Apr 14, 2016
Maadui Wakubwa Wa Mafanikio Walio Ndani Yako.
Wengi kulingana na uzoefu tumezoea kuona maadui
wengi wa mafanikio yetu walio nje yetu. Mara nyingi tunakuwa hatuko tayari
kukubali kuwa rafiki na mtu ambaye kwa namna moja au nyingine tumetambua ya
kwamba yeye ni kikwazo au adui wa mafanikio yetu, naamini hili unalijua vizuri.
Kwa hilo huwa tupo tayari kumweka kando mtu huyo kwa sababu ni chanzo cha kutufanya tushindwe kufanikiwa.
Hata hivyo pamoja na kuwa makini na wale tunaomini
ndio maadui wa mafanikio yetu, tumekuwa tukisahau kwamba wapo baadhi ya maadui wakubwa wa mafanikio ambao wako
ndani yetu. Kwa bahati mbaya sana maadui hawa tumekuwa hatupo makini nao sana
lakini ndio wamekuwa wakituzuia kufanikiwa kuliko hata wale maadui wa nje
tunaowajua. Je, unajua hawa ni maadui wapi ulionao na wanakufaya ushindwe
kufanikiwa?
1. Woga.
Kati ya kitu ambacho kinamsumbua sana binadamu ni
pamoja na woga. Binadamu kwa kawaida kimaumbile ni mtu wa kuogopa mambo mengi
sana ikiwemo hata woga wa mafanikio yake. Woga huu mara nyingi hupatikana kutokana
na kujifunza, uzoefu au kusikia lakini ukija kuungalia hata kile kinachoogopwa
kinakuwa sio halisi ama kwa lugha nyingine tunaweza kusema hakipo.
Inapofika mahali ukawa una woga mkubwa ndani yako
suala la kufanikiwa katika maisha linakuwa ni gumu. Hiyo yote inakuwa ni kwa
sababu hakuna hatua ambayo utaweza kuichukua zaidi ya wewe kuogopa na kujihisi
hutaweza. Kwa hiyo kama unaendekeza woga, tambua huyo ni adui mkubwa sana aliye
ndani yako ambaye anakuzuia kufanikiwa. Waangalie watu wengi waoga maisha yao
huwa ni ya kushindwa sana karibu siku zote.
Toa woga, utatengeneza mafanikio makubwa. |
2.
Wasiwasi.
Tukiachana na suala la woga pia adui mwingine
ambaye binadamu anambeba ndani yake ni wasiwasi. Watu wengi wanakuwa ni watu wa
kutilia wasiwasi au mashaka kwa mambo wanayoyafanya au wanayotaka kuyafanya. Utakuta mtu
anataka kufanya kitu fulani lakini ndani yake kunakuwa kuna maswali mengi sana
ndani yake anayojiuliza kama ‘hivi kweli
hapa nitafanikiwa’ na je ikitokea nimeshindwa itakuwaje?’.
Kwa wasiwasi huu mwingi ambao wengi wanakuwa nao
unakuwa unawafanya kushindwa kufanikiwa. Utakuta kweli mtu huyu amefanikiwa
kuushinda woga na kujaribu kuchukua hatua. Lakini, kitendo cha kuthubutu huku
ukiwa na wasiwasi mkubwa ndani yako wa ‘sijui nitafanikiwa au nitashindwa,
huwafanya kushindwa moja kwa moja. Na hii huwa inatokea kwa sababu ya mawazo ya
kina yanakuwa yanaamini kile unachokihofia ndicho unachokitaka mwisho wa siku
unajikuta umeshindwa.
3. Imani potofu.
Maisha yote ya mafanikio yanaongozwa na imani. Unaweza
ukawa una mipango na malengo mazuri kabisa ya kukusaidia kufanikiwa, lakini
kitu cha kujiuliza je una imani inayokusaidia kufikia mafanikio hayo? bila kuwa
na imani sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio ni rahisi kushindwa. Watu wengi
wanakuwa wanatafuta mafanikio lakini huku ndani mwao wakiwa na imani hasi, imani
potofu ambazo zinawazuia kufanikiwa.
Kwa mfano utakuta mtu anatafuta mafanikio lakini
wakati huo huo ndani yake anaamini watu wanaofanikiwa ni wezi, mafisadi au
wanyonyaji kwa wengine. Kwa imani kama hizi kufanikiwa inakuwa ni ngumu kwa
sababu ndani yako unakuwa na imani potofu inayokuzuia kufanikiwa huko. Ni lazima
kujenga mtazamo chanya ambao utakupa mafanikio. Acha kuwaza hasi ama kujenga
imani potofu utakwama kufikia mafanikio yako makubwa.
4. Maamuzi
mabovu.
Kila mtu katika maisha yake ana maamuzi ya aina fulani
ambayo anayatoa kila siku. Kwa maaumuzi hayohayo hupelekea maisha yako kuwa mabaya
au mazuri. Kama ndani yako unabeba maamuzi mabaya kila wakati basi elewa una adui
mkubwa anayekuzuia kufanikiwa. Kwani kwa kuwa na maamuzi hayo itasababisha
maisha yako kuwa mabovu na ya ajabu sana.
Kwa mfano maisha yako yapo hivyo kwa sababu ya maamuzi
ambayo ulishayafanya siku za nyuma. Kama ulifanya maamuzi mabovu ndivyo na
maisha yako yalivyo sasa. Kuwa na maamuzi mabovu ni adui mkubwa sana aliye
ndani yako ambapo usipokuwa makini anaharibu sana maisha yako pasipo wewe
kujua. Kitu cha msingi kwako ni kuwa makini na kujifunza kuwa na maamuzi sahihi.
Kinyume cha hapo utapotea.
5. Hamasa.
Ili ufanikiwe ni lazima uwe na hamasa kubwa sana
ndani yako kila siku. Bila kuwa na hamasa hakuna mafanikio utakayoweza
kuyafikia. Kwa bahati mbaya au nzuri hamasa huwa zinaanzia ndani mwetu. Kama ikitokea
umekosa hamasa pole pole unakuwa umebeba adui wa kukuangusha bila kujijua. Kwa hiyo
unahitaji kujijengea hamasa ili uweze kufikia mafanikio yako kwa kiasi kikbwa
siku hadi siku.
Kwa vyovyote vile, ni lazima kupambana na maadui
hao walio ndani yetu ili kufikia mafanikio makubwa. Chukua hatua mapema za
kubadili maisha yako.
Nakutakia kila la kheri na endelea kujifunza
kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Blog;- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.