May 12, 2015
Kanuni 12 Za Kukuongoza Kwenye Njia Sahihi Ya Kuufikia UTAJIRI.
Wataalamu mbalimbali wa mambo ya mafanikio wameweza kuthibitisha kuwa iko sayansi ya kuwa tajiri na ni sayansi hasa , kama ilivyo hisabati za aina mbalimbali. Sayansi hii ambayo wataalamu hawa wanaizungumzia ni rahisi kuifuta na ambayo mwanadamu yeyote anaweza kuitumia kuweza kufikia mafanikio makubwa anayotaka kama tu ataamua kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa sayansi hii
inadai kuwa katika maisha yetu tuwe tunajua ama hatujui lakini zipo sheria au
kanuni fulani zinazotawala mchakato mzima wa kupata utajiri, na mara nyingi
sheria hizi zinapoeleweka kwa mtu ama kufuatwa, mtu huyo atakuwa na kila
uwezekano wa kuwa tajiri katika maisha yake, bila kizuizi chochote kile.
Ni kweli. Wale waliofanikiwa
na kuwa matajiri, hujua namna wanavyoupata
kwa kufuata misingi, sheria na taratibu ndogondogo tu. Wale
wasiofanikiwa kuwa matajiri huwa hawajui sheria hizi ndogondogo na hivyo
huishia kudhani kwamba utajiri ni matokeo ya bahati au matokeo yasiyotarajiwa
ama kitu fulani cha ajabu ama cha kijinga.
Anthony Robbins ni mmoja wa
watu waliofanikiwa sana katika kuwafundisha watu mbinu za kufanikiwa, akiwa pia
anawafundisha wanamichezo kadhaa maarufu duniani, watu matajiri wakubwa na
wakuu wa makampuni zaidi ya 500. Kupitia yeye ameweza kutengeneza matajiri
wengi sana duniani kutokana na sayansi
ya mafanikio anayofundisha.
Katika taratibu yake
anayoiita FIKA HADI UKINGONI , Anthony
Robbins anaorodhesha kanuni ama sheria 12 za msingi anazosema ndizo zinazowaongoza
watu wengi kuweza kuufikia utajiri. Kiu na matamanio yake nikuona kila mtu
kufikia mafanikio makubwa sana. Kanuni hizo anazoziorodhesha ni hizi zifuatazo:-
1.
Kuwa na maamuzi sahihi ya kuwa tajiri.
Mara nyingi watu wanaokwama
huwa hawaamui ama kuwa na mwelekeo wa moja kwa moja wa utajiri wanaoutafuta.
Hili ni wazi kabisa. Ili uweze kufanikiwa ni lazima kuwa na maamuzi sahihi na
kuweza kujua umbali wa kule unakoelekea kabla ya kuanza kuufukuzia utajiri
unaoutaka. Kaa chini, kisha chukua maamuzi ya kuwa tajiri. Kama hujafanya
uamuzi, huwezi kuwa tajiri.
2.Tambua
kuwa utajiri ni kitu kinachowezekana.
Kwa kawaida mtu ana uwezo wa
kufanikisha kile anachokiona katika mawazo yake na siyo zaidi ya hapo. Kama
wewe ni mtu wa fikra hasi na kuona kuwa utajiri ni kitu ambacho hakiwezekani,
huo ndio ukweli hautaweza kuwa tajiri katika maisha yako yote hata ufanyaje.
Kitakachokufanya usifanikiwa si kingine ni mtazamo wako tu. Badili mtazamo wako
na amini kuwa unao uwezo wa kuwa tajiri, utafanikiwa.
3.
Anza kufanyia kazi ndoto zako mara moja.
Siri kubwa ya mafanikio ni
kuanza kufanyia kazi ndoto zako mara moja na kuachana na hali ya kusitasita.
Watu wasiofanikiwa mara nyingi huwa hawaanzi kabisa. Ikiwa utaendelea kufikiria
unalofikiria litaendelea kubaki hivyo milele. Ili uweze kuwa tajiri ni lazima
uanze , popote, si lazima iwe mahala maalum kama unavyofikiri, wewe anza tu,
mambo mengine yatajipanga mbele ya safari.
4.
Kuwa na mipango ya uhakika.
Kama unataka kufanikiwa
zaidi kwa kitu unachokifanya sasa, tafuta njia ya kufikia mafanikio yako kutoka
kwa mtu mwingine aliyewahi kufanikisha hilo. Weka mipango ya uhakika na
inayowezekana kwako kutekelezeka. Jifunze haya kwa waliofanikiwa kabla yako.
Lakini usiachane na uwezo wako wa kufikiria na kuangalia mambo mengine ya ziada
yatakayo kuwa msaada kwako pia katika kukufanikisha.
5.
Jiwekee utaratibu wa kufuatilia mipango yako.
Kuwa na mipango ya uhakika
peke yake haitoshi. Ili uweze kufanikiwa na kuwa tajiri ni muhimu kwako pia
kujijengea utaratibu wa kuifatilia mipango yako kwa karibu sana. Kama hutoweza
kufanya hivyo, itakuwa ni ngumu kufanikiwa kwa sababu mambo yako mengine
hayatafanyika kwa uhakika. Jaribu kujiuliza, ikiwa hufuatilii mipango yako nani
ataifatilia? Kazi yako inakuwa ni kupanga tu, unaanza, halafu kufuatilia
hakuna.
6.
Jifunze kutekeleza majukumu yako kwanza.
Ili kufanikiwa ni vyema,
kufanya kitu mwenyewe kwanza. Hiyo itakusaidia kukielewa wewe mwenyewe, hata
ukitoa jukumu la utekelezaji wake kwa mwingine ni sawa. Acha kutoa majukumu kwa
wengine sana na hata kujisahau wewe mwenyewe. Unapotoa majukumu sana kwa
wengine kinachokutokea, unakuwa hujifunzi namna ya kutekeleza mambo kwa ufanisi
na hata ikitokea kushindwa unakua hujui kwa nini ulishindwa.
7.
Fanya utajiri kuwa ni kitu cha lazima.
Katika maisha yako ili uweze
kufanikiwa na kuwa tajiri, weka utaratibu wa kufanya utajiri kuwa ni kitu cha
lazima na siyo jambo la hiari tu. Kwa kufafanua hili namaanisha kwamba, ni
kuelekeza matakwa yako yote, nia yako yote. mwelekeo wako wote, kwenye
mtiririko mmoja wa kuelekea kwenye lango kuu la utajiri. Ukiweza kuitumia
kanuni hii ndogo katika maisha yako ni lazima ufike ukingoni na kuwa tajiri.
8.
Kuwa king’ang’anizi katika maisha yako yote.
Kitu kitakachokufanya kuwa
tajiri katika maisha yako ni kuwa na uwezo wa kupambana na vikwazo mpaka mwisho
na sio kukata tamaa na kuacha. Tambua kwamba, katika safari ya mafanikio
kukutana na vikwazo ni kitu ambacho hakikwepeki na vikwazo vyote ni nafasi ya kufanikiwa vilivyo
vaa nguo za kazi, kumbuka hilo. Hivyo, zoea jambo hilo na kuwa king’ang’azi
bila kuchoka mpaka uufikie utajiri.Utaweza tu kufika kule unakotaka, ikiwa uko
tayari kupambana na vikwazo vinavyotekea njiani.
9.
Andaa bajeti maalumu itakayokuongoza.
Kitu ambacho unakihitaji
sasa, ili uweze kuelekea vizuri kwenye utajiri ni bajeti. Ni kweli, unahitaji
kuwa na bajeti na taarifa nyingi za matumizi na mapato ya fedha zako binafsi na
za biashara zako. Ikiwa hutaweza kuweka kumbukumbu za fedha zako, itakuwa ni
rahisi kwako kutokujua wakati unapopoteza fedha zako bila sababu hadi hali
itakapokuwa mbaya kabisa. Hii ni kanuni bora kwako ambayo unaweza kuanza
kuitumia sasa.
10.
Simamia maamuzi yako.
Ni lazima ufahamu kwamba
siku zote watakuwepo watu wasiokubaliana na jinsi unavyofanya mambo yako, walio
na wasiwasi na wanaojaribu kukurudisha chini kwa kila njia. Watu hawa wanaweza
kuwa marafiki zako wa karibu wakati mwingine, ama hata ndugu zako. Huwezi
kulizuia wala kulibadili hilo, wanayo haki ya kuwa kama walivyo. Katika hili
usifanye kosa la kuruhusu mawazo ya watu wengine kuathiri maamuzi yako bila
sababu ya maana. Simamia maamuzi yako unayoyaamini mpaka ufanikiwe.
11.
Jifunze kutokana na makosa.
Watu waliofanikiwa ni watu
wenye tabia ya kujifunza kutokana na makosa waliyoyafanya. Ikiwa kuna kushindwa
wanakuwa wanataka kujua ni kwanini walishindwa. Hivyo kama kuna uwezekano
wanakuwa wanatafuta njia nyingine mbadala ya kuweza kuepuka hayo makosa na
kufanya mambo yao kwa ufanisi zaidi mpaka kuweza kufikia lengo. Hii ni moja
kati ya kanuni rahisi ambayo unaweza kuitumia na kufanikiwa sana.
12.
Endelea kujifunza zaidi.
Hiki ni kitu muhimu sana
kwako leo na katika maisha yako yote. Unatakiwa kuendelea kujifunza kila siku
bila kuchoka. Watu waliofanikiwa sana huhudhuria semina, husoma vitabu,
magazeti, hujiunga na vikundi na warsha mbalimbali zinazohusika katika maeneo
hayo. Pia kuna wakati hutafuta watu wa kuwashauri na hata kuajiri washauri
binafsi katika maisha yao ili tu kuhakikisha ni lazima wanafanikiwa,. Hii ni
sheria ya msingi sana kwako kuijua na kuitumia ili kuufikia utajiri.
Tunakutakia mafanikio mema,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Nashukuru Sana kwa waandishi.mambo mengi nimeweza kujifunza ambayo natakiwa kuyafanya ili kufanikiwa na nitaendelea kufatilia na kuyatendea kazi asanteni Sana.
ReplyDelete