Jan 6, 2017
Wengi Wanashindwa Kufanikiwa Kwa Sababu Ya Mambo Haya Mawili.
Kuna wakati unaweza ukawa unashangaa kwa nini ndoto
zako hazitimii? Utakuta umejiwekea malengo
yako vizuri, lakini unashangaa ni malengo machache sana yanayotimia au wakati
mwingine hakuna kabisa.
Sina shaka yoyote umeshawahi kukutana na hali kama hii wakati
fulani katika maisha yako. Kiuhalisia, yapo mambo mawili ambayo kitaalamu hupelekea
ndoto zako kushindwa kutimia ikiwa hutayajua vizuri.
Jambo la kwanza, ni kutokujua kile unachokitaka
vizuri. Hili ni jambo ambalo hupelekea wengi kushindwa kufanikisha ndoto zao
kabisa. Kama hujui kile unachokitaka vizuri, suala la kufanikisha ndoto zako litakuwa
gumu kidogo.
Katika akili yako ili uweze kufanikisha ndoto yako
au jambo unalolitaka kwa urahisi, ni lazima kile kitu unachokitaka uweze
kukijua vizuri. Tambua njia utakazotumia hadi kukipata kitu hicho pia tambua
kitu hicho changamoto zake ni zipi.
Acha kufanya kosa la kuuchanganya ubongo wako kwa
kuupa vitu vingi. Kuwa maalumu kwa kujua vizuri kile unachokitaka. Usipojua kile
unachokitaka kwa uhakika na kukifanyia kazi, ni wazi hutaweza kufanikiwa na
hilo halina ubishi.
Hamasa na kujua kile unachokitaka vizuri, ni nguzo sahihi ya mafanikio. |
Wengi ni watu wa kutaka kufikia lengo fulani katika
maisha yao, lakini kwa bahati mbaya hujikuta ni watu wa kukosa hamasa ya
kuwasukuma kuweza kukamilisha malengo yao.
Ili kufanikiwa, fanya kila ufanyalo kuhakikisha una
hamasa ya kufanya hicho unachotaka kukifanya katika maisha yako. Inapotokea hamasa
hiyo umeikosa acha kusimama eti kwa sababu ya kukosa hamasa.
Maisha hayasimami eti kwa sababu wewe hujisikii
kufanya kitu fulani au umekosa hamasa. Endelea kusonga mbele, huku ukitafuta
hamasa ya kufanikiwa kwako kila siku. Ukifanya hivyo utafika mbali kimafanikio.
Katika hali ya kawaida, kama kila wakati unakosa
mambo haya mawili suala la kufanikiwa kwako linakuwa ni gumu sana. Hivyo, ni
lazima sana kwako kujua vizuri kile unachokitaka na kuwa na hamasa kubwa yaani ‘burning
desire’ ya kuhakikisha kitu hicho ni lazima unaweza kukipata.
Ukichunguza watu wengi ambao hawajafanikiwa
wanashindwa kufanikiwa kwa sababu hizi mbili tu na si vinginevyo. Kama unafikiri
natania anza kufatilia, huku lakini ukianza na wewe.
Kama unajiona hujafanikiwa vya kutosha jiulize binafsi
je, unakijua vizuri kile unachokitaka na huna tamaa ya kutaka hiki mara kile na mwisho wa siku kuwa na
malengo mengi yasiyotekelezwa?
Usiishie hapo tu, tena kama unaona hujafanikiwa vya
kutosha jiulize, je, una hamasa kubwa ya kuona ndoto zako zinatumia? Je,
unakosa usingizi na kuamua kujituma usiku na mchana hadi kufanikiwa?
Ukipata majibu ya maswali hayo yatakusaidia sana
kuweza kufanikiwa na kuwa mtu mwingine tofauti na hatimaye kuweza kufanikisha
zoezi zima la kutimiza ndoto zako. Jitoe kikamilifu kuona ndoto zako zinatimia
kwa kuyajua mambo hayo mawili.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI
NGWANGWALU,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.