Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, May 21, 2015

Tabia 4 Muhimu Za Kimafanikio Unazotakiwa Kuzijua.

No comments :
Mara nyingi watu wenye mafanikio huwa wana tabia za aina fulani ambazo huwa wanazifuata kila siku na hatimaye kuweza kutimiza ndoto na malengo yao waliyojiwekea. Kwa kuzifuata na kung’ang’ania tabia hizi, hujikuta ni watu wa mafanikio zaidi katika mambo wanayoyafanya na maisha kwa ujumla.
 
Kwa kawaida, ili uweze kufikia viwango bora vya mafanikio unayoyahitaji, kitu cha muhimu kwako unachotakiwa kufanya ni kujenga tabia za kimafanikio. Unapokuwa na tabia za kimafanikio zinakuwa zinakusaidia kukufikisha kwenye viwango fulani vya mafanikio uliyojiwekea.

Kitu cha kujiuliza hapa ni wangapi wanaojua tabia hizi za kimafanikio zinaweza kuwa msaada kwao?. Ukweli ni kwamba wengi hawajui katika hili na kutokujua huko hupelekea kubeba tabia ambazo huwa ni kikwazo kikubwa sana cha mafanikio katika maisha yao.

Hivyo basi, ni muhimu kwako kuwa na tabia za kimafanikio zitakazo kusaidia kutimiza malengo yako. Acha kupoteza muda kwa kubeba tabia ambazo ni mzigo kwako na hazikusaidii sana, zaidi ya kupoteza muda. Je, ni tabia zipi za kimafanikio ambazo unatakiwa kuzijua ili kufanikiwa zaidi?

Hizi Ndizo Tabia 4 Za Kimafanikio Unazotakiwa Kuzijua.

1. Tabia ya kuweka vipaumbele.
Watu wenye mafanikio, daima huwa ni watu wa kuweka vipaumbele katika maisha yao. Huwa ni watu ambao hawakosei na kwenda kinyume na suala zima la kuweka vipaumbele. Mara nyingi huwa ni watu wa kukaa chini na kufanya uchaguzi sahihi  kwa kitu muhimu kuliko vyote na kukifanyia kazi.

Kwa kuwa na tabia hii peke yake, ni nguzo muhimu kwako kukufikisha kwenye mafanikio. Ili kuweza kufanikiwa inabidi kujifunza juu ya kuweka vipaumbele katika maisha yako. Kama utakuwa unataka kufanya kila kitu na kukosa vipaumbele, elewa kabisa itakuwa ngumu kwako kuweza kufanikiwa.
2. Tabia ya kuwa na mitazamo chanya.
Ni muhimu sana kuwa na matazamo chanya kwa kila unachokifanya katika maisha yako ili uweze kufanikiwa. Unatakiwa kila mara kuulisha ubongo wako vitu chanya vitakavyokujenga siku hadi siku, na hatimaye kuwa bora zaidi. Hii ni tabia muhimu na ya lazima kwako kuwa nayo ili kujenga ,mafanikio makubwa.

Unapokuwa na mtazamo chanya hata pale inapotokea umekwama katika kile unachokifanya inakuwa ni rahisi kwako kuvuka. Watu wengi wenye mafanikio ni watu wenye mitazamo chanya na ndicho kitu kinachowasukuma zaidi kuweza kufanikiwa. Kama nia yako ni kujenga mafanikio ya kudumu, jifunze kuanzia sasa kuwa na mtazamo chanya.


3. Tabia ya kuweka nguvu za uzingativu pamoja.
Kati ya kitu kimojawapo muhimu unachotakiwa kujifunza katika maisha yako ni kuweka nguvu za uzingativu sana kwa jambo unalolifanya. Moja kati ya kosa kubwa ambalo watu wengi wanalifanya katika maisha yao ni kuzingatia ama kutilia mkazo katika mambo ambayo hayana umuhimu sana katika maisha yao.

Kama utaendelea kuweka makazo katika mambo ambayo hayakusaidii itakuwa ni vigumu kwako kufanikiwa. Zingatia zaidi mambo ambayo yanakusaidia, utapata matokeo chanya na ya haraka sana. Hii ni tabia mojawapo ya kimafanikio unayatakiwa kuijua na kuifanyia kazi katika maisha yako, ili kusonga mbele zaidi.


4. Tabia ya kuanza jambo na kulimaliza.
Kuwa na uwezo wa kuanza jambo na kulimaliza ni siri mojawapo muhimu ya mafanikio kwako. Wapo watu ambao huwa ni wepesi sana wa kuanza jambo lakini huwa hawamalizii. Unapokuwa unaanza jambo na kushindwa kumalizia, hicho ni kitu hatari sana katika safari yako ya mafanikio.

Ili uweze kufanikiwa, unatakiwa ujijengee tabia ya kuanza jambo na kuhakikisha umelimaliza mpaka mwisho. Watu wengi wenye mafanikio hichi ndicho kitu wanachokifanya. Ukija kuchunguza kidogo tu, utagundua wengi wanaoshindwa katika maisha huwa hawamalizi mambo yao.

Kiuhalisia, mafanikio yoyote huwa hayaji kwa bahati kama wengi wanavyofikiri. Mafanikio huwa yanajengwa kwa vitu vidogovidogo kama vile tabia na mienendo yetu ya kila siku. Kwa kulijua hilo tunatakiwa kuwa makini na tabia zetu na kujenga tabia za kimafanikio zaidi. Kwa kifupi, hizo ndizo tabia za kimafanikio unazotakiwa kuzijua ili kufanikiwa.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuboresha maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment