Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Saturday, April 18, 2015

Siri Kubwa Ya Mafanikio Unayoitafuta Katika Maisha Yako ipo Hapa…

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako huwa unahitaji kuona ndoto zako zikitimia na kuyafurahia maisha katika uzuri wake. Kuna wakati pia katika maisha yako huwa unatamani kubadili maisha yako kwa sehemu kubwa na kufikia hata kuwa huru kifedha. Pia kuna wakati katika maisha yako huwa unatamani ujue ama utambue siri ya mafanikio kwa ujumla ilipo ili ufanikiwe kwa viwango vya juu kabisa kama unavyotaka. Hata hivyo, umekuwa ukishindwa kutokana na kutokujua siri hii.

Kama hiyo kwako ndiyo nia na shauku yako kubwa ya kutaka kujua siri kubwa ya mafanikio ilipo ili nawe uweze kufanikiwa kama hao wengine wanaliofanikiwa, hujakosea kusoma makala hii upo sahihi kwa asilimia zote. Kupitia makala hii utajua na kuelewa kwa uwazi siri ya mafanikio ilipo ambayo itakufanikisha. Lakini je? Ulishawahi kujiuliza siri hii ipo kwenye mambo gani? Sitaki uumize kichwa sana, ukweli ni huu, siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye mambo haya kama utayatekeleza:- 

1. Penda kile unachokifanya.
Hautaweza kufanikiwa katika maisha yako kama utakuwa unafanya mambo ambayo huyapendi katika maisha yako. Unapofanya jambo ambalo hulipendi kitu kikubwa kinachokutokea kwanza hutaweza kufanya kazi hiyo kwa moyo wote, utakuwa unafanya ilimradi tu, kama vile umelazimishwa na mtu. Lakini, si hivyo tu bali hata utendaji wako utakuwa wa kiholela ambao ndani yake hauna ubunifu wowote ule.

Siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye kufanya kile kitu unachokipenda na si vinginevyo. Asilimia kubwa ya watu wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao wanapenda vitu wanavyovifanya. Kama unataka kubadili hali yako uliyonayo sasa na kufikia mafanikio makubwa, kitu cha kwanza unachotakiwa kukifanya ni kuchagua kile unachokipenda na kukifanya kwa moyo wote, utaona mabadiliko makubwa sana katika maisha yako.


2. Anza kwa  kidogo.
Kwa kila unachonza kukifanya ni muhimu kwako kuanza kufanya kwa kidogo. Hii ina maana gani au inaashiria nini kwako? Unapoanza kufanya kwa kidogo hiyo inakuwa inakupa uzoefu na ukomavu kwa lile jambo ambalo unalifanya na hii itakusadia zaidi hasa pale unapokumbana na changamoto inakuwa ni rahisi sana kwako kuweza kupambana nazo na kuzikabili kwa urahisi zaidi.

Kuanza kwa kidogo hii ni moja ya siri kubwa ambayo inatumiwa na watu wengi wenye mafanikio kuweza kufika mbali.ieleweke kuwa kabla hujaanza kukimbia marathoni ni vizuri kuanza kukimbia mita chache ili kuweza kupata uzoefu zaidi. Hivi pia ndivyo ilivyo katika maisha yetu, unataka kufanikiwa sana na ukawa ambaye hushikiki anza kujenga uzoefu kwa mambo madogo ambayo utayamudu kwanza kwa vizuri.

3. Kuwa na nidhamu binafsi.
Pia huu ndio ukweli usiouweza kuupinga kuwa, mara nyingi siri kubwa ya mafanikio yetu ipo kwenye sisi wenyewe kuwa na nidhamu binafsi. Bila kuwa na nidhamu binafsi kupata mafanikio makubwa katika maisha yako, sahau kabisa na kitu ambacho hakitakuja kuwezekana. Unapokuwa unajiwekea nidhamu binafsi hiyo inakuwa inakujengea nguvu kubwa ya kukusadia kuweza kusonga mbele zaidi.

Kama umekuwa kwa muda mrefu ukihangaika na kutafuta siri gani kubwa iliyojificha ambayo inaweza kukusaidia kuweza kufikia mafanikio makubwa, tambua kuanzia sasa ni nidhamu binafsi. Kama unafikiri natania anza sasa kujiwekea nidhamu binafsi kwenye mambo yako halafu utanipa matokeo yake. Kama kweli upo makini na maisha na unataka kufanikiwa kwa viwango vya juu jifunze juu ya hili, utabadilisha sana maisha yako.

4. Kuwa mwaminifu.
Mafanikio yoyote unayoyatafuta yanakutaka ni lazima uwe mwaminifu. Unapokuwa mwaminifu uwe na uhakika ni lazima utaweza kutimiza chochote kile katika maisha yake hata iweje. Kwa nini uaminifu ni kitu muhimu sana kwako? Unapokuwa mwaminifu hiyo  inakusaidia kukujengea imani na wengine na kukuza ushirikiano kwa sehemu kubwa katika biashara unayoifanya ama kitu chochote.

Pasipo kuwa mwaminifu huwezi  kufanikiwa sana katika biashara yako au tasnia unayoifanya hata iweje. Kila utakapojaribu kutaka kufanikiwa utapata tabu sana. Na ninapozungumzia uaminifu na maaninisha ni lazima  uaminifu uanze kwako wewe na kwa wengine pia. Ni muhimu kujijengea uaminifu katika maisha yako pia wewe binafsi. Unaposhindwa kuwa mwaminifu  kwako pia na kushindwa kutimiza ahadi ulizojiwekea hiyo itakupa tabu sana na utashindwa kutimiza chochote.

5. Kufanya kazi kwa bidii.
Siri kubwa ya mafanikio ipo pia kwenye kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Hakuna mafanikio makubwa uatakayoweza kuyapata kama wewe utakuwa sio mtu wa kuweza kufanya kazi zako kwa bidii, kwa maarifa na kujituma kwa hali ya juu. Ukichunguza kidogo tu, utagundua kuwa watu wengi wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao wamejitoa na kufanya kazi kazi kwa juhudi zao zote bila kuchoka.

Kama unataka kufikia mafanikio makubwa ambayo umekuwa ukiyahitaji na kuishi maisha yoyote yale ya ndoto zako, hilo linawezekana lakini litakuja tu kwa kufanya kazi kwa bidii. Unapofanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa mapema na kuwa king’ang’azi wa ndoto zako uwe na uhakika kwa sehemu kubwa ni lazima mafanikio utayafikia. Hakuna kitu kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa hata kidogo kama utakuwa mchapa kazi.

Kwa kuhitimisha makala hii, elewa kuwa utafanya kila unalofanya katika maisha yako, lakini siri kubwa ya kuweza kutimiza ndoto zako ulizojiwekea ipo katika hayo mambo na hiyo ndiyo siri ya kufikia mafanikio makubwa unayatafuta katika maisha yako, vinginevyo utasumbuka sana katika maisha yako kama utakuwa unaishi kinyume na hayo.

Kwa kujifunza zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment