Jun 19, 2015
Mambo 6 Yakukusaidia Kusonga Mbele Wakati Unapoona Mipango Yako Haiendi sawa.
Habari za leo mpenzi msomaji
wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO tunaamini ya kuwa umzima na unendelea vyema
na harakati zako za kuboresha maisha yako. Karibu tena mahali ambapo unapata
tena nafasi nyingine ya kuweza kujifunza mambo muhimu yanayoboresha maisha yako
kwa ujumla.
Katika makala yetu ya leo
tutaangalia mambo muhimu yatakayoweza kukusaidia kuweza kusonga mbele pale
ambapo unaweza ukaanza kuhisi umekwama au huendi mbele sana kama ambavyo
unataka ikutokee katika maisha yako. Kuna wakati katika maisha yetu huwa
tunajikuta yale mambo ambayo tunayafanya yanakuwa kama hayasogei ama kuna
kuzuiliwa fulani hivi.
Hali hii inapotokea kwa
wengi huwa wanahisi kukata tamaa na kushindwa kujua nini cha kufanya.
Kiuhalisia, unauwezo wa kusonga mbele zaidi katika maisha yako haijalishi ni
nini kinachokutokea katika maisha yako. Uwezo wa kuishi maisha ya ndoto yako
unayoyataka unao na hilo linawezekana kikubwa kwako ni kuchukua hatua ya kuamua
kuwa hilo linawezekana.
Kama nguvu ya maamuzi na
uwezo wa kusonga mbele unao ni kipi kinachokukatisha tamaa na kuona kuwa huwezi
kusonga mbele tena? Ni vizuri kwako ukaweza kukumbuka mambo muhimu yanayoweza
kukusaidia katika kipindi kigumu ambacho unahisi mipango yako haiendi sawa. Huu
ni uamuzi wako ambao unaweza kuufanya sasa ili kuweza kubadilisha maisha yako.
Mambo yapi ya kukusaidia Kusonga mbele?
Haya
Ndiyo Mambo 6 Yakukusaidia Kusonga Mbele Wakati Unapoona Mipango Yako Haiendi
sawa.
1.
Tambua Ni wakati wa kufanya mabadiliko.
Hili ni jambo mojawapo
muhimu sana la kukumbuka ambalo litakusaidia kusonga mbele ikiwa utaelewa kuwa
unahitaji kufanya mabadiliko tena ya haraka. Mambo yako kutokwenda vizuri hiyo
ni ishara tosha kwako kuwa ipo sehemu kuna tatizo. Inawezekana ukawa unatumia
muda vibaya ama unafanya matumizi ya pesa vibaya ambayo yanakukwamisha kila
mara.
Kwa kujiangalia na
kujichunguza kidogo unaweza ukagundua hilo. Ukishapata majibu hutakiwi kuchelewa
ni kuanza kufanya mabadiliko mara moja. Kwa kufanya mabadiliko hayo utakuwa umejiweka
kwenye nafasi nzuri ya kuweza kuzidi kusonga mbele. Kinyume cha hapo utakuwa
unajikwamisha wewe mwenyewe.
2.
Unahitaji kuwajibika zaidi.
Kama mambo yako unaona
kabisa hayasogei ama yanataka kwenda hovyo, unahitaji kujituma zaidi. Huu ndiyo
ukweli ulio wazi ambao naweza nikakwambia kuwa ni lazima uukumbuke mapema na uufuate vinginevyo
utakuwa unajidanganya mwenyewe. Huhitaji kulaumu mtu, hali ama serikali ndiyo
iliyokufikisha hapo, zaidi kama unataka kufanya hivyo jilaumu wewe.
Maisha yako ni yako
mwenyewe. Hakuna mtu wa kumtwisha mzigo wa lawama zaidi yako mwenyewe. Inatakiwa
uifikie mahali pengine ukubaliane na ukweli kuwa unahitaji kutumia nguvu nyingi
sana katika kuwajibika na siyo kulaumu. Kama wewe utabaki tu unalaumu nakupa
uhakika hautaweza kufanikiwa hata ufanye nini.
3.
Unahitaji kusahau yote yaliyopita.
Inawezakana ukawa unakwama
katika maisha yako kutoka pengine na kukumbuka sana matukio yaliyotokea nyuma.
Kama ndivyo hivyo ilivyo kwako achana na hali hiyo na ujifunze kusahau kila
kitu ili kuweza kusonga mbele na kufanikiwa zaidi. Hautafanya kitu kama utakuwa
ni mtu wa kukumbuka tu yale ya nyuma zaidi.
Watu wengi ambao huwa
wanakwama wengi wao huwa wanatabia hii ya kushikilia sana vitu vya nyuma kitu
ambacho ni hatari sana kwa maisha yao. Kumbuka kuwa tunafanikiwa kwa kufanyia
kazi mipango tuliyonayo sasa na siyo iliyopita. Kwa maana hiyo acha kujenga
kumbukumbu hasa zile mbaya ambazo zilipita, sahau kisha songa mbele.
4.
Kuwa mvumilivu.
Kwa mabadiliko yoyote ambayo
huwa tunayataka yawe katika maisha yetu huwa ni lazima yanahitaji uvumilivu
tena wa hali juu. Unaweza ukawa unaona kama mambo yako yametulia lakini kumbuka
ni vyema ukajipa uvumilivu fulani hivi ambao utaweza kukusaidia kusonga mbele.
Wakati unavumilia huko kwa
kujipa muda, lakini hata hivyo kumbuka kutafuta hasa kujua nini hasa sababu
ambayo inaweza ikawa imepelekea mambo yako yasiende kwa kasi kama ulivyotarajia.
Ukiweza kuigundua hiyo sababu fanya mabadiliko muhimu yanayotakiwa na kisha
songa mbele.
5.
Kuwa mtu wa vitendo.
Badala ya kukaaa chini na
kuanza kuwa na visingizio kuwa umekwama pengine kutokana na hili hiyo tabia
achana nayo, badala yake kuwa mtu wa vitendo. Visingizio vyako havitaweza
kukusaidia chochote zaidi utashangaa vinakukuwamisha hata wewe mwenyewe bila
kujielewa.
Kama unataka kufanya kitu
kitakachokupa mafanikio katika maisha jifunze kutafuta njia na siyo visingizio
kama unavyofanya. Ni wakati umefika wa kufanya madiliko katika maisha yako na
siyi tu visingizio kila mara. Mtu anayekurudisha nyuma sana katika maisha yako
ni wewe mwenyewe. Ukiwa mtu wa vitendo na kuachana na visingizio utafanikiwa.
6.
Simamia maisha yako mwenyewe.
Acha kuwa na tabia ya
kuruhusu sana watu wengine waingilie maisha yako. Ni vizuri kuwa na mpaka
katika maisha yako. Siyo na maanisha usiwe mtu wa kutokushaurika, hapana.
Sikiliza maoni kama umuhimu upo kisha fanyia kazi yale unayoona yanakufaa.
Lakini usije ukaruhusu ama
ukajiona mkosefu ikitokea wamekukosoa eti ulikosea sana hili na lile ndiyo
maana husongi mbele. Jifunze kusimamia maisha yako wewe kama wewe, pia kuwa na
msimamo wako ambao unaweza kukusaidia kusonga mbele na siyo kubeba kila kitu
ili kuwaridhisha wengine hiyo itakwa siyo nzuri na haifai kabisa.
Kumbuka kuwa, kwa vyovyote
vile iwavyo wewe ndiyo mtu wa mwisho wa kutengeneza maisha yako kwa jinsi
unavyotaka iwe. Kwa pale unapohisi mambo ama mipango yako haikuendei sawia kama
ulivyokuwa ukitaka unaweza ukarejea katika mambo hayo muhimu kwako.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa
maarifa bora, lakini usikose kuwashirikisha wengine kwa ajili ya kujifunza
zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.