Jul 7, 2016
Kilimo Cha Ufuta Na Faida Yake Kwa Mkulima.
Ufuta (sesamum indicum) ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa
ya Rukwa na Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara. Mbegu za
zao hili huwa na wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.
Kwa sasa soko la ufuta Tanzania ni zaidi ya mara tatu ya
uzalishaji wake, kwa mantiki hiyo zao hili lina soko kubwa sana. Uzalishaji
wake unafanyika kwa kiasi kidogo kwa sababu wakulima wamekuwa wakilima zao hili
la ufuta kwa mazoea na kutumia mazao yake kama nafaka ya kutengeza vyakula
mbalimbali kama kashata. Lakini kama utalima kibiashara ni zao ambalo linaweza
kukomboa jamii yetu kutoka katika dimbwi la umasikini.
UZALISHAJI WA ZAO LA UFUTA MBEGU.
Chagua aina ya mbegu inayotoa mazao mengi na bora, inayovumilia
mashambulizi ya magonjwa na wadudu, inayokomaa mapema na kutoa mafuta mengi.
Chagua mbegu inayokomaa kwa pamoja ili kurahisisha uvunaji na
pia kuepuka upotevu wa zao shambani. Aina nyeupe ya mbegu ya ufuta hupendelewa
zaidi kuliko aina nyeusi.
Mbegu bora ya ufuta inayopendekezwa ni LINDI 02, mbegu ambayo
imefanyiwa utafiti na chuo cha utafiti NALIENDELE. Kwa wastani mbegu hii hutoa
kati ya gunia 10 mpaka 15 ukifuata kanuni za kilimo bora.
Mbegu hii hukomaa ndani ya siku mia (100) mpaka mia na
kumi(110). Aina hii ya ufuta ina asilimia 55 ya mafuta. Hii ni habari njema kwa
wakulima kutoka kwa watafiti wetu wa Kilimo kutoka kituo cha Utafiti
Naliendele, Mtwara.
Mkulima akiwa kwenye shamba lake la ufuta. |
UPANDAJI.
Panda mbegu nusu inchi chini ya udongo, inchi sita umbali wa
mbegu na mbegu na futi mbili nafasi ya msitari na msitari, kabla ya kupanda
hakikisha ardhi imelowana vya kutosha na upande mbegu masaa mawili au matatu
baadae.
MBOLEA.
Ufuta unahitaji rutuba ya kutosha ili kutoa mazao bora. Katika
kudumisha rutuba ya udongo, tumia kilimo cha mzunguko wa mazao au weka mbolea
za asili pale inapobidi.
PALIZI.
Dhibiti magugu kwa kupalilia ili kuruhusu ufuta kutumia vizuri
unyevu na virutubishi. Magugu mengine huwa ni maficho ya wadudu waharibifu wa
zao la ufuta.
MAGONJWA.
Ufuta hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza
kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Hivyo kagua shamba mara kwa mara hasa
kwenye maua na mapodo ili kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili
zamashambulizi, chukua tahadhari mapema kabla ya uharibifu mkubwa haujatokea.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA.
Kagua shamba kuona kama ufuta umekomaa. Ufuta hukomaa, kati ya
miezi mitatu na minne tangu kupanda kutegemea aina. Aina ya ufuta usiokuwa na
matawi hukomaa mapema kuliko ile yenye matawi. Ni muhimu kuwahi kuvuna ili
kuepuka ufuta kupukutikia shambani.
DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI.
Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya manjano na
hatimaye kudondoka. Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia.
Mbegu za ufuta. |
VIFAA VYA KUVUNIA.
Tumia kamba, siko na panga kipindi cha kuvuna.
VIFAA VYA KUKAUSHIA.
Hakikisha Sehemu ya kukaushia ni safi na yenye Sakafu ya saruji na pamefunikwa
vizuri. Waweza tumia maturubai kufunika sehemu ya kukaushia.
USAFIRI.
Mikokoteni,Matela ya matrekta au Magari
KUVUNA.
Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana na kuanza kupasuka na kuachia
punje. Mapodo ya ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na upepo
hupasuka na kuachia mbegu, hali inayosababisha upotevu mkubwa. Mbegu za ufuta
ni ndogo na zikidondoka chini ni vigumu kuziokota. Vilevile mbegu zilizodondoka
ni vigumu kuzitenganisha na uchafu.
Uvunaji wa ufuta huhusisha ukataji wa mimea yenye mapodo kwa
kutumia vyombo vya mkono kama panga kwa kukata mashina. Kwa aina za ufuta zenye
mapodo yanayopasuka, uvunaji ufanyike wakati mimea bado ni kijani ili kuepuka
upotevu wa mbegu.
Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala jua kali. Baada
ya kukata mashina yafunge katika mizigo midogo na kuweka katika vyombo vya
kusafirisha kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu ya kukaushia.
Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika malundo madogo yasiyozidi mizigo
minane kwenye sehemu safi za kukaushia.
KUKAUSHA.
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa katika vitita. Vitita huwekwa kwa
kuegeshwa kwenye fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutegemea
hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa
punje kutokana na kupasuka kwa mapodo.
KUPURA.
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye sakafu safi.Vitita hupigwa
taratibu kwa kutumia mti au hutikiswa vikiwa vimegeuzwa vichwa chini ili
kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu safi au turubai.
KUPEPETA NA KUPEMBUA.
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa takataka kama vile
mawe, vipande vya mapodo,vijiti na vumbi.Njia bora ya kupepeta na kupembua ni
kwa kutumia mikono.
Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa kiasi cha kilo
mbili hadi tatu. Ufuta hurushwa hewani kwa kasi ndogo na takataka nyepesi
huchukuliwa na upepo.
KUFUNGASHA.
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye vifungashio kama vile magunia madogo
ya aina ya juti ya ujazo wa kilo 50. Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia
yenye uzito usiozidi kilo 50. Kabla ya kufungasha hakikisha mbegu zimekauka
hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.
KUHIFADHI.
Panga magunia ya ufuta juu ya chaga. Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu
mzunguko wa hewa kati ya magunia na magunia yako tiyari kupeleka sokoni.
GHARAMA ZA UZALISHAJI NA FAIDA KWA HEKA.
Gharama za uzalishaji mara nyingi hutegemea na eneo husika.
Kwa mfano mchanganuo ufuatao unaonyesha faida ya kilimo cha ufuta kwa maeneo ya Mbeya hususani maeneo ya Chunya. Gharama hizo zinaweza kupungua au kuongezeka na kutokana na msimu husika au eneo kama nilivyotangulia kusema awali.
1. Kuandaa shamba 70,000
2. Kulima 30,000
3. Kupanda 20,000
4. Mbolea 100,000
5. Kupalilia 30,000
6. Kuvuna 50,000
7. Usafiri 50,000
8. Gharama zingine 50,000
9. Jumla 400,000
10. Mapato (Forecasts) gunia 10*50kg*3000 1,500,000
11. Faida 1,100,000
Kwa mfano mchanganuo ufuatao unaonyesha faida ya kilimo cha ufuta kwa maeneo ya Mbeya hususani maeneo ya Chunya. Gharama hizo zinaweza kupungua au kuongezeka na kutokana na msimu husika au eneo kama nilivyotangulia kusema awali.
1. Kuandaa shamba 70,000
2. Kulima 30,000
3. Kupanda 20,000
4. Mbolea 100,000
5. Kupalilia 30,000
6. Kuvuna 50,000
7. Usafiri 50,000
8. Gharama zingine 50,000
9. Jumla 400,000
10. Mapato (Forecasts) gunia 10*50kg*3000 1,500,000
11. Faida 1,100,000
SOKO LA UFUTA.
Soko la ufuta kwa Tanzania ni mara tatu zaidi ya uzalishaji wake. Kuna
makampuni mbalimbali Tanzania ya unuzi wa ufuta. Makampuni hayo hununua na
kusafirisha nje ya nchi kama India na China. Makampuni hayo ni kama vile OLAM,
Export Traders n.k.
Katika msimu ulopita bei ya ufuta kwa kilo ilikuwa sh 3000 ambayo
ni sawa na sh 300,000 kwa gunia lenye ujazo wa kilo 100. Kwa maana hiyo uhakika
wa soko upo na ni mkubwa sana.
Mchanganuo huu ni matokeo ya kiutafiti wa kibiashara, ambayo
jitihada zimefanyika kuifanya iendane na hali ya kiuchumi ya sasa, hivyo
haitaathiri au kuathiriwa na tamko la wazi au la kiutendaji wa mabadiliko ya
kila siku ya kiuchumi duniani hasa ndani ya soko letu la Tanzania.
Matokeo yoyote utakayoyapata mtumiaji au msomaji
yatakayokuathiri moja kwa moja au kimchakato, bila kikomo cha muda maalumu
mpaka kuathiri faida iliyopangwa, hatutakua tayari kutupiwa lawama ya aina
yoyote ile.
Endelea kujifunza zaidi kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Kwa maswali na majibu kuhusu
kilimo bora cha kisasa kitakachokutoa kwenye umaskini pamoja na huduma za
ufungaji wa hema(Green House) Unaweza kuwasiliana na mtaalamu wetu wa kilimo
Ndugu John Mabalaga kwa mawasiliano 0754 282 448.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Naomba kufahamu ekali moja inatoa magunia mangapi ya ufuta
ReplyDelete