Mar 24, 2015
Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
Ni jambo ambalo mara nyingi huwa linafahamika na liko wazi kuwa, ili kuweza kufanikiwa na kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa ni lazima suala la kufanya kazi kwa ubunifu, juhudi kubwa na maarifa pamoja na kuwa king’ang’anizi kwenye mipango na malengo yako huwa linahusika kwa sehemu kubwa sana. Hutaweza na huwezi kuwa mjasiriamali mkubwa na kufikia mafanikio makubwa kama utakuwa huzingatii mambo hayo.
Pamoja na kufanya kazi kwa
ubunifu, juhudi kubwa na maarifa, kuwa ni nguzo muhimu sana kwako wewe
mjasiriamali ili kuweza kufikia mafanikio makubwa, lakini pia huwa kuna kitu
cha ziada ambacho ni lazima ukifanye na kukifuata ili kuweza kuona mafanikio
hayo unayoyataka. Kitu hiki ni wewe kuweza kujua hatua muhimu za kufuata ili
kuweza kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa.
kwa kadri unavyozidi kujua
hatua hizi zinakuwa zinakupa nguvu na hamasa kubwa ya kuendelea kung’ang’ania
na kushikilia ndoto zako mapaka kuona zinatimia. Hizi ni hatua muhimu sana
kwako na kwa kila mjasiriamali mwenye nia na kiu ya kutaka kufanikiwa na kufika
mbali hasa katika safari ya kibiashara na maisha kwa ujumla. Je, unajua ni
hatua zipi unazotakiwa kuzifuata ili kuwa majsiriamali mwenye mafanikio?
Hizi
Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
1.
Fanya kile unachokipenda kwa moyo wote.
Watu wengi huwa wana kawaida
ya kufanya mambo yale ambayo hawayapendi sana katika maisha yao. Hii huwa
inatokea au wanafanya hivyo kwa lengo hasa la kuingiza kipato. Kutokana na kufanya mambo kwa kutopenda iwe
kazi au biashara hii mara nyingi husababisha kutokuwa na mafanikio
makubwa kwa kile wanachofanya.
Mafanikio huwa hayawezi
kupatikana kwa sababu unapokuwa unafanya kazi ambayo huipendi kikubwa
kinachokutokea utajikuta unakuwa ni mtu wa kulalamika sana na pia unakuwa
unakosa ubunifu kitu ambacho ni hatari na
kitakufanya ushindwe moja kwa moja kwa kile unachokifanya. Kama unataka
kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, chagua kitu kimoja unachokipenda na
kifanye kwa moyo wote, mafanikio makubwa utayaona.
2.
Anza kwa kidogo.
Ni ushauri ambao pengine
umewahi kuusikia mara nyingi kwa namna
moja ama nyingine, lakini na mimi napenda kukumbushia leo kwa kile unachotaka
kukifanya kwenye biashara yako hiyo anza kwa hatua ndogo kwanza. Unapokuwa
unaanza kwa kidogo inakuwa inakusaidia wewe kuweza kupima kama utaweza kwenda
kwa hatua nyingine zaidi.
Acha kuogopa wala kukatishwa
tamaa na kitu chochote katika maisha yako kwa kuhofu kuwa pengine hayo malengo
yako hayawezi kutimia. Kila kitu kinawezekana na hakuna kitu kinachoshindikana
kwako hata kidogo. Anza kutekeleza malengo yako kidogo kidogo hata kama ni
makubwa vipi, lakini tambua kuwa ni lazima uyafikie.
3.
Jifunze kutoka kwa wengine.
Hautaweza kufanikiwa kama
utakuwa tu unaendesha biashara yako wewe mwenyewe na kushindwa kujifunza kutoka
kwa wengine. Unapojifunza kutoka kwa wengine inakuwa inakusaidia kukupa wewe
kuweza kutambua mapungufu uliyonayo ambayo yanaweza kukukwamisha na kukusaidia
kuweza kusonga mbele zaidi.
Hata hivyo unaweza pia
ukajifunza mikakati na mbinu za ujasiriamali zaidi kwa kujisomea kutoka kwa
wajasiriamali wengine wakubwa kupitia vitabu ambapo nako huko utapata
maarifa bora yatakayokutoa hapo ulipo.
Kama una nia na shauku kubwa kweli ya kutaka kufanikiwa na kuwa mjasiriamali
mwenye mafanikio makubwa ni lazima ukubali kujifunza kutoka kwa wengine kila
siku.
4.
Chukua hatua mapema.
Kusoma sana hakutakusaidia
kitu hata kama utasoma vipi hiyo itakuwa ni sawa na kazi bure kama tu utakuwa
huchukui hatua kwa vitendo kufanyia kazi kile kidogo unachojifunza. Kuwa mtu wa
vitendo ni hatua muhimu sana kwako wewe ya kukuwezesha kufikia mafanikio
makubwa katika safari yako ya ujasiriamali na biashara.
Watu wengi wenye mafanikio
makubwa siku zote huwa ni watu wa vitendo tu. Ndani ya maisha yao huwa
yametawaliwa na vitendo na huwa ni watu ambao hawajui kitu kinachoitwa
kuahirisha mipango waliyojiwekea. Jifunze kuchukua mapema katika kila kitu
unachokifanya katika maisha yako, hiyo itakusaidia kufika mbali sana katika
maisha yako.
5.
Kuwa na mipango imara.
Kila kitu unachokijua wewe
chenye mafanikio makubwa hapa duniani, huwa kinaanza na mipango tena mipango
iliyoimara. Hata biashara yako inahitaji kuwa na mipango mathubuti na imara ili
iweze kufanikiwa zaidi na kukuletea matunda unayoyataka. Kinyume cha hapo
utabaki ukilaumu tu kuwa mambo magumu kama wengine wanavyofanya.
Jifunze kujiwekea mikakati
na mipango endelevu kwa biashara yako. Hakikisha mipango utakayojiwekea iweze
kukusaidia kuisimamisha biashara yako na kuwa imara zaidi kwa miaka mingi
zaidi. Chukua muda wa kutafakari na kujiuliza baada ya miaka miwili, mitatu au
mitano kuanzia leo utakuwa umefika wapi kibiashara? Kuwa na mipango imara ni
nguzo muhimu ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyahitaji.
6.
Tengeneza ‘timu’ imara itakayokusaidia.
Mara nyingi huwa hakuna
jeshi la mtu mmoja au mafanikio makubwa yatakayoonekana kwa mtu mmoja pekee. Kuna
wakati katika maisha yetu huwa tunalazimika kutafuta watu watakaotusaidia
katika biashara zetu hilo ni lazima. Hii huwa ni muhimu sana kwa sababu sio
kila kitu tutaweza kukifanya sisi wenyewe tunahitaji wasaidizi ambayo ndiyo
timu yenyewe.
Katika zoezi zima la zima la
kujenga timu hakikisha unatafuta watu ambao watakusaidia kupigania kile
unachotaka kitimie katika maisha yako. Nikiwa na maana kuwa timu yako inatakiwa
kuwa msaada na kuweza kufanya kazi na wewe bega kwa bega mpaka malengo yako
uliyojiwekea yanatimia yanatimia. Kuwa na timu imara ni kitu muhimu sana katika
safari yako ya ujasiriamali.
7.
Acha kufikiria kuwa umechelewa.
Unaweza ukawa unakwama au
kushindwa kuendelea mbele kama inavyotakiwa iwe katika biashara yako, kutokana
na mawazo ambayo unayo ya kuhisi kwamba pengine umechelewa kwa kile unachotaka
kukifanya. Kwa mawazo haya yamekuwa yakikupelekea wewe kushindwa kufanya
mabadiliko makubwa yako katika biashara.
Kitu usichokijua hakuna kitu
kinachoitwa kuchelewa katika maisha yako. Wapo watu ambao mwanzoni walijihisi
na kujiona wamechelewa katika maisha yao, lakini walipokuja kugundua ukweli huu
walikuja kufanya mabadiliko makubwa sana. Kisikuzuie kitu chochote kufikia
ndoto zako. Unaweza ukawa na maisha yoyote unayotaka ukiamua.
8.
Kuwa na mitazamo chanya.
Hiki ni kitu muhimu sana
kukufikisha katika ngazi ya juu ya mafanikio na hatimaye kuwa tajiri kama
utaamua kuwa na mitazamo chanya. Unapokuwa na mitazamo chanya inakuwa inakusaidia
kukupa hamasa na nguvu ya kuona mambo yako yanawezekana hata katika maeneo
ambayo kweli yanakuwa yanachangamoto.
Ikumbukwe kuwa watu wengi
huwa wanakosa kufikia mafanikio makubwa kibiashara kutokana na kuwa watu wa
hasi sana katika maisha yao. Hali hii huwa inawapelekea wao kushindwa
kukabiliana na changamoto hata zile ndogo ambazo walikuwa wanauwezo wa
kuzivuka. Kuwa na mawazo chanya ni muhimu sana kwa mafanikio yako.
Kwa kumalizia, ukumbuke kuwa kiu ya mafanikio yako
unayoitaka uitimize itafanikiwa tu endapo, utakuwa mtu wa kujifunza na kuchukua
hatua muhimu zitakazoweza kubadili maisha yako. Chukua hatua leo na acha
kusubiri kesho au kesho kutwa utakuwa umechelewa sana na hautabadili kitu. Hizo
ndizo hatua muhimu za kufuata ili kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com,
- dirayamafanikio.blogspot.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.