Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, June 5, 2015

Jiulize “Kwa Nini Maisha Yangu Yako Hivi Yalivyo”

No comments :
Ni siku nyingine tena msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO tunapokutana tena ili kujifunza vitu vya msingi ambavyo vinaboresha na kubadilisha maisha yetu. Mojawapo ya mambo  ya kuzingatia  sana ni kutafakari juu ya maisha unayoishi ili kuona kama uko sahihi au la. Na pale penye makosa unalazimika kurekebisha kwa haraka sana.

Huwezi ukawa unakimbia shule halafu utegemee matokeo mazuri darasani. Huwezi kuwa hujali kazi halafu ukategemea utaendelea kuwa na mafanikio mazuri sehemu za kazi. Si ndiyo jamani? Huwezi ukawa hujitumi, mwongeaji sana katika maisha yako na hakuna hatua muhimu unayoichukua halafu ukategemea pia mafanikio makubwa.

Maisha yanatuhitaji tuwe ni watu wa kujiuliza mara kwa mara kwanini maisha yangu yao hivi ili kuyaboresha zaidi. Hatuhitaji kuwaogopa ama kuwahofia sana watu kwa sababu ya pesa, madaraka au kwa sababu nyingine unazozijua wewe na kusahau kuchukua jukumu la kujifunza. Kama watu hao wana vitu vya msingi ni vyema tukajifunze badala ya kuwaogopa.


Ni makosa sana kuamini kuwa wewe eti hufai labda ni kwa sababu umezaliwa katika familia maskini, hujasoma ama mlemavu. Kusoma ni suala moja, kufanikiwa na kuweza kuishi vizuri ni suala lingine lingine tofauti, ambalo hata linaweza kuwasumbua wasomi zaidi wa elimu ya juu kote duniani.


Ninachokifahamu mimi duniani kote hakuna mtu mwenye elimu ya uprofesa ambaye ni tajiri. Matajiri wote ni watu wa kawaida tu, kama wewe ambao hawajasoma sana. Kilichowafikisha hapo na kuwa matajiri ni kutokana na kuchukua jukumu la kujifunza vitu vipya na kujiuliza kila mara na kila wakati kwa nini maisha yao yako hivyo.

Kuwa na maisha bora ni pamoja na kujiwekea mikakati imara kila mara. Mikakati hii utaipata tu ikiwa utakuwa ni mtu wa kujiuliza swali hili mara kwa mara la kwanini maisha yangu yako hivi. Kwa kujiuliza swali hilo ndivyo utajikuta unpata nguvu ya kuboresha maisha yako kabisa siku hadi siku. Wengi wanakuwa maskini hasa kwa sababu ya kushindwa ama kuogopa kufanya kitu fulani, ambacho hata kingeweza kuwa rahisi kwao.


Mara nyingi nimekuwa nikilisema hili mara kwa mara kila ninapopata nafasi ya kuongea na watu wengine kuhusu maisha ya mafanikio kuwa watanzani wengi wanaishi maisha magumu kwa sababu ni waoga wa kujaribu mambo katika maisha yao. Na huu ndiyo ukweli. Kama unafikiri natania kwanza anza kujichunguza wewe, utaelewa vizuri ninachosema hapa.

Kwa kujiuliza kwa nini maisha yangu yako hivi, hii ni siri mojawapo muhimu itakayoweza kukufikisha kwenye maisha ya mafanikio. Kwa nini iko hivyo? hiyo ni kwa sababu  kila mara utakuwa unagundua kitu gani unachotakiwa kuboresha katika maisha yako ili  kusonga mbele.

Kwa hiyo badala ya kukaa na kuanza kulalamika chukua hatua zaidi ya kuweza kutafakari juu ya maisha yako. Weka mikakati imara na tambua kuwa kiongozi na mwamuzi wa mwisho juu ya maisha yako ni wewe mwenyewe. Kulalamika na kupiga kelele kwako sana hakutakusaidia kitu zaidi ya kukupotezea muda.


Uelewe kuwa mwenye uchungu wa maisha yako ni wewe mwenyewe. wengine wote wanaosema wanataka kuboresha maisha yako, wanakudanganya. Kwa kulijua hilo katika safari yako ya mafanikio penda kile unachokifanya na kuwa mvumilivu wakati unasubiria kutimiza ndoto na mipango yako mikubwa uliyojiwekea.

Ninachotaka utambue na kukusisitizia hapa ni kwamba ili tuwe na maisha bora kesho ni lazima tuwe makini sana na yale tunayoyanya leo, ikiwa ni pamoja na kujiuliza kila wakati kwa nini maisha yangu yako hivi? Lakini zaidi ya yote ni muhimu tuache woga na kujaribu mambo hasa kama tunaona yanaweza kutusaidia.

Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuboresha maisha yako. Ombi letu kubwa kwako endelea kuwashirikisha watu wengine kuweza kujifunza kupitia mtandao huu. Kwa kujifunza kwa pamoja tutaweza kuimarisha maisha yetu na kufikia mafanikio makubwa na kuachana na umaskini.

Tunakutakia kila la kheri katika safari ya ukombozi wa maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,No comments :

Post a Comment