Feb 23, 2017
Kama Unabomoa Misingi Hii…Hutaweza Kufanikiwa Tena.
Tumia kile ulichonacho kwa uhakika na vizuri
kabisa. Acha kujidanganya kwamba unataka mafanikio makubwa wakati hata ile
misingi ya kutengeneza mafanikio makubwa unaiharibu hovyo hovyo.
Haiwezekani eti unasema unataka mafanikio makubwa
wakati unatumia muda, pesa na nguvu zako hovyo, ambapo vitu hivyo kwa pamoja
vingekusaidia kufikia mafanikio makubwa kama ungevitumia vizuri na kwa busara.
Hata Pesa unazozipata hazijiamulii zenyewe kwamba ‘sasa mimi pesa ninakwenda kununua kitu hiki
au kile.’ Wewe ndiye mwenye jukumu la kupanga pesa zako zitumike wapi na
kwa sababu ipi.
Sasa kama hiyo iko hivyo, kwa nini unafanya maamuzi
mabovu ambayo yanakupotezea pesa nyingi na kwa kiasi kikubwa? Kuwa makini sana
na matendo yako ili yasikupotezee pesa ambayo ni moja rasilimali muhimu
kukusaidia kufanikiwa.
Hapo ulipo najua una pesa za kiasi fulani hata kama
ni ndogo, najua una muda na nguvu fulani, sasa kwa nini hivi vitu usivitumie
kwa uangalifu ili viweze kukusaidia kukupa mafanikio makubwa na badala ya
kuvipoteza tu kiholela.
Tumia kidogo ulichonacho, ili kufanikiwa. |
Watu matajiri, wanajua namna ya kutunza pesa zao
vizuri, kwa nini wewe usiwe miongoni mwao? Huna pesa za kutosha si kwa sababu
pesa zinakukimbia bali ni kutokana na matendo yako yanayofukuza pesa.
Kitu cha kufanya jiulize, ni hatua zipi utaweza
kuzichukua ili kuweza kulinda hata zile rasilimali zako za kukusaidia
kufanikiwa ambazo ni pesa, muda na nguvu zako. Kama hujui tafuta watu wenye mafanikio kisha
wafatilie na ujue nini cha kufanya.
Lakini kitu ambacho nataka uelewe hapa jifunze sana
kutumia kile kidogo ulichonacho kikusaidie kufanikiwa. Najua unaelewa wapo watu
ambao wanadharau sana hasa ikiwa wanacho kile kidogo.
Watu hawa mara nyingi hawajui thamani ya kutumia
kile kidogo walichonacho. Iwe ni pesa kidogo watazitumia hovyo mpaka
zitakwisha. Iwe ni muda kidogo pia watautumia hovyo hata bila kupata faida ya
muda huo.
Kwa kuwa wewe umeshalijua hili leo, amua kutumia kiasi
kidogo cha pesa ulichonacho kwa busara ili kikusaidie kutengeneza pesa nyingi. Pia
amua kutumia muda, nguvu zako au chochote ulichonacho ambacho unaona ni kidogo
kikusaidie kufanikiwa.
Hata Musa wakati anawaongoza wana wa Israeli kuvuka
bahari ya shamu, alitumia fimbo aliyonayo kupiga bahari na ikagawanyika, hapo ndipo wana wa Israeli wakaokolewa.
Leo hii ni kipi ambacho huna. Najua una kidogo
ulichonacho ila hujaona sana kama kinaweza kukusaidia. Sasa hebu anza leo
kukiangalia kwa jicho la tofauti ili kikusaidie kujenga mafanikio makubwa.
Kabla sijaweka kalamu yangu chini pengine nikwambie
hivi, kama unabomoa misingi hii ya kushindwa kutumia kile angalau kidogo
ulichonacho kwa busara na vizuri…kufanikiwa kwako itabaki kuwa hadithi.
Hiyo iko hivyo kwa sababu, mafanikio yanajengwa na
vitu vidogo vidogo sana ambavyo mwanzo huonekana si kitu wala si chochote,
lakini vitu hivyo ndivyo hatimaye vinavyofanya mafanikio yakaonekana kwa nje.
Sasa wewe ni nani hadi ufanikiwe wakati unajiona
kabisa unavunja sheria za asili za mafanikio? Huwezi kufanikiwa. Ila kikubwa utakachofanya
ni kujidanganya tu kwamba ipo siku lazima nitafanikiwa.
Mpaka hapo ulipo jiulize je, hicho ulichonacho unakitumia
kwa vizuri ili kikusaidie kupata kingine kikubwa? Lakini ikiwa unataka kufika
katika ngazi fulani ya mafanikio, huku hapo ulipo hujiwekei misingi imara
hutaweza kufika huko.
Kila wakati jitathimi katika kila eneo unalotaka
kufika kwa kujiuliza je, kile kidogo ulichonacho unakitumia ili kukusaidie
kufanikiwa? Ukiweza kupangilia vizuri matumizi ya kidogo ulichonacho na kuhakikishia
UTAFANIKIWA.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI
NGWANGWALU,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.