Sep 14, 2016
Sababu Moja Muhimu Inayofanya Utajiri Wako Uchelewe.
Kwa jinsi binadamu
tulivyo, tunaweza kuona vitu vyote ambavyo havionekani mbele ya macho yetu.
Ukifuatilia kwa undani unagundua kuwa vitu ambavyo tunaambiwa na kuamini kuwa
havionekani, kiuhalisia vitu vyote vyaweza kuonekana endapo ukiamua. Kwa
mazoea, wengi tunafikiri kwamba kama kitu hakionekani mbele ya macho yetu ya
kawaida, basi tunasema hakipo.
Ajabu na kweli ni kwamba, mtu asipoona kitu kwa macho yake ya kawaida,
basi usidhani kwamba kitu hicho hakionekani na wengine ufikiri kwamba kitu
hicho hakipo kabisa duniani. Kumbuka kuwa kuendelea kufikiri na kuamini kwamba
kitu fulani hakionekani au hakipo haina maana kwamba hakionekani kwa wengine!
Wewe usipoona wengine wanaona.
Tunapodhani kwamba kitu fulani hakipo duniani, wakati kipo, moja kwa
moja tunapoteza uwezo wetu wa ndani na nje wa kukifanya kile kisichoonekana
kionekane mbele ya macho ya wengi.
Kwa binadamu ni akili yake pekee iliyo na uwezo wa kuona vitu vyote
vinavyoonekana na visivyoonekana. Unapofikiri kwa kutumia akili (ubongo), hapo
tunasema kuwa umeona kwa macho ya akili au ubongo. Pia, kile uonacho kupitia
fikra zako, ndicho ambacho hukusukuma wewe kutumia rasilimali zilizopo, ili
kukiweka katika uhalisia.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya “kuona” na “kutazama”.
Kutazama siyo kuona, na kuona ni zaidi ya kutazama. Dhana nzima ya “KUONA” ni
pale tunapoweza kutumia akili kuota ndoto, halafu tukapiga picha, halafu
tukapanga, tukaamini, na kisha tukatenda.
Kwa maana nyingine ni kwamba, akili (ubongo) ni kiwanda na karakana ya
kuzalisha mambo mapya. Lakini pale tuonapo picha ya kitu kutokea nje (kwa macho
ya kawaida), basi huko siyo “kuona” bali ni “KUTAZAMA”.
Binadamu wengi tunao uwezo wa kuona kila kitu endapo tunataka kufanya
hivyo. Pamoja na uwezo mkubwa tuliopewa, bado hatuutumii katika kuona fursa za
kujiondoa kwenye majanga ya umaskini.
Watu waliofanikiwa mara nyingi wanatwambia kila siku kuwa popote tulipo
Tanzania tumezungukwa na fursa nyingi. Kwanini sasa watu wengi ni maskini
katika nchi iliyo na fursa nyingi? Jibu ni moja tu nalo ni “watu
wengi hawaoni fursa bali wanatazama fursa”.
Utajiri wa uhakika hautapatikana kutokana na watu wengi kutazama fursa
BALI ni pale tu watu watakapoweza kutumia akiri zao kuona fursa na kisha kuanza
kuchukua hatua za maksudi ili kuzifikia fursa hizo.
Kumbe watu wengi tumekuwa ni watu wa “kutazama” fursa na
siyo “kuona” fursa. Unapoona fursa unakuwa na ujasiri, nguvu
na shauku ya kutenda ili kufaidi fursa husika. Lakini unapotazama fursa, mara
nyingi unajawa sana na uoga, hofu inayotokana na wewe kukosa majibu muafaka ya
maswali unayojiuliza baada ya kuona kwa macho yako kile kilichofanywa na
wenzako.
Unapotazama kitu kilicho mbele ya macho yako, mara nyingi utajiuliza
maswali mengi bila majibu juu ya jinsi kilivyotengenezwa. Unapokosa majibu
sahihi ya maswali yako, mara nyingi utapata hitimisho moja tu! Nalo ni
“HAIWEZEKANI”.
Ukishajiridhisha kuwa haiwezekani, basi unaamua kwenda kutazama fursa
nyingine ambayo nayo utapata hofu na woga wa kuifanyia kazi. Mwisho wake
unaishia kuwa ni mtu wa kutazama na kuongea tu! Huku ukizidi kuandamwa na
maisha ya taabu na umaskini.
Watu wenye kuona fursa ndio wenye “maono”. Maono ni ndoto kujumlisha na
ukweli wa mambo. Ukiwa na maono yafanyie kazi. Tumia macho ya akili au ubongo
kuona fursa.
Ukitumia macho ya ubongo au akili, utaweza kuona vinavyoonekana na
visivyooekana. Fursa za uhakika hazionekani kwa macho ya kawaida.
Usipoona fursa machoni mwako haina maana kwamba fursa hizo hazipo! ni uamuzi
wako tu! ukiamua zionekane na ziwepo basi, itakuwa hivyo.
Lakini, ukiamua zisiwepo basi, hazitakuwepo wala hazitaonekana mbele ya
macho yetu ya kawaida. Jambo hili aliwahi kulisisitiza mwanafalsafa wa
Kifaransa aliyejulikana kama Henri Bergson kuwa “Jicho linaona kile
ambacho akili iko tayari kukiona au kuelewa”
Kutokana na maneno hayo ya Bwana “Henri Bergson”, tunajifunza kwamba
fursa ambazo hazionekani machoni mwako, ni lazima uziite wewe mwenyewe ndipo
zitakuja kwako na usipofanya hivyo watu wengine watafanya hivyo, mwisho wake
fursa ulizotakiwa kuzifaidi wewe, utabakia KUZITAZAMA kwa jirani.
Endapo jirani au watu wengine wasipoziita fursa hizo, basi zitaendelea
kubakia katika hali yake hiyo ya kutoonekana, mpaka zitakapoitwa na vizazi
vijavyo.
Leo hii Tanzania kama taifa tunaishi maisha duni kutokana na ukweli
kwamba watu wengi wanaanzisha miradi ya biashara baada ya kutazamia kwa
wengine. Ni bora ukaona mradi anaoufanya mwingine kuliko kuutazama.
Watu wengi hasa Tanzania, huwa hawaoni miradi bali huitazama tu basi.
Kwa maana nyingine ni kwamba, unapoona mwenzako akijishughulisha na mradi
fulani wa kibiashara na wewe ukafanya kama anavyofanya bila kuongeza kitu
chochote kipya, basi ujue kuwa mradi huo “haujauona” BADALA
yake “umeutazama” tu!.
Ni nini faida za kufanya mradi ambao umeuona?
Kimsingi nchi inapokuwa na watu wengi ambao tunafanya miradi tunayoiona
kwa macho ya ubongo au akili zetu, ni wazi kwamba tutakuwa na uwezo mkubwa wa
kutatua changamoto na kero nyingi ambazo zinasababisha maisha magumu kwa jamii
tunayoishi nayo.
Pili, tutaweza kutengeneza bidhaa na huduma za thamani kubwa kwa watu wa
Tanzania na dunia kwa ujumla. Tatu, tutasaidia katika kuharakisha ukuaji wa
uchumi wetu binafsi na taifa letu kwa ujumla.
Watu wengi tukiona na siyo kutazama miradi ya maendeleo, tutaweza kutegeneza
bidhaa nyingi ambazo ni tofauti tofauti. Tukiwa na bidhaa nyingi zenye ubora wa
hali ya juu, ni wazi kwamba tutaweza kuvuta pesa nyingi kutoka kwa watu wengine
hasa nje ya nchi. Watu wenye pesa zao, watapenda watume pesa zao kwetu, ili
kupata bidaa na huduma na hivyo kutufanya sote tuwe na pesa nyingi.
Kwa ngazi ya kitaifa ni kwamba watu kutoka mataifa ya nje watapendelea
kutuma pesa zao Tanzania ili kununua suruhisho tulizonazo juu ya changamoto
walizonazo kwao – hali hii ndiyo itachangia uwepo wa ajira na hatimaye nchi
kuwa na uchumi mkubwa.
Hili tuwe na uwezo wa kuona miradi tufanye nini?
Katika hili hakuna namna na hakuna njia muafaka zaidi ya kuzidi kuwekeza
sana kwenye fikra. Ninaposema kuwekeza kwenye fikra ni zaidi ya watu kusoma
hadi vyuo vikuu au kubobea kwenye taaluma fulani.
Uwekezaji mzuri kwenye fikra ni ule ambao unajifunza kila siku kwa
kutumia njia mbalimbali, kama vile kujenga tabia ya kuwa mdadisi wa kila
jambo/kitu na hasa yale yanayohusu kile ambacho unakifanya au unatarajia
kukifanya.
Kabla ya kuanzisha mradi wako hakikisha unafanya utafiti wa kero na
changamoto zinazowakabili watu waliokuzunguka au wengine wa mbali --- kwa
kawaida kero inayo wapata watu waliokuzunguka mara nyingi huwa inawapata pia
watu wengi walioko mbali na wewe.
Uzuri wa uwekezaji katika fikra hauna usumbufu na wala hauhitaji gharama
kubwa. Kinachohitajika ni nidhamu ya kufanya kile ulichopanga kukifanya hata
kama ni kigumu. Kwahiyo, huu ni uwekezaji ambao unaweza kufanywa na karibu wa
aina yoyote, ilimradi mtu awe anajua kusoma na kuandika.
Endelea kujifunza kupitia
dirayamafanikio.blogspot.com kila siku. Kama makala hii imekusaidia na unapenda
kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili uweze kujifunza. Kujiunga
tuma neno MAFANIKIO YANGU, kisha ikifutia na jina lako kwenda 0713 048035 ili
uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI
KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.