google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jun 23, 2015

Hii Ndiyo Siri Ya Mafanikio Iliyojificha Kwenye Kushindwa Kwako.

No comments :
Kama kushindwa ingekuwa ndiyo mwisho wa safari ya mafanikio basi leo hii kusingekuwa na mtu ambaye angekuwa amefanikiwa. Kwa bahati nzuri sana dunia imejaa watu wengi ambao kabla ya kufanikiwa kwao walishashindwa sana. Watu hawa hawakuweza kukata tama pale waliposhindwa ila walichukulia kushindwa kwao kama fundisho na kuzidi kusonga mbele.

Ukifatilia hili utagundua kuwa watu wote wenye mafanikio makubwa  hao ndio walikuwa washindwaji  sana katika kile walichokuwa wakikifanya. Kwa maana hiyo hakuna mtu ambaye amefanikiwa sana hakuwahi kushindwa kwa namna yoyote ile. Unaweza kuthibitisha juu ya hili kwa kuangalia maisha ya Thomas Edson. Katika maisha yake alikosea karibu mara 999 kabla hajaja na ugunduzi rasmi wa balbu(glopu).

Kwa makosa aliyokuwa akiyafanya Thomas Edson aliyachukulia kama fundisho na kuamua kusonga mbele. Pengine leo hii dunia ingekuwa giza kama sio ubishi wa Edson kung’ang’ania ugunduzi wake huo wa taa mpaka ukafanikiwa. Ipo siri kubwa sana katika kukosea kwetu ambayo wengi wetu hawajui. Wengi hujikuta wanakatishwa tamaa sana na makosa yao na kurudishwa nyuma.


Kwa vyovyote vile iwavyo pale inapotokea umekosea usitoke mikono mitupu, jifunze kitu. Kwa kujifunza itakusaidia kuweza kuendelea zaidi kwa ujasiri na mafanikio makubwa. Ni mara ngapi umekuwa ukikosea na kukata tamaa, bila shaka ni mara nyingi. Kukosea kwako mara mbili, tatu, au nne kusikukatishe tamaa, wapo waliokosea zaidi ya mara elfu moja lakini walijirekebisha na kusonga mbele.

Nimekuandikia makala hii kukutia moyo kuwa mafanikio katika maisha yako yapo na yanakusubiri hata kama umeshindwa mara ngapi. Unachotakiwa kufanya ni kuwa mvumilivu kwa muda ili kuyafikia. Kama nilivyoanza katika makala hii, watu wengi wenye mafanikio walianza kwa kushindwa kwanza kisha wakafanikiwa. Hicho ndicho kitu unachotakiwa kukifanya kwa sasa badala ya kujilaumu.

Ni muhimu kujua kuwa kushindwa ama kukosea ni hatua nayo mojawapo katika safari ya mafanikio ingawa hatua hiyo huja kwa kuumiza. Tukubali kujifunza pale tunapokosea kisha baada ya hapo tusonge mbele na kuachana na tabia ya kulalamika. Kama unafikiri makosa na kushindwa kumekurudisha nyuma sana, angalia maisha ya watu hawa na kisha jifunze kitu na kuwasha moto wa mafanikio ndani yako.

1. Soichiro Honda, huyu ndiye mwanzilishi wa kampunni kubwa  ya kutengeneza pikipiki aina ya Honda. Maisha yake kimafanikio yalianzia pale ambapo alienda kuomba kazi katika kampuni ya utengenezaji wa magari aina ya Toyota na kukataliwa sana kuwa alikuwa hafai na hawezi kitu chochote akatafute kazi nyingine na sehemu nyingine.

Kwa Honda hilo halikumkatisha tamaa, aliamini anaweza na anao uwezo mkubwa ndani yake utakaomsaidia, ndipo akaamua kuanzisha kampuni yake ya Honda ambayo baadaye ikaja kuwa kampuni kubwa ya magari duniani inayoshindana na kampuni ile ya Toyota ambayo walimkataa mwanzo. Ikiwa kuna kitu cha kujifunza hapa kupitia maisha ya Honda kamwe USIKATE TAMAA kwa kile unachoamini kuwa kitakufanikisha.


 
2. Stephen king's, huyu ni mwandishi maarufu wa vitabu lakini wengi hawajui alikotokea zaidi ya kuishia kusoma vitabu vyake tu. Stephen King’s ni mwandishi pekee ambaye kitabu chake cha kwanza kilikataliwa sana na kampuni nyingi za uchapishaji alikotaka kwenda kuchapisha kwa kuambiwa kuwa hakifai. Hata hivyo  hakukata tamaa mpaka alipotimiza lengo lake.Kwa hiyo unakuja kuona kwa vyovyote hata ukataliwevipi, unao uwezo wa kubadili matokeo na kufanikiwa ikiwa unajiamini.

3. Oprah Winfrey's, katika maisha yake ya sasa huyu ni moja kati ya wanawake wenye pesa nyingi sana duniani, mhamasishaji wa mafanikio na mwendeshaji wa vipindi vya TV. Kwa kazi hiyo ya utangazaji imempa pesa nyingi sana kiasi kwamba naweza kusema ni moja kati ya wanawake matajiri duniani na mwenye umaarufu mkubwa sana. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo, Oprah Winfrey kabla hajafika hapo kituo kimojawapo cha kwanza walichomwajiri walimfukuza kazi kwa madai kuwa hafai. Hilo yeye halikuwa pigo alikaa chini na kuongeza juhudi hatimaye kufika juu kwenye kilele cha mafanikio makubwa.

4. Bill gates, huyu ni mwanzilishi wa kampuni inajulikana sana duniani ya Microsoft ni mmoja kati ya wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa sana dunia. Pamoja na hayo, lakini je? unajua kwamba wazo lake la kutengeneza kompyuta ambayo ingekuwa inatumia ‘mouse’ lilikataliwa kabisa katika kampuni alikolipeleka wazo hilo kwa mara ya kwanza?. Lakini yeye hakujikatia tamaa na wazo lake aliweza kuliendeleza na kumpa mafanikio makubwa.  Sasa ndiyo huyu Bill Gates unayemjua sasa alikotoka na kwa sasa ndiye tajiri wa kwanza duniani.


Nini cha kujifunza kupitia maisha ya watu hawa.

1. Kukataliwa au kuambiwa huwezi kitu isiwe sababu ya wewe kushindwa na kuamua kuachana na ndoto zako. Jiamini na kisha songa mbele, utafanikiwa sana tena sana.

2. Kushindwa katika kile unachokifanya sio tatizo hata kidogo, kikubwa jifunze kupitia kushindwa kwako huko. Jiulize ni wapi ulipokosea, jirekebishe na zidi kuendelea mbele kukamilisha ndoto zako.

3. Kujiamini wewe kwanza, kuwa unaweza na hakuna kitu cha kukuzuia, huo ndiyo ufunguo halisi wa kukufikisha kwenye njia ya mafanikio.

4. Watu wanaokukatalia wewe kuwa huwezi, ni wazi hawajui kitu kukuhusu wewe kwamba ni mtu mafanikio.

5. Kama ukishindwa kitu leo, haimanishi umeshindwa milele. Unaweza ukajipanga upya na kufikia mafanikio makubwa zaidi ya mwanzo.

Kumbuka, unaweza kufanikisha malengo yako yote unayotaka ikiwa utaamua na kuishi kwa vitendo na hakuna wa kukuzuia. Suala la kufanikiwa katika maisha yako siyo la bahati kama unavyofikiri. Inapotokea umeshindwa jipe moyo na kusonga mbele kwani katikati ya kushindwa ipo siri kubwa ya mafanikio yako ambayo unatakiwa kitumia na kufanikiwa zaidi na zaidi.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio iwe ya ushindi. Na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.