Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, April 14, 2015

Ukishajiwekea Malengo, Kinachofuata Ni Hiki Hapa…Ili Kutimiza Malengo Yako Kwa Urahisi.

No comments :
Ni ukweli uliowazi, mara nyingi ukishajua unataka kwenda wapi katika safari yako ya mafanikio ina maana kwamba kila kitu kwako ni rahisi. Kama unataka kuwa muuza ndizi maarufu, kuwa dereva mkuu, mpiga kiwi mwenye sifa mjini kote, mwanamziki wa kimataifa, ni rahisi kujua ufanye nini kufika huko unakotaka kwenda.
 
Inakuwa kwako ni rahisi kuweza kuvumilia shida, kusubiri, kutokata tamaa, kujipa moyo na kuwa na matumaini yasiyofifia kwa kuwa unajua unachokitafuta . Unaweza kuuingiza mtaani ndizi zisinunuliwe hata moja, lakini kwa kuwa unajua unachokitafuta, yaani kuwa muuza ndizi maarufu baadaye, kikwazo hicho kimoja hakitakuvunja nguvu. Kwanini? Kwa sababu hapa utakuwa unaangalia picha kubwa, badala ya kapicha kadogo.

Hii ya kuangalia picha kubwa badala ya ndogo, pia ndiyo siri kubwa ya mafanikio mengine maishani. Kuangalia picha kubwa badala ya ndogo ina maana kwamba, unapoingia kwenye matatizo au changamoto, itakusaidia kukabiliana na changamoto hizo kwa urahisi. Kama umeanzisha mgahawa, lakini lengo lake ni kuja kuwa na hotel kubwa ya hadhi, unapopata matatizo, chukulia hayo ni mafunzo unayoyapata kuelekea kwenye hilo jambo kubwa unalolitaka.

Kila unapokuwa unafikiri kuwa kuna jambo kubwa sana ambalo ni lazima uweze kulitimiza na ndilo lengo lako kuu, hutaweza kukatishwa tamaa na matatizo katika hiki kidogo unachoanza nacho. Hata kama utafungua biashara fulani kwa muda, halafu ukaja kuifunguka kutokana na matatizo au changamoto hizo, lililo muhimu kwako ni kujifunza kwa changamoto hizo na kuanza upya mpaka kufikia lengo ulilojiwekea.


Mtu anayejua anaelekea wapi kwenye safari yake haamui kuvunja safari hiyo kwa sababu basi limeharibika. Atasubiri mpaka litengenezwe ili aendelee na safari. Lakini kama hajui hasa anaelekea wapi, lakini yumo kwenye basi liloharibika, likipita lori kuelekea kule alikotokea, anaweza kulidandia, kwani anachotaka yeye ni kuonekana tu yuko safarini, bila kujali anaelekea wapi hasa.


Kwa kawaida tukishachagua tunataka kuwa nani au kufanya nini, tutajiuliza namna tutakavyoanza kuelekea huko. Kwa bahati mbaya, wengi wetu tunataka tunapoamua leo, basi asubuhi inayofuata tuwe tumeshakamilisha kila kitu au kufanikiwa. Kama tumeamua kumiliki duka au kufanya biashara ya mazao au kuja kuwa madaktari, ni lazima tujiulize kama tuna chochote cha kutusaidia kuanza safari ya kuelekea huko. Ukishajua una chochote au tayari  umejiwekea malengo kinachofuata kwako ili kutimiza malengo hayo ni:- 

1. Kwanza, ni lazima uwe na  elimu na maarifa.
Kuna malengo fulani yanahitaji tuwe na elimu fulani, mengine yanahitaji tuwe na uzoefu fulani na mengine yanahitaji muda kwani yana hatua kadhaa ambazo ni lazima tuzipitie kwanza. Kama mtu anapenda sana na ameamua kuwa mpambaji wa maharusi na mpishi wa keki za harusi, itabidi asomee utaalamu huo. 

Kwa mfano kama mtu atakuwa ameamua kwamba, atakuwa anasafirisha vyakula kutoka mikoani na kuvipeleka jijini Dar es salaam, ni lazima ajue vyakula gani na vinatokea maeneo gani ya nchi, vinasafirishwa vipi na msimu upi ambao unafaa kupelekwa jijini Dar es salaam na sababu gani? Kama ni mwanafunzi anataka kuja kuwa mwandishi wa habari, ni lazima tangu awali ajue ni masomo gani anatakiwa kuyazingatia.

Elimu na maarifa siyo lazima viwe vitu vya darasani kama unavyoweza kufikiri. Kama tumegundua jambo au mambo ambayo tunataka kuyafanya maishani, ufahamu kuhusu jambo au mambo hayo ni muhimu sana kwako. Ufahamu huu huweza kupatikana kwa njia mbalimbali na kwa kawaida upo, ni juu yetu kuutafuta.


2. Pili, ni lazima uwe na ushirikiano na wengine.

Kuna shughuli nyingine inabidi tuwe na watu ambao tayari wamo humo kutuelekeza. Inawezekana kabisa tunataka kuwa wafanyabiashara, inabidi muda mwingi kutafuta ushirikiano na wafanyabiashara ili kuweza kutuonyesha mwanga wa kile ambacho tunataka kukifanya.

Ni jambo la kushangaza kugundua kwamba mtu ana kipaji fulani, ana ujuzi fulani ana maarifa fulani, lakini hana uwezo kuonyesha na pengine kuyatumia kwa faida kutokana na ukosefu wa rasilimali. Wakati huohuo inawezekana kwamba kuna watu wenye raslimali ambao wanatafuta mtu au watu wa kipaji chake, lakini hawawaoni.


Kama unataka kufika mbali ni lazima tukubali kushirikiana na wengine kwa njia moja au nyingine. Tukiwa wachoyo kamwe hatutamudu. Wakati mwingine siyo uchoyo, bali hatujui kwamba vipaji, maarifa na uwezo tulionao tunaweza kutafuta watu wa kushirikiana nao na kwa pamoja tukamudu. Tunakaa na kusubiri hao wengine watubaini ili watutembelee katika kufanya nao mambo fulani. Ni sisi ndiyo tunaotakiwa kuwatafuta wengine ili tufanye nao.

Hakikisha unaendelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa maarifa na elimu bora itakayoboresha maisha yako.

TUNAKUTAKIA USHINDI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
No comments :

Post a Comment