepo wake kuthibitika.
Niliposoma pia sababu za
mwanafunzi kama yule kutafuta wengine kuweza kumjali sana kwa kiwango kiasi
kile. Nilijitahidi kusoma ili niweze kujua namna ya kuweza kumsaidia au kwenda
naye vizuri bila kukwaruzana.
Ukweli ni kwamba, kila mmoja
wetu anapenda kuona wengine wakimjali au kumkubali, lakini tunaweza kusema
wengine kumwona. Kutaka wengine watujali ni jambo muhimu sana kwa karibu kila
binadamu. Kuna wataalamu wanaodai kwamba, hitaji hili ni muhimu, sawa kabisa na
chakula au hewa maishani.
Kila mmoja wetu, hujitahidi
sana kutafuta wengine wamjali au kumwoa kwa njia mbalimbali , bila kujali kama
anaita jambo hilo kutafuta wengine kumjali au anaita vingine. Lakini, pale haja
ya wengine kutujali au kutuona, kutambua uwepo wetu mahali inapopindukia
mipaka, hapo tunasema kuna tatizo.
Siyo tu yule mwanafunzi
aliyenichefua siku ile ya kwanza kwangu kuingia darasani, bali kuna watu wengi
ambao hutafuta sana kuonwa na wengine, hutaka wengine kuwajali na kutambua
uwepo wao.
Kuna watu ambao hukera sana
kwa sababu ya kile kitu ambacho tunakiita kutaka au kutafuta sifa. Hawa ni watu
ambao wanapenda kuonwa wao ni wa kwanza kwenye kundi la watu na wanataka watu
wengine wawatambue au kuwajali wao zaidi.
Unaweza kukuta watu wote
kwenye kundi wamekubaliana na mawazo ya mtu Fulani. Lakini mtu mmoja tu ndiye
atakayebisha, tena kwa nguvu sana. Siyo kwamba anabisha kwa sababu mawazo yake
yana mantiki, hapana, hayana kitu chochote, bali anachotaka yeye ni sifa, ili
watu wamtambue kwamba yupo.
Kuna watu ambao
hawajahusishwa kwenye mazungumzo ya watu wengine, lakini hujiiingiza kwenye
mazungumzo hayo na kuyanunua, hasa kama ni mazungumzo ambayo yatawafanya watu
wengi kuwasikiliza. Hebu jaribu kuchunguza abiria kwenye mabasi ya daladala
mijini, kuna watu ambao huwa wako tayari kununua ugomvi usiowahusu ili watu
wengine wawaone kuwa wapo.
Kuna watu wengi ambao hubisha
chochote, mahali popote, siyo kwa sababu wanajua zaidi au wanaleta mawazo mapya, hapana. Hubisha kwa sababu,
wengine wajue kwamba wapo.
Watu hawa, ni matokeo ya
malezi mabovu au ya wazazi ambao hawakuwa wakijali kuhusu watoto wao. Watoto wanapokuwa
kwenye umri fulani na hasa kuanzia miaka miwili (Kwa wenye uwezo mkubwa kiakili)
huanza udadisi na pia kutafuta kufanyiwa tathimini kwa kile wanachokifanya
katika maisha yao hayo ya utotoni.
Mtoto anaweza kupanga
maboksi na kumwita mama au baba kutazama alivyofanya. Wakati mwingine mzazi ana
shughuli zake na hivyo kumpuzia mtoto. Hii inapotokea sana, mtoto hukua akiwa
anatafuta mtu wa kumjali, mtu atakayeonesha kwamba, anajua kuwa amefanya jambo fulani.
Kwa hiyo, mwalimu
anapofundisha darasani, kijana husukumwa na kutaka kufanya jambo ili usikivu
kwa wengine uweze kwenda kwake. Anajaribu kwa nguvu zote kutafuta kile ambacho
baba au mama yake hakumpa utotoni, yaani kujali alipohitaji mtu wa kumjali kwa
kile anachokifanya.
Tukikutana na mtu wa aina
hii tusikasirike sana kwa sababu, hata yeye yuko kwenye moto, anaumia,
anatafuta ahueni, ndiyo maana anahangaika kwa kiasi chote hicho. Tunaweza kuzungumza
naye kwa upendo kumwelimisha kwamba, hapaswi kuwa hivyo na kumwelezea sababu za
yeye kuwa hivyo.
Wazazi, kwa hali hiyo
wanashauriwa kuwa makini zaidi katika namna wanavyowatendea watoto wao. Mtoto akimwambia
mzazi, ‘baba, ona nimjenga nyumba,’ inabidi mzazi aangalie na kusema jambo,
hasa kumpa moyo. Anapompuuzia, ndipo ambapo kasoro kama hizi huweza kuzaliwa.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari ya mafanikio, ansante kwa kuwa msomaji mzuri wa DIRA YAMAFANIKIO, endelea kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza zaidi.
UNAWEZA
KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII DEOGRATIUS GUNJU KWA 0718 610 022
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.