Oct 15, 2015
Kama Na Wewe Utazidi Kung’ang’ania Fikra Hizi, Umaskini Ni Halali Yako.
Katika
hali ya kawaida, fikra ulizonazo ndizo zinazoamua maisha yako yaweje. Kama
unafikiria chanya ni wazi maisha yako yatakuwa ya mafanikio, lakini kama pia
utakuwa na fikra hasi nalo hilo halina ubishi ni lazima utaishia kwenye
umaskini tena wa kutupwa. Je, wewe binafsi huwa una mawazo gani? Yakukufanikisha
au kukwamisha?
Wengi
wanakwamishwa sana na mawazo yao badala
ya kuwasaidia. Utakuta ni watu wa kulalamikia sana watu wengine lakini ukija
kuchunguza kinachowatesa ni mawazo yao na si kingine. Mara nyingi huwa nashangaa
sana hasa pale ninapokutana na watu wengi wakiwa na fikra kama za kutaka kusaidiwa sana katika maisha yao. Bila shaka umeshawi
kuliona hili, tena nina uhakika sana tu.
Hizi
ni moja kati ya fikra au mawazo mabovu yanayowarudisha watu wengi nyuma sana
kimafanikio. Wengi wanafikra hizi sana za kutaka kusaidiwa badala ya kusaidia.
Kila mmoja anakuwa anajitahidi sana kufikiria namna atakavyoweza kusaidiwa na
ndugu yake, serikali, mfadhili au tajiri fulani. Ni jambo la ajabu sana kuona
watanzania wengi wanafikra kama hizi.
Tangu
tukiwa wadogo tumefundishwa kwamba, maana ya ndugu ni kusaidiwa naye, siyo
kumsaidia. Tunakuja kujua kuhusu kumsaidia ndugu, pale tunapokuwa watu wazima
na kuwa na uwezo ambao unawafanya hao ndugu kutujia kutuomba msaada. Lakini
muda wote huwa tunajua kwamba, wajibu wetu ni kusaidiwa.
Kwa
hali hiyo, tumejengewa dhana kwamba, serikali inawajibu wa kutusaidia na ndugu
na jamaa zetu wapo kwa ajili ya kutusaidia. Hivyo tunasahau kwamba, ni wajibu
wetu kusaidia kuliko kusaidiwa.
Kuna
msemo maarufu sana duniani ambao uliwahi tolewa na Rais wa zamani wa marekani
kwamba, kabla hujauliza nchi yako imekufanyia nini, jiulize wewe umeifanyia
kitu gani nchi yako. Msemo huu una mantiki kubwa sana ndani. Lakini pia kabla
hujadai ndugu yako akusaidie, jiulize wewe umewahi kumsaidia nani maishani mwako?
Kwa kawaida, wasiosaidia wala kujisaidia, ndiyo wanaodai sana kusaidiwa.
Ni
jambo la kusikitisha kwamba, kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo
watu wengi wanazidi kuamini kwamba, wajibu wao ni kusaidiwa na kamwe kusaidia
hakuwahusu. Kwa hali hiyo, mtu anakwepa kulipa kodi, halafu analaumu barabara
haihudumiwi, hakuna dawa hospitalini au hakuna huduma za jamii kwa ujumla.
Kuna
watu ambao kazi yao kubwa ni kuwalaumu ndugu zao kwamba, hawataki kuwasaidia,
kuilaumu serikali kwamba, haiwajali, bila kujiuliza ni nani aliwaambia kuna
kudai haki bila wajibu.
Inabidi
kila mmoja atimize wajibu wake, ili kuomba haki kwake liwe ni suala lenye
mashiko. Kuomba haki bila kutimiza wajibu ni aina ya ukichaa. Wajibu wa kila
mmoja wetu ni kuuliza yeye amesaidia wapi, amemsaidia nani, na amesaidia nini,
na siyo amesaidiwa na nani, lini na wapi.
Siyo
suala la mzaha kwamba, wengi wanazidi kuwa wataalamu wa kuomba, wataalamu wa
kusubiri kusaidiwa wafanyiwe, bila wao kujiuliza mchango wao kwenye kutenda
ambayo yatawasaidia wengine hata serikali pia. Kuna haja ya kubadilika kwani
tunaelekea kuchelewa. Na ndio maana kama unandelea kung’ang’ania fikra hizi,
mafanikio kwako yatakuwa ni ndoto za mchana.
Tuanze
kujifunza na kuwafundisha watoto wetu kwamba, wajibu wao ni kusaidia na siyo
kusaidiwa. Ni lazima tuwafundishe kwamba, wasione aibu kusaidiwa, lakini
wasiishi kwamba, kusaidiwa ndiyo wajibu wao.
Ni
lazima tuanze kujifunza kuwajibika badala ya kudai haki kwanza. Kwa kujifunza
kuwajibika, tunajikuta tukisaidia badala kuishi kwa kusubiri kusaidiwa.
Nakutakia
mafanikio mema
na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.