Jun 13, 2015
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukabiliana Na Changamoto Katika Maisha Yako.
Kuna wakati maisha yako yanaporomoka kutokana na kupatwa na
misukosuko ya maisha kama vile kufiwa na mke, mume au mtoto wako, kusalitiwa na
marafiki uliowategemea maishani mwako, kukimbiwa na mke au mume wako,
kufilisika, kupoteza kazi uliyokuwa ukiitegemea, au daktari kukuambia kuwa
ugonjwa unaokusumbua si rahisi kupona.
Hali hiyo inapokutokea, unajikuta unakata tamaa ya maisha na
kujiona kuwa hustahili kuishi katika dunia hii inayokuzunguka, lakini kumbuka
hiyo ni njia ya kupitia katika maisha haya tunayoishi. Hivyo ni vizuri
kumtafuta rafiki yako wa karibu au kiongozi wako wa dini kwa msaada zaidi.
Kwani viongozi wa dini mara nyingi wamekuwa washauri wazuri katika maisha yetu
ya kila siku.
Pia ukubaliane na hali ile ambayo huwezi kuibadilisha katika
maisha yako. Na kukataa kuendekeza nafsi yako katika hali ya kujisikitikia
kwani hali ya kujihurumia ni ugonjwa, kama vile acid. Hali hiyo itakuondolea
hadhi yako, itakuongezea sononeko na kukata tamaa. Itakuharibia uhusiano wako
na wengine. Itakusababishia hali ya kuwa na chuki. Hakuna jambo zuri
litakalokujia katika maisha yako kutokana na hali hiyo ya kujisikitikia.
Usichukue maumivu yako kwa wengine. Unaporuhusu maumivu huumizi
watu wengine bali unajiumiza wewe mwenyewe. Iambie nafsi yako kuwa unahusika na
vitendo au tabia zako mwenyewe. Hakuna atakayeiumiza nafsi yako ila wewe
mwenyewe. Usifanye ukaidi. Kubaliana na ukweli. Si wakati wote maisha
yanakuwa sawa na ya kuridhisha. Haijalishi hali inayokutokea katika maisha
yako, hali ya kukata tamaa, ndoto zako hazikutimia bado kuna tumaini katika
maisha yako.
Baada ya usiku inakuja siku mpya, baada ya kipindi cha baridi huja
kipupwe, baada ya mvua kubwa huja jua, baada ya dhambi huja msamaha, baada ya
maangamizo nafasi nyingine hutokea. Tuangalie mfano wa kijana mmoja wa
miaka 15 ambaye alidondoka kutoka juu ya mti na kuvunjika mgongo. Kwa bahati
aliokolewa akiwa mzima, lakini tokea kipindi hicho hakuweza kutembea tena.
Alitembelea kiti cha watu wenye ulemavu, katika maisha yake yote.
Katika kipindi kigumu kama hiki, inakuwa ni rahisi kujihurumia na
kujiona huna thamani tena katika maisha yako. Lakini haikuwa hivyo wa kijana
huyu ambaye alivunjika mgongo. Kwani hakujiweka katika hali ya unyonge. Alitaka
kuondoa hali aliyonayo na kuwa mtu mashuhuri. Kitu cha kwanza alicholenga
kukifanya ni kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Alichohitaji ni kupata
alama nzuri ili kufikia matarajio yake. Alimwambia mama yake anataka kuchukua
masomo ya sanaa na uchoraji.
Kijana huyo ndoto yake ya maisha bora ilianza kung’aa tokea hapo
na kufanikiwa katika maisha yake kutokana na kazi yake nzuri aliyoifanya. Kwani
alikuwa mchoraji mzuri kiasi kwamba aliweza kupata mialiko mbalimbali kwenye
vyuo vikuu vingine kutokana na bidii yake aliyoionyesha kwenye michoro
aliyoichora.
Baada ya masomo yake, kijana huyo alipata barua ambayo ilimtaka
kwenda kufanya kazi ya kuchora katika kiwanda cha nguo. Kazi hiyo
imempatia pesa nzuri na kuweza kuisaidia familia yake. Kazi yake imempatia
mahitaji yake yote ambayo alifikiri anahitaji. Anayapenda maisha katika hali
ile aliyonayo. Kijana huyo ni mmoja wa watu wenye matarajio makubwa ukiachilia
mbali hali aliyonayo ya kuwa mtu maarufu.
Kamwe usiishi maisha ya kushindwa. Unaona njia katika hali ya
ugumu unayokabiliana nayo. Siri ya ushindi ni hii, usijione mshindwa, usikubali
kushindwa kamwe usiishi katika hali ya kushindwa. Iambie akili yako kuwa
hukuumbwa ili uwe mtu wa kushindwa.
Huwezi kuwa mtu wa kushindwa kama hujaruhusu hali hiyo katika
maisha yako. Watu siku ya leo wanakata tamaa kutokana na sababu mbalimbali za
maisha. Katika mtiririko wa mambo hayo, hakuna haja ya kukata tamaa katika
maisha. Mtu ambaye hana kitu kinachofanya ajishughulishe anaona kuwa hana haja
ya kuishi. Kila mtu anahitaji kitu cha kushikilia fikra zake na kumpa
changamoto ili kufikia malengo anayotarajia.
Kumbuka, hakuna mafanikio pasipo kutaabika. Njia ya mapambano ni
njia ambayo inamwezesha mtu binafsi kuongezeka, kukua, kuwa na maendeleo. Kila
mtu anapitia maisha magumu kwa jinsi yake. Ni jinsi gani utakabiliana na hali
hiyo ili uweze kuondokana nayo? Ni kwa kukataa hali hiyo na kusonga mbele.
Fanya jambo fulani kubwa ambalo hujawahi kulifanya kabla ya hapo.
Unaweza kufanya mambo makubwa ambayo hukuwahi kuyafanya kabla ya hapo. Hiyo ni
kwa sababu maumivu yako yamegeuka kuwa nyota ya mafanikio, tumia fikra zako,
panua akili yako, jenga na tarajia. Uje na wazo kubwa, jambo fulani kubwa
kuliko ilivyo kawaida yako. Songa mbele usikate tamaa mpaka pale matarajio yako
yatakapotimia.
Tunakutakia mafanikio mema endelea kutembelea mtandao huu wa DIRAYA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.