Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, May 22, 2015

Unahitaji Kitu Hiki Cha Ziada Ili Uwe Na Mafanikio Makubwa Unayohitaji.

No comments :
Daktari mmoja maarufu sana duniani na hasa kwa nchi za joto kama kwetu, anaitwa Ronald Rose. Daktari huyu alifanya utafiti mkubwa na wa miaka mingi kule nchini India kuhusiana na malaria. Wakati anafanya utafiti huu mgumu, bila shaka kulikuwa hakujagunduliwa hasa chanzo cha malaria. Kwa hiyo, unaweza kufikiria kuhusu mtu, ambaye anaanza kutafuta chanzo cha tatizo akiwa hana msaada wa tafiti za kutosha za kabla. Bila shaka ilikuwa ni kazi ngumu sana kwake.

Daktari huyu alifanyia utafiti huu kwenye mazingira magumu sana ya kimaskini. Alikuwa akifanyia kazi yake kwenye maabara ambayo mchana ilimlazimu lazima atumia pangaboi ili kujinga na joto kali sana la India. Lakini pangaboi hilohilo likawa linapeperusha mbu ambao alikuwa akiwatafiti. Basi, ikawa ni shida kubwa sana ya afanye kipi na aache kipi. Hiyo haitoshi usiku kulikuwa na baridi sana na usumbufu mkubwa wa mbu.

Najua utasema, angejikinga kwa mbu kwa kufanya hivi au vile ni sawa. Utakuwa unasema hivyo kwa kuzingatia zaidi mazingira ya siku hizi. Kwa wakati ule, mbu alikuwa hajabainika kuwa adui wa maradhi na hivyo hakukuwa na njia rasmi za kujikinga naye. Akiwa na matumaini ya kugundua na kuthibitisha kwamba, mbu ndiye anayeeneza malaria, alifanya kazi kwa nguvu zake zote. Lakini hata baaada ya kuwafanyia utafiti mbu kwa maelfu, alikuwa hajahisi hata kwamba, angeweza kupata jibu.
  
Kila mbu alikuwa anachukua zaidi ya saa mbili kufanyiwa utafiti. Kwa maelfu ya mbu, ilikuwa na maana ya siku nyingi za kazi ngumu isiyolipa. Bado, alikuwa na haja ya kujaribu tena na tena na siyo kwa sababu analipwa chochote, hapana. Alikuwa anafanya kwa sababu, alitaka kufanya kilichomleta duniani, kugundua kitu kitakachosaidia wengine. Kumbuka muda wowote kwake ungeonekana mrefu sana , kwa sababu ya shida mbalimbali kama zilizotajwa.


Pamoja na shida zote hizo, mbaya zaidi wahindi ambao ndiyo waliokuwa wanaathiriwa sana na mbu kuliko watu wengine wowote duniani wakati ule, hawakuwa wema kwake. Walikuwa wakijazana kumwangalia wakati akiwanyia utafiti mbu hao na walimbeza sana. Walikuwa wanamcheka, wanamwita kichaa na wengine walisema ni mchawi. Hivyo, hata maisha yake yalikuwa hatarini pia kutokana na mazingira ya kigeni aliyokuwa akifanyia kazi hayakuwa rafiki kwake.

Hapa angeweza kusema, ‘nimtoka kwetu kuja kuchunguza kinachouwa watu hawa, halafu wao wananibeza,’ halafu angenawa mikono nakurudi kwao ulaya. Hakufanya hivyo, badala yake, aliwapuuza na kuendelea na utafiti wake. Lengo lake halikuwa sifa, bali kuchangia kwenye maisha ya binadamu wengine. Aliendelea na hatimaye alihisi kuanza kukata tamaa. Alifikia hatua hiyo, baada ya siku moja kukamata aina mpya ya mbu nakujiambia, ‘huyu atatoa jibu.’ Lakini kwa bahati mbaya, wala hakutoa kitu hata kinachokaribia jibu.

Alipokosa kupata kile alichotarajia kwenye mbu huyu, alijiinamia na kujiuliza, ni kwa nini imeshindikana? Wakati anajiuliza hivyo, msaidizi wake alikuja na aina nyingine ya mbu wapya. Dk. Ronald alitaka kumwambia msaidizi wake Yule awaachie mbu hao waende zao, kwa sababu alijua mbu wote wapya wasingempa jibu, hakukuwa na jibu. Lakini alibadili mawazo yake ghafla na kumwambia msaidizi wake ampe mbu wale.

Akiwa amechoka na kazi nzito ya siku nyingi isiyo na majibu anayoyataka alianza kuwafanyia utafiti mbu wale mmoja baada ya mwingine. Akiwa amebaki mbu mmoja, alikuwa hajapata jibu na alijua angelazimika kufunga virago kurudi kwao, baada ya miaka mingi ya ‘kusota’. Alimchukua mbu wa mwisho na kuanza kumfanyia utafiti. Halafu alishindwa kuamini, mbu yule alitoa jibu alilokuwa amelitafuta kwa miaka mingi kwa shida na mateso.  Aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria. Alimgundua maikrobu, aliye mwenezi wa malaria.

Ni kitu gani kinachotokea tunapokuwa watu wanaoweza kwa vitendo kuvuta subira na kuwa na imani kubwa kwa yale tunayoyatenda? Bila shaka ni mafanikio mwishoni kabisa. Kupitia maisha aliyoishi Dk. Ronald tunajifunza mengi kuhusu maisha yetu ya mafanikio. Tunaonyeshwa kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, subira ya kutosha lakini zaidi ili uweze kufanikiwa unahitaji unapofanya jambo lolote uwe na uhakika unalipenda jambo hilo kwanza, hiki ndicho kitu cha ziada unachohitaji ili kuwa na mafannikio makubwa.

Kupenda tunachofanya ni sifa muhimu sana kwetu, kuliko ujuzi wetu au fedha zetu tulizonazo.  Dk. Ronald alidhamiria na akasema, kuna siku nitagundua, kuna siku nitapata jibu ninalotafuta. Alifanikiwa kupata jibu kweli. Ndani ya kero, shida, kebehi na dharau, hatimaye ikawezekana. Lakini kubwa la kujifunza ni hili. Mtu anapofika mahali anajikuta anaanza kukata tamaa kwenye kile anachokifanya, inabidi ujue kwamba, huenda upo karibu kufikia mafanikio unayoyataka.

Ni kama Dk. Ronald alipokuwa amefikia mahali ambapo alikuwa amejiandaa kusema, ‘sasa kinachofuata ni kufunga virago.’ Lakini kabla hajaweka chini vifaa jibu likaja. Hii yote inaonyesha ni kwa jinsi gani hatutakiwi kukata tamaa hata mambo yawe magumu vipi kwetu, tunatakiwa kuwa wavumilivu. Unaweza ukajikuta biashara uliyokuwa ukiitegemea kuwa italipa sana haikupi faida uliyokuwa ukitaka hicho nacho ni kipindi cha kutokata tama kama ambavyo Dk. Ronald hakuweza kukata tamaa.

Kwa kuwa umeamua kuwa mjasiriamali kuwa na roho ya paka usikubali kufa au kushindwa kiurahisi, hata watu wakutukane ama wakupigie kelele vipi, wewe ziba masikio kisha songa mbele na amini kile unachofanya ndio kipo sahihi. Acha kuyumbishwa na kitu chochote katika maisha yako kuwa na msimamo wako utakaousimamia. Kumbuka, usipokuwa na msimamo juu ya maisha yako huwezi kufanikisha kitu utakuwa unayumbishwa tu kama bendera.

Uwezo wa kutoka hapo ulipo unao, jipe moyo, kuwa na subira na mvumilivu katika kipindi unachotafuta mafanikio, zaidi penda kile unachokifanya hapo utakuwa upo kwenye mstari sahihi wa mafanikio.

Nakutakia mafanikio mema, karibu katika mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO uendelee kupata maarifa bora yatakayokutoa kwenye umaskini, kwa pamoja tunaweza.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,
No comments :

Post a Comment