Apr 25, 2015
Hii Ndiyo Kanuni Rahisi Kwako Unayoweza Kuitumia Kukupa Mafanikio Makubwa.
Ni hivi. Ili uweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa unayotaka iwe katika masomo, kupata kazi, kuvuna sana mazao shambani, kupata faida katika biashara au kuwa na uhusiano mzuri na ndoa nzuri, ni lazima kwanza ujue kwamba hayo yote yanawezekana na yanakuhusu wewe moja kwa moja kwa asilimia zote na siyo bahati.
Unapotaka mafanikio ambayo
huamini kwamba unastahili kuyapata, huwezi kamwe kuyapata hata kama ungefanya
nini. Unapotaka kupata ajira, lakini ukajiambia kwamba kuna watu wengi wenye
sifa kuliko wewe, ambao watapata kazi hiyo na siyo wewe, ni wazi pia hutapata
kazi hiyo unayoitafuta.
Unapoamini kwamba utapata
kazi hiyo kwa juujuu, lakini ndani kabisa mawazoni mwako unajua ni jambo gumu
litakuwa gumu kweli. Unapoingia kwenye biashara kwa kuamini kwamba hutaweza
kufanikiwa kwa sababu haijawahi kutokea ukafanikiwa au kwa sababu wewe una
mtaji mdogo, hufahamiki na pengine hukusoma sana kama wengine, ni wazi
hutafanikiwa.
Unaposema na kuamini kwamba
una mkosi, utaendelea kuwa na mkosi hadi unaingia kaburini. Sisi binadamu ni
kile tunachoamini. Kwa nini inakuwa hivyo, kwamba tunapoamini kuwa hatuwezi au
tuna mkosi, mambo yanakuwa kama tunavyoamini?
Kwa hiyo, ili kuweza kupata
kile unachokihitaji katika maisha na kuenda sawa na kanuni hii ambayo ni rahisi
kwako kuitumia na kukupa mafanikio, ni lazima kuweza kutambua umuhimu wa
kufikiri vizuri. Kwa kufikiri kwetu vizuri itatusaidia kuweza kumudu na kutenda
kwa mkabala wa kimafanikio na kuweza kuvuta mafanikio makubwa kwa upande wetu
zaidi.
Kwa kufikiri kwamba hatuwezi
au hatustahili, bila wenyewe kujua, tutafanya kwa mkabala wa kutoweza na
kutostahili. Kumbuka kuwa upo uhusiano mkubwa sana kati ya fikra zetu, hisia
zetu na tabia au matendo yetu. Tunapofikiri kwamba hatuwezi, bila kujua,
tutakuwa na tabia zitakazotupeleka mahali ambapo hatutaweza kweli.
Mwandishi na mwanafalsafa
maarufu duniani Shakespeare aliwahi kusema: ‘Hakuna jambo baya au zuri, bali kufikiri kwetu ndiko kunakolifanya
jambo kuwa hivyo’. Huu ndiyo ukweli , kwamba, kufikiri vibaya hutudhuru
sana , tuwe tunajua au hatujui. Ubaya au uzuri wa mawazo yetu, hasa yale ya
kina ni kwamba, kile tunachokifikiri na
kukiamini ndicho kinachotokea au kufanyiwa kazi, hayachagui au kutuhurumia ati
kwa sababu hatujui juu ya ukweli huo.
Kwa hiyo, hatua ya awali
kabisa ya mafanikio ya binadamu yako kichwani au mawazoni mwake. Kuna familia,
koo, hata makabila ambayo yamekuwa na fikra kwamba hayawezi au hayastahili. Mtu
kutoka familia, koo au makabila hayo anaweza kuwa na uwezo mkubwa sana katika
kutenda, kipaji na ufahamu mkubwa ajabu, lakini akabaki kuwa mbumbumbu ambaye
familia , ukoo au kabila lake limefanywa kuaminika kwamba ndilo linalostahili
kuweza au kuwa nacho.
Bila kuanza kukagua namna
tunavyofikiri, inaweza kuwa kazi bure kujaribu kutafuta au kuzungumzia
mafanikio kwa ngazi yoyote, iwe mtu binafsi au taifa. Ni lazima tuanze kwa
kujiuliza kile tunachoamini kuhusu mafanikio, yaani kupata kile tukitakacho maishani.
Inawezekana kabisa, bila sisi wenyewe kujua tulishawekewa mipaka ya mafanikio
tangu wakati tukiwa wadogo. Mipaka kama hii huwekwa vipi?
Inawezekana kabisa wazazi au
jamii yote tulimokulia ilikuwa ikisema na kutenda kwa njia ambayo ilituonyesha
kwamba tunachoweza sanasana ni kuhangaika na kupata ajira mahali, basi. Pengine
ilisema na kutenda kwa njia ambayo ilituonyesha kwamba, ni vigumu kwetu
kumiliki gari. Inawezekana kwamba ilisema na kutenda kwa njia ambayo
ilituonyesha kwamba hatupaswi kuinuka sana kimaisha kwani sisi kwa ukoo au
kabila fulani hatustahili.
Pia kuna wakati tunajikuta
tukitamani kusonga mbele katika kutafuta kile tunachokitaka, lakini tunazuiwa
na uvivu wa aina fulani tu tusioujua sababu yake, tunazuiwa na kuahirisha
kufanya hivyo, bila kujua ni kwa nini. Inawezekana kabisa kwamba hiyo inatokana
na malezi, mazingira tulimokulia au uzoefu wetu maishani.
Kumbuka kuwa kuna vizuizi
vingi vilivyowekwa kwenye mawazo yetu katika hatua hizo tulizopitia maishani. Lakini
ili uweze kumudu kuondokana na vizuizi hivyo ni muhimu kwako kujua mambo mawili
tu, ambayo ni kuweza kutumia kanuni
tuliyoongelea ya kuamini kuwa katika maisha yetu tutaweza, tutamudu, tutashinda
na tutatekeleza na jambo la pili ni kubadili mtindo wako mzima wa kufikiri.
Unapoamua kubadili mtindo
wako wa kufikiri sio kwamba tu unakuwa unajiondoa kwenye vizuizi vya
kutofanikiwa, bali pia unakuwa unajiweka katika nafasi nzuri ya kupata kile
unachokihitaji. Je, unawezaje kubadili mfumo wako mzima wa kufikiri na
kukuwezesha kukupatia kile unachohitaji ama kufanikiwa kwa ujumla? Kujua hilo hakikisha
unafuatilia makala ijayo katika DIRA YA MAFANIKIO bila kukosa, ili kujua mawazo
yako jinsi yanavyoweza kufanya kazi na kukupa utajiri.
Ansante sana kwa kuwa msomaji
mzuri wa DIRA YA MAFANIKIO, endelea kuwashirikisha wengine kujifunza zaidi
kupitia mtandao huu. Kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kabisa kufika mbali
kimafanikio na kuufuta umaskini.
DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI
NGWANGWALU,
0713048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.