google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

May 19, 2015

Hizi Ndizo Mbinu Muhimu Za Kimafanikio, Ambazo Ukizitumia Ni Lazima Uwe TAJIRI.

No comments :
Habari za leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Tunaamini unaendelea vyema  na majukumu ya kuboresha maisha yako. Pia tunapenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kuendelea kuwa msomaji mzuri wa mtandao  huu. Karibu sana na usichoke kujifunza kila siku hapa ilikuweza kuboresha maisha yako.

Ieleweke kuwa kwa kadri unavyozidi kujifunza zaidi ndivyo unavyozidi kuwa bora hata kwa yale unayoyafanya katika maisha yako. Hivyo unakuja kuona kuwa silaha pekee ambayo hutakiwi kuiacha katika safari yako ya mafanikio ni kujifunza kila mara na kila siku. Unapokuwa unajifunza unakuwa unapata mbinu mbalimbali ambazo zitakuwezesha kufanikiwa.

Kwa kuzijua mbinu hizo itakusaidia wewe kukurahisishia kufika kwa urahisi katika safari yako ya mafanikio. Watu wengi wenye mafanikio wanajua mbinu muhimu za kimafanikio zilizowasaidia kuwafanya kuwa matajiri, lakini mara baada ya kujifunza sana. Katika makala hii ya leo tutajifunza juu ya mbinu muhimu za kimafanikio, ambazo ukizitumia ni lazima ufanikiwe.

Mbinu hizi zimeweza kuleta matokeo ama mabadiliko makubwa sana kwa wale wote ambao wamezitumia. Kama utazitumia hata wewe katika safari yako ya mafanikio, utafanikiwa. Lakini tambua kuwa kwa kuzielewa mbinu hizo tu, haitoshi wewe kuwa tajiri tu kwa ghafla. Muda unahitajika ili uweze kufikia malengo yako. Je, unajua mbinu hizo ni zipi?


Hizi Ndizo Mbinu Muhimu Za Kimafanikio, Ambazo Ukizitumia Ni Lazima Uwe TAJIRI.

1. Jitoe mhanga juu ya maisha yako.
Hakuna ubishi juu hili, kama kweli nia yako nikutaka mafanikio ni lazima kujitoa kikamilifu. Hautaweza kufanikiwa kama utayachukulia maisha yako kama mchezo fulani. Kitu pakee unachotakiwa kufanya ni kujitoa mhanga juu ya maisha yako na kukubali kulipia kila gharama inayohitajika ili kuweza kufikia mafanikio unayoyataka.

Ni lazima ujifunze kufanya mafanikio kuwa ni kitu cha lazima. Ukiwa na wazo hili uwe na uhakika ni lazima ufanikiwe kwa vyovyote vile. Watu wengi wenye mafanikio ni watu wa kujitoa na kupigania ndoto za maisha yao kila siku. Hicho ndicho  kitu unachotakiwa hata wewe kukifanya ili kutimiza malengo yako kwa uhakika. Kwa kujitoa mhanga katika maisha yako ni mbinu muhimu kwako itakayokufanikisha ikiwa utaitumia.



2. Jilipe kwanza wewe.
Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukikwambia mara kwa mara sana, juu ya umuhimu wa kujilipa wewe kwanza. Kiasi chochote cha pesa unachokipata ni lazima utenge asilimia kumi ambayo utajilipa wewe ukiwa kama mtafutaji wake. Haiwezekani ukamlipa kila mtu ama ukalipia huduma muhimu kama bili ya maji, umeme, kodi na zinginezo halafu ukajisahau wewe ambaye ni mzalishaji wake.

Kujilipa wewe kwanza, ni mbimu muhimu sana kwako wewe ambayo ukiitumia ni lazima ikufikishe kwenye utajiri. Unachohitaji kufanya wewe sasa kama huna tabia hii ni kuweza kuelekeza nguvu zako kwenye kujilipa wewe kwa kila shilingi unayoipata. Kumbuka itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kuwa tajiri ikiwa utakuwa unamlipa kila mtu na kujisahau wewe. Ukijilipa kwanza, hiyo pesa itakusaidia kwenye kuwekeza zaidi, pale itakapokuwa nyingi.

3. Jitengenezee miradi mingi.
Haitawezekana na haitakuja kutokea hata siku moja eti ukawa tajiri kwa sababu ya kutegemea kazi yako hiyo tu moja unayoifanya, hiyo itakuwa ni ngumu sana kwako. Kama nia yako ni kutaka kuufikia utajiri hakikisha unajitengenezea miradi ya kutosha, ambayo itakuwa inaingiza pesa nyingi zitakazoweza kukusaidia kukamilisha lengo lako hilo.

Na kama ikitokea wewe unataka kuanzisha biashara ya aina moja basi, hakikisha biashara yako hiyo unaitengenezea matawi ambapo hapo itakuwa inakuwa zaidi. Hii ndiyo siri mojawapo kubwa ambayo matajiri wengi wanaitumia kufikia utajiri wao. Kama unafikiri natania angalia ama jaribu kufatilia na kuchunguza kidogo tu, utagundua ama kuona wingi wa miradi waliyonayo.


4. Andaa bajeti ya kukuongoza.
Hili ni jukumu muhimu sana kwako ambalo unatakiwa kulianzisha ili kufikia kule unakotaka kufika katika safari yako ya mafanikio. Ni lazima kama hutaki kupotea katika safari yako, jitengenezee bajeti itakayo kuwa ikikuongoza katika matumizi ya pesa zako. Acha kutumia tu pesa zako eti kwa sababu zipo mfukoni.

Weka utaratibu kila kitu unachokinunua unakiandika katika kijitabu chako cha bajeti ambacho utakuwa nacho. Kwa kufanya hivyo utajikuta hutaweza kupoteza pesa nyingi hovyo. Kwani pesa hizo zinakuwa zinautaratibu maalum unaoeleweka. Kabla hujanunua kitu unaweza ukajiuliza ni kweli kina umuhimu na nisiponunua itakuwaje. Ukiwa na kijitabu kidogo ambacho kinaweka bajeti yako wazi ni lazima ufikie mafanikie makubwa.

5. Kuwa na pesa ya dharura.
Ni ukweli uliowazi mara nyingi katika jamii zetu tunazoishi matatizo ni kitu ambacho hakikwepeki kwa namna yoyote ile. Ili kuweza kukabiliana na hali hiyo ni vizuri ukawa na ‘account’ maalum kwa ajili ya dharura tu. Pesa hii itakusaidia wewe pindi tu unapopata matatizo ndipo utakapoitumia na si vinginevyo.

Kama itatokea huna pesa hii, kila utakapokuwa unapata tatizo kidogo kitu kitakachokuwa kikitokea ni lazima utakuwa unakwenda moja kwa moja kwenye kuharibu mtaji wako kwa maana huna pesa kwako ya dharura. Kwa kuishi maisha ya kuwa na pesa ya dharura ama ‘account’ ya dharura hiyo itakusaidia sana katika safari yako ya kuelekea kwenye utajiri.


6. Kuwa na tabia ya kutoa.
Hii pia ni mbinu muhimu ya kimafanikio, ambayo matajiri wengi wanaitumia kufikia malengo yao. Unapopata kiasi fulani cha pesa ni muhimu pia ukajijengea tabia ya kutoa kwa lengo la kusaidia. Hii inakuwa ni kama sadaka ama shukrani kwako na kwa ulimwengu ambao umekusaidia kukupa kile ulichonacho. 

Mbinu hii, ina matokeo makubwa sana chanya hasa pale inapotumika. Hata hivyo pia ni kanuni ya kiroho. Unashauriwa pia kutoa asilimia kumi ya mapato yako kwa jamii, hii ni kama shukrani kama nilivyosema. Hautakiwi pesa zako kutumia wewe tu, bila kuwa na msaada kwa jamii hiyo itakuwa ni sawa na uchoyo.

Kwa kuhitimisha makala hii, hizo ndizo mbinu muhimu za kimafanikio ambaza unaweza ukazitumia na kukupa mafanikio makubwa na hatimaye kuufikia utajiri unaoutafuta katika maisha yako.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuboresha maisha.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE, 

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.