Mar 2, 2016
Siri Iliyopo Kati Ya Mafanikio Na Mwonekano Wako.
Habarini za leo
mpendwa msomaji wa DIRA YA MAFANIKIO. Karibu tena katika siku nyingine ya
kuweza kujifunza. Leo katika somo letu tutazungumzia haiba ya mtu au mwonekano
wa mtu katika kuleta mafanikio. Nawaletea siri iliyoko katika mwonekano wa mtu
na uhusiano wake katika mafanikio.
Thamani ya mtu haiko katika
mwonekano wa nje tu. Vipo vingine vya ndani vinavyoweza kumwonesha mtu haiba au
mwonekano wake na kuwa eidha chanzo cha mafanikio au kutofanikiwa kwake. Mafanikio
ya binadamu yanaanzia kwenye thamani aliyonayo kwa binadamu wenzie.
Mwonekano wako unaweza
kukuweka katika daraja la juu au kukushusha daraja na hata thamani kwa watu.
Tabia ya mtu inaweza kubadilika lakini haiwezi kubadilishwa. Hapa najua wengi
nimewaacha njia panda. Ni kuwa tabia ya binadamu anaweza kuibadili mtu mwenyewe
kwa kuamua kubadilika na sio kuamuliwa na mtu abadilike.
Kuamua kubadili tabia
ni uamuzi wa mtu mwenyewe lakini kubadilishwa tabia ni hatua nyingine ni rahisi
kurudia asili yake. Kila binadamu amezaliwa ili afanikiwe na kila binadamu
ameumbwa kwa makusudi maalumu. Hakuna ambae ameletwa duniani bila ya kusudi
maalumu.
TEMBEA YA MTU INAONYESHA MAFANIKIO YAKE |
Lakini ukweli ni kwamba
90% ya watu wanaishi, ingawa hawajui makusudi ya kuwepo kwao duniani na ndio
maana tunaishi maisha ya kubahatisha. Tunasoma elimu kubwa lakini mafanikio
kidogo, tunasomea udaktari wakati, tunauwezo mkubwa katika mahesabu, tunasoma
kilimo wakati tunapenda kufundisha na mengineyo mengi.
Hii yote binadamu
anafanya kwa sababu ya kutojua kusudi lake la kuumbwa na kuwepo duniani. Mzee
wa nyundo nakuhabarisha leo. Ni namna gani utajenga haiba yako na kutambua
kusudi lako hapa duniani? Fuatana nami nikupe siri ya mafanikio leo. Nataka
nikupe siri ambayo itakuangazia pale penye Giza.
Mwalimu wangu wa saikolojia aliwahi kuniambia hata mwandiko wa mtu
hujulisha tabia yake aliyonayo. Tukacheka lakini baadae alituthibitishia ukweli
wa kauli yake na leo nakufahamisha nawe vitu vinavyoonyesha tabia na haiba ya
mtu.
1. Mavazi, mavazi
yanamshepu mtu na kutoa thamani au kupunguza thamani ya mtu. Vile unavyovaa
inatoa mwonekano wako ulivyo.
2. Kauli au mazungumzo
ya mtu, hili halina ubishi ukiongea na
mtu mkorofi au mpole na mwenye hekma utajua tu.
3. Tembea ya mtu, kila
mtu anatembea yake lakini kila tembea ina ishara yake kimwonekano. Mtu mwenye
dharau hutembea kwa maringo na mtu anaejiamini hutembea mwendo wa
haraka najua hapa utahoji ndio ni kweli.
4. Kujibu au
kuuliza kwako maswali nayo huonyesha tabia yako kwa urahisi sana kuwa ni
mwema au unadharau, unajiamini au hujiamini.
5. Kula kwako nako kunaonyesha
ni mlafi au mkarimu. Hizi ni moja ya tabia au mwonekano wa mtu ambao kwa namna
moja au nyingine unaweza kumpelekea mtu kuaminiwa na wengine na kupata
mafanikio au kutoaminika na kukosa mafanikio.
Kila tabia ina faida
na hasara zake pia. Saikolojia inatuaminisha kuwa tabia ya mtu ya nje ndio
tabia yake ya ndani. Ni ngumu sana mtu kuigiza tabia asiyokuwa nayo ndani mwake
labda aamue kubadilika kabisa mwenyewe na kuachana na tabia yake ya awali.
Tabia ya mtu
kimafanikio au kutofanikiwa huanzia ndani mwake katika kufikiri, kuwaza na
kutenda kwake. Kwa kumalizia somo letu ni tambua, binadamu sote tunaishi kwa
Imani. Na Imani ndio pekee inayomfanya mtu eidha kufanikiwa au kutokufanikiwa katika
maisha yake. Imani ndiyo inayotuongoza au kutupotosha katika kutimiza malengo
yetu. Ili tuweze kufanikiwa katika maisha yetu hatuna hiyari tena ni lazima
tubadili haiba au mwonekano wetu wa nje na ndani.
Inatakiwa pia tubadili
tabia zetu katika kusema na kutenda. Tuwe na fikra chanya na kuacha kuishi
kimazoea. Mafanikio ni haki yetu sote tukiamua inawezekana sana tena bila ya
kutumia nguvu kubwa wala uchawi. Tuamue kuanzia leo kubadili Haiba zetu na
kuishi kimafanikio tuweze kutimiza ndoto zetu na kufikia Uhuru wa kipesa na
kiuchumi.
Kama
una maswali , ushauri au mapendekezo usisite kuwasilliana na mshauri wa
mafanikio, mwanasaikolojia na mwandishi wa makala haya Sharrif Kisuda
alimaarufu Mzee wa Nyundo kali. Lakini
usisite kumshirikisha mwenzako ili aweze kujifunza pia kupitia mtandao huu wa
DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Simu; +255 (0) 079 993
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.