Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, September 28, 2015

Kama Unataka Kuwa Na Furaha Ya Kweli, Zingatia Mambo Haya.

No comments :
Kila mmoja kati yetu anatamani sana kuwa na furaha ya kweli maishani mwake. Nina uhakika kama furaha ingekuwa inauzwa, mfanyabishara wake ndiye mtu ambaye angekuwa tajiri zaidi duniani. Asingekuwa tajiri tu, bali angekuwa tajiri wa kufuru.
Kwa nini? kwa sababu, kila binadamu anatamani kuwa na furaha ya kweli kwenye maisha yake. Kila mmoja wetu, awe anajua au awe hajui, anachotafuta hapa duniani ni furaha tu. Kuhangaika kwetu kote, ni kutafuta furaha ya kweli.
Lakini kwa bahati mbaya wengi wetu hatujui namna ya kuipata furaha ya kweli. Wengi tumekuwa tukifanya mambo ambayo tunafikiri yanaweza kutupa furaha, lakini baada ya muda tunagundua mambo hayo hayatupi furaha ya kweli tunayoihitaji kama tulivyokuwa tukifikiri.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya utambuzi wanadai kuwa kutafuta furaha ya kweli maishani, kunahitaji juhudi na kila mmoja anaweza kuipata furaha hiyo kama kweli ataamua. Wanasema, kimsingi furaha ni ujuzi ambao inabidi mtu ajifunze kuupata.
Na ili kuliweka jambo hili wazi, na kueleweka kwa kila mtu hadi kumudu kupata furaha ya kweli, wataalamu hawa wautambuzi wameweka mambo au vigezo vya kuzingatia ili kuweza kujijengea furaha ya kweli. Kwa kuyajua mambo hayo yanauwezesha ubongo wako kufanya mabadiliko ya kukupa furaha ya kweli.

Moja ya sababu au nguzo ya kukupa furaha ya kweli ni kufanya tahajudi (Meditation) au sala za uzingativu kwa muda mrefu. Watu wengi  wanaofanya aina fulani za tahajudi au meditation huweza kumudu kuongeza furaha katika maisha yao kwa kiwango fulani.
Hiyo huweza kutokea hivyo kwa sababu, kwa kadri mtu anavyofanya sala au tahajudi hupelekea kwa nguvu nyingi hasi kukandamizwa katika ubongo wake na matokeo yake nguvu chanya kuongezeka na kupelekea kumudu kujenga furaha ya kweli anayoitaka kwake. Hivyo tahajudi ni jambo la muhimu sana katika kujenga furaha halisi.
Pili, furaha ya kweli inakuja kwa kutambua kuwa inatoka ndani mwako na siyo vinginevyo. Hii ina maana kwamba, haiwezekani kwa mtu kupata furaha ya kweli kama ndani yake mtu huyo hajikubali na haioni furaha hiyo kwake.
Wengi wanategemea mambo ya nje kama fedha, elimu au umaarufu  kupata furaha. Lakini kitu cha kushangaza hawaipati furaha hiyo, hata kama wakiipata inakuwa ni ya muda mfupi sana na kutoweka.
Wakati mwingine hata furaha ya muda mfupi hawawezi kuipata , kwani kwa mfano, mara wanapopata fedha nyingi, sekunde hiyohiyo mawazo yenye kukera na hofu kuhusu fedha hizo huanza kujitokeza kwao na mwisho hujikuta furaha yao ikiyeyuka.
Kwa kulitambua hilo usiwe mtumwa kwa mambo hayo ya nje ambayo yanaweza yakatoweka muda wowote na kukupotezea furaha yako. Kitu cha msingi tambua wewe ndiye chanzo cha huzuni au furaha katika maisha yako.
Tatu, jifunze kuyachukulia mambo kama yanavyokuja ili kujijengea furaha ya kweli. Acha kushindana sana  baadhi ya hali zinazokuja kwako, kwani utashindwa kuzimudu hali hizo na mwisho wa siku utajikuta unakosa ile furaha halisi. Usiwe mtu wa kubadilika asubuhi na jioni kwa kutegemea kitu gani kinaendelea nje.
Mtu mwenye furaha ya kweli anakubaliana na maisha kama yalivyo bila kujali kama kuna mvua au jua, kama mambo yameenda vizuri au vibaya, kama kuna fedha au hakuna, kama kuna kusifiwa au hakuna. Tunasema ni watu ambao ndani zao hazitegemei sana ni kati gani kinaendelea nje.
Nne, unaweza upata furaha ya kweli kama utaamua kuwapenda wengine pia.  Kuwapenda wengine ina maana kuwapokea na kuwakubali watu wengine kama walivyo na mapungufu yao. Hili huwa ni jambo gumu kwa wengi kuwapenda watu wengine.
Kama nilivyosema awali, kila binadamu anataka kupata furaha maishani. Katika kutafuta furaha binadamu hujikuta akitafuta kazi nzuri, gari nzuri ya kutembelea, kujenga nyumba nzuri, kuoa au kuolewa na mke au mume mzuri na mengine mengi, yote hayo hufanywa kwa ajili ya kutafuta furaha.
Kwa sababu, furaha haiko kwenye mambo hayo tu, watu hujikuta wanapata vitu hivyo, lakini bado hawana furaha. Kwa sasa itakuwa ni rahisi sana kwa binadamu kupata furaha ya kweli kama ataamua na kuzingatia mambo hayo tuliyojadili, badala tu ya kuhangaika kutafuta mara hiki mara kile.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.


No comments :

Post a Comment