May 14, 2015
Kama Utazingatia Kitu Hiki katika Biashara Yako, Ni Lazima Uwe Tajiri.
Mara nyingi huwa tunaona na kushudia kwa wenzetu wakiwa ni watu wa kufanya biashara ambazo kwa macho ya nje huwa zinaonekana ni kubwa na zinawalipa sana. Wengi wetu kwa kutokuja hubaki tukijiuliza maswali ya kutaka kujua nini hasa siri ya mafanikio yao. Kwa bahati mbaya wengi kwa kutojua huishia kusema wale ni wezi ama ni ma freemason ili mradi tu kujitetea na kutosumbua akili zetu kujua ukweli wa mambo ulivyo.
Hivi karibuni nilipata nafasi
ya kumtembelea rafiki yangu ambaye kwa kipindi hicho nilisoma naye chuo.
Tulipokutana naye katika eneo la Muheza(Tanga) tuliweza kuongea mambo mengi
ikiwa pamoja na mambo ya kibiashara. Lakini pia aliweza kunieleza biashara
ambayo anafanya katika eneo alipo. Sikutaka kuishia hapo nilimuuliza ni
biashara gani? Aliniambia na nilishikwa na mshangao jinsi ambavyo ilikuwa
ikimlipa na amepiga hatua.
Bwana huyu kwa kifupi,
alikuwa akifanya biashara ya ‘saluni’ ambayo ni ya kawaida kabisa, ninaposema
ni ya kawaida nikiwa na maana haijafikia kiwango cha kuwa Barber shop.
Kilichonishangaza kwenye ofisi yake ni idadi kubwa ya wateja aliyonayo kwa siku, ambao niliwaona wakipishana
wakihitaji huduma yake na wengine kusubiri kwenye viti vya ziada ili kunyolewa,
ingawa mle ndani alikuwa na viti sita vyote vyenye wateja.
Kwa harakaharaka sikutaka tu
kuishia kupata mshangao ambao naamini usingenisaidia kitu, bali nilitaka kujua
nini siri aliyonayo na inayofanya wateja wengi wamkimbilie yeye na kuacha
saluni nyingi ambazo zipo mjini? Nilikuja kugundua kitu muhimu na cha ziada
alichokuwa akikifanya tofauti na wengine. Kitu
hiki ni huduma bora aliyokuwa akiitoa na
ndicho kitu hata wewe, kama utazingitia kitu hiki katika biashara yako ni
lazima ufanikiwe sana.
Kwa muda mchache tu niliokuwa
nae niliweza kushuhudia akiwajali wateja hasa anapowakaribisha na kuagana nao,
lakini hata pia wasaidizi wake ni watu ambao nyuso zao zilionekana zenye tabasamu. Na kwa hali hiyo
hakuna mteja ambaye angeweza kujisikia vibaya ama kero kwa kupewa huduma kama
hiyo. Hicho ndicho kitu ambacho mimi na wewe tunatakiwa tukifanye na kukitilia
mkazo zaidi kwenye biashara zetu, ili kufanikiwa kwa viwango vya juu.
Kwa wengi wetu suala la kuwa
na huduma nzuri zaidi inayoendana na mteja wako ni kitu kigumu kidogo. Wengi
huwa ni watu wa kufanya biashara zao kwa kujisikia tu. Huwa ni watu wa
kutokujali sana ama kusikiliza hasa mteja anataka nini. Kutokana na hili,
naweza kusema moja kwa moja hii ndio sababu mojawapo inakufanya ukose wateja
zaidi katika biashara yako kuliko unavyodhani.
Kabla hujajilaumu kuwa
wateja hakuna ama siku hizi biashara ni ngumu kama ulivyo wimbo wa wengi,
jaribu kukaa chini na kukagua kama kweli huduma zako ni bora. Haiwezekani ukawa
ni mtu wa kununa, usiyeweza hata kuchangamkia wateja halafu kesho ukategemea
uwe una wateja wengi katika biashara yako. Hakuna muujiza kama huo ambao
unaweza ukakutokea, vinginevyo uchukue hatua ya kubadilika.
Watu wengi wenye mafanikio
makubwa katika biashara zao pia huwa ni watu wa kuboresha sana huduma zao kila
mara. Jaribu kuangalia kampuni kubwa
kama vile za simu jinsi zinavyofanya vizuri, bila shaka utathibitisha
hili ninalosema. Ukiweza kutoa huduma bora katika biashara yako hiyo ni dalili
tosha ya kuweza kufikia mafanikio makubwa katika biashara yako.
Mimi mwenyewe mara nyingi
nimekuwa shahidi kwa jambo hili. Kuna wakati huwa ninalazimika kusafiri umbali
mrefu wa mji kwenda kona ya pili kwa ajili ya kununua bidhaa ambayo hata
ningeweza kuipata tu jirani na ninapoishi. Ninao marafiki ambao mara nyingi
hawawezi kula katika hotel yoyote mjini, wanapendelea hotel fulani hata kama
iko mbali. Ukija kuangalia yote hiyo inasababishwa na huduma bora wanayopewa.
Kumbuka huduma unayotoa
ingawa unaweza ukaona ni kitu kidogo sana katika biashara yako, lakini ndiyo
inayoamua ama kukupa wateja wa kiwango gani. Kama huduma yako mbovu sahau kuwa
na wateja wengi na hiyo itakusumbua sana kama hutabadilika. Acha kujali ‘pesa, pesa, pesa’ tu, zingatia kwanza
huduma yako, mambo ya pesa yatafuata baadae. Wafanye wateja wako wajisikie
vizuri kuhudumiwa na wewe kesho na kesho kutwa watakuja tena.
Ieleweke kuwa pia ukiweza
kumshawishi mteja mmoja katika biashara yako utakuwa umewapata marafiki zake
hata na jirani zake. Hivyo ni muhimu sana kwako na wasaidizi wako ambao
mnafanya kazi pamoja kuweza kuijua vizuri lugha ya kibiashara. Kwa kujua lugha
hii itasaidia kumvutia mteja kitu ambacho kitakuwa ni faida kwako na maendeleo
ya biashara kwa ujumla.
Kwa kumalizia makala hii,
tutambue kuwa tunatakiwa kubadilika sisi wenyewe kwanza, hasa katika suala zima
la kutoa huduma ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kinyume cha hapo itakuwa
ngumu sana kwetu kuweza kupiga hatua tunazozihitaji katika maisha yetu. Ni
vizuri tukajifunza hata kwa wenzetu waliofanikiwa katika hili.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kuwashirikisha wengine kutembelea
mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza zaidi kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.