Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, September 28, 2016

Hatua Muhimu Za Kutengeneza Uhuru Wa Kifedha.

No comments :
Ili uweze kuishi maisha ya mafanikio makubwa kwako na kuwasaidia wengine ni lazima kwanza uwe huru kifedha. Unapokuwa upo huru kifedha ni hatua inayokufanya kuweza kutekeleza mahitaji yako yote ya kifedha, ikiwa pamoja na hata kusaidia wengine bila tatizo lolote lile.
Hivyo mpaka hapo unaona kwamba, ni lazima sana kuufikia uhuru wa kifedha ili kuishi maisha yenye manufaa kwetu na kwa wengine wanaotuzunguka. Sasa jambo la muhimu kuelewa hapa, tunawezaje kuufikia huo uhuru wa kifedha? Ni hatua zipi ambazo tunatakiwa tuzifuate?
Zifuatazo Ni Hatua Muhimu Za Kutengeneza Uhuru Wa Kifedha.
1. Jiwekee malengo ya kifedha.
Tambua kwamba Ili kufikia uhuru wa kifedha, kabla ya kuanza kuwekeza, kuweka akiba, kutengeneza bajeti au kuweka pesa ya dharura, kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya ni kujiwekea malengo ya kifedha. Hiki ni moja ya kitu muhimu sana katika kuufikia uhuru wa kifedha.

Jiwekee malengo ya kifedha.
Jiwekee malengo ya kifedha yaliyowazi na yanayoeleweka. Kwa mfano, unaweza ukajiwekea malengo  kwamba baada ya miaka mitano ijayo nataka kumiliki milioni mia moja. Pengine unaweza ukajiwekea malengo ya kifedha kwamba ili kutimiza lengo hilo, kila mwaka ni lazima niingize milioni ishirini.
Unapokuwa na malengo ya wazi kama hivi ya kifedha, inakuwa ni rahisi kwako kuufikia uhuru wa kifedha. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu unakuwa unajua unakotaka kufika kifedha na pia inakuwa sio rahisi kwako kupoteza pesa zako kwa mambo yasiyokusaidia kuufikia uhuru huo unaotaka.
Kwa hiyo, ili uweze kuufikia uhuru wa kifedha, jambo la kwanza la kuzingatia, jiwekee malengo ya kifedha. Tafuta daftari lako la kumbukumbu na andika unahitaji pesa ngapi kwa mwaka, unahitaji pesa kiasi gani baada ya miaka mitano. Kwa kufanya hivyo utaufikia uhuru wa kifedha kwa sababu juhudi zako zitakuwa kubwa sana kukusaidia kutimiza lengo lako.
2. Tengeneza bajeti.
Mara baada ya kujiwekea malengo ya kifedha, hatua inayofuata ni  kutengeneza bajeti yako. katika hiyo bajeti utakayoitengeneza ni lazima uifuate na kuitekeleza kila siku. Unapokuwa unaifuata bajeti yako inakusaidia zaidi kuwa karibu na lengo lako la kuufikia uhuru wa kifedha.
Ili kufanikisha hili vizuri, kabla hujapata pesa andaa orodha ya vitu utakavyokwenda kununua kabla. Kisha baada ya hapo fanya manunuzi kama orodha yako inavyosema na sio kinyume chake. Kwa hiyo unaona, Kila unapokuwa na bajeti yako na ukaitekeleza, inasaidia kuokoa pesa ambazo zingepotea bila sababu na inakuwa ni chanzo cha kuufikia uhuru wa kifedha.
3. Weka akiba.
Kwa kiasi chochote cha pesa unachokipata hata kiwe kidogo vipi, jifunze kuweka akiba angalau kwa sehemu. Watu wengi hili ni somo gumu sana kulielewa juu ya uwekaji wa akiba na ni kiwazo kikubwa cha kuufikia uhuru wao wa kifedha.
Sasa kwa lugha rahisi ili uweze kuufikia uhuru wa kifedha ni lazima uweke akiba. Unapokuwa unaweka akiba inakuwa inakusaidia sana kutengeneza mtaji kidogo kidogo kama huna mtaji huo au unaazia chini kabisa kimaisha.
 4. Jiwekee pesa ya dharura.
Hata uwe unaingiza pesa nyingi vipi lakini moja ya jambo ambalo unatakiwa kulifanya ili uweze kuufikia uhuru wa kifedha ni kutenga fedha ya dharura. Kiuhalisia binadamu tunachangamoto nyingi sana. Hivyo ni lazima pesa hii uwe nayo unapoelekea kwenye uhuru wa kipesa.
Hakuna sababu ya kusema sina mtaji au sijawekeza katika hili kwa sababu pengine niliumwa na nikatumia pesa zote. Ili kuepuka ‘majanga’ kama hayo unatakiwa kujiwekea pesa ya dharura. Pesa hiyo inakuwa mkombozi wako kwa lolote linatokea ambalo hukupanga.  
5. Wekeza.
Sasa baada ya hatua hizo ambazo tumetoka kuzijadili, ili kuufikia uhuru wa kifedha kiuhakika hatua inayofuata ni kuwekeza. Bila kuwekeza itakuwa ni kazi ngumu sana kuweza kuufika uhuru wa kifedha.
Hapa ni lazima ukae chini na kutafuta ni kitu gani ambacho unakiwa ufanye au uwekeze na kikakuletea pesa nyingi. Kwa kitu hicho utakachokichagua, anza kukitekeleza mara moja kwani kitakufanikisha na kukupa uhuru wa kifedha.
Kama kweli nia yako ni kuufikia uhuru wa kifedha, unalazimika sana kujiwekea malengo ya kifedha, kutengeneza bajeti yako, kutenga pesa za dharura, kuweka akiba na kuwekeza katika eneo ambalo litakupa faida kubwa. Hizo ndizo hatua muhimu za kutengeneza uhuru wa kifedha.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili uweze kujifunza. Kujiunga tuma neno MAFANIKIO YANGU, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

No comments :

Post a Comment