Jun 27, 2020
Ni Muhimu Kutambua Mafanikio Ni Utamaduni.
Utamaduni
ni kigezo cha msingi kwa maendeleo ya jamii yoyote. Hakuna taifa lilowahi
kuendelea bila kujali utamaduni, kutii, na kufuata misingi muhimu ya utamaduni
wao.
Nchini
kwetu vitabu vingi vimeeleza maana ya utamaduni kwa ama upotoshaji mkubwa au tafsiri
nyonge, kwa mfano, vitabu vingi vinaufafanua utamaduni kama ngoma, harusi,
mavazi, vyakula, lugha, nyimbo, mila na desturi.
Kweli
hivi vinaweza kuwa viashiria au vipengele vya utamaduni, lakini ni kweli
utamaduni ndiyo huo? Matokeo ya tafsiri hizi na dhalimu ni kwamba watoto wetu
wanakuwa na kuelewa kuwa utamaduni ni ngoma au nyimbo, kuvaa manyoya, kucheza
na nguo zilizochanika mbele ya viongozi uwanja wa ndege kwa lengo la
kuwaburudisha wazungu wanaokuja kutembelea nchi yetu. Huo ni udhaifu mkubwa wa
mitaala yetu.
Kimsingi
utamaduni unatafsiriwa katika nyanja kuu tano;
Moja, ni fikra na namna mtu anavyofikiri. Eneo hili ndilo limekamata
sehemu kubwa ya matendo ya utamaduni wa mtu na matendo yake ya kila siku.
Pili, mitazamo, ni
eneo muhimu la utamaduni. Hapa akili imekamatwa na desturi zilizozaa mitazamo
inayomuongoza mtu kufanya anachotaka na
kuamini anachokiamini.
Tatu, mielekeo/utashi wa kimaisha, nalo
ni sehemu ya utamaduni wa jamii yoyote ile. Kila mtu ana mwelekeo anaouweka
katika kupambana na maisha ili kufikia maendeleo yake na familia. Mielekeo ndiyo
inayomtengeneza mtu kuwa mnyonyaji au mzalishaji.
Nne, imani,
Yaani kile mtu anachiokiamini na kukiishi ni kigezo muhimu cha kumfanya yeye
aendelee au abaki maskini. Imani ya mtu husanifu mitazamo na uamuzi wa
kimaisha.
Tano, mila, jadi na desturi.
Hizi zinajenga mtu na kumuumba awe alivyo. Na mara nyingi hujenga kanuni au
taratibu za kuishi. Mila jadi na tamaduni ndizo huunda michepuo ya akili ya
watu. Binadamu anaijua dunia kwanza kupitia jadi, mila na desturi ambayo ni
kanuni za msingi za kujenga ufahamu kwenye akili ya mtu. Ndiyo maana mila
desturi na jadi hazijaandikwa popote.
Haya
ni mambo ya muhimu katika utamaduni wa jamii yoyote ulimwenguni. Kuyadharau na
kukimbilia ngoma, nyimbo na mavazi ya asili ni sehemu ndogo ya ukweli wa nini
maana ya utamaduni.
Tukifahamu
hivyo tunaweza kuweka sera na mikakati ya maendeleo kwa kuzingatia utamaduni wa
jamii husika. Na ikumbukwe kwamba hakuna jamii hata moja duniani yenye
utamaduni mbaya. Kila linalofanyika ndani ya jamii linasababu yake, hata kama
ni mbaya kwa mwingine.
Kwa
Waarabu nguruwe ni haramu, lakini kwa Wazungu nguruwe ni nyama nono; Utamaduni
kwa Waafrika nyoka ni adui mkubwa lakini kwa Wachina nyoka ni nyama nono!
Hakuna utamaduni mbaya hapa duniani bali kuna desturi na vitendo vibaya ndani
ya jamii fulani.
Pili,
utamaduni hauna madaraja, kwamba, utamaduni wa jamii fulani ni mzuri kuliko
utamaduni wa jamii nyingine. Wengi wamepotoka na kuvurugwa na utamaduni wa
kizungu ulioletwa na wakoloni. Wanajaribu kudharau tamaduni zao na kujaribu
kuishi uzungu ambao wengi umewapeleka kuzimu na kuvuruga akili zao, sasa
wamegeuka kuwa watumwa wa wazungu. Michepuo ya akili hujengwa na tamaduni asili
siyo za kigeni. Ndiyo maana tunasoma lakini hatuna wabunifu wala wavumbuzi.
Utamaduni
unabeba vipengele vya msingi vya mchakato wa maendeleo na unasaidia kuimarisha
kujitegemea, mamlaka ya kujiamlia mambo yako mwenyewe na ni kitambulisho cha
taifa na ndiyo maana ni muhimu kutambua mafanikio ni utamaduni pia.
Bila
kutii na kuchambua fursa na vikwazo vya utamaduni wa jamii unayotaka
kuiendeleza, kamwe huwezi kupata maendeleo. Hii ni sababu inayofanya maelfu ya
miradi ya Benki ya dunia kushindwa kuleta maendeleo yoyote katika nchi maskini
ni kutotii utamaduni wa jamii husika.
Mathalani
mwananchi wa Uingereza anachofikiria kwanza akipata fedha ni tofauti na
mwananchi wa China na hata Vietnam. Vivyo hivyo, ukimpa laki moja Mchaga wa
Moshi, na Mnyiramba wa Singida kiasi hichohicho na uwaulize wanataka kufanya
nini, fikra na mipango inatofautiana pia.
Ukitumia
mabilioni ya fedha kununua chakula na vijiko vya misaada kuwapelekea waathirika
wa Tsunami huko India kaskazini na Bangladeshi, itakuwa ni upotezaji wa fedha.
Maana utamaduni wa Wahindi ni kula kwa mkono, hawatatumia vijiko kamwe.
Hii
ni mifano michache ya kuonyesha jinsi gani utamaduni una nguvu katika kuchochea
na kuzuia maendeleo. Miradi yoyote ya maendeleo duniani inabidi itanguliwe na
uchambuzi wa utamaduni wa mahali husika ili kuona fursa na vikwazo vilivyomo
kwenye utamaduni huo. Vinginevvyo ni kupoteza fedha na muda bure.
Miradi
ya maendeleo ni lazima iweze kutokana na jamii yenyewe. Ndiyo maana ni muhimu
jamii ichague vipaumbele vya maendeleo, kwani yenyewe ikachagua itaakisi utamaduni
na mahitaji yake, na kuifanya ishiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wake.
Yapo
hata mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yalifanya juhudi kubwa za kuanzisha
miradi ya maendeleo vijijini bila kuzingatia utamaduni wa mahali hapo. Miradi
mingi imeishia kupoteza fedha na muda. Umaskini umebaki palepale. Mradi unaobuniwa
Ulaya na wazungu, ukaletwa kijijini Chabutwa, kamwe hauwezi kuzaa matunda wala
kudumu.
Unaweza
kukua kwa siku za mwanzo lakini hauwezi kuondoa umaskini wala kuwa endelevu.
Lakini mradi utakaobuniwa na wanakijiji wa Chabutwa wenyewe, ukapata msaada wa
mashirika au serikali huo utakuwa endelevu na utaleta mafanikio makubwa na ya
kudumu kwa wanakijiji. Hii ni kwa sababu utakuwa umetoka kwao na umezingatia
utamaduni wao.
Wanafunzi
na jamii kwa ujumla wanapaswa kufundishwa ukweli kuwa kile ambacho utamadani
unagusa cha kwanza kabisa ni fikra, mitazamo, miiko, mwelekeo na wala siyo
ngoma na nyimbo tu kama ilivyozoeleka.
Lazima
wafundishwe mambo mazuri katika utamaduni wetu na yale mabaya ili wajue namna
ya kuyaepuka mabaya na kuyaendeleza mazuri.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTEMI ZOMBWE,
DAR ES SALAAM.
MAWASILIANO- 0713 000027
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.