Feb 29, 2016
Mbinu Za Kukabiliana Na Ushindani Katika Biashara.
Mara nyingi wote tunajua wakati mwingine ili kuendesha biashara
hadi ikakuletea mafanikio makubwa, inahitaji uvumilivu na kujituma sana hasa
kutokana na changamoto nyingi zinazojitokeza kila siku kwenye biashara
tunazozifanya.
Bila shaka utakubaliana nami moja ya changamoto kubwa
zinazojitokeza katika kuendesha biashara iwe ndogo au kubwa ni pamoja na
ukosefu wa masoko ya kutosha, mfumko wa bei, ushindani wa kibiashara na
changamoto nyinginezo, ambapo usipokuwa makini unaweza ukakwama.
Leo katika makala haya tutaangalia moja ya changamoto hizo kubwa
inayowakabili wafanyabiashara wengi sana. Changamoto hii si nyingine ni
changamoto ya upinzani au ushindani unaojitokeza kwa kasi katika biashara kila
kukicha.
Naamini hakuna asiyejua kwamba, kwa sasa ushindani kibiashara uko
juu. Kila siku kumekuwa na biashara nyingi zinazoanzishwa. Na imekuwa si kitu
cha ajabu kujikuta watu ishirini mkifanya biashara ya aina moja na kwenye mtaa
mmoja.
Kutokana na ushindani mkubwa, wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa
wakifanikiwa na wengine kukwama kwa sababu ya kushindwa na nguvu ya ushindani. Lakini
kwa kusoma makala haya, itakusaidia kujua mbinu za kukabiliana na ushindani
kwenye biashara yako. Karibu sana kujifunza.
1. Toa bidhaa bora.
Ili uweze kumudu kukabiliana na washindani wako vizuri, njia
bora ya kukabiliana nao ni kutoa bidhaa bora. Hakikisha wateja wako wanaridhika
kabisa na kile unacho wahudumia. Isije ikatokea au ukasikia eti wateja wako
wanalalamika kwa kukosa bidhaa bora. Kama itatokea hivyo, jirekebishe na toa
bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Kwa mfano wewe una duka la kuuza vifaa vya umeme. Jitahidi
dukani kwako uwauzie wateja wako vifaa hivyo 'orijino' na sio 'feki'.
Hiyo itakupa sifa kwanza na pia itakusaidia kuwashinda kirahisi wale wanaotoa
bidhaa zisizofaa ambazo zikitumika kwa muda mfupi zimekufa. Kumbuka hili, kila
wakati, kila siku, kutoa bidhaa bora ni njia nzuri ya kuwashinda
washindani wako.
KUWA MBUNIFU |
2. Angalia udhaifu wa washindani wako.
Hata kama washindani wako unaona wana bidhaa bora sana pengine
hata kuliko wewe hilo lisikutishe sana. Kitu cha kufanya wewe, boresha bidhaa
zako na kisha nenda hatua ya ziada kwa kujifunza udhaifu wao.
Ukishagundua udhaifu wao ni nini, utumie udhaifu huo kukusaidia kukufanikisha.
Tuchukulie kwa mfano wote mna mgahawa na mnatoa huduma ya
chakula. Halafu ukaja kugundua jirani yako na ambaye ni mshindani wako, kwanza
hawakaribishi wateja vizuri na pia wateja wanalalamika chakula ni kidogo.
Kitu cha kufanya wewe, ni kuhakikisha unawakaribisha wateja wako vizuri sana na
ikiwezekana kutoa chakula kingi kidogo ili kufanya wateja wako wasilalamike
kama yeye. Kwa kufanya hivyo utaweza kujipatia wateja wengi hata waliokuwa kwa mshindani
wako.
3. Kuwa mbunifu.
Mpaka hapo umeshajifunza ili kuwashinda washindani wako ni
lazima utoe bidhaa bora na kuangalia udhaifu wao. Lakini hiyo haitoshi, pia
unalazimika kuwa mbunifu zaidi kwa wateja wako. Ni muhimu kujua wanataka nini
kwa wakati, ni kitu gani ambacho ukiongeza watavutika au ni huduma ipi ambayo
wataitaka zaidi ambayo kwa sasa huna. Huo ni ubunifu unaotakiwa ili kukabiliana
na ushindani hasa kwa kipindi cha sasa.
Kwa biashara yoyote inayoendeshwa kwa ubunifu ni rahisi kushinda
ushindani na kusonga mbele. Lakini kama unaendesha biashara kimazoea kufanikiwa
itakuwa ngumu. Tafuta kitu ambacho huna, kiongeze kwenye biashara yako. Kama
una biashara ya saluni na ukagundua pengine ukiweka televisheni huku ukionyesha
baadhi ya mipira ya ulaya itavuta wateja, basi fanya hivyo ili upate wateja
kutosha. Kama nilivyosema ubunifu katika biashara yoyote unalipa sana na
pia ni njia sahihi ya kukabiliana na ushindani.
4. Toa punguzo la bei.
Biashara yako inaweza ikawa ina mvuto mkubwa sana ikiwa kuna
wakati fulani kunakuwa kuna punguzo maalumu la bei. Punguzo hili unaweza
ukalifanya katika kipindi maalumu mfano cha sikukuu au ukaamua kushusha bei
bidhaa fulani fulani hivi ili kuweza kuwavuta wateja na kuushinda upinzani.
Kwa mfano unaweza ukawa unafanya biashara ya kuuza simu. Ni
vyema kwa baadhi ya simu ukashusha bei na kuwatangazia wateja wako ofa hiyo
ambayo uwe na uhakika wataipenda. Kwa kutoa ofa hizo siku hadi siku zitaifanya
biashara yako ing'ae na kuzidi kwenda juu na kuushinda upinzani.
5. Toa huduma bora kwa wateja wako.
Tatizo kubwa walilonalo wafanyabiashara wengi hasa wadogo ni
kule kushindwa kutoa huduma bora. Wamekuwa ni wafanyabiashara wa kufanya
biashara, bora liende na kusahau kutoa huduma bora. Kwa vyovyote vile unaposhindwa
kutoa huduma bora unajiwekea mazingira ya kushindwa kukabiliana na ushindani.
Huduma bora inahitajika sana ili kuifanye biashara yako iende na wakati na
kuwashinda washindani wako.
Katika kutoa huduma bora jifunze kuwafurahia wateja wako,
jifunze kuwasikiliza na pia jifunze kuomba msamaha kama kuna kosa linaweza
likawa limetokea la kibiashara. Hiyo ni mifano michache ya kutoa huduma bora
lakini lilokubwa kwako ni kuhakikisha kwa namna yoyote ile unatoa huduma bora
kwa mteja wako itakayomfanya afurahie huduma hiyo na kesho kurudi kwako tena.
Bila kufanya hivyo, utapoteza wateja na watakimbilia kule zinakotolewa huduma
bora.
6. Toa matangazo ya
biashara yako.
Kwa kawaida hakuna biashara ambayo inaweza ikajiendesha kwa
mafanikio makubwa na kushinda ushindani bila kuwa na matangazo. Biashara yako
inategemea sana matangazo kuliko unavyofikiri. Unajua ni kwa nini? Ni kwa
sababu biashara yako inatakiwa kujulikana kila eneo ilina kuwavutia wateja
wengi.
Tunapozungumzia matangazo kama huna mtaji wa kutosha si lazima
yawe ya redioni au kwenye televisheni. Unaweza ukatengeneza vipeperushi kwa
gharama ya kawaida au unaweza ukatumia wateja wako hao hao kuitangaza biashara
yako na kupanua soko kwa kiasi kikubwa na kuwashinda wapinzani wako.
Kwa kufanya mambo haya, yatakusaidia kwa kiasi kikubwa
kukabiliana na ushindani mkubwa unaojitokeza katika biashara yako.
Tunakutakia kila la kheri katika biashara yako na endelea
kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
Email; dirayamanikio@gmail.com
Feb 26, 2016
Ndoa Imara Huweza Kutibu Hata Kansa.
Maradhi
ya kansa yamekuwa yakiwasumbua watu wengi sana kwa nyakati za hivi karibuni. Hata
hivyo kuna aina nyingi za kansa, mojawapo ni ile ya kibofu cha mkojo.
Kulingana
na utafiti mmoja uliofanywa nchini marekani, imeonesha kwamba, msaada wa karibu
unaotolewa na wanandoa kwa wanandoa wenzao ambao, wameathirika na gonjwa wa
kansa ya kibofu cha mkojo, ni aina
mojawapo ya tiba inayoweza kuwafanya wagonjwa hao wajisikie vizuri na kuishi
kwa muda mrefu.
Utafiti
huo ulionyesha kwamba, watu wanaougua ugonjwa huo ambao wako kwenye ndoa, wana
nafasi kubwa ya kuishi muda mrefu zaidi ukilinganisha na wenzao ambao hawajaoa
au kuolewa. Hali hii haichagui umri, rangi au hata kiwango cha athari ya
ugonjwwa wenyewe.
Vilevile,
tafiti mbalimbali za huko nyuma ziliwahi kuonesha kwamba, ndoa bora na imara
zina uwezo wa kuwaongezea ahueni wanandoa wanaougua maradhi ya kansa ya matiti
na ile ya mkojo.
NDOA IMARA INATIBU MARADHI MENGI. |
Watafiti
hao walizidi kusema kwamba utafiti huo mpya unaweza ukawa na manufaa zaidi kwa
aina nyingine ya kansa. Hali kadhalika utafiti huo ulionesha kwamba,wagonjwa wa
kansa ambao walikuwa wamefiwa na wenzi wao wa ndoa na wale waliotengana ama kutalikiana,
waliathirika na ugonjwa huo zaidi.
Ingawa
umri mkubwa nao ulichangia kwa kiwango kikubwa kwenye hali hiyo, kutokuwa na
mpenzi kulionesha wazi kuwa na madhara makubwa.
Sababu
hasa, inayoyaofanya kuwa na tofauti hiyo, bado haijaulikani. Hata hivyo, yapo
maelezo machache yanayoweza kutolewa
kuhusiana na hali hiyo. Kwa mfano, mume au mke anaweza kumshauri mwenzi
wake amwone mapema daktari, wakati dalili za mwanzo kabisa za ugonjwa
zinapojitokeza. Na pia anaweza kumshauri mwenzake abadili mwenendo wa tabia
zinazoweza kuuongeza madhara yatokanayo na ugonjwa huu kwa mfano, kuacha kuvuta
sigara, kwani tabia ya uvutaji wa sifara huzidisha kiwango cha ugonjwa huu.
Na
pia msaada wa mume au mke, kwa njia moja au nyingine, huzipa nguvu chembechembe
hai za mwili zinazohusika na mfumo mzima wa wa ulinzi. Uchunguzi huo ulionesha
kuwa, wagonjwa wa kansa ya matiti waliokuwa wameolewa na ambao walihisi kuwa
wana uhusiano mzuri na imara na wenzi wao wa ndoa na kuwa wanapewa kila msaada
wanaouhitaji, chembechembe zao hai zinazolinda mwili, zilionekana kufanya kazi
kwa kiwango cha juu kabisa na hata ziliweza kuua baadhi ya vijidudu
vinavyosababisha ugonjwa huo.
Ndoa
bora na imara imekuwa ikitajwa sana kama ni tiba inayoweza kutibu maradhi mengi
ikiwemo kansa na pia imekuwa ikielezwa kwamba, huufanya mwili wa binadamu kuwa
imara zaidi, watu wenye ndoa za mashaka na vurugu, wanapoingia katika maradhi,
wameonekana kudhoofu na pengine kufa haraka, ukilinganisha na wale ambao wako
kwenye ndoa imara.
Kwa
hiyo hapa utajua, inaposisitizwa kwamba,wanandoa wajenge ukaribu ambao
utawezesha ndoa zao kuwa bora na imara, siyo tu kwa sababu ya ya kufurahia
mahaba, lakini pia ni kwa sababu ya kunusuru afya ya miili yao. Tafiti nyingi
zimekuwa zikionesha kwamba, wanandoa ambao wako kwenye vurugu za kindoa hupata
madhara mengi ya kimwili, wanawake wanaelezwa kwamba huathiriwa zaidi na jambo
hilo.
Kumbuka huu ni utafiti tu uliofanya na wenzetu. Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku, ili uweze kuboresha na kubadili maisha yako.
Tupo
pamoja,
Imani
Ngwangwalu,
Simu;
0713 048035,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Feb 25, 2016
Misingi (3) Ya Kuweka Juhudi Katika Safari Ya Mafanikio
Nafahamu
ya kwamba kila mmoja anafanya mambo mbalimbali kama vile kusoma, kufanya
biashara, na kutoa huduma mbalimbali. Lakini yote hayo huleta matokeo chanya
endapo utaweka juhudi za kweli katika endaji wako na kinyume cha hapo
utakuwa unashindwa. Watu wengi huwa tunafanya vitu ili mradi tu, siyo kama
tunapenda kufanya vitu hivyo ila kwa kulazimishwa tu au kwa kuiga kutoka kwa
watu wengine mwisho wa siku tunajikuta hatufanyi tena vitu hivyo.
Hebu
tuendelee kidogo tuone maana ya neno JUHUDI ni kile kitendo cha kufanya kitu kwa kutumia bidii, maarifa, nguvu
na umakini wa hali ya juu ili kupata matokeo sahihi. Pia juhudi ni maarifa,
njia, nguvu ambayo unaipata hata pale wanaokusaidia kwa sasa wakikuucha je, unauwezo wakusimama peke yako?
Mfano wewe ni mwanafunzi wazazi au ndugu zako wanakusomesha kwa hali na mali, swali la kujiuliza wewe mwanafunzi je una uwezo wa kusimama peke yako endapo wanaokusaidia watakuacha? Je utatumia juhudi gani katika kutafuta njia zako binafsi za kukamilisha jambo fulani?
Mfano wewe ni mwanafunzi wazazi au ndugu zako wanakusomesha kwa hali na mali, swali la kujiuliza wewe mwanafunzi je una uwezo wa kusimama peke yako endapo wanaokusaidia watakuacha? Je utatumia juhudi gani katika kutafuta njia zako binafsi za kukamilisha jambo fulani?
Ifuatayo
ndiyo misingi ya kuweka juhudi katika safari yako ya mafanikio;
Kwanza, Kujitoa.
Ili
kuona unapata mafanikio makubwa hakikisha ya kwamba unajitoa kwa moyo wote
katika kupata kile unachokihitaji. Kwa kitu chochote unachofanya jitoe kukipenda
kitu hicho. Kwa mfano wewe ni mfanyabiashara eneo fulani hakikisha unaipenda
kazi yako kwa kujifunza kila siku vitu vipya juu ya jambo unalolifanya. Pia kwa jambo lolote unalolifanya weka juhudi zote
na kuhakikisha utapata kile unachokihitaji.
WEKA JUHUDI KWENYE KAZI ZAKO BILA KUCHOKA. |
Pili, uvumilivu.
Wengi
wetu huwa hatuna chembe ya uvumilivu hata kidogo hasa pale changamoto
zinapojitokeza katika mambo tunayofanya. Pia tukumbuke ya kuwa changamoto ni
sehemu anayopitia mtu yeyote msaka mafanikio. Jambo la msingi la kuzingatia ni
uvumilivu na siyo kukata tamaa. Kuna usemi wa wahenga unasema ‘mvulivu hula mbivu’ Hivyo tuishi usemi
huu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzikubali changamoto na kujua jinsi gani ya
kuziepuka ili tupate mafanikio tunayoyahitaji.
Tatu, kuwa mbunifu.
Hii
ndio siri kubwa katika kutafuta mafanikio makubwa ambayo yapo upande wako. Kuwa mbunifu katika mambo
mbalimbali huku ukiyatendea kazi hayo uliyoyabuni kwa juhudi zote. Kama wewe ni
mwanamziki basi fanya kazi hiyo kwa juhudi zote huku ukiamini ya kuwa kipaji
hicho ndio sehemu ya maisha yako na kipato chako, usifanye kitu kwa kujaribu.
Katika
suala la kuwa mbunifu kuna msomi mmoja amewahi kusema ya kuwa dunia ya leo
haitaki kujua wewe una nini ila ioneshe dunia wewe una nini? Nafikiri kwa mfano
huo utakuwa umenielewa vizuri zaidi. Pia tukumbuke ya kuwa ubunifu sio
lazima kuvumbua kitu kipya bali hata kwa kukiongezea ubora kitu cha zamani pia
ni ubunifu pia.
Wapo
baadhi ya watu wana pesa lakini hawana
juhudi. Kama wewe ni miongoni mwa watu hao kumbuka pesa hizo zitakuwa ni za
msimu na pindi zitakapoisha utabaki unashanga tu. Watalamu mbalimbali wamebaini
ya kuwa na pesa bila juhudi sio kufikia malengo. Tenda mambo yako
katika mtiririko unaoelewaka na ambao unaweza kuutimiza kwa muda muafaka , ukifanya
hivyo kuwa tayari kuyapokea mafanikio makubwa
Ewe
rafiki yangu wa DIRA YA MAFANIKIO, tukumbuke ya kuwa JUHUDI ndio msingi rasmi
wa mafanikio ambayo unayahitaji. Swali la kujiuliza je, upo tayari kulifanya
jambo hilo kwa juhudi dhabiti? Kama jibu lako ni ndio basi weka juhudi zako
zote katika utendaji wa jambo fulani kwa kuzingatia muda. Ukifanya hivyo
mafanikio makubwa yatakuwa upande wako siku zote.
Ansante
kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku. Ombi letu kwetu kwako, endelea
kuwashirikisha wengine waweze kujifunza zaidi kutokana na makala tunazozitoa
hapa.
Kama
una maswali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii Benson chonya mtalamu wa maendeleo na
mipango.
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 24, 2016
Mambo 8 Yatakayosaidia Kufikia Malengo Yako.
Kila
wakati wengi wetu katika maisha, ni watu wa kujiwekea malengo. Mara nyingi huwa
tunaweka malengo haya, kwani kwa
kujiwekea malengo hayo ndiyo hutuongeza
na kutuhakikishia kule tunakotaka kufika
kimafanikio. Kwa kujua hili, karibu kila mtu msaka maendeleo, kwake malengo
huwa ni kitu cha lazima sio cha kuuliza tena.
Lakini
hata hivyo, pamoja na kujiwekea malengo mazuri,
kwa bahati mbaya sana tena wengi wetu huwa bado hatuyafikii malengo
hayo. Hapo ndipo maswali mengi sana ya kwanini huanza kuibuka vichwani kwetu?
Kama mambo ni hivyo usikate tamaa, Kwa kufatilia makala haya utajifunza juu ya
mambo muhimu yatakayokusaidia kufikia malengo yako.
1. Yajue malengo yako vizuri.
Huwezi
kufanikiwa kama huyajui malengo yako vizuri. Ni lazima malengo yako yawe ya
wazi kwako. Ikiwezekana yaandike vizuri kwenye karatasi nayaweke sehemu
inayoonekana. Kwa mafano kama lengo lako ni kufanya biashara ya ‘stationary’ liandike lengo hilo mahali
na lionekane. Kama pia lengo lako ni
kufungua duka weka wazi lengo lako kwa kuliandika.
Watu
wengi mara nyingi wanashindwa kufikia malengo yao kwa sababu malengo yao
yanakuwa sio wazi sana. Siku zote mawazo yetu ya ndani hutusaidia kufikia malengo
yetu, kama malengo hayo yana eleweka. Kinyume cha hapo, utakaa sana kusubiri
malengo yatimie lakini wapi. Hivyo siri ya kufikia mafanikio jitahidi kuweka
malengo yako wazi.
HAKUNA CHA KUKUZUIA KWENYE MAFANIKIO UKIAMUA. |
2. Jitoe kikamilifu.
Siri
ya mafanikio ni kujitoa kikimalifu kwa kile unachokifanya. Hata malengo yako
ambayo umeshajiwekea na yako wazi ili kuweza kuyafikia ni lazima ufanye juu
chini kujitoa kikamilifu na wala sio nusunusu. Ikiwa utakuwa unayaendea malengo
yako, huku ukiwa hujaamua kujitoa kikamilifu tambua ikatokea umeshindwa
usishangae hapo kwa hilo.
Kwa
kuwa unanajua malengo yako nini, kama kuna kazi unatakiwa kuifanya ifanye kweli
kwa nguvu zako zote bila kuchoka. Weka juhudi na maarifa yako yote na
kuhakikisha unajitoa kweli. mafanikio yako hayatakuja kirahisi eti kwa kufanya
kazi kilegevu. Jitoe kwa kupiga kazi kwelikweli mpaka kieleweke.
3. Kamilisha majukumu yako kila siku.
Unaweza
ukawa unayajua malengo yako na umejitoa kikamilifu, lakini huwezi kuyafikia
malengo yako kama kila wakti unakuwa hukamilishi zile kazi zinazotakiwa kukusaidi kuyafikia malengo yako. Hapa sasa
ndipo unapotakiwa kujilazimisha na kuhakikisha kila jukumu ulilonalo unalikamilisha kwa siku husika.
Kwa
mfano kama wewe ni mfnyabiashra ulitakiwa kupga mahesabu Fulani ya kukusidia,
fanya hivyo bila kuacha. Halikadhalika akama wewe ni mwandishi na umejipangia
kuandika kurasa mbili kwa siku, pia fanya hivyo bila kuacha wala kuahirisha.
Kwa kukamilisha majukumu yako kila siku itakusaidia kufikia malengo yako kuliko
ambavyo ungefanya mambo nusunusu.
4. Yagawanye malengo yako.
Malengo
yoyote ulinayo yanaweza kufikika. Haijalishi malengo hayo ni makubwa kivipi
lakini uwezo wa kuyafanikisha upo, ikiwa tu lakini utafuata hatua za
kuyakamilisha malengo hayo. Pengine unajiuliza kivipi au nitawezaje
kuyakamilisha malengo yangu makubwa? Ni rahisi tu na hata wewe unaweza.
Kulielewa
hilo vizuri ngoja nikupe kisa kimoja moja ambacho kinaelezea siku moja fisi
mkubwa alimkuta fisi mdogo akimla tembo. Fisi Yule alivyoona vile alicheka sana
na kumuuliza utamaliza lini? Fisi Yule mdogo alimwambia nitamla kidogo kidogo
mpaka ataisha. Kwa kutumia mfano huo hivyo, ndivyo unavyotakiwa na wewe kufanya
kwa malengo yako makubwa. Unajiona una malengo mkubwa yagawe vipande vipande
mpaka uyafikie..
5. Tafuta msaada.
Ni
rahisi kuyafikia malengo yako, kama utatafuta msaada wa kukusaidia kuyafikia
malengo hayo. Acha kung’ang’ania kukamilisha malengo hayo ukiwa peke yake.
Yaangalie malengo yako yana husu nini kisha baada ya hapo jiulize je, ni mtu
gani au watu gani ambao wanaweza kunisaidia
kukamilisha malengo haya.
Kwa
kujua watu ambao watakusaidia kukamilisha malengo yako itakusaidia sana kushirikiana
nao kwa ukamilifu na kwa ubora wa hali ya juu hadi kufikia mafanikio yako.
Tambua na elewa sio kwa sababu malengo ni yako, hivyo unatakiwa kuyakamilisha mwenyewe,
hapana. Tafuta kile unachokosa, kisha omba msaada.
6. Kuwa chanya wakati wote.
Kuna
wakati tunapokuwa tunajiwekea malengo huwa tunakutana na changamoto nyingi sana
ambazo zinatukatisha tamaa. Sasa hali hii inapokutokea ni vyema ukajitahidi
ukawa chanya wakati wote. Acha kukataa wala kujiona hufai, endelea kusonga
mbele kati kati ya changamoto hizo ulizonazo wewe.
Kuwa
chanya wakati unatafuta mafanikio inalipa sana. Tuchukulie kwa mfano unafanya
biashara halafu ukapata hasara, hapo unafanyaje? Utaacha au itakuaje? Jibu ni
kuendelea na safari ya mafanikio kwa
kutambua kwamba hiyo nayo ni hatua ya mafanikio pia. Ndiyo maana tunasema ni
muhimu na lazima kuwa chanya ili kuyafikia mafanikio yako.
7. Kuwa tayari kuyapitia malengo yako
kila wakati.
Pamoja
na kwamba umejwekea malengo vizuri, umejitoa kabisa kwenye malengo hayo, lakini
hutakiwi kusahau kabisa kuyapitia malengo yako. Ni muhimu kuyapitia tena na
tena malengo kwa kutambua wapi ulipofikia, nini kinachokukwamisha na ufanye
nini ili uweze kusogea hapo ulipo kwa kasi zaidi.
Watu
wengi wenye mafanikio wanayapitia malengo yao. Wanapita malengo yao asubuhi,
wanapitia malengo yao mchana, wanapitia malengo yao jioni. Picha kamili ya
malengo yao inakuwa ipo kichwani mwao tayari. Hiki ndicho kitu ambacho
unatakiwa ukifanye hata wewe. Pitia malengo yako kila wakati ili yaumbieke
vizuri na itakusaidia kuyakamilisha.
8. Jifunze kufurahia mafanikio kila
hatua unayopitia.
Pamoja
na kujiwekea malengo yetu makubwa, lakini kumbuka kuna yale malengo yetu madogo
madogo ambayo huwa tunayashinda. Inapotokea umefanisha jambo fulani, hata kama
kwako ni dogo ni vyema ukajifunza kulifurahia. Furahia mafanikio yako siku hadi
siku kwa jinsi unavyoyapata. Hiyo itakupa nguvu ya kufanikisha mambo mengine.
Kama
kweli una nia njema ya kufikia mafanikio makubwa, basi hayo mambo ni ya msingi
sana katika kukusaidia kufikia malengo yako makubwa uliyojiwekea. Jukumu lako
kubwa ni kuhakikisha unayaweka kwenye vitendo mambo hayo. Na kwa kufanya hivyo basi utaweza kufikia
malengo yako na kutakuwa hakuna wa kukuzuia.
Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila wakati. Usikose kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia makala tunazozitoa hapa.
Ni
wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani
Ngwangwalu,
Simu;
0713
04 80 35,
Feb 23, 2016
Siri Ya Kufanikiwa Katika Katika Kila Jambo.
Haijalishi
hapo ulipo unafanya kitu gani, lakini ninachotaka kukwambia hapa leo, tambua ipo siri ya kuweza kukusaidia kufanikiwa kwa asilimia zote mia moja, kwa lile
jambo unalolifanya. Watu karibu wote wenye mafanikio makubwa wanaitumia siri
hii kuweza kufanikiwa.
Kama
watu hawa wenye mafanikio wamekuwa wakiitumia siri hii kuwafanikisha, basi hata
wewe unaweza kuitumia siri hii kukufanikisha na kubadili maisha yako kabisa.
Pengine umekuwa ukishindwa sana kwenye maisha yako miaka na miaka kwa sababu ndogo
tu, ya kushindwa kuijua siri hii na kuitumia.
Ninachotaka
kusema na kukusisitiza ni kwamba kwa malengo yoyote uliyonayo, unao uwezo wa kuyafikia
ikiwa tu utaamua kuitumia siri hii ya ushindi kukufanikisha. Kumbuka siku zote hakuna
uchawi wala muujiza katika mafanikio. Hata wewe unaweza kufanikiwa kwa kishindo
ikiwa utazingatia na kufanyia kazi siri hii.
Usijali
sana kwa sehemu ulipo kimaisha kwa sasa. Hiyo itabaki kwako kuwa historia.
Angalia mbele nakutumia siri hii kubwa ya mafanikio ambayo unakwenda kujifunza
sasa. Siri ambayo unatakiwa ujifunze na kuilewa vizuri ni siri ya kutengeneza tabia za mafanikio.
TENGENEZA TABIA ZA MAFANIKIO. |
Hautaweza
kufanikiwa ikiwa wewe hutajitengenezea tabia za kuelekea kwenye mafanikio
unayoyataka. Mara nyingi miili yetu inapenda sana tuendelee kukaa katika hali
tulizozizoea. Sasa mafanikio hayawezi kuja kwa namna hiyo ya mazoea. Ni lazima
kuna mambo utatakiwa kuyabadilisha au
kutengeneza tabia za mafanikio.
Jaribu
kumuangalia Mohamed Ally katika kipindi chake alichokuwa akishinda mapambano
mengi ya masumbwi, asingeweza kufika huko kama asingetumia muda mwingi kufanya
mazoezi na kujitengenezea tabia za mafanikio. Kilichomfanya afanikiwe ni
kujitengenezea tabia za mafanikio na kuwa mtii. Hiyo ndiyo ilikuwa siri ya mafanikio
yake.
Lakini
si hivyo tu, hata ukichunguza maisha ya watu waliofanikiwa sana, kikubwa
kilichowafanikisha na kuwafikisha walipo ni kule kujitengenezea tabia za
mafanikio kila siku. Hapa ndipo mafanikio makubwa yanapoweza kuanzia na sio
kinyume chake.
Kuna
wakati niliwahi kusoma maandiko ya mwanasaikolojia Julia Kristina Mah, amabapo
alikuwa akiongelea thamani ya kutengeneza tabia za kukufanikisha. Alisema moja
ya tabia inayowafanya watu washindwe kuafanikiwa ni kule kupenda kufanya mambo
kwa kujisikia au kuongozwa na hisia sana.
Aliendelea
kusema watu wengi wana tabia ya kufanya mambo kwa kujisikia, kama anaona
kachoka kidogo basi hafanyi atasubiri mpaka atakapokuwa sawa, hiyo ni tabia
inayowarudisha wengi nyuma. Hivyo, dawa ya kutoka hapo ni kutengeneza tabia za
mafanikio na si kusubiri.
Kaa
chini na ujiulize ni kitu gani unakitaka katika maisha yako? Ukishakijua kitu
hicho tengeneza tabia itakayokusaidia kukufikia kitu hicho. Kwa mfano kama
unataka kuwa msomaji mzuri, basi tenga muda wa kujisomea kila siku hata kwa
dakika ishirini kwa siku, baada ya muda utafikia lengo lako.
Kwa
chochote unachokitaka inawezekana kukipata ikiwa utajitengenezea tabia imara za
kukufanikisha. Ikiwa lengo lako ni kutafuta mtaji ni sawa, jiwekee akiba kidogo
kidogo kila wakati, utafanikisha lengo lako hilo. Hakuna tena nasema hakuna
utakachoshindwa kukifanikisha ikiwa una tabia sahihi za mafanikio.
Ni
vyema ukaitambua siri hii ukaitumia kukufanikisha. Kumbuka, tabia ni kitu
ambacho hufikirii kukifanya bali kina kuwa kwenye damu. Hivyo ndivyo
unavyotakiwa kujitengenezea tabia zako za mafanikio. Bila kuchoka kila siku.
Kwa kufanya hivyo utajikuta zile kazi ulizokuwa ukizifanya kwa ugumu zinakuwa
rahisi sana kwako na kukupa mafanikio.
Ansante sana kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila wakati. Endelea kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia makala tunazotoa hapa.
Ni
wako rafiki katika kuyasaka mafanikio ya kweli,
Imani
Ngwangwalu,
Simu;
0713 048035,
E-mail;
dirayamafanikio@gmail.com
Feb 22, 2016
Sababu Zinazoweza Kufanya Biashara Yako Ikafa, Hata Kama Ina Mtaji Mkubwa.
Mara
nyingi wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mara kwanza huamini sana mtaji ndio
kila kitu. Kwa imani hiyo, hujikuta mara baada ya kuingia kwenye biashara
wanakuwa hawaweki nguvu nyingi katika maeneo mengine muhimu ili kuboresha
biashara zao. Na matokeo yake hupelekea biashara hizo kuanza kufa huku zikiwa
zina mtaji mkubwa kabisa.
Kinaweza
kuonekana ni kitu cha kushangaza lakini huo ndio ukweli. Unajua ni kwa nini ? Ni
kwa sababu waliaminishwa toka siku nyingi kwamba ukiwa na mtaji mkubwa basi,
kila kitu kimekwisha. Lakini, leo katika makala yetu tutaangalia sababu
zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa.
Kwa
kupitia makala haya itakuonyesha na kukupa ukweli wa wazi kwamba, mtaji mkubwa peke yake sio ‘gerentii’ ya kukufanya wewe ukafanikiwa
kibiashara. Yapo mambo mengine ya ziada
ambayo unatakiwa kuyazingatia na kuyatilia mkazo kila siku, ili biashara yako
iweze kukupa yale matunda unayoyataka.
Kumbuka
haijalishi biashara yako ina mtaji kiasi gani, lakini elewa ukweli huu inaweza
ikafa usipozingatia mambo haya ya msingi. Sasa nataka twende pamoja kujifunza
na kujua mambo au sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama
ina mtaji mkubwa vipi. Karibu sana
tujifunze pamoja.
1. Kukosa usimamizi imara.
Kama
unaona unataka kuanzisha biashara yako, halafu ukagundua huna usimamizi imara
ni bora ukaachana na hiyo biashara. Na kama ungekuja kwangu leo na kunieleza
hali hiyo ilivyo, ningekushauri hivi ‘ Chukua pesa hizo kisha nenda mjini, katafute
sehemu wanakochoma nyama nzuri kula pesa yote usibakize hata Shilingi mia moja.’
Sikutanii.
Kwa nini nakwambia hivyo, kufanya biashara yako huku ukiwa huna usimamizi wa
kutosha ni sawa na kupoteza pesa hizo. Tena unazipoteza bila kufaidi hata tone.
Hapa unaona hata kama ungekuwa na mtaji mkubwa vipi, kama huna usimamizi ni
lazima biashara hiyo itakufa tu, hakuna ubishi.
KUKOSA USIMAMIZI BORA, NI SUMU YA BIASHARA. |
2. Kukosa elimu ya biashara.
Najua
umeshawahi kusikia sana fulani alipata mkopo wa
benki milioni sitini, lakini biashara zake zimekufa. Unajua chanzo chake
kimojawapo ni nini? Ni kukosa elimu ya biashara. Wengi wanapokosa elimu hii
huwekeza kiholela sana matokeo yake kupoteza pesa nyingi bila sababu ikiwa
pamoja na mtaji.
Kwa
hiyo ili kufanikiwa kibiashara ni lazima wewe kuwa na elimu ya kutosha
kibiashara. Pengine unataka kujiuliza nitaipata wapi sasa? Sikiliza huhitaji
gharama kubwa sana kuipata. Unaweza kujifunza kupitia semina, huwezi hilo
unaweza kujifunza kupitia mitandao ya kuhamasisha au ukanunua vitabu
vinavyohusu biashara ukajifunza polepole. Lakini kikubwa usiikose elimu hii,
vinginevyo utapoteza mengi ikiwa pamoja na biashara yako.
3. Matumizi mabaya pesa.
Sio
kwa sababu biashara yako ina mtaji mkubwa na inaingiza pesa nyingi kwa siku,
basi na matumizi yako yanakuwa yako juu bila sababu. Kama unafanya hivyo kwenye
biashara yako nikupe tu uhakika huu, huwezi kufika mbali. Ni lazima uwe na
mpangilio mzuri wa matumizi yako ya pesa ili kuifanya biashara yako ikazidi
kuendelea.
Acha
kujidanganya kwa kuendelea kutumia pesa vibaya, utazipoteza zote mpaka
utashanga. Kikubwa unajua jinsi huo mtaji ulivyoupata. Kama ni hivyo kwa nini
uutumie hovyo? Kuwa makini na pesa zako. Tofauti na hapo biashara yako itakufa
tu hata kama sio leo, lakini lazima itakufa.
4. Kukosa ubunifu.
Ili
uweze kukabiliana na ushindani, ubunifu ni muhimu sana katika biashara yako. Bila
kuwa mbunifu huwezi kufanikiwa katika hiyo biashara kutokana na mazingira ya
ushindani mkubwa tulionao kwa sasa. Kwa hiyo ni lazima kuwa mbunifu na kuifanya
biashara yako ikaonekana ya tofauti na kukupa wateja wa kutosha.
Wengi
wanaoshindwa kwenye biashara ni wale walioingia kwa kiburi cha mtaji mkubwa na
kusahau ubunifu. Haijalishi unafanya biashara ndogo au kubwa weka ubunifu. Kila
wakati tafuta ni kitu gani biashara yako inakosa, kisha kiboreshe zaidi. Jitahidi
sana kuweka ubunifu ili kuifanya biashara yako iwe hai siku zote, vinginevyo utaiua.
5. Kukosa nidhamu.
Kama
unaendesha biashara yako na ukakosa nidhamu ya kuiendesha biashara hiyo, elewa
kabisa utakuwa na mchango mkubwa sana wa kuiua. Nidhamu ni msingi mkubwa sana
wa mafanikio yoyote na sio biashara tu peke yake. Jaribu kuangalia watu wote
wenye nidhamu ya kazi mafanikio yao yakoje? Bila shaka ni makubwa.
Biashara
nyingi sana zinazokufa huku zikiwa na mtaji mkubwa mara nyingi hukosa nidhamu. Tuchukulie
una duka la reja reja, huwezi kufanikiwa ikiwa unafungua na kufunga unavyotaka.
Ni lazima uwe una nidhamu ya muda, nidhamu ya kuwajali wateja au nidhamu ya
kauli nzuri. Kwa kukosa nidhamu hizi biashara itakufa tu hata iwe kubwa vipi.
6. Kukosa wateja.
Kati
ya kiungo muhimu sana kwenye biashara yako ni wateja. Bila wateja hakuna
biashara inayoweza kufanyika. Sasa kama utakuwa huna wateja hiyo inamaanisha
biashara yako kwa vyovyote vile itaenda kufa hata ufanye nini. Maana hao ndio
wawezeshaji wakubwa kwenye biashara yako kuendelea.
Sasa
huwa zipo sababu zinazopelekea biashara hii ikakosa wateja na nyingine ikawa na
watej wengi. Hivyo ni vyema ukazijua sababu hizo ili zikusaidie kuweza kujenga
biashara ya uhakika na yenye mafanikio makubwa.
7. Kukosa vipaumbele.
Biashara
yoyote iwe inanza au inaendelea ni lazima iwe na vipaumbele vya msingi ambavyo
vinatakiwa vifuatwe kila siku. Kama kipaumbele chako kimojawapo ni kutaka
kukuza mtaji ni vyema ukawa makini kuhakikisha hilo linatimia na kutekelezeka kwa
haraka sana.
Lakini
kama pia vipaumbele vyako ni kuhakikisha unadumisha mahusianao mazuri na wateja
wako, pia ni bora ukatekeleza. Unapokosa vipaumbele hata vile unavyoviona ni
vidogo ni rahisi sana kwa biashara yako kuweza kufa na kushindwa kuendelea hata
kama ina mtaji wa kutosha. Kwa sababu hapa tunasema biashara inakuwa inakosa
dira maalumu.
8. Kukosa mgawanyo wa majukumu.
Pia
biashara inaweza ikafa hata kama ina mtaji wake mkubwa, ikiwa itakosa mgawanyo
wa majukumu. Ni lazima biashara iwe na
mgawanyo wa majukumu ili iweze kusonga mbele. Kama unaona unafanya biashara
huku kila kitu umeshikilia wewe na hakuna wa kukusidia elewa upo kwenye hali
mbaya.
Ni
lazima utafute watu wa kukusaidia hata kama pale haupo mambo yaweze kwenda sawa
kabisa. Siri mojawapo kubwa ya kufikiwa mafanikio makubwa kwenye biashara yako
ni kutengeneza mgawanyo mzuri wa majukumu kwa wasaidizi wako. Kushindwa kufanya
hivyo ni lazima utaua biashara yako.
Kama nilivyoanza kwa kusema zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa. Kwa leo naomba niishie hapo. Tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine nzuri ya biashara. Kumbuka kuchukua hatua. KILA LA KHERI.
Ni
wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Feb 19, 2016
Faida Kubwa Za Nidhamu Binafsi Katika Kuyafikia Mafanikio Yako Makubwa.
Nidhamu maana yake ni utaratibu au sheria anayojiwekea mtu au
kuwekewa mtu katika kufanya au kutofanya kitu ama jambo fulani katika maisha.
Mara nyingi nidhamu humwongoza mtu na kumwekea mipaka kwa baadhi
ya vitu kuvifanya au kutokuvifanya ima kwa kupenda au kutopenda.
Nidhamu ziko za aina mbili nidhamu binafsi anayojiwekea
mtu binafsi kwa makusudi ya kutimiza malengo fulani aliyojiwekea katika maisha
yake. Na kuna nidhamu inayowekwa na kikundi, taasisi, kampuni au serikali ya
nchi kwa madhumuni maalumu.
Leo tunaangalia zaidi katika nidhamu binafsi. Nidhamu binafsi
ndio imekufanya wewe uwepo hapo ulipo na uwe hivyo ulivyo. Ni kutokana na
nidhamu binafsi ndiyo imekufanya ufanikiwe au usifanikiwe katika maisha
yako. Nidhamu binafsi ndiyo inayomwongoza mtu katika kufanya maamuzi sahihi au
yasiyo sahihi katika maisha yake.
Zifuatazo ni faida za mtu kuwa na nidhamu binafsi;-
1. Nidhamu binafasi
humfanya mtu kujitambua yuko wapi, ni nini wajibu wake katika maisha yake na
jamii inayomzunguka.
2. Humwongoza mtu katika kufanya maamuzi sahihi katika maisha
yake kwani humfanya atafakari kwanza hasara na faida ya kile anataka, kabla ya
kulifanya.
3. Humfanya atimize malengo yake kirahisi kwa sababu hufikiri
kabla ya kufanya mambo.
KUWA NA NIDHAMU BINAFSI. |
4. Nidhamu binafsi humfanya mtu kupendwa na watu kwa sababu ya
kufanya vitu sahihi na mwenye uhakika navyo.
5. Humfanya mtu asikurupuke na kuiga vitu asivyo na uhakika
navyo.
6. Humfanya mtu kutimiza majukumu yake kwa wakati.
7. Humfanya mtu kujiamini na kuondokana na hofu katika maisha.
8. Humafanya mtu kuwa na matumizi mazuri ya muda na pesa.
9. Humfanya mtu kufanya vitu kwa malengo na kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
10. Humfanya mtu kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Mbali na faida hizo za nidhamu binafsi, Zifuatazo ni hasara za mtu kutokuwa na
nidhamu binafsi katika maisha yake.
1. Huishi kwa kufuata Mkumbo hawi na utaratibu ktk maisha yake
ni kama bendera fuata upepo.
2. Mtu ambaye hana
nidhamu binafsi anakuwa hana maamuzi sahihi katika maisha yake na kamwe huwezi
kumwomba ushauri mtu asiye na nidhamu binafsi atakupoteza
3. Humfanya mtu kutokujiamini na hivyo kuwa na wasiwasi na hofu
katika kufanya jambo lolote. Sijui nitaweza nimtafute nani anishauri ili nisikosee.
4. Humfanya mtu kutumia vibaya muda wake na pesa zake kwani hutumia
bila umiliki wowote ule.
5. Ni mtu asiye na malengo huishi kwa kubahatisha na kudra za
Mungu. Anasema tutafika tu, ipo sikunami nitafanikiwa tu Siku na miaka inaisha
hadi kifo kinamfika hakuna alichofanya.
6. Humfanya mtu kuvunjika moyo haraka pindi anapoanguka au
kutifanikiwa katika jambo analofanya.
8. Hukushelewesha au kukunyima kabisa fursa ya mafanikio na
kutimiza ndoto zako katika maisha.
9. Ni rahisi kubadilisha maamuzi uliyojipangia na kuanza kufanya
kitu kingine ambacho hukukipanga kukifanya.
10. Kukosa nidhamu binafsi humfanya mtu kudharaulika na jamii
inayomzunguka kwa kukosa busara na ueledi katika kusema kwake, kutembea kwake
na hata kutenda kwake.
Ansante kwa kufatilia makala haya na endelea kuwaalika wengine
waweze kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO.
Ni wako katika kupeana hamasa ya kuyafikia mafanikio na uhuru wa
kipesa.
Shariff H. Kisuda alimaarufu mzee wa Nyundo Kali.
Simu; 0715079993.
E-mail; kisudashriff@gmail.com
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com
Feb 18, 2016
Jifunze Kuendesha Kilimo Hiki Cha Kisasa, Ili Uweze Kutoka Kwenye Umaskini.
Habari rafiki na mpenzi msomaji wa DIRA YA MAFANIKIO. Naamini umzima
wa afya na unaendelea kujifunza ili kuboresha maisha yako. Katika makala yetu
ya leo tutaangalia namna unavyoweza kuendesha kilimo bora cha kisasa ili uweze kukabiliana na changamoto za maisha ikiwemo na
kuutokomeza umaskini kabisa.
Ikumbukwe kwanza kuna aina mbili kubwa za kilimo. Aina ya
kwanza ni kilimo cha nje yaani ‘outdoor farming’. Hiki ni kilimo ambacho
hutegemea mvua au umwagiliaji, lakini
mkulima hana uwezo wa kutawala kiasi cha maji au kiasi cha jua. Mazao huweza kuzalishwa
nje kama ambavyo wakulima wengi tumezoea kuwaona.
Aina ya pili ni kilimo cha greenhouse/ kitalu nyumba
Kilimo hichi hufanyika ndani ya nyumba maalumu iliyotengenezwa
kwa kutumia aina maalumu zinazoruhusu mwangaza kupenya ndani.
Pembeni huzungushiwa wavu maalumu unaoruhusu hewa kuingia na
kutoka. Na chini huwekewa mipira maalumu kwa ajili ya kufanya umwagiliaji wa
zao lako.
Faida za kulima kwenye kitalu nyumba/greenhouse. Mkulima anaouwezo wa kudhibiti hali ya hawa
mfano kiwango cha maji yanayohitajika, kiwango cha joto, kiwango cha unyevu
angani/ humidity. Na hivyo kumruhusu mkulima kufanya uzalishaji hata wakati ambapo
mvua kubwa zinaendelea kunyesha sehemu mbali mbali.
KILIMO HEMA/GREEN HOUSE. |
‘Greenhouse’ inapunguza mashambulizi ya wadudu waharibifu kwakua
nyumba huzungushiwa wavu maalumu hupata mavuno mengi zaidi kwenye eneo dogo
kutokana na mazingira maalumu ya uzalishaji. Mfano kwenye greenhouse’ yenye
ukubwa wa mita 8 kwa mita 15 ambapo huingia miche 500 ya nyanya mkulima huweza
kuvuna kuanzia kilo 5000 (tani 5) za nyanya na kuendelea.
Cha muhimu kukumbuka, kuwa na greenhouse pekee sio uhakika wa
asilimia zote kukupatia mazao mengi kwasababu ni lazima iendane na upandaji wa
mbegu bora ambazo ni maalumu kwa kilimo cha greenhouse.
Lazima uandae shamba lako vema kwa kulima vizuri na kuweka
mbolea samadi yakutosha. Lazima umwagilie kwa wakati. Lazima pia uzingatie
udhibiti wa wadudu na magonjwa.
Wakulima wengi wanaolima kizamani wanalalamika kilimo hakilipi na
kweli kilimo cha kizamani hakiwezi kukulipa kamwe yaani Kilimo cha zama za
kwanza za mawe. Kwa mfano watu wanaolima kwa kuangalia angani walioapanda
matikiti kwa kutumia mvua za mwezi wa 11 sasa hivi wamevuna na wamejaza
matikiti sokoni hayana wateja.
NYANYA |
Hiyo ni kwa sababu kila mtu anaweza kulima tikiti kirahisi
wakati mvua ya vuli iliponyesha. Sio wote mnakutana sokoni muda huu. Vile vile
wakulima wakizamani muda wa miezi ya kwanza au ya pili hawawezi kulima sana
nyanya kwa kuwa mabonde yao yamejaa maji na pia wanaogopa kupambana na magonjwa
ya aina mbalimbali.
Matokeo yake wanajikuta wakipishana na pesa ambapo mwezi wa pili
au watatu nyanya bei yake inakuwa juu sana. Sasa basi kumbe muda huu ungekuwa
na kitalu nyumba/greenhouse ndio ilikuwa muda wako wakuvuna pesa mpaka mwezi wa
sita wakati wale wanaosubiri kilimo cha kuangalia juu watakapoenda shamba.
Kwa kawaida green house zipo za aina tofauti kulingana na
mkulima anavyotaka iwe. Huwa zipo ‘greenhouse’
za ukumbwa kama huu;
Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x15 ni shilingi milioni 4.5
Greenhouse ya ukubwa wa mita 8 x20 ni shilingi milioni 5.5
Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x30 ni shilingi milioni 7.5
Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x40 ni shilingi milioni milioni
8.5.
Kwa mkulima yoyote anayehitaji huduma ya kutengenezewa
Greenhouse atafuatwa popote pale alipo na kampuni yetu bila bei yoyote
kubadilika. Mkulima atapewa somo la zao analotaka kuzalisha na utunzaji wake
mpaka atakapovuna.
Makala hii imeandaliwa na John Mabagala, ambaye ni mtaalamu wa
masuala ya kilimo na anahusika pia na usambazaji wa pembejeo za kilimo katika
kampuni ya JM AGROCHEMICALS iliyopo
Morogoro mjini.
Kama unataka kufahamu vizuri zaidi juu ya kilimo hiki au
unahitaji huduma ya kufungiwa Greenhouse, popote ulipo wasiliana naye kwa email jmabagala@gmail.com au 0754 282 448 .
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)