Oct 6, 2015
Kama Unayumbishwa Sana Na Kitu Hiki, Huwezi Kufanikiwa.
Habari
za leo rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO bila shaka
umzima wa afya. Nakukaribisha katika siku nyingine tena ya kuweza kujifunza na
kuboresha maisha yetu. Leo katika makala yetu, nitakusimulia kisa kimoja
ambacho kinaelezea habari za mzee mmoja ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuuza
maandazi na nyama pembezoni mwa barabara siku zote.
Kutokana
na kukosa elimu ya kusoma na kuandika mzee yule hakuweza kusoma magazeti, na
pia kutokana na uhafifu wa macho na masikio yake yake hakuweza kutazama
televisheni wala kusikiliza redio. Licha ya haya yote mzee huyu alijitahidi
sana katika biashara yake na kujikuta mtaji wake unapanda na kuwa juu hata
kufikia hatua ya kuuza maandazi na nyama hizo sehemu mbalimbali.
Mzee
huyo akiwa anaendelea na shughuli zake mtoto
wake ambaye alikuwa mhitimu wa chuo kikuu aliamua kuangana na baba yake katika
biashara hiyo. Mzee huyo alifurahi kupata msaidizi msomi ambaye aliamini
atamsaidia sana katika suala zima la kupandisha
uchumi juu na hatimaye kufikia mafanikio makubwa kuliko yale aliyokuwanayo
kwa wakati huo.
Siku
moja mtoto huyo alikuja na wazo ambapo alimshauri baba yake akisema huko mbeleni
uchumi utashuka kwa kiwango kikubwa kitaifa na kimataifa, hivyo ajihadhari.
Yalikuwa ni maneno ambayo kwa baba yake hayakuwa mazuri sana . Kutokana na maneno
hayo mzee huyu akaamua kupuuzia biashara yake na kuacha kuuza bidhaa zake
sehemu mbalimbali kama mwanzoni.
Kitu
pekee kilichopelekea mzee huyu kufanya hivyo ni kuogopa hali ya uchumi ambayo
ilikuwa inaenda kubadilika muda siyo mrefu na kuwa mbaya kabisa. Hali hiyo
ilisababisha wateja wake wengi kupungua sana na biashara yake ilifika
mahali ikafa na hali mbaya ya kushuka
kiuchumi ikaanza kumkabili. Chanzo cha yote hao yalisababishwa na mtoto wake.
Ni
kitu gani ambacho umejifunza kupitia simulizi hii? Naamini ni mengi. Lakini ikumbukwe,
wengi wetu katika maisha ndivyo tulivyo. Huwa ni watu wa kupokea taarifa sana
hata bila ya kuzifanyia uchunguzi huwa tunazifanyia kazi moja kwa moja au
kuziamini. Kwa kufanya hivyo hujikuta taarifa hizi zikiua mipango na malengo
yetu bila kujijua.
Ili
uweze kufanikiwa huhitaji kupokea kila taarifa. Hata kama ikitokea umepokea
taarifa hizo unatakiwa kuzifanyia uchunguzi kama ni za kweli kwako au la. Hiyo
yote inatuonyesha ni muhimu sana kufikiri kabla ya kutenda na pia tusikate
tamaa hata pale inapotokea tunapewa taarifa mbaya za kutukatisha tamaa.
Maisha
ni kupanda na kushuka, kwa hiyo tunapoambiwa kuwa kuna mabaya mbeleni yanakuja,
tusidharau wala kufa moyo kwa namna yoyote ile zaidi ‘tukazae buti’ ili kuyaepuka mabaya hayo nakufikia mafanikio
makubwa tunayoyahitaji. Tusiwe wa kukatishwa tamaa na kukubali kama ilivyokuwa
kwa mzee huyu kwenye simulizi yetu.
Hivyo,
kitu cha kuzingatia hapa ni kwamba kuwa makini na kile unachoambiwa. Kwa sababu
kinaweza kukusaidia kukufanikisha au kuua ndoto zako kabisa ikiwa utakuwa mtu
wa kukurupuka na kufanyia kazi kila jambo. Kuwa na misimamo yako
itakayokusaidia kufanikiwa. Ila kama unayumbishwa sana na kitu hiki, huwezi
kufanikiwa. Hakikisha taarifa yoyote isikuyumbishe, bali iwe msingi wa
kuendelea mbele zaidi.
Nakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI
NGWANGWALU,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa
ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.