Jul 30, 2015
Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu
Vitunguu ni zao la
pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania.
Afrika Mashariki, na Dunia Nzima.
Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa
mijini. Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga,
nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika
kutengeneza supu n.k
Aina Za kilimo Cha Vitunguu
Aina Za kilimo Cha Vitunguu
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili
- Green House
- Shambani
Kilimo cha kitunguu Green House
Kilimo cha vitunguu katika shamba la kawaida.
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.
Kutayarisha shamba
|
Shamba litayarishwe
sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
vitunguu kwa muda wa
miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
umwagiliaji. Matuta 1m
x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
majaruba yanarahisisha
umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.
Upandaji wa mbegu za vitunguu
Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.
Matunzo ya bustani ya vitunguu
- Umwagiliaji
Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba. Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua.
Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu. Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.
Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.
Hali ya hewa na maji
Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.
Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati
wa kukomaa na kuvuna vitunguu.
Aina za vitunguu
Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta. ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
- Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
- Msimu wa kupanda
- Uwezo wa kuzaa mazao mengi
- Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Mbegu bora
Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-
|
Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
- Chanzo cha mbegu
- Tarehe ya uzalishaji
- Tarehe ya kuisha muda wa
- Kifungashio cha mbegu.
Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja |
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama:
- ALPHA Seed Co, Popvriend,
- · Rotian Seed,
- · Kibo Seed,
- · East African Seed Company nk.
Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
Nikutakie siku njema na kilimo bora, katika makala ijayo tutaangalia magonjwa yanashambulia vitunguu na jinsi ya kuweza kuyazuia.
Makala hii imeandikwa na mtaalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com
,
Jul 28, 2015
Mambo Muhimu Ya kukusaidia Kukupa Furaha Katika Maisha Yako.
Mara
nyingi katika maisha yetu iwe kazini au katika jamii tunayoishi huwa ni watu wa
kukutana na hali tofauti tofauti ambazo wakati mwingine huwa zinatupa furaha au
huzuni katika maisha yetu. Lakini, pamoja na hali zote hizo kuweza kujitokeza
katika maisha yetu suala la kuwa na furaha ama huzuni huwa linabaki mikononi
kwetu sisi wenyewe.
Hii huwa
iko hivyo kwa sababu, sisi ndiyo huwa ni watu wa mwisho wa kuamua maisha yetu
tuyape furaha au huzuni. Kama tutakuwa ni watu wa kuchagua mambo ya kutupa
furaha basi ni wazi maisha yetu yatajawa na furaha, lakini pia kama tutakuwa ni
watu wa kuchagua mambo yakutupa huzuni pia maisha yetu yatakuwa ya huzuni
hivyohivyo.
Hivyo,
mpaka hapo unaweza ukawa unaona kuwa suala la kuwa na furaha au huzuni ni suala
linalolenga uchaguzi zaidi katika maisha yetu. Kitu cha msingi na cha
kuzingatia ili kuwa na furaha ni kuhakikisha wewe huathiriwi sana na mazingira
ya nje katika kukupa furaha yako. Sasa je, ni mambo gani ambayo wewe unatakiwa
kuyajua ili yakupe furaha ya kweli katika maisha yako?
1. Badili mtazamo wako jinsi
unavyo yaangalia mambo.
Mtazamo
ulinao juu ya maisha yako au jinsi unavyoyatazama mambo mara nyingi huo ndio
unaokupa furaha au huzuni katika maisha yako. Watu wegi huwa wanatabia ya kuangalia
mambo kwa mtazamo hasi sana. Kutokana na kuyaona mambo kwa mtazamo hasi ndivyo
hujikuta wakipoteza furaha katika maisha yao.
Kama
unataka kujenga furaha zaidi katika maisha yako kuwa na mtazamo chaya. Kama ulikuwa
unahisi na kuona fulani ni mbaya sana kwako badili mtazamo wako na anza
kumwangalia katika upande wa uzuri wake. Kwa jinsi unayozidi kuyaangalia mambo
mengi kwa mtazamo chanya ndivyo utakavyoweza kujikuta unafurahia zaidi maisha
na kuwa na furaha.
2. Fikiria majibu ya kile unachokitaka.
Wengi
wetu huwa ni watu wa kufikiria sana matatizo waliyonayo badala yakufikiria njia
za kutoka kwenye matatizo hayo. Hujikuta ni watu wa kuumia na kuwaza pengine
kutokana na ugumu wa maisha walionao. Kwa kuendelea kufikiria matatizo badala
ya kutafuta suluhu hivyo hupotezea wengi furaha.
Furaha
ya kweli katika maisha yako haiji tu kwa kufikiria sana matatizo uliyonayo, inakuja
kwa kutafuta suluhisho la matatizo hayo. Unaweza ukawa unajiona una mtatizo
mengi sana yanakufanya ukose furaha, hiyo ni kweli lakini kitu cha msingi
tafuta njia ya kuondokana na matazo hayo. Kwa kufanya hivyo utaijenga furaha
siku hadi siku.
3. Angalia mambo uliyoyafanikisha.
Inawezekana
ikawa unakosa furaha kutokana na malengo yako mengi kuona kama vile
hayajatimia. Kwa kuangalia hivyo hiyo itakuumiza sana. Ili iweze kuondokana na
hali hiyo jifunze sana katika maisha yako kuanglia mambo yale uliyoyafanikisha.
Hata kama ni kidogo lakini kama ulifanikiwa kwa namna fulani jipongeze kwa hayo
kwanza.
Kwa jinsi
utakavyozidi kuangalia mambo uliyofanikiwa nakuyaweka katika orodha ndivyo
itajikuta unaanza kupata nguvu ya kutenda zaidi na kuwa na furaha ambayo
ulikuwa unahisi pengine umeipoteza kabisa. Siku zote kumbuka hili, jifunze kuyaangalia
mambo uliyoyafanikisha. Mambo haya yatakusaidia kukupa furaha zaidi kuliko
unavyofikiri.
SOMA;
Haya ndiyo mambo mawili usipokuwa nayo makini yatakutesa na kukusumbua sana katika maisha yako.
4. Fanya mambo yatakayowapa furaha
wengine.
Katika
maisha yako kila siku fanya jambo, hata kama ni kidogo litakaloweza kumpa mwingine furaha na siyo
huzuni. Kama utamfanya mtu mwingne awe na furaha ni wazi kabisa lazima na wewe
utajikuta unafuraha. Hiyo ni kanuni rahisi kabisa ambayo unaweza ukawa
unaitumia kila siku katika maisha yako kukujengea furaha.
Watu
wengi huwa wanategemea kupata furaha kwa wengine wakati wao huwa hawatoi hiyo
furaha. Katika dunia hii mara nyingi unapata kile unachokitoa. Kama unatoa
mafanikio, tegemea kupata mafaniko. Kama unatoa furaha, tegemea kupata furaha
pia katika maisha yako. Hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda.
5. Ishi na watu wenye furaha.
Kama
utakuwa ni mtu wa kutafuta marafiki ambao muda mwingi wao ni watu wa huzuni,
usitegemee kuwa na furaha katika maisha yako. Furaha ya kweli utaipata katika
maisha yako kama utakuwa unazungukwa na watu wenye furaha zaidi. Unaweza ukawa
unaanza kushangaa kwa nini hii iko hivyo?
Mara
nyingi watu hawa watakusaidia kukuambukiza furaha hiyo nawe utajikuta ni mwenye
furaha kama wao. Lakini kama unaishi na watu hasi watu wa kuhuzunika mara kwa
mara, tambua utakachovuna hapo ni huzuni hizohizo. Watu wanaotuzunguka
wanaathari kubwa sana katika maisha yetu iwe katika suala la furaha au
mafanikio kwa ujumla.
6. Kila siku fanya kitu unachokipenda.
Inaweza
ikawa ni kitu kidogo tu na cha kawaida unachokipenda lakini kama unakipenda
kifanye kila siku kitakuongezea furaha. Kama wewe ni mtu wa kupenda kusoma
vitabu soma walau kurasa chache tu, utaweza kutimiza furaha yako. Kama umezoea
kuimba na unapenda kuimba, halikadhalika fanya hivyo hiyo itakuongezea furaha
pia.
Kwa kawaida
yale mambo tunayoyapenda hayo ndiyo huwa yanatuongezea furaha. Haijalishi mambo
hao ni madogo au mkubwa kiasi gani lakini ni muhimu sana kwetu kuyafanya kila
mara kama tu yanatupa furaha katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kufanya hivyo
tutakuwa tunayapa maisha yetu vile tunavyovihitaji na kujikuta ni watu wa
furaha.
Kwa vyovyote
vile iwavyo maisha yako unayouwezo wa kuyapa furaha ukiamua iwe hivyo kwako. Kwa
kutegemea na kuamini kila siku kuwa maisha yako ni lazima yawe ya furaha na
kufanya mambo yatakayokupa furaha katika maisha yako, hivyo ndivyo
iatakavyokuwa ni lazima utakuwa na furaha. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo muhimu
ya kukusaidia kukupa furaha maisha yako.
Ansante
kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, endelea kuwashirikisha wengine
kujifunza zaidi kila siku.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Jul 23, 2015
Nguvu Kubwa 5 Za Mafanikio Ulizonazo Ndani Mwako.
Habari
za siku rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO Kwa nguvu
zake Mungu naamini umzima na unaendelea na harakati nzima za kuhakikisha maisha
yako yanakuwa imara kufikia viwango vya juu vya mafanikio.
Karibu
tena katika siku nyingi nzuri ambapo tunakuwa katika darasa huru la kuweza
kujadili mambo muhimu ya kimafanikio. Leo katika makala yetu ya leo tutaangalia
nguvu kubwa za kimafanikio ambazo binadamu kama binadamu huwa anazo ndani yake
na zinapotumiwa kikamilifu huwa zinaleta matokeo makubwa ya kimafanikio kwa
maisha ya mtu.
Hizi
ni nguvu ambazo kila binadamu aliye chini ya jua huwa anazo ingawa kwa wengi inakuwa
ni ngumu kuweza kuzijua. Ni nguvu hizihizi ambazo zinapotumika katika maisha ya
wengine huweza kuleta maajabu na kuonekana maisha yao kama vile ya ajabu hivi
kumbe ni matokeo ya nguvu ambazo hata wewe unaweza ukazitumia na kufanikiwa.
Ni
nguvu ambazo huwa ni zaidi ya bomu la nyukilia zinapotumika kikamilifu. Na ni
nguvu ambazo nataka hata wewe uweze kuzijua ili kuweza kujiweka katika nafasi
nzuri yamafanikio. Ikumbukwe kuwa mara nyingi binadamu anapoambiwa kuwa ana
nguvu nyingi za ziada kwa wengi huonekana ni kichekesho na huwa hawaamini kitu kama
hicho.
Kwa
pamoja napenda nikushirikishe nguvu hizi muhimu kwako ambazo ukizitumia kwa
namna yoyote ile lazima uwe mshindi na uachane na maisha ya kulalamika ambayo
umekuwa nayo sasa kwa muda mrefu. Je, unajua ni nguvu zipi hasa ambazo unazo
ndani yako zenye uwezo wa kukufikisha kwenye mafanikio makubwa?
1. Nguvu ya Uzingativu.
Hii
ni moja kati ya nguvu kubwa sana uliyonayo ndani mwako lakini inapotumiwa huwa
ina uwezo mkubwa wa kukupa mafanikio unayoyataka. Mara nyingi unapokuwa unaweka
nguvu kubwa ya mawazo katika kitu kimoja na kuamua kuachana na vitu vingine
kabisa visivyoendana na kile unachokitafuta hapo ndipo unapokuwa unatumia nguvu
ya uzingativu kwa usahihi zaidi.
Nguvu
hizi za uzingativu unapozidi kuziweka katika jambo moja iwe malengo yako au
kitu chochote kile ni lazima uweze kufanikisha jambo hilo hata iweje. Itakuwa
ni ngumu sana kwako kuweza kushindwa kutokufanikiwa kama kweli utakuwa umeweka
nguvu yako ya uzingativu sehemu moja tu
na kutoisambaza sehemu nyingine. Hii ni siri mojawapo nzuri ya kimafanikio kama
utaitumia.
Unaweza
ukalijua hili zaidi kwa kuangalia mfano wa kioo ambacho kisayansi kinafahamika
kama lensi. Hiki ni kioo ambacho wengi tumewahi kukutana nacho tukiwa shuleni.
Kioo hiki huwa kinatabia na sifa moja kubwa ya kuweza kukusanya mwanga au miale
ya jua na kuweza kuiweka sehemu moja. Kama ilivyo kwa kioo hicho ndivyo ambavyo
nguvu ya uzingativu inavyofanya kazi kwetu na kuleta matokeo chanya ikiwa
itatumiwa vizuri.
2. Nguvu ya maamuzi.
Hii
pia ni moja kati ya nguvu kubwa iliyondani mwako lakini kwa wengi pia huwa
haijulikani. Kama ilivyo kwa nguvu ya uzingativu na jinsi ambavyo inavyofanya
kazi, nayo pia nguvu hii huwa ina matokeo yake ambayo yanaweza kuwa hasi ama
chanya kulingana na jinsi ambavyo ilivyotumika kila siku katika maisha yako.
Kumbuka
maisha yako, yapo hivyo kutokana na nguvu ya mamuzi ambayo uliweza kuifanya
katika kipindi cha nyuma. Kama uliweza kufanya maamuzi sahihi basi upo kwenye
njia sahihi ya kuelekea mafanikio, lakini kama maamuzi yako yalikuwa mabovu
ndivyo ambavyo na maisha yako yalivyo kutokana na maamuzi uliyofanya.
Haijalishi
unapitia kwenye utata au ugumu wa maamuzi kiasi gani, lakini kitu kikubwa
ambacho unatakiwa kukijua ni lazima uwe na maamuzi sahihi ambayo yatakusaidia
kukupa mafanikio unayoyahitaji katika maisha yako. Kinyume cha hapo utakuwa ni
mtu wa kupoteza muda wako bure kwani hutoweza kufikia mafanikio makubwa
unayoyahitaji katika maisha.
3. Nguvu ya ung’ang’anizi.
Katika
maisha yetu kuna wakati huwa tunakutana na vikwazo vingi sana ambavyo huwa vina
uwezo mkubwa wa kuturudisha nyuma. Vikwazo hivi huwa tunauwezo wa kuviweza
kuviepuka kwa kufanya kitu kimoja ambacho nacho ni kuweza kung’ang’ania mpaka
kuhakikisha kuona matokeo tunayoyataka katika maisha yetu.
Kwa
kung’angania jambo ambalo tunataka kulifanya ndivyo ambavyo huwa tunajikuta tunatumia nguvu hii ambayo huwa
tunayo ndani mwetu. Kumbuka huwezi kung’ang’ania kitu mpaka kuweza kuwa na
msukumo fulani ndani yako. Msukumo huo ambao unakuwa unauhisi unachemka ndani
mwako huo ndio nguvu mojawapo ya kimafanikio ambayo unakuwa nayo bila kujua.
Watu
wengi ambao unaweza ukawaona wanashindwa katika maisha yao kwa namna moja au
nyingine huwa ni watu ambao mara nyingi wameshindwa kutumia nguvu hii ambayo
ipo ndani mwao. Kwa kawaida unaposhindwa kutumia nguvu hii ya kung’ang’ania
changamoto kidogo tu ikijitokeza katika maisha ni lazima kwako uweze kushindwa
hata ufanyanye nini.
4. Nguvu ya kufikiri kile unachokitaka.
Ili
uweze kupata kile unachokihitaji hii ndiyo nguvu pekee unayotakiwa kuitumia.
Nguvu hii ni nguvu ambayo huweza kufanya kazi kwa kuweka picha kwenye ubongo au
akili yako yale mambo unayoyata tu. Kwa mfano kama unataka kujenga nyumba
nzuri, picha ipi inayokujia kichwani mwako? bila shaka ni aina ya nyumba
tofauti tofauti zinakuja kichwani mwako.
Picha
hizo unazoziona hizo ndizo nguvu ya kufikiri kile unachokitaka. Nguvu hii
wakati mwingine kitaalamu hufahamika kama ‘Power
of imagination’. Hivyo unaona kabisa hata wewe unaposema nataka gari nzuri,
kichwani mwako hayaji maneno G-A-R-I N-Z-U-R-I. kinachokuja ni picha za hizo
gari za aina tofauti.
Kufikiri
kile unachokitaka ni nguvu mojawapo muhimu ambayo binadamu anayo ndani yake na
inauwezo mkubwa wa kumsaidia kufikia mafanikio yoyote anayotaka. Kwa vyovyote
vile iwavyo katika maisha yako, jizoeze kuujaza ubongo wako picha ambazo
unataka zikutokee. Kwa kufanya hivyo ni lazima uweze kufanikiwa.
5. Nguvu ya hamasa.
Hii
ni nguvu ambayo huwa tunayo ndani yetu ambayo mara nyingi huweza kuipata
kutokana na kuona wengine ambavyo wananya vizuri katika mambo yao ama wakati
mwingine huwa tunaweza kuipata kupitia vitabu, mitandao ya kuhamasisha na
kuelimisha kama huu wa DIRA YA MAFANIKIO na semina au warsha mbalimbali.
Jaribu
kufikiri kidogo, bila haka unaweza ukawa shahidi mzuri wa hili hasa pale ambapo
huwa unajisomea vitabu vya mafanikio. Kuna msukumo au nguvu fulani ambayo huwa
unaipata kutoka ndani mwako, pengine kutokana na kile kilichoelezwa kuweza
kukugusa zaidi katika maisha yako. Nguvu hiyo mbayo huwa unaipata hiyo ndiyo
nguvu ya hamasa, ambayo ipo ndani mwako.
Kwa
kumalizia makala hii, tambua kuwa binadamu kama binadamu anazo nguvu nyingi
sana ndani yake ambazo akiweza kuzitumia zinaweza kumfanyia mambo makubwa na
kumfikisha kwenye kilele cha mafanikio. Hizo ni baadhi tu ya nguvu tulizonazo
ndani mwetu.
Tunakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza zaidi.
Kama
una maoni, maswali au ushauri karibu sana.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Jul 21, 2015
Kipaji Chako Ni Ajira Namba Moja.
Tunu
muhimu za mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya kila mtu ni vipawa/talanta.
Kwa bahati mbaya sana na pengine kutokujua umuhimu wa vipawa, watu wengi
hawatilii maanani vipaji walivyonavyo. Wengi wanaishi kwa kuiga maisha ya watu
wengine kana kwamba wao ni nakala ya wengine. Kipaji chako ni mtaji mkubwa kama
utaamua kukitumia vizuri ipasavyo. Kipaji chako ni fursa ya kufanikiwa
maishani. Ni daraja la maendeleo kwa binadamu yeyote yule.
Kipaji
ni umahiri wa kipekee aliouweka Mungu ndani ya akili ya mtu unaongoza usadifu
wa viungo na fikra zake kufanya jambo Fulani kwa upekee kabisa. Ni talanta
ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni ujuzi wa kuzaliwa nao, elimu
inakusaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake kwa ufanisi na kwa manufaa
zaidi. Kwa mfano, michezo mbalimbali, sanaa kama mziki, kuchora, kucheza mpira,
kuimba, kusanifu, kubuni program za kompyuta, mitandao, na wakati mwingine
kuchonga. Wapo watu ambao wana vipaji katika eneo mojawapo wanachotakiwa
kufanya ni kuvitumia vipaji vyao.
Watu
mashuhuri na wale waliofanikiwa sana ni wale waliotumia vipaji vyao vizuri.
Kuna mifano hai mingi kama Filbert Bayi wa Tanzania alitumia talanta yake ya
kukimbia mbio, wanamuziki kama vile Michael Jackson, Rose Muhando walitumia
sauti zao kufanikiwa. Na hata wachezaji maarufu wanatumia vipaji vyao kucheza
mipira na wanafanikiwa kuliko hata wasomi wenye shahada lukuki.
Wasanii
na wana michezo wengi ni miongoni mwa watu maarufu na matajri sana duniani,
japokuwa walio wengi hawana elimu kubwa kiasi cha kushangaza , walichofanya ni
kutumia vipawa vyao kama ipasavyo. Maana hata sukari iliyo katika chai bila
kukorogwa chai inaonekana haina sukari. Vivyo hivyo vipaji tunavyo, ili vifanye
kazi vizuri inabidi tuvikoroge.
Mungu
alituumba na vipaji na talanta nyingi tofauti ili tuvitumie kufanikiwa
maishani. Kila mtu ana talanta yake imejificha ndani ya umaizi wa akili yake.
Tunahitaji kuweza kuziibua talanta hizo
kule ziliko fichika, na kuzitumia huku tukibadili mitazamo na kasumba.
Huwa nasikitika sana kumsikia mtanzania anasimama kwenye chombo cha habari
akisema yeye ni maskini anahitaji msaada. Wakati huo kafunika talanta zake
kibindoni, na nyuma kaacha ardhi kubwa, misitu mingi na hata watoto wengi ambao
ni nguvu kazi muhimu katika kuchangia maendeleo.
Wapo
watanzania wanadiriki kusema kuwa “sisi tutaendelea kubaki maskini hivihivi” na
wengine wanadai umaskini wao ni mpango wa Mungu. Huu ni uongo na ni dhambi.
Mungu angetaka sisi tuwe maskini asingeweza kutupa ardhi kubwa, asingetupa mvua
nyingi na maji mengi, asingetupa samaki wengi, asingetupa ndege na wanyama
wengi wa mwituni. Asingutupa afya njema na nguvu. Mungu alitupatia vyote hivi ili
tuwe matajiri tuwasaidie na wale wanaoishi nchi zisizo na ardhi (mawe tu), nchi
zisizo na bahari, nchi zisizo na msitu, mto wala bwawa. Sisi siyo maskini
kamwe.
Na
kiongozi au mwanasiasa anayetamka Tanzania ni maskini(wakati yeye ni tajiri)
huyo ni mpotoshaji. Tusiwafundishe watoto wetu mtazamo hasi hata kama
tunachangamoto. Kuwa na matatizo ni sehemu ya changamoto za maisha, tunazipaswa
kuzikabili. Maana hakuna mtu au nchi inayojitosheleza. Ndio maana hata wao
walioendelea huko ulaya bado wanakuja kwetu kununua malighafi ili wakutumie
huko kwao.
Tena
nadhani hata walioita mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini(MKUKUTA)
walikosea sana. Ingefaa ukaitwa “mkakati wa kukuza uchumi na ustawi wa maisha
ya watu”. Kuutaja umaskini wakati tupo ndani ya utajiri mkubwa ni kujitafutia
laana ya kudumu .Maana kama tunakubali sisi ni maskini kamwe hatuwezi kuweka
mikakati ya maendeleo. Tunabaki na mikakati ya kimaskini.
Nafadhaishwa
na mtazamo unaotaka kuzoeleka hapa Tanzania miongoni mwa vijana kuwa mtu yeyote
akifanikiwa: kumiliki nyumba nzuri, shamba zuri lenye mavuno mengi, gari zuri,
kiwanda na hata kuwa na elimu nzuri anaitwa fisadi, yaani mwizi. Unakuta vijana
wenye nguvu wanapita makazi ya watu wenye nyumba nzuri wanasema “unayaona
mahekalu ya mafisadi” wakimaanisha kuwa kila nyumba nzuri, kiwanda kikubwa,
shamba kubwa ni la fisadi au mwizi. Kwao maendeleo ni wizi na siyo jitihada za
kazi. Hawa wamepotoka sana.
Umaskini
siyo mpango wa Mungu wala siyo ngozi ya kuzaliwa nayo isiyobadilika. Hata
vitabu vitakatifu kama vile bibilia na msahafa vimesema wazi kwamba umaskini
siyo mpango wa Mungu. Mungu anataka kila mtu aishi maisha mazuri yenye ustawi
huku akimpenda na kutii mwongozo wake. Kila binadamu anahitaji maisha bora. Kila
binadamu anahitaji kulala pazuri, kula vizuri, kusafri vizuri, afya bora,
kupata elimu bora, mazingira safi, kucheza pazuri na kufurahia maisha kwa
ujumla.
Watu
wanakuwa kwenye shida kama vile kuishi katika nyumba mbovu, na kula chakula
kibaya au kisichotosheleza siyo kwa sababu wao wanapenda, au kudhani kuwa
maskini ndiyo sifa ya uadilifu. La hasha ni kwa sababu hawana. Fikra za kuyaona
maendeleo yoyote ya mtu au kikundi cha watu ni ufisadi ni dalili kupoteza dira
na kukosa matumaini kuelekea ufukara wa kudumu na dhiki kuu.
Na
ukiona kijana mwenye nguvu anatamka kuwa hayo majumba ni ya mafisadi, fahamu
kuwa familia yake na jamii inayomzunguka iko msibani. Si tetei wizi ama ufisadi
na si sahihi kuwa mwizi au fisadi. Na ni dhambi hata kwa mungu wezi waadhibiwe
tena vikali.
Lakini,
pia sikubaliani na mtazamo kwamba kila anayefanikiwa ni mwizi au fisadi. Kuna
watanzania wengi tu ambao wanakesha, wanafikiri na kubuni mbinu za kufanikiwa
huku wakiongozwa na jitihada kubwa ya kufanya kazi na kuchangamkia fursa ndani
na nje ya nchi na kutumia pesa kwa kwa makini katka uwekezaji binafsi bila
ufujaji.
Hawatapanyi
mapato kwa starehe na kuulimbukia utandawazi. Kila senti yao inatumika kwa tija
na manufaa. Hawa wanastahili pongezi siyo kuitwa wezi. Kazi kubwa tliyonayo
hasa vijana ni kutambua vipaji vyetu na kuvitumia ipasavyo.Tpunguze kulalamika
tuongoze juhudi zetu katika ufanya kazi zaidi. Tutafanikiwa sana maishani.
§ MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTEMI ZOMBWE,
DAR ES SALAAM.
§ MAWASILIANO 0713 000027
Jul 3, 2015
Hatua Tano Muhimu Za Kuelekea Kwenye Mafanikio.
Mara
nyingi sana katika maisha yetu tumesikia maneno kama “nipe tano” “chukua tano”
maneno hayo yamekuwa maarufu na katika mazingira tofauti, yamekuwa yakiashiria
ushindi , au hali ya mafanikio au furaha baada ya hali fulani.
Vivyo
hivyo katika maisha yetu ya kutafuta kufanikiwa katika yale yote tunayoyafanya
kila siku viko vitu au hatua ambazo huwa zinatulazimu kuzijua au kuzipitia kama
kweli tunamaanisha na tunadhamiria hayo mafanikio tunayoyatafuta.
Watu
wengi hutamani mafanikio na kuyazungumzia sana katika maneno yao ya kila siku
lakini hawajawahi kuyaishi mafanikio hayo kwa sababu ya kutokuwa na dhamira
madhubuti katika kuyaelekea. Je, unajua ni hatua zipi muhimu za kuelekea kwenye
maisha ya mafaniko?
1.Kuwa na uwezo binafsi wa kuvikagua
vile ulivyo ndani yako.
katika
maisha yetu ya kila siku hatuna budi namna ya kujifunza kujikagua sisi wenyewe,
kuvikagua vile tulivyonavyo ndani yetu kwa sababu ni ukwelli kwamba pasipo
kujikagua sisi wenyewe basi hatutaweza kuyatambua mapungufu tulionayo na kama
hatutoyatambua mapungufu hayo hayatoweza kushughulikiwa na kuondelewa, maana
yake ni kwamba tutazidi kushi na upungufu wetu na hivyo kuathiri ufanisi wetu
na mwisho wake mafanikio yetu kwa ujumla yataathirika.
Labda
nikupe mfano wa mtu mwenye duka , mara kwa mara huwa na muda wa kuvikagua vitu
au mali aliyo nayo dukani kwake na hapa huweza kutambua nini kimepungua , nini
hakipo kabisa na nini hakipo kwa wingi. Katika kujikagua sisi wenyewe sio tu
tutapata uhakika wa vile tusivyonavyo
bali pia tutapata kufahamu vile tulivyonavyo kwa wingi. Jifunze kufanya
tathmini ya maisha yako kila wakati, tathmini matendo yako ya kila siku, maneno
yako ya kila siku, mitazamo yako ya kila siku, halafu angalia wapi kuna
upungufu na wapi kuna fursa.
2. Uwezo wa kuwa na msimamo.
Wengi
wetu tumeshindwa kuyafikia malengo tuliyowahi kujiwekea kwa sababu tu hatuna msimamo
katika vile tunavyoviamini kwa hiyo inakuwa ni rahisi kuyumbishwa na
kupeperushwa na kila upepo unaokuja upande wetu. Ili kufikia mafanikio
tunayoyatamani hatuna budi kuwa na misimamo fulani katika maisha. Naupenda msemo
unaosema kama huwezi kuwa na msimamo na chochote basi utachukuliwa na chochote.
Kama
wewe ni kijana na huna msimamo katika baadhi ya mambo basi ni rahisi kujikuta
unabebwa na mengi kama vile rushwa na ubadhilifu. Ni vyema kufahamu kila wakati
maishani kuwa kama huna msimamo katika ufanisi basi utaangukia katika uzembe na
kutokuwajibika na kama hautakuwa na msimamo katika kuhakikisha unafanikiwa basi
utaangukia katika umaskini.
3. Uwezo wa kupiga hatua.
Yamkini
unatamani sana kufanikiwa na kila siku unaongelea sana mafanikio, ni vyema
kujua kwamba mafanikio yetu hayaji kwa kuyatamani au kuyaongelea bali katika
uwezo binafsi wa kuamua kupiga hatua. Yawezekana upo katika chombo kizuri tu
cha usafiri lakini utajikuta unapitwa na kila mtu, hata wale wenye vyombo
vibovu vya usafiri nao watakupita kama utakuwa umekaa tu kwenye chombo chako
pasipo kuruhusu mwendo.
Chukua
hatua kuelekea mustakabali wako, angalia mbele yako unaona nini? Niniambacho
unakiona kwenye mustakabali wako? Nini ungetamani
ukipate kwenye mustakabali wako? Anza kufanya kila kinachohusika ili kuona hiyo
ndoto yako ikiwa dhahiri.
Anza
kupiga hatua ya kwanza na hatua nyingine zitakuwa ni rahisi kufuatia. Kamwe usitishike
na umbali unaouona kuelekea mustakabali wako, jinsi unavyopiga hatua ujasiri
wako unafunguka na kukua, kumbuka kuwa kila hatua unayoipiga hata kama ni ndogo
kiasi gani inakusogeza karibu na mustakabali wako.
4. Uwezo wa kujitengenezea sura ya
maisha yako.
Katika
maisha yetu ya kila siku ni ama uamue kuitengeneza sura ya maisha yako au
kuibomoa sura hiyo, wengine wetu maisha yetu hayajawahi kuwa na sura nzuri ya
kuvutia.
Sisi
wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kuamua kuitengeneza sura hiyo kuwa kama vile
tunataka iwe, ukiamua kukaa tu pasipo kufanya chochote basi umekusudia kwa
dhamiri halisi kuiharibu sura ya maisha
yako mwenyewe.
Ulimwengu
wa leo unabadilika kwa kasi sana, ili kuweza kubakia kwenye maana na wenye
umuhimu basi hatunabudi kuwezana na mabadiliko hayo. Kama hutoweza kuyaweza
mabadiliko ya karne hii basi mabadiliko hayo yatatuweza.
5. Uwezo wa kukikalia kiti na kuyaongoza
maisha yako mwenyewe.
Ziko
nyakati ambazo wengi wetu hatuwezi kufika tunapotamani kufika kwa sababu dereva
anayeendesha chombo chako siyo wewe, wakati huohuo unafikiria kuelekea pale
unapopatamani wewe.
Ni ngumu
katika maisha kama unaifahamu ndoto yako na unaiona kesho yako na unaitamani
sana kuifikia basi amua kukaa kwenye
kiti cha dereva wewe mwenyewe na kuendesha chombo kuelekea huko.
Watu
wengi siyo kwamba tumewakabidhi wengine udereva wa safari yetu kwa kujua bali
ni kwa kutokujua, mara unaona muelekeo wa safari siyo ule unaoutarajia, yamkini
sasa dereva uliyemkabidhi kiti anakupeleka kwenye ndoto yake na siyo ya kwako
tena.
Sasa
amua kuingia kwenye kiti cha dereva wewe mwenyewe, hayo ni maisha yako na siyo
mwingine. Kamwe usiache furaha ya mafanikio yako katika mikono ya mwingine. Kubali
na kuwa tayari kubeba majukumu. Kama unatokea unafanya makosa basi usijitetee
na kukwepa, chukua tano!
Tunakutakia kila la
kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO
kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTAALAMU WA
SAIKOLOJIA,
CHRIS MAUKI WA GAZETI LA MWANANCHI.
Jul 1, 2015
Mawazo Yako Ndiyo Nguvu Uliyonayo.
Upo uhusiano mkubwa
sana baina ya namna unavyofikiri, na jinsi unavyoishi. Kushindwa kwako,
hakutegemeani na nguvu yoyote ulivyonayo isipokuwa ufahamu wako. Kuanguka kwako
hakutegemei maadui wengi ulionao, isipokuwa aina ya mtazamo ulionao. Kurudi
nyuma kwako hakutegemei historia yoyote uliyowahi kuwa nayo, isipokuwa namna
unavyoendekeza mawazo yako ya kushindwa.
Naelewa kwamba panahitaji mjadala wa kina kuhusu kipi kinachomtawala mwenzie:
mawazo yetu ndiyo yanayotuongoza ama ni sisi ndio tunayaongoza mawazo. Hapo
inapidi tushukie penye uelewa na namna mawazo yetu yanavyojengeka vichwani
mwetu.
Kwa haraka haraka, nadhani, tuwaza vile tulivyoviingiza ubongoni iwe kwa hiari
yetu wenyewe ama pasipo hiari hiyo. Kwa maneno mengine sisi ndio watawala wa
mawazo yetu.
Hiyo ni kusema kwamba unavyojiona, ndivyo ulivyo. Ukijidharau, hakuna mtu
atakuja kukufanyia kazi ya kukuonyesha thamani uliyonayo. Ukianza leo kujiona
masikini, ni wazi kuwa akili yako itakubaliana nawe na kusema kweli, utakuwa
umeukaribisha umasikini wako kwa mikono yako miwili.
Ningependa kukuachia ujumbe huu mfupi na makini kwako utambue kuwa katika kila
unalojaribu kulifanya, dhania kwamba haiwezekaniki jambo hilo likashindwa kwa
namna yoyote. Kwa sababu, haiwezekani ukashindwa katika jambo lolote, isipokuwa
kama utakubali akilini mwako kwamba umeshindwa.
Achana na mawazo ya kushindwa shindwa. Achana na watu ambao hawaishiwi stori za
ubaya ubaya. Amua kuyaelekeza mawazo yako kwenye mafanikio. Kwa sababu mawazo
yako ndiyo nguvu yako kuu uliyonayo! Itumie nguvu hiyo! Ikusaidie kufanikiwa
zaidi.
Lakini pale
utakapoweza kujiona huwezi na umeshindwa kutumia nguvu hiyo basi huo ndiyo
utakuwa mwisho wa mafanikio yako wewe mwenyewe. Ni muhimu kulijua hili na
kutumia nguvu hizi kikamilifu kwa ajili ya mafanikio zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA
MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
MAKALA HII IMEANDIKWA NA CHRISTIAN BWAYA WA
JIELEWE BLOG
Huyu Ndiye Mtu Pekee Anayekufanya Ushindwe Katika Maisha Yako.
Habari
za siku ya leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Ni matarajio
yetu ya kuwa umzima wa afya na karibu sana katika siku nyingie ambapo unapata
nafasi ya kujifunza mambo muhimu ya kimafanikio. Katika makala ya leo tutaangalia
jambo muhimu la kujifunza kupitia simulizi liliyotolewa na mwandishi nguli wa
vitabu John Mason.
Katika
kitabu chake cha ‘Limitation is Imitation’ mwandishi huyu anaelezea hadithi ya kijana mmoja ambaye siku
moja aliweza kutoka na baba yake na kwenda kutalii katika eneo moja la mlimani
ambapo wote kwa pamoja waliweza kupata nafasi ya kupanda juu ya mlima huo.
Wakiwa
juu ya mlima ule kijana yule mdogo pengine kutokana na uchovu ilifika mahali
alitaka kudondoka yaani nikiwa na maana aliteleza na kutaka kuanguka chini. Kutokana
na hofu hiyo ya kutaka kudondoka chini kijana yule alijikuta akipiga kelele ‘Yaaaa!
Yaaaa!’. Kwa mshangao tena, kutokana na kelele hizo alizozipiga alishangaa
tena kelele hizo hizo za kwake zinasikika upande mwingine.
Kijana
yule kitu hicho kilimshangaza sana na kujikuta akimuuliza baba yake nini hicho
alichokisikia ambacho kilitoa sauti kama yake. Lakini kabla hajajibiwa na baba
yake swali lake, kijana huyu alishangaa tena maongezi hayohayo anayomuulizia
baba yake yanasikika upande wa pili tena. Hali hiyo ilizidi kumtia hofu zaidi
na wasiwasi mwingi na kuwa na kulikoni nyingi kwenye kichwa chake.
Baba
yake baada ya kuona hivyo aliamua kumwambia mtoto wake kuwa kitu hicho anachokisikia
kinafahamika kama mwangwi na kisha akamfafanuliwa jinsi inavyokuwa na kwa
sababu gani huo mwangwi huo unatokea na kisha mwisho kabisa akasisitiza kwa
kijana wake kuwa hivyo ndivyo maisha yetu huwa yako hivyo kama mwangwi.
Kijana
alistaajabu na kushangaa, lakini aliambiwa na baba yake huo ndiyo ukweli
anaotakiwa aujue kuwa maisha yetu
yanakuwa kama mwangwi ama sauti inayojirudiarudia kwa sababu yanatupa kila kitu
kama tulivyokitoa. Kama utatoa upendo jiandae kupokea upendo, kama huwa unatoa mafanikio
na kufanya kila kinachoendana na mafanikio jiandae kupokea mafanikio pia katika
maisha yako. Kwa tafsiri hiyo maisha yako ni mrejesho wa vitendo vyetu
tunavyovifanya katika maishayetu.
Maisha
uliyonayo siyo ajali kama unavyofikiria, ni matokeo ya mrejesho wa yale mambo
unayoyafanya. Jaribu kuangalia na kujichunguza kidogo utagundua ukweli wa hilo
kuwa unavuna ulichokipanda huo ndiyo mrejesho ninao taka kukwambia. Hivyo kama
unajiona maisha yako ni mabaya acha kulaumu watu wengine, mtu wa kwanza kumlaumu
ni wewe mwenyewe kwani huyu ndiye mtu pekee anayekufanya ushindwe katika maisha
yako.
Kuna
wakati pia mwandishi Stewart Johnson aliwahi kusema kuwa kitu
kikubwa katika maisha yetu ni siyo kushindana na wengine ni bali kushindana
sisi wenyewe na kuwa bora zaidi na zaidi siku hadi siku, hili ndilo jukumu na
lengo kubwa ambalo tunatakiwa tuwe nalo katika maisha yetu. Na huu ndiyo ukweli
usiopingika unaotakiwa uujue ili kuboresha maisha yako.
Katika
maisha yako kama unataka mafanikio zaidi jifunze kutambua kwamba maisha yako ni
kama mwangwi. Ukishajua hilo lipia gharama za mafanikio hayo kwa kufanya
vitendo ambavyo vitakufanya lazima ufanikiwe. Acha kujidanganya wewe mwenyewe
na kuamini kuwa yupo ‘mchawi’
anayeweza kukwamisha mipango na malengo yako.
Hakuna
mtu hata mmoja ambaye anaweza kukuharibia maisha yako ni wewe mwenyewe kutokana
na vitendo vyako. Jifunze sasa kutokuwaangalia wengine kama chanzo cha matatizo
yako, badala yake anza kujiangalia wewe kwanza kuwa ndiye unayesababisha
ushindwe kufanikiwa. Hakuna mtu anayekufanya ushindwe zaidi ya wewe mwenyewe
kujiaminisha kuwa huwezi na unajikuta umeshindwa kweli.
Kumbuka
siku zote maisha yako yapo hivo kutokana na mambo yale uliyoyapanda, ama
uliyoyatoa. Hakuna kujuta wala kulalamika kwa kuwa tunapata vitu vinavyotokana
na sisi wenyewe ni matokeo ya matendo yetu ambayo tunayafanya mara kwa mara na
kila siku. Hivyo ni rahisi kusema kuwa katika maisha yetu tunavuna kile
tulichokipanda na siyo vinginevyo.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kwa kujifunza na kuelimika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)