Nov 30, 2016
Sifa Kuu Za Mjasiliamali Ndizo Hizi.
Naamini katika kujifunza, hii ndiyo
kauli yangu ambayo inaongoza maisha yangu kila wakati. Kama na wewe unaamini
katika kujifunza nakusihi twende sawa.
Somo letu la leo nililipenda sana, na
nikaona na niweze kukushirikisha katika somo hili, somo hili alinifindisha
mwalimu wangu wa saikolojia, mtoa siri za mafanikio, au huwa napenda sana
kumuita mzee wa nyundo kali huyu si mwingine ni Sharrif Kisuda.
Ambapo katika somo hilo alinifundisha
kiundani kuhusu maana halisi ya mjasilimali. Mwalimu wangu huyu alianza
kunieleza kwa kusema maana ya
Ujasiliamali.
"Watu wengi tunapenda kutumia jina hili la ujasiriamali
lakini wengi wetu hatujui maana yake.” Aliendelea kueleza ya kwamba
Ujasiriamali ni Fursa ya mafanikio ambayo mtu yeyote bila kujali elimu yake au
hali yake anaweza kuanzisha biashara au mradi wowote mkubwa au mdogo na
kumwingizia kipato bila kutumia nguvu kubwa hatimaye kupata faida.
Watu wengi pia tunashindwa
kutofautisha kati ya mfanyabiashara na mjasiriamali. Hawa ni watu wawili tofauti
kabisa. Mjasiriamali ni mbunifu au mtoa wazo la Bbiashara linaloweza
kuzalisha Bidhaa. Lakini mfanyabiashara ni mtu anaye uza bidhaa iliyokwisha
zalishwa na mjasiriamali kwa lengo la kupata faida. Hapo ndipo utapogungua
mfanyabiashara ni mtumwa wa mjasiriamali.
Japokuwa wote wanategemeana ili mmoja
asipokuwepo mwingine anaweza kupoteza kabisa mwelekeo wake. Kwahiyo mjasilimali
lazima ashirikiane na mfanyabiashara katika kutimiza lengo mahususi la
muhusika.
Na kila wakati lazima utambue ya
kwamba Ujasiriamali una kanuni ambazo unapaswa kuzijua ili kutengeneza au
kuzalisha Kitu chenye ubora, ila katika Biashara haina kanuni ni
kuangalia uhitaji wa soko na idadi ya Wateja.
Kuwa mjasiriamali sio lazima usome
mpaka upate digrii ya ujasiriamali zaidi unahitaji kusoma na kuzingatia taratibu
na kanuni sahihi. Msingi wa awali wa Mjasiriamali ni wazo lakini msingi wa
kwanza wa mfanyabiashara ni Pesa ya mtaji.
Kila Mjasiriamali ni mfanyabiashara
lakini si kila mfanyabiashara ni mjasiriamali. Mjasiriamali ni mtu mwenye imani
katika kila jambo analofanya na pia mtu aliyetayari kufanya maamuzi bila ya
kujali sana matokeo.
Mjasiriamali ana tabia ya kufanya
Kitu anachokipenda na ndio maana huwa vigumu kukata tamaa hata kama kukitokea
changamoto kiasi gani. Ni mtu jasiri na anaethubutu kufanya vitu ambavyo
wengine huviogopa kuvifanya.
Na zaidi mjasiriamali ana nidhamu ya
hali ya juu katika matumizi ya muda pesa na mali zake. Tofauti na
mfanyabiashara akipata pesa ya ziada ni lazima aongeze matumizi na starehe
zisizo na ulazima.
Ngoja tuangalie sifa za
mjasiliamali.
1.Hufanya kazi kwa bidii.
Mara kadhaa hauna haja budi kuchukia
kuwepo katika ulimwengu huu eti kwa sababu Maisha ni magumu, ugumu wa maisha
una sababishwa na wewe mwenyewe.
Na hii yote inatokana na kuweza
kufanya kazi kimazoe, Mara nyingi ukiwa na tabia ya kufanya kazi kimazoea hata
kwa kile kidogo unachokifanya hautakiona thamani yake. Hivyo nakusihi kila
wakati hakikisha unafanya kazi kwa bidii huku ukiondokana na dhana ya ya
kufanya kazi kimazoea.
2. Lazima awe mbunifu na mvumbuzi.
Hii ni tabia kubwa muhimu ambayo kwa
kila mjasiliamali yeyote yule lazima awe nayo, bila ubunifu kwa hicho
unachokifanya Ni bure. Ubunifu si kutengeneza kitu awali/ au Ni kitendo cha
kufanya maboresho.
Kwa mfano utaona kila siku kampuni
fulani za utengenezaji simu, kila kukicha wanafanya ubunifu kwenye bidhaa zao,
hufanya hivyo ili kuongeza wateja. Kama ilivyo katika utengenezaji wa simu
tumia kanununi hiyo hiyo katika kuboresha vitu ambavyo unavitengeneza au
kuvifanya.
3. Yupo tayari kujifunza kila wakati.
Kama nilivyoeleza hapo awali ya
kwamba ujasiriamali ni imani, hivyo mara kadhaa kuamini ya kwamba mafanikio
yanakuja kwa kujifunza vitu ambavyo vitamfanya aweze kukua kwa kile
akifanyacho. Na vilevile yupo tayari kwa chochote ambacho huwa anafanya.
Ukitaka kuwa mjasilimali wa kweli,
hakikisha ya kwamba unayazingatia hayo, kwa umakini zaidi na kuyafanyia kazi.
Imeandikwa na Afisa mipango Benson
Chonya.
Nov 29, 2016
Kanuni Ya Usumaku (Law Of Attraction).
Na Apolinary Protas wa Jitambue sasa.
Kwa wengine hupenda kuita ni Law of Attraction, lakini kwa upande wangu naona sio lazima niipe jina kwa kuitafsiri moja kwa moja kwenye kiswahili kama ilivyo kwenye kingereza lakini napendelea kuipa jina la Sheria ya Sumaku kwani jina hilo inakuwa rahisi kuielewa vyema.
Kama inavyofahamika kuwa Sumaku ni
kifaa ambacho kinavuta Chuma. Kama una sumaku, ukiiweka karibu na chuma utaona
inavuta vitu vyenye asili ya Chuma. Usumaku ni ile hali ya uwezo wa kuwa na
nguvu kama za sumaku, uwezo wa kuvuta vitu vyenye hali ya chuma. Je usumaku ni
nini?
Kanuni ya Usumaku ni nini?
Ni kanuni inayotazama kuwa Ufahamu wa
mwanadamu una sifa ya Sumaku. Kile kilichopo kwenye ufahamu wako unakiumba na
kukipelekea kuwepo katika dunia yako. Kila jambo unaloliona halipo kwenye
ufahamu wako tu lakini linaweza likawa kwenye ufahamu wa mwingine hivyo lipo
kwenye ufahamu (ufahamu fulani). Chukulia ulimwengu kama umeme. Umeme huo upo
katika hali mbalimbali ya nguvu na kila hali ina upekee wake. Ufahamu ni umeme,
na ndio maana kwenye Ubongo kuna neva, neva hupitisha umeme kutoka kwenye
ubongo na kwenda kwenye sehemu nyingine za mwili kama vile msuli na milango ya
ufahamu.
UNA UWEZO WA KUUMBA MAISHA YAKO. |
Ufahamu ni kiini kikuu cha Mwanadamu
na kila kiumbe. Kila kiumbe kina ufahamu wake kulingana na hali iliyopo lakini
mwanadamu ndiye mwenye ufahamu wa kujitambua yeye ni nani. Na kuutambua ufahamu
wake, lakini aina nyingine za uhai haziwezi kufahamu ufahamu wake ni nini na
umeumbwa na aina gani ya ufahamu.
Ndani yako kuna sehemu kubwa sana
iliyo na nguvu kubwa sana ambayo huijui. Unaweza ukajiuliza ulipokuwa mdogo
nani alikuwa anahakikisha unakua vyema, nani anahakikisha sasa hivi mapafu yako
yanasukuma hewa, nani anayehakikisha moyo wako unadunda, ni sehemu ambayo unayo
akilini mwako lakini tangu uumbwe mpaka leo hujawahi kuitazama na kujifunza
kuitawala. Simaanishi ujue kutawala mapigo yako ya mwili bali namaanisha kuwa
ndani mwako kuna nguvu kubwa, ambayo ukiamua kuiamuru kufanya chochote inaweza
kukusaidia na kukupa chochote. Nguvu hiyo inaungana na ufahamu wako.
Unachokiamini, unachokitafakari, na unachokisema kinaungana na nguvu hiyo vyema
na kupelekea kufanyika. Unaweza ukawa hujaona hilo lakini ukiwa makini
utagundua hilo.
Kanuni ya USUMAKU inatufunza kuwa,
unaumba uhalisia wa maisha yako wewe mwenyewe. Wewe ni kama Sumaku, unavuta
uhalisia wowote ule ambao unaushikilia akilini kwa muda mrefu.
Ukiamini kuwa wewe ni mtesekaji utazidi kuwa mtesekaji, ukiamini
umebarikiwa basi unapata baraka, na ukiamini unaweza kutimiza jambo fulani nawe
utaweza kulitimia.
Hata Yesu alisema; Ukiwa na
imani kidogo kama vile Punje ya Haradani unaweza kuuamuru mlima kuhama na
ukahama. Jitambue Sasa na yatengeneze maisha yako vyema.
Ansante kwa kusoma makala haya
na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kjifunza.
Nov 28, 2016
Tumia Mbinu Hizi Ili Uweze Kuishi Ndoto Yako.
Tuanze kwa kujiuliza je hilo ambalo
unalifanya ni la kwako au ni la mtu mwingine? Je kama si ndoto yako unahisi ni
lini utaishi ndoto yako? hivi hupendi watu watu wajifunze kupitia kwako?.
Usinipe majibu, nimeona ni vyema
tuanze na kujiuliza maswali hayo kwani ni ya msingi sana, na majibu yake
yatadhihirisha kuwa umekuja duniani kwa lengo la kutimiza ndoto zako na si
ndoto wengine, hata pale unaposema Mwenyezi Mungu bariki kazi mikono yangu
baraka hizo zikujie moja kwa moja.
Zifuatazo ndizo mbinu za kuzitumia ili kuishi Ndoto zako.
1. Usipoteze Muda kwa vitu visivyo vya msingi.
Mara kadhaa tumekuwa tukitumia muda
mwingi kwa vitu ambavyo vimekuwa si lolote kwetu. Tumeshindwa kufanya tathimini
ya kutosha juu ya ndoto zetu tulizonazo, tumekuwa tukiishi ndoto ambazo si
zetu, tumekuwa tukiishi maisha ya wengine.
Mara nyingi tumekuwa tukilalama bila
kutoa sauti ya kwamba maisha ni magumu, na muda mwingine tumekuwa tukidiliki
hata kusema ya kwamba dunia hii haina usawa, yote hayo hutokea hasa pale
tunaposhindwa kufanikiwa, huku tukisahau ya kwamba wengi wetu tunafanya vitu
vya watu wengine.
Usipoteze muda kufanya vitu visivyo vya maana kwako, ishi kwenye ndoto zako. |
Hivi hujawahi kuona ya kwamba mtu
ndoto yake ilikuwa ni Kuwa muigizaji na leo hii ni fundi mjenzi? Unadhani nini
ambacho kimesababisha hali hiyo kutokea? Usinipe majibu.
Ila nikusihi ya kwamba dunia hii
inahitaji mtu ambaye anaishi ndoto zake, hivyo kila wakati unachotakiwa kufanya
ni kuhakikisha unaishi ndoto zako kwa kuzingatia lile likusukumalo kutoka
nafsini mwako, usibadili mwelekeo wa kutimiza ndoto zako eti kwa sababu maisha
ni magumu, eti kwa sababu ya ndugu, jamaa na marafiki.
Amini ya kwamba ndoto zako
zinawezekana, na hivyo anza kuishi ndoto zako sasa kabla ya kuifikia ndoto
hiyo, kama unataka kuwa mwalimu anza kuifundisha jamii ambayo inakuzunguka
sasa, ukifanya hivi hautautumia muda mwingi kufanya vitu visivyokuwa vya
maana kwani utakuwa umeanza kuishi ndoto zako. Mafanikio hayana kesho anza leo.
2.Usikubali kukatishwa tamaa.
Kuishi ndoto zako ni moja ya kitu
kikubwa ambacho naamini unakitafuta katika maisha yako. Lakini wengi wetu,
hushindwa kufikia ndoto hizo hii Ni kutokana na mazingira ambayo yanamzungumka
mtu huyo. Lakini ipo siri ambayo wengi hawaijui ni kwamba siku zote kuwa wewe,
usiwe wao.
Inawezekana ukawa hujanielewa ni hivi
wengi hukatishwa tamaa na watu wengine, na kwa kuwa wewe hupagawishwa zaidi na
aina hiyo ya watu unajikuta unaliacha jambo unalolifanya na kuanza jambo
jingine, lakini kabla sijaweka nukta katika muktadha huu nikwambie ya kwamba
chagua fungu lililo bora acha kukatishwa tamaa na watu ambao hawana msaada
wowote.
3. Uwe tayari kupokea ushauri na kuufanyia kazi.
Dunia hii imejaa watu wa aina tatu,
wapo wale washauri, wapo wakatishaji tamaa, wapo wale ambao wanasubiri wewe
uanze kufanya jambo fulani ili na wao waanze kujifunza kupitia kwako, wala
usijali hii ndio dunia bwana, unachatakiwa kufanya ni kujifunza kutoka kwa aina
hizo zote tatu.
Lakini kujifunza huko si kila jambo
la kuchukua mambo mengine yaache kama yalivyo, ila jifunze yale mambo ya
muhimu kutoka kwa washauri sahihi hasa wale ambao wanafanya mambo ambayo
yanafanana na ndoto zako.
Najua kila kitu katika kujifunza kina
changamoto zake unachotakiwa kufanya si kukata tamaa bali ni kupambana mpaka
mwisho ili ujue hatima ya maisha yako.
4. Jifunze kwa waliofanikiwa.
Maisha ni kujifunza, si kujifunza tu
bali kujifunza kitu kipya, kujifunza kitu kipya pekee yake haitoshi bali
unatakiwa kukiweka katika matendo, kama utaamua kujifunza pekee yake
haitakusaidia kitu.
Ni vyema kila wakati ukajua thamani
ya kufanyia kazi kile ulichojifunza. Mabadiliko ya kitu chochote yanatokana na
wewe kujua kitu kipya, haitawezekana hata siku moja eti unataka kutimiza ndoto
zako kama haupo tayari kujifunza.
Mara kwa Mara wanasema hakikisha
unajifunza kwa watu ambao wamefanikiwa, watu hawa wawe ambao wana mfanano wa
ndoto zako.
Mwisho afisa mipago niweke nukta kwa
kusema ya kwamba kutimiza ndoto zako inawezekana kabisa endapo utaamua kuchukua
maamuzi ya kuanza kuchukua hatua ndogondogo siku leo. Maana mafanikio ni Leo
wala si kesho.
Ni wako rafiki katika Mafanikio;
Afisa mipango Benson Chonya
Nov 25, 2016
Siri Nyingine Ya Mafanikio Kwa Richard Branson Ni Hii Hapa.
Kuna
wakati mwandishi, mhamasishaji na mfanyabishara maarufu duniani Richard Branson
alipoulizwa ni nini siri ya mafanikio yake alisema kwa kifupi tu kwamba, siri ya
mafanikio yake ipo kwenye umakini.
Richard
Branson alisema ‘kuanza siku yako, bila
kuwa makini na vitu unavyotakiwa kuvifanya, ni sawa na kuipoteza siku hiyo
kabisa’. Branson aliendelea kusema ‘bila
umakini hakuna mafanikio wala uzalishaji wowote wa maana utakaoupata.’
Kwa
mujibu wa maelezo ya Branson anadai kwamba unapokuwa makini, unakuwa unajitengenezea
ndani yako msukumo wa mafanikio, msukumo unaokuongoza kufanikiwa zaidi.
Kwa
chochote kile unachokifanya iwe biashara, uandishi au mpiganaji wa masumbwi ili
uweze kufanikiwa kwa viwango vya juu sana, ni wazi kabisa unahitaji kujijengea tabia
ya kuwa na umakini.
Tatizo
la watu wengi hawapo makini sana katika mambo yao au mfumo mzima wa kuendesha
maisha yao. Kama vile madereva wa magari walivyo makini wawapo barabarani,
vivyo hivyo nawe unatakiwa kuwa makini sana kwenye maisha yako.
Umkini wako ndio utakaokupa mafanikio |
Hebu
piga picha kama dereva wa gari asipokuwa makini awapo barabarani ni nini
ambacho huwa kinatokea? Bila shaka hakuna jibu jingine ambalo utanipa zaidi ya
ajali.
Hata
kwenye maisha yetu hivyo ndivyo tunavyosababisha ‘ajali’ za kushindwa sana
wakati mwingine kwa sababu ya kupoteza ule umakini. Unatakiwa kujiwekea umakini
katika kila eneo la maisha yako ili ufanikiwe.
Na
ili uwe makini yapo mambo kadhaa mbayo unatakiwa kuyafanya na kuyazingatia sana
kila siku kwenye safari yako ya mafanikio. Unaposhindwa kuzingatia mambo hayo, ni
lazima umakini utapotea na utaanza kuishi maisha ya kushindwa.
1. Anza siku yako upya.
Haijalishi
jana yako ilikuwaje, kilicho kikubwa kwako ni kuanza siku yako upya. Sahau changamoto
zote ulizokutana nazo jana ambazo pengine zilikukatisha tamaa sana.
Kitu
cha msingi kwako anza siku yako upya kwa kuzingatia kile unachotaka kukifanya. Ikiwa
utakuwa unazingatia sana mambo ya jana, hapa ni lazima umakini utakutoka na utashindwa
kufanikiwa.
2. Andika malengo yako ya siku.
Acha
kuishi kiholela, ishi kwa mipango kwa kuandika malengo yako ya siku, Hiyo itakusaidia
kukuongezea umakini na kujua hasa ni kipi ufanye au kipi usiweze kufanya.
3. Tumia muda wako vizuri.
Matumizi
mazuri ya muda ni chanzo kingine kikubwa cha kukusaidia kuweza kuwa makini. Kama
unatumia muda wako hovyo, ni wazi au dalili ya wewe kutokuwa makini, zingatia sana
matumizi yako ya muda.
4. Jiwekee mipango yako ya mbele.
Unapokuwa
na mipango yako ya mbeleni uliyojiwekea, kwa mfano kujua ni nini utakifanya
mwezi ujao au mwaka kesho, hiyo inasaidia sana kuongeza nguvu ya umakini kwa
kile unachokifanya.
Naomba
utambue kwamba siri nyingine ya mafanikio yako ipo kwenye umakini ulionao. Umakini
ulionao ndio unaonyesha kwamba upo na nia ya kufikia kwenye mafanikio yako.
Hata
hivyo kumbuka huwezi kuwa makini mpaka ujijengee tabia ya kuanza siku yako
upya, kutumia muda wako vizuri, kuandika malengo kila siku na kujiwekea mipango
ya mbeleni.
Nikutakie
siku njema na mafanikio mema.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Nov 24, 2016
Ijue Elimu Hii Muhimu Ya Fedha Na Mafanikio, Ili Uwe TAJIRI.
Leo ngoja tuzungumze juu ya fedha na vitu vinavyoambatana na
fedha(Assets au Liabilities) ambavyo ni chanzo kingine cha kupima mafanikio
yako au hata kujua utapita njia ipi kufikia malengo yako.
Watu wengi wamedumaa na kushindwa kusonga mbele kwa kukosa maarifa
sahihi juu ya neno FEDHA. Na bahati
mbaya ualisia wa somo hili kivitendo halielezwi kisahihi shuleni au vyuoni,
hapa naomba usinielewe vibaya na wala usije sema najifanya mjuaji la hasha.
Labda nitoe mfano. Shuleni au vyuoni ukifeli wewe unaambiwa mjinga
lakini kwenye usakaji wa fedha uhalisia wa kufeli ni hatua mojawapo kufikia
malengo maana ukiogopa kufeli kamwe sahau kuhusu mafanikio, maana hutaweza
kujaribu kitu.
Pili shuleni/chuo unafundishwa kila swali lina jibu moja tu
sahihi (1+1=2) lakini kwenye uhalisia inawezekana kabisa 1+1=6 na bado likawa
jibu sahihi.
Shuleni/vyuoni hauruhusiwi kuigilizia hasa wakati wa mtihani
lakini kwenye uhalisia wa kusaka mafanikio kudesa unaruhusiwa-bila shaka umeona
kwanini nilipinga hapo juu.
Kuza ufahamu wako wa fedha kila siku. |
Elimu ya fedha ni muhimu sana kuijua kwa undani na hapa
nisisitize usije ukaridhika kamwe na ‘material’
yako ya darasana na A+ zako halafu ukajiona unaweza ukatoboa kirahisi kwenye
uhalisia, hizo zilikuwa nadharia tu, vitendo ndiyo mpango mzima.
Hakikisha unasaka elimu zaidi juu ya fedha na matumizi yake
sahihi. Huwa nasikitika sana kumwona kijana kwanza amepata kazi na kitu cha
kwanza anachowaza ni gari!! Eti kwa kuwa ana kamshahara kaa milioni moja na
laki mbili.
Kijana huyu anakuwa anajisahau kuwa amechimba shimo la kuchoma
pesa hata kabla hajaimalika kifedha. Gari, nyumba unayomiliki, flat screen,
radio, smart phone na vinginevyo hizo ni ‘liabilities’
ambazo zitaendelea kukumalizia kamshahara kako na kukufanya usimame pale ulipo
kwa miaka mingi.
Kuwa makini, ishi maisha ambayo yanaendana na malengo yako. Kidogo
ulichonacho kina thamani kubwa kama utakitumia vizuri, acha kuishi ili watu
wakuone ishi wewe na usiishi wao!!
Nunua ‘asset’ maana
zitakufanya uzalishe fedha na si kukimbilia kununua mchwa wa kutafuna hata kile
kidogo ulicho nacho! Mfano wewe unakimbilia kununua viti vya kutembelea na
mwenzako akanunua bodaboda ya kuzungusha machoni pa wengi wewe wa viti vyako utaonekana mjanja lakini kiuhalisia
mwenye bodaboda ni bora mara 1000 zaidi yako!
Hebu nikuambie kitu leo, acha uoga wa kuanza kidogo kwa kamtaji
kidogo ukidhani si chochote, na ukasubiria hadi upate mamilioni ndiyo uanze
safari yako ya mafanikio.
Utakuwa unajidanganya maana njia ya mafanikio iliyobora na
matajili wengi wameitumia ni kuanza kidogo lakini kuwa na malengo makubwa. Na
hiyo inasaidia sana kuendelea kujifunza kadili unavyokua (Nyani mzee amekwepa
mishale mingi).
Hata Dangote tajili wa Afrika anakushauri (start small dream
big). Cha msingi hakikisha unajifunza kuhusu pesa kila iitwayo siku kupitia
vitabu, machapisho, semina za ujasiliamali au warsha mbalimbali (Kama kweli
unataka kubadilika lazima uwekeze huko).
Jifunze kuwa mpya kila siku/mwaka kwa kuongeza marafiki wapya
hasa wale ambao wanafanya vizuri katika nyanja unazopenda! Na si dhambi
kuachana na marafiki ambao wanakukatisha tamaa kila uchwao.
Hamna lisilowezekana chini ya jua kama utakuwa na imani ya
kumtumaini Mungu na kuamini ana mpango na uwepo wako hapa dunia. Fanya kwa moyo
bila chembe ya shaka hakika utafika.
Waliofanikiwa wengi ukiwauliza walifikaje walipo watakuambia kwa
kweli hawajui ila wanachojua walifanya kazi kwa moyo na imani kubwa kuelekea
kwenye malengo yao na Mungu atimaye amewawezesha.
Sasa kwanini wewe usite!!? Kuwa mdadisi na mwenye kiu halisi ya
kile ukitakacho hata kama kijiji/mtaa mzima watakucheka kuwa hutaweza wewe
jisemee tena ukijiamini kuwa unaweza kwani Mungu akiwa upande wako hakuna
linalo shindikana!!
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com
kila siku.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA SHARIFF KISUDA alimaarufu mzee wa
nyundo.
Mawasiliano 0715 079 993
Nov 23, 2016
Tumia Mbinu Hizi Kupanga Malengo Yako Ya Kimafanikio.
Umbali uliopo kati ya
malengo yako na mafanikio ni mrefu sana, na una vikwazo vingi sana, nafahamu
fika ya kwamba hilo unalitambua vizuri sana.
Umbali huo ambao upo baadhi
ya watu ambao wana Mafanikio wameweka mikakati thabiti ambayo imewafanya
wameweza kufanikiwa.
Pia kwa upande watu ambao
hawajafanikiwa kwa kiwango juu na wao katika malengo yao wameweka mikakati, ila
wengi wao hukata tamaa njiani katika utekelezaji wa mambo mbalimbali
yatayowalete mafanikio.
Hali hiyo hutokea kwa
sababu wengi wao hushidwa kuhimili changamoto ambazo hujitokeza katika safari
hiyo ya kutoka katika malengo hadi Mafanikio.
Kama na wewe ni miongoni
mwa watu ambao hukata tamaa katika safari yako ya kuelekea mafanikio, naomba
nichukue nafasi hii kuweza kukaribisha katika makala haya ambapo tutazungumzia
masuala ya kupanga malengo yako hadi kufikia mafanikio.
Wengi hujikuta wakishindwa
wakiishia njiani katika safari yao ya mafanikio hii ni kutokana kutokujua namna
ya kuzitambua mbinu za kukuza malengo hadi mafanikio.
1. Malengo ni lazima yaandikwe.
Malengo lazima uyaandike
sehemu ambayo inaonekana, hapa ni maana ya kwamba uandike sehemu ambayo
inaonekana, kufanya hivi kutakuwa kuna kutakufanya malengo hayo uwe
unayakumbuka na kujua namna ya kuayatekeleza.
Unaweza ukayaandika malengo
hayo kuyaweka katika simu yako katika (screen saver), kioo ambacho unakitumia
kujitazama asubuhi na sehemu nyingine ambayo utayaona malengo hayo.
2. Weka vipaumbele katika malengo yako.
Inawezekana fika ukawa na
malengo mengi, yaandike malengo hayo katika makundi matatu.
Kundi la kwanza jua yapi ni
malengo ya muhimu yapi si malengo ya muhimu, yapi ni malengo ya haraka na yapi
sio malengo, na tatu andika malengo ambayo sio ya muhimu sana.
Endapo utagawa malengo hayo
utajua ni kipi kinatakiwa kuanza na kipi kinatakiwa kufuata na kwa muda gani.
3. Anza kwa kuanza na hatua ndogo.
Siku zote kama ilivyo
ukuaji Wa kiumbe chochote chenye uhai huanza ukuaji wake katika hali ya chini.
Kama ilivyo kwa kiumbe yeyote katika ukuaji hata katika ukuaji wa mafanikio yako
huanza katika ngazi za chini.
Kitu cha msingi ni kuweza
kupanua wigo mpana kwa ajili ya kupata mafanikio zaidi kwa kila jambo ambalo
unalifanya. Na kwa kuwa mafanikio hayana ukomo hakikisha ya kwamba kila iitwayo
leo unapata kiu ya kutaka kufanikiwa zaidi.
4. Malengo ni lazima yawe chanya.
Mara kadha watu huwa na
ndoto nzuri sana, na pia wengi wao hupanga mambo mazuri kwa ajili ya utekelezaji
wa ndoto hizo, ila changamoto kubwa ambayo huwa inakuja ni pale ambapo linakuja
suala la utekelezaji wa jambo hilo.
Hapo sasa ndipo utakapoanza
kumsikia mtu anasema aaah hivi nitaweza kweli, inatakiwa uondokane na kukata
tamaa, vinginevyo kufanikiwa utaendelea kusikia kwa akina Donald Trump.
5.Malengo lazima yawe katika muda maalumu.
Ni lazima uweke muda kamili
kwa ajili ya kutekeleza malengo yako, ifike mahali Malengo yako yafananishe na
makampuni yanayohusika ujenzi kwani wao kabla ya kuanza kwa mradi huwa wanafanya
mahesabu ili kujue mradi huo wa ujenzi utachukua muda gani mpaka ukamilike.
Ukiishi katika utaratibu Wa
kuweka mbinu hiyo itakuwa ni rahisi kwako kutekeleza mambo ambayo unataka
kutekeza. Kwa mfano lengo lako ni kujenga nyumba unaweza ukaandika katika lengo
lako ya kwamba baada ya muda fulani inabidi uwe umekamilisha ujenzi huo.
Kupanga malengo bila kujua
muda Wa kutekeleza malengo ni sawa na bure. Hivyo ni vyema ukajua ya kwamba
muda ni mali katika kufanikisha malengo yako kwa wakati sahihi.
6. Malengo ni lazima yawe na mbinu za utekelezaji.
Watu wengi wana malengo ya
kusema kwa mdomo tu. Lakini nikwambie ya kwamba ukitaka kufa maskini basi
endelea na utaratibu huo Wa kuweka malengo mdomoni.
Kama kweli unataka
kufanikiwa hakikisha ya kwamba malengo ambayo umejipangia umeyaandika na
kuandika mbinu au njia kwa ajili ya utekelezaji wa malengo hayo.
Kufanya hivi kutakusaidia
kujua jinsi ambavyo utayatekeleza malengo hayo ili kupata mafanikio. Kwa mfano kama malengo yako
ni kujenga nyumba basi huna budi kuandika mbinu ambazo zitakusaidia kutengeza
nyumba hiyo, pia hapa huenda sambamba na bajeti ya utekelezaji wa malengo yako.
7. Malengo ni lazima yapimike.
Kila malengo ambayo
umejipangia Ni lazima yaweze kupimika. Kama nilivyoeleza hapo awali ya kwamba
malengo ni lazima yawe na muda maalum kwa ajili ya utekelezaji.
Hivyo ni lazima upime
malengo yako ni wapi ambapo umefikia? Katika muda ambao umepanga
kuyatekeza malengo hayo je unahisi utafikia malengo hayo?
Pia uchunguzi yakinifu juu
ya malengo yako ni lazima ufanyike ili kujua fursa na changamoto ambazo
zimejitokeza katika kuteleza malengo yako.
Mpaka kufikia hapa sina la
ziada, tukutane siku nyingine.
Ndimi Afisa Mipango Benson Chonya
0757909942
Nov 21, 2016
Acha Kurudia Kufanya Kosa Hili, Wakati Unatafuta Mafanikio.
Kati ya kitu muhimu sana ambacho kinaweza kukusaidia katika safari ya
kuelekea mafanikio yako, ni yale makosa unayoyafanya. Mara nyingi makosa hayo
ukiyatumia vizuri ni nguzo kubwa ya kukusaidia kufanikiwa.
Lakini pamoja na makosa hayo kuwa ni msingi wa kukufikisha kwenye
mafanikio, naomba ieleweke kwamba si makosa yote, yanaweza kukusaidia
kufanikiwa. Yapo makosa ambayo hutakiwi kurudia kuyafanya kwenye maisha yako
kabisa.
Ikiwa utakuwa ni mtu wa kurudia rudia kufanya makosa hayo mara kwa mara ni
lazima safari yako ya mafanikio itakwama. Moja ya kosa kubwa ambalo hulitakiwi
kulifanya tena katika maisha yako ni kosa la kutokuchukua hatua ndogo ndogo.
Acha kufanya kosa la kutokuchukua hatua ndogo ndogo kwenye maisha yako.
Hatua hizi ndogo ni muhimu sana katika kukufikisha wewe katika mafanikio
makubwa, ingawa unaweza kaziona hazina maana.
Kila hatua ni mafanikio. |
Wakati wote acha kabisa kujijengea dharau kwamba, hatua ndogo haziwezi
kukufikisha popote, kwa chochote kile kidogo ulichonacho usikione eti hakiwezi
kukusaidia katika safari yako ya mafanikio, hicho kina msaada mkubwa sana kuliko
unavyofikiri.
Kwa mfano, kama unaona una muda kidogo, tumia muda huo kidogo kufanya jambo
la maana, hata kujisomea ila usiupoteze. Kama unaona una pesa kidogo, hata kama
ni shilingi elfu moja, iweke pesa hiyo na usiipoteze eti kwa sababu ni ndogo.
Pia kama unaona una mtaji kidogo, tumia mtaji huo uweze kuwekeza na
kukusaidia kutoka hatua moja na kuelekea hatua nyingine. Chochote kile kidogo
ulichonacho, chukua hatua ya kukitumia kwa manufaa ili uweze kufanikiwa.
Utapoteza fursa nyingi na mafanikio makubwa kwa sababu ya tabia ya kudharau
mambo madogo. Pengine tu, naomba nikukumbushe mafanikio yanajengwa na kanuni au
vitu vidogo vidogo sana ambavyo wengi wanavidharau na kuviona havina msaada
kwao.
Unachotakiwa kuelewa ni kwamba kila wakati kwa wewe kuwa makini na kutambua
mchango wa mambo madogo madogo katika suala zima la kukufanikisha. Ikiwa
utaendeleza dharau au tabia ya kutokuzingatia mambo madogo na kuona hayafai,
nakupa uhakika huwezi kufika mbali kimafanikio.
Jenga mafanikio yako leo kwa kuchukua hatua ndogo sana hata kama zinaitwa
hatua za kutambaa. Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyoanza, yanaanza kidogo
kidogo sana.
Najua ni shahidi mzuri wa hili, ukiangalia makuzi ya mtoto, baadhi ya miti
mikubwa kama mibuyu, ilianza kidogo kidogo sana, lakini leo hii ukuaji wake ni
mkubwa sana ambao hauna mfano.
Tafakari juu ya hili na chukua hatua za kufanya chochote kile hata kama ni
kidogo, lakini tambua kina msaada mkubwa sana kwa mafanikio yako leo na kesho,
isitoshe naweza kusema huo ndio msingi mkubwa wa kimafanikio unavyojengwa
duniani kote.
Dira ya mafanikio inakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe upande
wako.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku na pia
endelea kuwashirikisha wengine makala nzuri zinazotolewa hapa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Nov 18, 2016
Ili Ufanikiwe zaidi, Unahitaji Kuishi Na Watu Hawa.
Katika
kufikia mafanikikio makubwa unayoyatafuta, ieleweke wazi wapo watu ambao ni lazima
sana uwe nao kwa karibu ili uweze kujifunza kwao na hadi kufanikiwa.
Kumbuka,
sisi ni matokeo ya watu watano wanaotunzunguka. Kama unazungukwa na watu watano
ni maskini, basi ni wazi upo uwezekano hata wewe kuelekea kwenye njia hiyo ya
umaskini.
Mpaka
hapo unaona upo ulazima wa wewe kuwa na watu sahihi kila wakati kwenye maisha yako ili ufanikiwe.
Usipate shida sana kujiuliza ni watu gani hawa ambao na unatakiwa kuwa nao ili
kufanikiwa?
Ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuishi
na watu hawa.
1. ‘Mentors’/Washauri.
Kwa
chochote kile unachokifanya, wapo watu ambao wamekutangulia na wanakifanya kitu
hicho tena kwa mafanikio. Watu hawa, ikiwa utajifunza kwao na kuwafanya wakawa
ndio taa yako ya mafanikio, utafanikiwa.
Hawa
ndio watu wa kuishi nao karibu kwa kuwafanya kuwa ‘Mentors’ wako au washauri
wako wa karibu wa mafanikio. Hiyo iko hivyo kwa sababu njia unayotaka kupita
wao tayari wameshaipita. Hivyo ni rahisi sana kukuelekeza.
Inawezekana
unakwama kwenye maisha kwa sababu huna ‘mentor’
au hata mlezi mmoja wa mafanikio ambaye unamfuata. Sasa kama unaishi hivyo, sio
rahisi sana kufanikiwa. Ni lazima uwe na mtu anayekuongoza kufikia mafanikio
yako.
Unaweza
ukawa unajiuliza sasa nitawapata wapi? Kama ni watu wenye pesa mbona wako ‘bize’ sana? hilo lisikupe shida, jifunze kupitia kazi zao wanazotoa kama vile
vitabu. Hapo utapata mawazo yao yote na ushauri wao kwa karibu sana.
Pata mshauri wa kukuza kipaji chako. |
2. Watu wenye uzoefu kwa kile
unachokifanya.
Mara
nyingi wengi wetu tunakuwa tunapotea na kukosea sana kwenye maisha kwa sababu
ya kuishi au kuzungukwa na watu ambao si
wazoefu sana na kile tunachokifanya.
Kwa
mfano utakuta mtu ana duka la vipodozi, lakini ana shauriwa sana na watu ambao muda
wote ni wafanyabiashara wa nguo. Hiyo pekee tu ni kosa ambalo linakufanya kufanikiwa kwako isiwe rahisi.
Ili
uweze kutoka kimaisha, jifunze kuwa na watu ambao wana uzoefu na jambo unalolifanya.
Watu hao watakusaidia sana kukuonyesha
njia sahihi ya kufikia mafanikio yako kwa haraka. Ili kufanikiwa kwa hili
usijifanye mjuaje, kuwa mpole kubali kujifunza.
3. Watu wanaokufanya ufikiri zaidi.
Pia
mbali na ‘mentors’ na watu wenye uzoefu,
watu wengine ambao unahitaji kukaa nao karibu sana ili wakusaidie kufikia mafanikio
ni watu wanaokufikirisha zaidi.
Ni
hatari sana kukaa na watu ambao hawakupi changamoto za kimaisha. Ni lazima
uishi na watu ambao kila kukicha ni kama wanawasha kichwa chako ‘moto’ kutokana
na changamoto wanazokupa.
Unapokuwa
na watu hawa watakutia hasira na utafanya kazi kwa mwehu ili kuhakikisha
unafanikiwa zaidi na zaidi. Maisha yako kumbuka yanataka changamoto ili yaweze
kufanikiwa. Hivyo ni lazima kuwa na watu hawa.
4. Watu wanaosikiliza.
Kuna
watu ambao katika maisha ni wabishi karibu kwa kila kitu. Hawa ni watu ambao
hata wakielekezwa kitu kidogo wao hukimbilia kwenye kubisha. Ikiwa hutawajua
watu hawa watakupotezea muda sana.
Kitu
cha kufanya, epuka watu hawa na ishi na watu ambao wanasikiliza. Ishi na watu
ambao mnaendana. Ikiwa kila mtu anakuwa ni mbishi jiulize hayo mafanikio yatapatikana vipi?
Kwa
kuhitimisha makala haya, naomba ieleweke hivi, wapo watu ambao unatakiwa uwe
nao karibu, unatakiwa uishi nao ili uweze kufanikiwa. Na hao ndio watu unaotakiwa
kuishi nao kama tulivyowajadili kwenye makala haya.
Endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha
yako.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)