Mar 14, 2016
Mambo 6 Ambayo Mjasiriamali Anatakiwa Kuyafanya Kila Siku.
Kati ya kitu ambacho kila mjasiriamali mwenye nia
ya kufanikiwa anacho ni kule kutaka kuona anakifikia mafanikio makubwa ya
kibiashara. Lakini pamoja na kuwa na nia hiyo ya kufikia mafanikio hayo,
mjasiriamali huyu hawezi kufanikiwa mpaka ajue mambo ya msingi yanayoweza
kumsaidia kufanikiwa na kuyafanya karibu kila siku.
Kwa mjasiriamali yoyote atakayeelewa mambo hayo
itamsaidia sana kuweza kufikia mafanikio makubwa anayohitaji. Kwa kujifunza
kupitia makala haya, itakuonyesha mambo ya wazi ambayo unatakiwa kuyajua kama
mjasiriamali na kuyafanya kila wakati ili kuweza kufanikiwa. Sasa twende pamoja kuweza kujifunza mambo
unayotakiwa kuyazingatia kila siku katika safari yako ya mafanikio.
1. Panga
siku yako mapema.
Ni rahisi sana siku yako kuwa ya mafanikio ikiwa
utaipangilia mapema. Ni vizuri ukaipangilia siku yako mapema ikiwezekana siku
moja kabla ili kuweza kujua ni kitu gani utakachokifanya kesho. Hiyo
itakusaidia kuweka malengo na kupanga mikakati muhimu ya kutekeleza mapema
kichwani mwako kwanza.
Kwa mfano usiku kabla hujalala andika kwenye
kitabu chako ni nini utachokwenda kufanya kesho. Kwa kufanya hivyo kila siku
itakusaidia kufanya mambo mengi kwa urahisi na bila kupoteza muda hovyo. Acha
kulala na kuamka kiholela. Unaweza ukaona ni jambo kama dogo, lakini lina
msaada mkubwa sana katika safari yako ya mafanikio na ni muhimu kufannya hivi kila siku.
PANGA MALENGO YAKO MAPEMA |
2. Amka
asubuhi na mapema.
Siku zote jifunze kuamka asubuhi na mapema.
Unapoamka asubuhi na mapema inakusaidia sana kukamilisha zile kazi ngumu ambazo
unatakiwa uzifanye kwa siku husika. Kuamka asubuhi na mapema ni muhimu hiyo
yote ni kwa sababu akili yako inakuwa bado na nguvu kubwa ya kutenda mambo
mengi na kwa ufanisi mkubwa bila kuchoka.
Unaweza ukaamka asubuhi na mapema ukajisomea. Kama
wewe ni mwandishi unaweza ukaamka asubuhi na mapema ukaandika au ukapitia
malengo yako. Kwa kuamka asubuhi na mapema itakusaidia sana kama mjasiriamali
kukufanikisha kwa sababu mipango yako mingi unaweza ukaifanya asubuhi na mapema
hata kabla jua halijazama.
3. Anza
siku yako kwa kuwa chanya na maliza ukiwa chanya.
Amka asubuhi kwa kujifunza kuwa chanya. Hiyo
itakuwa rahisi kwako ikiwa utajisomea kitabu au utasikiliza kitabu cha sauti kupitia
simu au redio. Unapoianza siku yako ukiwa chanya utaifanya siku yako iwe nzuri
zaidi. Mambo yako mengi utayafanya kwa hamasa kubwa. Kitu pekee
kitakachokufanya uwe hivyo ni kwa sababu uliianza siku yako ukiwa chanya.
Lakini si hivyo tu, kama ulivyoanza siku yako
chanya ndivyo unatakiwa uimalize kwa namna hiyo. Imalize siku yako kwa kujikumbushia
tena malengo yako. Imalize siku yako kwa kujisomea kitabu cha mafanikio hata
kwa dakika kumi na tano. Hivi ndivyo unavyoweza ukawa chanya kwa siku yote na
itakusaidaia kuwa mjasiriamali wa mafanikio.
4. Tunza
na thamini muda wako.
Muda ni kitu cha thamani sana kwa mjasiriamali
yoyote. Muda ndio unaotufanya tufanikiwe ama tusifanikiwe. Matumizi ya muda
sahihi yanahitajika sana katika kila eneo la maisha yetu kuliko wengi
wanavyofikiri. Hivyo kwa maana hiyo ni muhimu sana kuthamini muda tulionao na
kufanya yale yaliyo ya muhimu kwetu.
Kama ulikuwa ni mtu wa kupoteza muda, achana na
hiyo tabia mara moja. Sasa unatakiwa kuishi maisha ya kimafanikio kwa kuthamni
na kutunza muda wako sana. Usikubali mtu yoyote akakupotezea muda wako.
Wajasirimali wengi wenye mafanikio wanatunza sana muda wao. Kama lengo ni kuwa
mjasirimali wa mafanikio ni vyema kujifunza kutunza na kuthamini muda sana kila siku.
5. Jiwekee
lengo la kusonga mbele kila siku.
Mjasiriamali mwenye mafanikio lengo lake kubwa ni
kusonga mbele. Haijalishi unakutana na nini? Lakini ukiwa kama mjasirimali
unayetaka kufanikiwa thamani kuendelea mbele. Acha kuganda na kung’ang’ania
sehemu moja ulipo hiyo haitakusaidia
sana. Kikubwa uwe mtu wa kusogea hatua kwa hatua kila siku.
Najua kuna wakati tunakutana na changomoto nyingi
sana. Pamoja na changamoo hizo zichukulie kama ngazi ya kukupandisha kwenye
mafanikio yako. Lakini ikiwa utakubali kukaa chini nakutulia basi elewa wewe
mwenyewe utakuwa umeamua kuyapoteza maisha yako bila kujua. Tambua kusonga
mbele liwe ndilo lengo lako la kwanza kama mjasiriamali unayetaka mafanikio
makubwa.
6. Jifunze
kila siku.
Yafanye maisha yako kila siku yawe shule. Kila
unachopitia iwe changamoto au kile kizuri unachokiona kutoka kwa watu wengine
kifanye kiwe sehemu ya darasa kwako la kukutoa kutoka sehemu moja kwenda sehemu
nyingine. Andika yale mambo ya msingi ambayo unaweza ukawa umejifunza na kisha
yafanyie kazi kila siku. Hapo itakusaidia sana kuwa mjasiriamali wa mafanikio.
Naamini kwa kujifunza mambo hayo, yatakuwa msaada
kwako wewe kama mjasiriamali kuweza kufanikiwa kwa kile unachokifanya katika
maisha yako. Kumbuka kuchukua hatua na kufanyia kazi kile ulichojifunza.
Nikutakia siku njema na endelea kutembelea DIRA YA
MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza mafanikio kila wakati. Kumbuka, endelea
kuwashirikisha wengine waendelee kujifunza kupitia mtandao huu.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani
Ngwangwalu,
Simu;0713
04 80 35,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.