Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, June 4, 2015

Mambo 7 Yanayofanya Maisha Yako Kuwa Magumu.

No comments :
Maisha tuliyonayo huwa sio magumu sana kama wengi tunavyofikiri. Ugumu wa maisha mara nyingi huwa tunautengeneza wenyewe bila kujua. Huwa ni watu wa kufanya maisha yetu magumu kutokana na fikra ama maneno ambayo tunayasema na kujiambia mara kwa mara juu ya maisha yetu. Kwa wengi huwa tuna kawaida ya kujiambia maisha yetu ni magumu, hatujiwezi na wala hatuna haki ya kupata mfanikio makubwa.

Lakini sio maneno peke yake tu hata matendo na mienendo na tuliyonayo kila siku, pia huweza kufanya maisha yetu kuwa magumu kwa namna moja au nyingine. Kwa kadri tunavyozidi kujiambia maneno hasi na kuwa na matendo ama mienendo mibovu, ndivyo tunavyojikuta tukizidi kuharibu masha yetu. Hivyo tumekuwa tuna mchango mkubwa wa kubomoa maisha yetu sisi wenyewe bila kuelewa ukweli wa hilo.

Ni wakati umefika wa kuweza kutambua mambo yanaharibu maisha yetu. Hatuna haja tena ya kulaumu na kupiga kelele kila wakati kuwa ‘Maisha yetu ni magumu sana’. Inatakiwa tuijue kweli itakayoweza kutuweka huru na kutoka kwenye ugumu wa maisha. Tuache tabia ya kung’ang’ania mambo yanayotuharibia maisha yetu, vinginevyo hatutafika mbali. Mambo tunayotakiwa kuyajua na yanayofanya maisha yetu kuwa magumu ni kama haya:- 

1. Kupoteza pesa zisizo za lazima.
Hiki ni kitu ambacho kimekuwa kikiwatoa wengi katika mstari wa mafanikio. Wengi wetu mara kwa mara tumekuwa tukijiingiza katika matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanatupotezea pesa nyingi. Pesa hizo zinapopotea huwa siyo rahisi sana kugundua kwa sababu ya udogo wake na kutokujali.

Tuchukulie mara kwa mara umekuwa ukiacha pesa ndogo ndogo zile unazoziita ‘chenji’ dukani. Na hiyo haitoshi umekuwa ukitoa ofa bila kujiuliza kwa rafiki zako. Pesa za namna hii ikifika muda kama miezi miwili ama mitatu  zinakuwa nyingi, kiasi kwamba kama ungezitunza ungeweza kuanzisha kitu cha maana cha kukusaidia.


Kwa matumizi kama haya kwa kadri tunavyozidi kuyaongeza, ndivyo tutakavyojikuta tunazidi kupoteza pesa nyingi na kufanya maisha yetu kuwa magumu siku hadi siku. Wengi wetu tunao lalamika ‘Oooh maisha yangu ni magumu’ ukija kuchunguza kidogo,  hao ndio huwa wa kwanza kwa matumizi mabaya ya pesa zao pale wanapozipata.

Nini Kifanyike Sasa?
Kwanza, tujaribu kujikagua mwenyewe binafsi na kuangalia jinsi tunavyotumia pesa zetu. Kama matumizi ni ya hovyo, ni muhimu kujirekebisha na kuwa na matumizi mazuri ya pesa yatakayoweza kutuongoza kwenye maisha bora. Pili, tuwe tuna bajeti maalum inayotuongoza na sio kutumia pesa tu kwa sababu eti zipo mfukoni.

2. Kutumia muda mwingi kuwa na watu hasi.
Muda mwingi tumekuwa tukiishi maisha na watu hasi ambao   wamekuwa wakiturudisha nyuma sana. Tumekuwa tukiishi na watu hawa wanaotukatisha tamaa na kutuonyesha kila aina ya ubaya katika maisha yetu. Kwa kuendelea kuishi na watu hawa, ndivyo ambavyo tumekuwa tukijikuta tukifanya maisha yetu kuwa magumu zaidi.

Watu hawa wamekuwa wana nguvu kubwa hasi, ambayo imekuwa ikituvuta na kujikuta tukitenda mambo mengi kwa mkabala hasi na kuharibu maisha yetu. Ni watu ambao tumekuwa tunao, tukiishi nao kila siku. Inawezekana wakawa ni ndugu, jamaa au hata marafiki zetu wa karibu sana ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa mambo mengi.

Kipi kifanyike sasa?
Kikubwa ni kuanza kuanza kuishi na watu chanya ambao kwa vyovyote vile watatusaidia kutufikisha kwenye ndoto zetu bila kigugumizi. Chagua watu marafiki ambao utafurahia kuwa nao na wataweza kukusaidia kukufikisha kwenye ndoto. Kuwa chanya ni siri mojawapo nzuri ya kukufikisha kwenye mafanikio.

3. Kupoteza muda sana.
Hili ni moja ya jambo muhimu ambalo limekuwa likitupoteza na kutuvuruga bila kujua. Hii yote huwa inakuja ama kutokea kutokana na wengi wetu kujikuta ni watu wa kupoteza muda bila sababu ya msingi. Kitu usichojua kwa kadri unavyozidi kupoteza muda wako, ndivyo unavyozidi kupoteza maisha yako na kuzidi kufanya maisha yako kuwa magumu zaidi.

Kwanini hii huwa iko hivyo? Hii ni kwa sababu muda wako unahusika sana katika shughuli nzima ya uzalishaji. Hivyo kwa vyovyote vile kwa kadiri unavyopoteza muda wako, ndivyo ambavyo unapoteza masaa ya uzalishaji. Ukijaribu kuchunguza utagundua ukweli huu kuwa wengi wetu ni watu wa kupoteza muda bila sababu ya msingi.

Ni nini cha kufanya sasa?
Ili utuweze kuondokana na hali hiyo ni vyema tukajifunza kutunza muda wetu na kwenda na ratiba. Ni lazima tujue muda fulani tutakuwa wapi na tunafanya nini? Siyo suala la kuamka tu na kujiendea. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunauokoa muda mwingi ambao utatusaidia, badala ya kuupoteza na kuwa majuto kwetu.

4. Kuahirisha mambo.
Kwa sehemu wengi wetu tumekuwa kama ni watu wenye  ugonjwa fulani kuhusu hili. Tumekuwa ni watu ambao kila mara tunaahirisha kazi ambazo tulitakiwa kuzifanya mara moja, pengine hata bila sababu. Hata tu pale inapotokea kazi nyepesi nayo pia huweza kuahirisha na kusogezwa mbele zaidi.

Kwa maisha hayo ya kuahirisha kwa uhakika na ukweli uliowazi hatuwezi kufanikisha lolote katika maisha yetu. Hili ni mmoja ya jambo dogo lakini ambalo limekuwa likifanya maisha yetu kuwa magumu. Jaribu kufikiri kazi zote ambazo umewahi kuziahirisha jinsi ambavyo kwa baadae zinavyoweza kuwa ngumu kutokana na uharaka unaokuwa nao.

Kitu cha kufanya ili usiahirishe mambo yako tena.
Jambo lolote lile tunalotakiwa kulifanya kwa namna yoyote ile, hatutakiwi kuwa wepesi wa kulisogeza mbele. Kwa kulisogeza mbele, tutambue kuwa, tutakuwa tunaleta ugumu bila ya sisi wenyewe bila kujua. Tufanye mambo yetu leo leo na tuachane na habari ya kesho hiyo itakuwa inatupotezea muda mwingi.

5. Kuwa msemaji na mlalamikaji sana.
Hakuna mtu atakayeweza kusimama na kupigania maisha yetu kama wengi tunavyofikiri. Maisha yetu ni maisha yetu hata iweje yatabaki kuwa yetu na sisi ndiyo waamuzi wa mwisho wa kutaka maisha yetu yaweje. Wengi wetu kwa kutokujua hujikuta ni watu wakulaumu tu kuwa maisha yetu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa ama kuharibiwa na wengine.

Kwa kulalamika kwetu hivyo haiwezi kusaidia hata tufanye nini, zaidi kutufanya tuzidi kurudi nyuma bila sisi wenyewe kujitambua. Tangu tuanze kulalamika tujiulize tumebadili maisha yetu kwa kiasi gani? Nina uhakika hakuna kitu ambacho tumebadilisha zaidi tu ya kuweza kuumia na kuteseka na kulalamika kwetu huko.

Tufanyaje  sasa?
Kitu cha kufanya hapa ni kuchukua hatua chanya yenye nia halisi ya kubadilissha maisha yetu. Tuache kufanyia kazi kwenye midomo na ni lazima tuchukue hatua kwa vitendo tena kwa haraka vitakavyoweza kutubadilisha na hali zetu kwa sasa na baadae.


6. Kutaka Kufanya mambo mengi kwa pamoja.
Ni kweli wengi wetu huwa tuna nia ya kutaka kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yetu. Mabadiliko ambayo huwa tunataka ni kuona kuwa maisha yetu tuliyonayo yanabadiklka ikiwezekana kwa haraka tena sana. Kutokana na wengi wetu kuwa na kiu hiyo hapo ndipo huwa tunajikuta tukifanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Kwa kufanya mambo hayo kwa wakati mmoja ndivyo ambavyo wengi huweza kujikuta ufanisi ukipungua na kushindwa kufanikisha hata malengo yetu. Hili ndilo kosa ambalo pia hupelekea wengi kuanza kuishi maisha magumu kutokana na mambo mengi kutoleta matunda yaliyotarajiwa.

Kipi kifanyike?
Pamoja na kuwa tuna nia kubwa ya kufanikiwa kitu kimojawapo cha muhimu cha kuanza kufanya  ni kuhakikisha kuwa hatufanyi mambo mengi kwa wakati mmoja. Ni bora tukafanya mambo kwa wakati ili kuleta manufaa zaidi.

7. Kutaka kuepuka makosa sana.
Kama tutakuwa tunaishi maisha ya kuogoapa sana kutokukosea na kutaka tuwe tu sahiihi muda wote, basi ni wazi kuwa hatutaweza kufika mbali sana katika mafanikio yetu. Kutokana na hili la wengi kupelekea kuepuka makosa hujikuta ndivyo ambavyo maisha yatu kuwa magumu zaidi.

Kwa kifupi hayo ndiyo mambo yanaweza kufanya maisha yetu yakawa magumu kwa namna moja ama nyingine. Kitu cha kufanya tuchukue hatua zaidi ili kuweza kubadilisha maisha yetu.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE, 

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment