Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, September 18, 2015

Siri 6 Za Kuishi Maisha Yenye Afya Bora.

No comments :
Habari za siku rafiki  na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu umzima wa afya na unaendelea kujifunza ili kuboresha maisha yako. Karibu tena katika siku nyingine ambapo tunapata fursa ya kujadili mambo ya kimafanikio kama ilivyo kawaida yetu.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia kuhusu afya kama sehemu muhimu sana kwa mafanikio yoyote yale. Bila shaka utakubaliana nami kuwa kama afya yako ni mbovu huwezi kufanikiwa hata iweje. Mafanikio yote unayoyatafuta yanahitaji uwe na afya njema ili kuyafikia, vinginevyo utakwama.
Ikumbukwe kuwa hakuna mtu anayependa kuumwa au afya yake kuwa mbovu hata kidogo. Kila mtu anahitaji afya yake iwe bora tena hata siku zote ikiwezekana ili kuishi maisha ya furaha. Lakini ubora huo wa afya tunaoutaka hauji hivihivi tu huwa zipo kanuni au siri za kufanya ili kuweza kujijengea afya bora zaidi.
Hapa zipo siri sita za kufuata endapo wewe kweli unataka kuishi maisha yenye afya na yenye manufaa mengi zaidi.
1. Fanya Mazoezi ya mwili kila siku.
Mazoezi ya mwili ni ya muhimu sana kwa afya yetu na yanafaida nyingi kwetu. Unapofanya mazoezi hiyo inakuwa inakusaidia kuupa mwili afya kutokana na ukweli kwamba yanapunguza magonjwa mengi kama ya msongo wa mawazo na shinikizo la damu. Hivyo unapofanya mazoezi hata kama ni kidogo unakuwa upo katika hali nzuri kiafya tofauti na yule ambaye hafanyi kabisa.

2. Pata muda wa kupumzika
Baada ya kazi zetu tunazozifanya, mwili huu ni lazima upumzike ili upate kujitengeneza upya wenyewe. Yatupasa kuwa na muda wa burudani na wa kupumzika ili kupunguza msongo utokanao na kazi pamoja na majukumu ya kifamilia. Bila kuwa na muda wa kutosha kupumzika mara nyingi watu wanakuwa na wasiwasi, mfadhaiko na hasira kali.  Hivyo ni lazima kutenga muda huu ili kujijengea afya bora.
3. Kula chakula bora.
Ili kujihakikishia usalama wa hili epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi. Kama unazidisha vyakula hivi vyenye mafuta hali hiyo inaweza ikawa hatari kwa afya yako. Vyakula hivi vinaweza vikawa nyama au vinginevyo. Hakikiha unajipatia vyakula vyenye virutubisho muhimu vya mwili, lakini siyo lazima viwe vya mafuta. Kwa kujijengea tabia hiyo mwili wako kwa namna yoyote ile ni lazima utakuwa na afya bora.
4. Epuka Vitu Vinavyokuletea Madhara.
Vitu hivi inaweza ikawa ni pamoja na matumizi mbaya ya pombe hususani pombe kali au uvutaji wa sigara wa kupitiliza. Unapokuwa unafanya mambo kama hayo tambua tu moja kwa moja yatakuharibia afya yako. Kitu cha msingi hapo ni kuhakikisha unaachana na tabia hiyo ili kujijengea afya bora na endelevu kwako.
5. Kunywa maji safi na ya kutosha.
Tunapozungumzia afya safi huwezi kulikwepa hili la kunywa maji safi. Unalazimika kunywa maji safi na ya kutosha ili kuipa akili yako nguvu ya kufanya kazi kwa ufanisi. Unapokunywa maji mengi yanakuwa yanasaidia ubongo wako kufanya kazi vizuri kwa sababu yanakuwa yanaiongezea akili yako oksijeni kwa hali ya juu kabisa.
6. Dumisha usafi.
Usafi ni suala la muhimu sana katika kuboresha afya zetu. Usafi huu unaweza ukaanzia kwenye miili yetu, mavazi na hata pia katika mazingira yetu. Tunapoimarisha usafi katika maeneo yote hayo inakuwa ni rahisi kuweza kukabiliana na magonjwa mbalimbali ambayo yangeweza kutushambulia.
Kumbuka,  kuwa na afya bora ni msingi mkubwa wa mafanikio kwa binadamu. Hivyo ni lazima kwetu kudumisha afya bora siku zetu ili kujihakikishia hata usalama wa maisha yetu kwa kiasi kikubwa.
Nakutakia kila la kheri katika maendeleo ya afya yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
 Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.  

No comments :

Post a Comment