Mar 16, 2016
Jinsi Ya Kutoa Huduma Bora Kwa Mteja Wako.
Siku zote biashara ni mteja, bila mteja hakuna
biashara yoyote ambayo inaweza ikawepo hapo. Biashara nyingi zinafanywa na
kufanikiwa kwa sababu kuna wateja wanayoifanya biashara hiyo iendelee kuwepo.
Kwa maana hiyo kitu cha msingi kabisa
katika biashara yoyote inayofanyika ni mteja.
Lakini pamoja na umuhimu huo wa mteja huyo
katika biashara, kwa bahati mbaya sana biashara nyingi zimekuwa zikiendeshwa
kiholela au kimazoea sana na kusahau
suala zima la utoaji wa huduma bora itakayomfanya mteja aweze kurudi kwenye biashara yako kwa mara
nyingine tena. Kwa sababu hii wengi wamekuwa wakipoteza wateja bila kujijua.
Kwa kusoma makala haya ya leo utajifunza mbinu
au njia muhimu utakazoweza kuzitumia ili kuweza kumhudumia mteja wako kwa ubora hali ya juu. Sasa je, unawezaje kutoa
huduma bora itakayomvutia mteja wako wakati wote na kuwa na hamasa ya kuipenda
biashara yako? Twende pamoja kujifunza kupitia makala haya.
1. Kuwa na lugha nzuri kwa wateja.
Katika biashara yako ili uweze
kuwapata wateja wengi, jijengee mazoea ya kuwa na lugha nzuri kwa wateja wako.
Naelewa kuna wakati wateja wanakuwa wanakera sana. Lakini hilo lisikufanye
ukamfokea mteji wako na kuanza kumrushia lugha isiyofaa. Mjali mteja wako na
kumuonyesha lugha nzuri hata kama amekukera. Hiyo itakuwa ni njia bora ya kutoa
huduma bora kwa wateja wako na itakupa sifa wewe na kupelekea kujenga biashara
bora.
WAPE HUDUMA BORA WATEJA WAKO. |
2. Ukaribisho mzuri kwa wateja.
Jenga mazoea ya kumkaribisha
mteja wako vizuri. Mwonyeshe sura ya tabasamu ambayo hata bila kusema chochote
itaashiria kwamba unamkaribisha kwa kumjali. Kuna watu ambao wanafanya biashara
lakini utamaduni huu wa kumkaribisha mteja vizuri hawana. Kwa mfano kama una
duka na mteja wako amefika na amekukuta unafanya kazi fulani. Achilia hiyo kazi
na umsikilize mteja wako kwanza.
3. Kuwa na bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Siri kubwa ya kutoa huduma bora
kwa mteja wako ni pamoja na kumpa mteja bidhaa zenye viwango vya juu. Kama
utakuwa unatoa huduma bora inayoendana na thamani ya pesa ya mteja itasaidia
sana kukuza wateja wako. Lakini hiyo haitoshi unapotoa huduma bora ya bidhaa
inasaidia ili mteja akinunua bidhaa yoyote kwako anakuwa ana hamasa kubwa ya
kurudi kwako tena kununua na hata kuwaambia wengine waje wanunue.
4. Jipe muda wa kuwasikiliza wateja wako.
Katika biashara kuna wakati huwa
kuna malalamiko kutoka kwa wateja. Inawezekana kabisa mteja wako akawa
hajaridhika na huduma fulani au ubora wa bidhaa unazotoa. Sasa inapotokea hali
kama hii na akakwambia jifunze kuwasikiliza wateja wa namna hii na kufanyia
mabadiliko mara moja. Ikiwa utamsikiliza na kufanyia kazi kile anachokitaka
basi kesho elewa mteja huyo atakuwa wa kwako.
5. Mfanye mteja wako ajione wa thamani sana.
Unapokuwa kwenye biashara ni
vyema ukajenga mazingira ya kumfanya mteja akijiona wa thamani. Mteja wako
akishatambua hilo kwamba yeye ni wa thamani kwako, basi elewa kesho atakuwa ni
wako tu hata iweje. Unaweza ukafanikiwa kwa hili ikiwa utajifunza kusimsikiliza
mteja wako kwa makini, kujibu maswali yake vyema, ikiwezekana kwa mifano. Acha
kupuuza chochote anachokwambia mteja wako, hata kama kinaonekana ni cha
kijinga.
6. Kuomba msamaha haraka sana kama bidhaa ina mapungufu.
Inapotokea kwenye biashara yako
kukawa kuna mapungufu fulani, omba msamaha haraka sana. Tuchulie wewe unafanya
biashara ya kuuza chakula halafu ikatokea chakula hicho hakijawa kizuri sana.
Ili mteja wako aridhike na huduma yako, njia bora hapo kwako ni kuomba msamaha
mara moja. Kama utaomba msamaha na kuahidi kesho utampatia huduma bora zaidi
basi atakuelewa na hata kuwa na hasira na wewe tena na atakuwa mteja wako kwa
siku nyingine. Kwa kumueleza, hiyo itampelekea kujenga imani kubwa na wewe.
7. Kuokoa muda wa mteja.
Pia huduma bora ni lazima
iendane na kuokoa muda wa mteja. Acha kumfanya mteja wako kama mtoto kwa
kumgandisha na kumtozea muda wake bila sababu. Mpe huduma mteja wako
inayostahili kwa muda mwafaka. Kama unaona kuna eneo utachelewa ni bora
ukamwambia ajue kuna kusubiri. Tatizo walilonalo wafanyabiashara wengi ni
kuwapotezea wateja wao muda wakati mwingine bila sababu. Ili kuepuka
kutokupoteza wateja, okoa muda wa mteja wako kwa kadri unavyoweza.
8 . Toa shukrani kwa mteja wako.
Mteja akishanunua kitu
kwako au ukishampatia huduma ambayo wewe unatoa, jifunze kuwa na shukrani
kwake. Mwambie tunashukuru kwa kuwa mteja wetu na karibu sana siku nyingine. Pia
kwa kuongezea katika hili unaweza ukampa hata na mkono wa kumuaga. Unaweza
ukaona ni kitu kidogo katika hili, lakini kitamfanya ajisikie vizuri na kesho
atakuwa tayari tena kuweza kuja kwako.
Katika biashara wakati mwingine
hauhitaji mtaji mkubwa sana ili kuweza kufanikiwa. Ila kwa kujijengea tabia ya
kuwa na huduma bora kwa mteja ni njia nzuri sana ya kukuhakikishia mafanikio
makubwa kibiashara. Chukua hatua na kuamua kutoa huduma bora kwa mteja wako
kila siku.
Dira ya mafanikio tunakutakia
mafanikio mema katika utoaji bora wa huduma kwenye biashara yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA
YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713048035,
Email;
dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.