Oct 16, 2015
Hizi Ndizo Athari Mbovu Za Malezi Kwa Watoto Wetu.
Tumekuwa
tukishangaa au kama siyo kushangaa, kukerwa na kuachiwa maswali na tabia hii. Inasemekana
wasichana wa mijini wanadanganyika kirahisi sana zaidi kwa magari. Utakuta msichana
anakubali kuwa na uhusiano na mwanamume kwa sababu amegundua kwamba, ana gari.
Lakini,
wengine wanajua kabisa kwamba, gari siyo la huyo mwanamume, lakini hujikuta
wakikubali kuwa na uhusiano naye kwa sababu ya gari tu. Ndiyo maana madereva
wengi, hasa wale wa teksi wanajisifu kwamba, wanawake wanawapapatikia sana. Kuna
ukweli wa aina fulani.
Lakini,
je wasichana ni wote ambao
wanawapaptikia madereva au watu wenye magari? Ndilo swali gumu sana kwenye
suala hili. Kila kitu kinachohusu uhusiano wa kimapenzi, tunajifunza kutoka kwa
wazazi au walezi wetu, labda asilimia 10 tu ndiyo tunajifunza nje ya nyumbani.
Siyo
suala la gari peke yake, bali ni suala la karibu kila kitu. Je watoto wetu
tunawajengea dhana gani kuhusu kila kitu kwenye maisha? Halafu tunawaambia kitu
gani kuhusu kupenda? Siku zote na tulio wengi, tunawaambia watoto wetu uongo
mwingi sana.
Uongo
huo unatokana na sababu nyingi. Kwanza, nasi tulidanganywa na wazazi wetu. Pili
hatujiamini. Tatu, hatuna uhakika sisi ni akina nani na nne, tunadhani uongo
huo utawasaidia watoto kuwapa moyo.
Hebu
chunguza kwa makini, utagundua kwamba, wasichana wanaobabaikia magari ni wale ambao
wamelelewa kwenye malezi ya uongo mtupu.
Unaweza
kudhani wale waliotoka kwenye familia maskini ndiyo ambao wanababaikia magari,
hapana. Msichana anaweza kutoka kwenye familia maskini na asibabaikie utajiri
wala mali ya mtu. Wako wengi wa aina hiyo.
Kama
nyumbani, wazazi wanasifu wenye magari, wanaonesha kwamba, ukiwa na gari ndiyo
unakuwa na maana, kwamba, gari ni kiwango cha juu cha mafanikio, unatarajia
kitu gani kutoka kwa watoto? Kuna wakati wazazi wanasema, ‘ameshafika mbali siyo mwenzio, yule ana akili bwana. Ana magari mawili
na nyumba tatu’
Wakati
mwingine inatosha mara moja tu jambo kusemwa na mzazi na mtoto kuamini, kwamba,
mwenye gari au magari na nyumba, ndiye aliyekamilika, ndiye mwenye akili.
Kumbuka,
mtoto anaingiza akilini mwake maarifa kutoka kwa watu anaowaamini na anaokutana
nao maishani. Kwenye suala la uhusiano, wazazi ndiyo wanaoaminika zaidi.
Kwa
sababu ya umaskini wetu tulio wengi, gari na nyumba ndiyo tunayoyachukulia kuwa
ni malengo ya juu kabisa kuyapata. Kwa hiyo mtoto anakuwa ana akili ya aina
hiyo , kigezo chake kuhusiana na mtu kitakuwa ni gari na nyumba au mali kwa
ujumla.
Kwake,
binadamu, mwenye maana na anayefaa ni yule anayemudu kumiliki vitu hivyo, hii
siyo kwa wasichana peke yake, bali hata wanaume, kama mtoto wa kiume alioneshwa
thamani ya mtu inatoka kwenye gari, nyumba, na mali, naye bila shaka atakuwa
anababaikia vitu hivyo.
Linapokuja
suala la uhusiano, anajitahidi kumwonesha msichana kwamba, anavyo vitu hivyo
au anao uwezo wa kuvimiliki. Anafanya hivyo, kwa sababu, aliambiwa thamani yake
inakuwepo pale anapokuwa na vitu hivyo.
Wazazi
wengi wameegemeza thamani zao kwenye vitu, badala ya wao wenyewe. Bila hiari
yao wanawafundisha watoto watoto wao kujali na kuthamini vitu, badala ya utu
wao. Kwa kadri mfumo wa maisha ulivyokuwa ukiendelea, ukilinganisha na zamani,
utagundua binadamu alijitoa thamani na kuiweka kwenye vitu, hasa mali.
Bahati
mbaya, wale watoto wa wazazi ambao wana maisha ya kati, ndiyo ambao
wanasumbuliwa sana na mali. Kwa nini? Wazazi hao hawajui kama wako juu au chini
kimapato.
Katika
kujitafuta hufanya mambo na kutoa kauli zenye kuonesha kwamba, maisha ni mali,
basi. Wazazi walio chini kabisa, wanaweza nao kuwaathiri vibaya watoto kwa
kuzungumza na kutenda kwa njia ambayo watoto wataamini kwamba, umaskini huondoa
kabisa thamani ya mtu.
Wale
wa juu kabisa, wanaweza wasifikirie kuwa gari au nyumba ni mambo ya maana sana,
hata kama wamefundishwa kuhusu mali. Wao watafikiria mali kwa mkabala mkubwa
zaidi.
Labda
watafikiria kuhusu ndege ya kutembelea, boti ya kifahari na mengine. Lakini, yote
ni ileile, kuamini mali ni kubwa kuliko thamani ya binadamu. Mali ambayo
unaitengeneza na kuitafuta mwenyewe iwe kubwa kuliko wewe.
Wazazi
ambao wanakuchukulia mali kwa ujumla, kama kitu cha kawaida sana, ambacho uwe
nacho au usiwe nacho, maana ya maisha haibadiliki, na thamani yako haiondoki,
hawa ndiyo ambao watoto wao tunawapenda.
Nikisema
tunawapenda, nina maana kwamba, ni watu ambao kwao, kila binadamu ana thamani
bila kujali anamiliki au hamiliki kitu gani. Wazazi ni wepesi sana kusema, ‘hawa watoto wetu nao, wakiona mwanamume ana
gari, basi wanamkubali tu, bila hata kuchunguza’
Lakini,
nyumbani akina mama kauli zao ni hizi; ‘ukiwa
na gari na wewe mbele ya watu unasimama ati’ halafu wanatarajia mtoto
anayesikia kauli hizo aje ajue kuwa ana thamani kuliko gari. Hizo ni ndoto za
mchana.
Ni
wazazi hawahawa ambao hawaishi kusema, ‘umefanya
kazi miaka yote, hata nyumba wala gari huna, una akili kweli wewe?’ watoto
wanasikia, wanaamini kwamba, asiyemiliki nyumba au gari hana akili. Halafu leo
watoto wetu wakiyumbishwa na vitu hivi hadi wanakuwa kama vichaa, tunashangaa.
Nakutakia
siku njema iwe ya ushindi kwako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na
kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.