Sep 30, 2015
Mambo 12 Yakujifunza Kutoka Kwa Watu Waliofanikiwa.
Ipo haja kubwa sana ya kujifunza kupitia watu waliofanikiwa ili
kuweza kufikia mafanikio mkubwa. Kupitia maisha yao kuna mambo mengi ya msingi
tunakuwa tunajifunza na kuachana na makosa ambayo wao waliyafanya bila kujua.
Na kiuhalisia yapo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa watu
waliofanikiwa ambayo yanaweza kuwa msingi mkubwa wa mafanikio yetu. Kuyajua
mambo hayo itakusaidia kujiamini na kuendelea mbele. Mambo hayo ya kujifunza
kutoka kwa watu waliofanikiwa ni kama haya yafuatayo:-
1. Watu waliofaniwa ni watu wa kutegemea mafanikio makubwa kutoka
ndani mwao na siyo kinyume cha hapo. Ni watu wa kuamini ule uwezo walionao ndani
mwao kuwa ndiyo utakao wafanikisha.
2. Watu waliofanikiwa ni watu wa kuishi kwa bajeti. Mara nyingi hujikuta
wakikata au kupunguza kile ambacho siyo cha muhimu katika bajeti yao na kutengeneza
bajeti upya itakayowafanikisha. Kwa kifupi, matumizi yao kwa sehemu kubwa
yanaongozwa na bajeti.
3. Watu waliofanikiwa ni watu wa vitendo. Mara nyingi siyo waongeaji
sana. Ni watu wa kuchukua hatua ambazo zinaleta matokeo halisi na chanya
yatakayojitokeza kwenye maisha yao.
4. Watu waliofanikiwa wako makini na suala zima la uwekezaji. Kila
wakati wanafungua macho yao kuangalia ni wapi ambapo wanaweza kufanya uwekezaji
ambao utawaletea matunda na mafanikio makubwa badala ya kukaa na kutumia pesa
hizo tu.
5. Watu wenye mafanikio wanatumia muda wao mwingi kujifunza. Kwa
kifupi hawa ni watu wa kujifunza kupitia vitabu mbalimbali wanavyovisoma hata pia
kuhudhuria semina au warsha za mafanikio.
6. Watu wenye mafanikio ni watu kuendelea mbele hata pale
inapotokea wameshindwa katika jambo fulani. Huwa hawasimami kusikilizia sana
maumivu hayo. Hujifunza pale walipokosea na kisha safari ya mafanikio kuendelea kama kawaida.
7. Watu wenye mafanikio mara nyingi wanazungukwa na watu wenye
mitazamo chanya kama ya kwao. Watu hawa wanaowazunguka huwasaidia zaidi kimtazamo
na kuwafanya wawe na mafanikio muda wote.
8. Watu wenye mafanikio hawana kauli za kushindwa kwenye maisha
yao. Muda mwingi wamebeba kauli za mafanikio. Hutaweza kuja kuwasikia wakisema
‘siwezi hili, au lile’ badala yake
hukaa na kusema ‘nitaweza vipi kufanya
jambo hili nakufanikiwa’ hizo ndizo kauli za watu wenye mafanikio siku zote.
9. Watu wenye mafanikio ni watu wa kujitoa mhanga. Siku zote wako
tayari kufanya na kutoa chochote ili mradi tu mipango na malengo yao yaweze
kutumia na kufika kule wanakotaka kufika.
10. Watu wenye mafanikio ni watu wa kufanya mambo yako kwa kuweka
nguvu nyingi za uzingativu katika eneo moja. Kama kuna jambo wameamua kulifanya
wanaling’ang’ania hilohilo mpaka liwape matokeo kamili.
11. Watu wenye mafanikio ni watu wa kutunza muda siku zote. Hawako
tayari kupoteza muda wao kwa kufatilia mambo ambayo wanaona hayana msaada kwao.
12. Watu wenye mafanikio ni watu wenye uvumilivu wa kutosha. Kuna
wakati huwa wanashindwa katika mambo yao, lakini huvumilia mpaka kuweza
kufanikiwa.
Yapo mambo mengi sana ambayo unaweza kujifunza kupitia watu waliofanikiwa,
lakini unaweza ukayafanyia kazi mambo hayo kwanza ili yawe msingi bora katika safari
yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
Nakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 29, 2015
Sababu 8 Kwanini Unatakiwa Kumiliki Biashara Yako Sasa?
Inawezekana
mara kwa mara umekuwa ukiwaza namna unavyoweza kuanzisha biashara yako na
kujenga uhuru wa kifedha. Mawazo hayo umekuwa ukiyapata hasa kutokana na kila
ukiangalia unaona kama vile kipato chako hakitoshi kutokana na kazi unayoifanya
sasa. Kama hayo ndiyo mawazo yako upo kwenye njia sahihi.
Nikiwa
na maana kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuanzisha biashara yako mwenyewe kuliko
hata unavyofikiri. Kwani mbali na faida ya kifedha yapo mambo mengine mengi utakayojifunza
kutokana na kumiliki biashara yako mwenyewe. Je, unajua ni kwa sababu gani
unatakiwa kumiliki biashara yako mwenyewe na kuacha kutegemea kuajiriwa kwa
asilimia zote ?
Hizi Ndizo Sababu 8 Kwanini Unatakiwa Kumiliki Biashara
Yako Sasa?
1. …Ni njia bora ya kukufikisha
kwenye uhuru wa fedha.
Inawezekana
ukawa umechoka na kazi unayoifanya na unaoina haifai kwa namna moja au
nyingine. Lakini njia bora ya kuweza kuondokana na utumwa huo ambao unakukabili
ni kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo utaisimamia mpaka ikuletee mafanikio
unayoyahitaji.
2. …Ni Njia bora ya kujifunza.
Hakuna
njia bora ya kujifunza kuhusu kutunza na kumiliki pesa kama biashara. Hili
ndilo eneo ambalo utajifunza mengi
kuhusu masoko, namna ya kukuza mtaji na jinsi ambavyo unaweza ukaufikia uhuru
wa kipesa. Kwa hiyo kama una biashara yako inakusaidia kujifunza yote hayo
hatua kwa hatua.
3. …Ni njia bora yakujifunza
kujitegemea.
Unapokuwa
kwenye ajira kwa kawaida unakuwa unamtegemea mtu fulani ambaye ndiye akuamulie
juu ya maisha yako. Lakini kwenye biashara mambo hayako hivyo. Wewe ndiye
unakuwa mwamuzi mkubwa wa maisha yako. Na unakuwa unakikisha unafanya kila
linalowezeka mpaka biashara yako ifanikiwe.
4. …Inakuwa inakupa hamasa ya
mafanikio zaidi.
Huo
ndiyo ukweli unaotakiwa ujue kuwa, unapokuwa na biashara inakuwa inakupa hamasa
ya kuweza kufanikiwa na kusonga mbele zaidi. Tofauti na ajira ni rahisi kusema
kuwa ‘aaah kazi yenyewe siyo yangu
kwanza’ kwa hiyo unakuwa unafanya kwa jinsi unavyojisikia. Lakini kwenye biashara
mambo hayako hivyo ni lazima kujituma ili kufanikiwa.
5. …Inakuongezea ujasiri.
Unapokuwa
mfanyabishara ni hatua nzuri sana kwako ya kukupelekea kuwa na ujasiri wa hali
ya juu. Hiyo yote ni kwa sababu unapofanikiwa katika biashara moja unakuwa ndani
yako una hamasa kubwa ya kutaka kufanya biashara nyingine tena kwa mafanikio. Kwa hali hiyo
unakuwa una maamuzi mengi ya kijasiri ambayo ni rahisi kukusaidia
kukusonga mbele.
6. …Ni njia rahisi ya kufuata mipango
na malengo yako.
Mara
unapoanzisha biashara yako unakuwa upo kwenye njia sahihi ya kufuata ndoto za
maisha yako. Hii yote ni kwa sababu unakuwa unakifanya kile kitu ambacho
unakipenda kwa dhati toka moyoni mwako. Wakati unapokuwa kwenye ajira unakuwa
unafanya tu ilimradi mkono uende kinywani. Hiyo ndiyo faida kubwa mojawapo
ya kuwa kwenye biashara.
7. …Inakufanya unakuwa ni mtu wa
vitendo.
Watu
wengi mara nyingi ni waongeaji bila ya kuwa watu wa vitendo. Lakini kitendo cha
kuwa na biashara yako mwenyewe inakupelekea unakuwa ni mtu wa vitendo. Utaelewa
vizuri umuhimu wa kuchukua hatua katika biashara tofauti na ambavyo ungekuwa
hufanyi biashara ingekupelekea wewe kuwa na maneno mengi bila utekelezaji.
8. …Ni njia bora ya kufanya mambo
mengine zaidi.
Unapokuwa
kwenye biashara inakuwa ni njia bora ya kufanya mambo mengine bora zaidi. Kama
ulikuwa una lengo moja na umelikamilisha inakuwa ni rahisi kuweza kulifatilia
lengo lingine mpaka tena kulifanikisha. Na hiyo nguvu yote ya kufanya mambo
mengine inakuja kutokana na ujasiri ambao tayari unakuwa umeshajijengea kwenye
biashara yako.
Kama
ulikuwa ni mtu wa kusubiri subiri, achana na hiyo habari. Wakati wa kumiliki
biashara yako ni sasa, ili iweze kukupa mafanikio mkubwa na endelevu.
Nakutakia
kila la kheri maendeleo ya biashara yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO
kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
dirayamafanikio@gmail.com
Sep 28, 2015
Kama Unataka Kuwa Na Furaha Ya Kweli, Zingatia Mambo Haya.
Kila
mmoja kati yetu anatamani sana kuwa na furaha ya kweli maishani mwake. Nina
uhakika kama furaha ingekuwa inauzwa, mfanyabishara wake ndiye mtu ambaye
angekuwa tajiri zaidi duniani. Asingekuwa tajiri tu, bali angekuwa tajiri wa
kufuru.
Kwa
nini? kwa sababu, kila binadamu anatamani kuwa na furaha ya kweli kwenye maisha
yake. Kila mmoja wetu, awe anajua au awe hajui, anachotafuta hapa duniani ni
furaha tu. Kuhangaika kwetu kote, ni kutafuta furaha ya kweli.
Lakini
kwa bahati mbaya wengi wetu hatujui namna ya kuipata furaha ya kweli. Wengi
tumekuwa tukifanya mambo ambayo tunafikiri yanaweza kutupa furaha, lakini baada
ya muda tunagundua mambo hayo hayatupi furaha ya kweli tunayoihitaji kama tulivyokuwa
tukifikiri.
Kwa
mujibu wa wataalamu wa masuala ya utambuzi wanadai kuwa kutafuta furaha ya kweli
maishani, kunahitaji juhudi na kila mmoja anaweza kuipata furaha hiyo kama
kweli ataamua. Wanasema, kimsingi furaha ni ujuzi ambao inabidi mtu ajifunze kuupata.
Na
ili kuliweka jambo hili wazi, na kueleweka kwa kila mtu hadi kumudu kupata
furaha ya kweli, wataalamu hawa wautambuzi wameweka mambo au vigezo vya
kuzingatia ili kuweza kujijengea furaha ya kweli. Kwa kuyajua mambo hayo
yanauwezesha ubongo wako kufanya mabadiliko ya kukupa furaha ya kweli.
Moja
ya sababu au nguzo ya kukupa furaha ya kweli ni kufanya tahajudi (Meditation) au
sala za uzingativu kwa muda mrefu. Watu wengi
wanaofanya aina fulani za tahajudi au meditation huweza kumudu kuongeza
furaha katika maisha yao kwa kiwango fulani.
Hiyo
huweza kutokea hivyo kwa sababu, kwa kadri mtu anavyofanya sala au tahajudi
hupelekea kwa nguvu nyingi hasi kukandamizwa katika ubongo wake na matokeo yake
nguvu chanya kuongezeka na kupelekea kumudu kujenga furaha ya kweli anayoitaka
kwake. Hivyo tahajudi ni jambo la muhimu sana katika kujenga furaha halisi.
Pili,
furaha ya kweli inakuja kwa kutambua kuwa inatoka ndani mwako na siyo
vinginevyo. Hii ina maana kwamba, haiwezekani kwa mtu kupata furaha ya kweli
kama ndani yake mtu huyo hajikubali na haioni furaha hiyo kwake.
Wengi
wanategemea mambo ya nje kama fedha, elimu au umaarufu kupata furaha. Lakini kitu cha kushangaza
hawaipati furaha hiyo, hata kama wakiipata inakuwa ni ya muda mfupi sana na
kutoweka.
Wakati
mwingine hata furaha ya muda mfupi hawawezi kuipata , kwani kwa mfano, mara
wanapopata fedha nyingi, sekunde hiyohiyo mawazo yenye kukera na hofu kuhusu
fedha hizo huanza kujitokeza kwao na mwisho hujikuta furaha yao ikiyeyuka.
Kwa
kulitambua hilo usiwe mtumwa kwa mambo hayo ya nje ambayo yanaweza yakatoweka
muda wowote na kukupotezea furaha yako. Kitu cha msingi tambua wewe ndiye chanzo
cha huzuni au furaha katika maisha yako.
Tatu,
jifunze kuyachukulia mambo kama yanavyokuja ili kujijengea furaha ya kweli.
Acha kushindana sana baadhi ya hali
zinazokuja kwako, kwani utashindwa kuzimudu hali hizo na mwisho wa siku
utajikuta unakosa ile furaha halisi. Usiwe mtu wa kubadilika asubuhi na jioni
kwa kutegemea kitu gani kinaendelea nje.
Mtu
mwenye furaha ya kweli anakubaliana na maisha kama yalivyo bila kujali kama
kuna mvua au jua, kama mambo yameenda vizuri au vibaya, kama kuna fedha au
hakuna, kama kuna kusifiwa au hakuna. Tunasema ni watu ambao ndani zao
hazitegemei sana ni kati gani kinaendelea nje.
Nne,
unaweza upata furaha ya kweli kama utaamua kuwapenda wengine pia. Kuwapenda wengine ina maana kuwapokea na
kuwakubali watu wengine kama walivyo na mapungufu yao. Hili huwa ni jambo gumu
kwa wengi kuwapenda watu wengine.
Kama
nilivyosema awali, kila binadamu anataka kupata furaha maishani. Katika
kutafuta furaha binadamu hujikuta akitafuta kazi nzuri, gari nzuri ya
kutembelea, kujenga nyumba nzuri, kuoa au kuolewa na mke au mume mzuri na mengine
mengi, yote hayo hufanywa kwa ajili ya kutafuta furaha.
Kwa
sababu, furaha haiko kwenye mambo hayo tu, watu hujikuta wanapata vitu hivyo,
lakini bado hawana furaha. Kwa sasa itakuwa ni rahisi sana kwa binadamu kupata
furaha ya kweli kama ataamua na kuzingatia mambo hayo tuliyojadili, badala tu ya
kuhangaika kutafuta mara hiki mara kile.
Nakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 25, 2015
Jinsi Ambavyo Unavyoweza Kuitumia Dakika Moja Kubadili Maisha Yako.
Inaweza
ikawa ni kitu cha kushangaza kidogo kwako, lakini huu ndiyo ukweli, unao uwezo
wa kutumia dakika moja tu kubadili maisha yako. Kama wewe ni mtu wa visingizio
kila wakati mara ‘oooh mimi sina muda’
utachelewa na utaacha mipango yako mingi ipotee bure. Dakika moja ni ya thamani kubwa kwako na
inakutosha kufanya uamuzi wa msingi utakao kuletea mabadiliko kwenye maisha
yako.
Ni
rahisi kusema haiwezekani, lakini inawezekana. Unawezaje kufanya mabadiliko
hayo kwa kutumia dakika moja ili kubadili maisha yako na wengine pia? Kumbuka
tu kwamba:-
1.
Inakuchukua dakika moja tu, kuchukua uamuzi wa kutafakari kile unachokwenda
kukifanya katika siku yako ya leo.
2.
Inachukua dakika moja tu, kuchukua uamuzi wa kufanikiwa au kushindwa katika
maisha yako.
3.
Inachukua dakika moja tu, kuamua kujenga hofu ama kujimini katika maisha yako
katika kila jambo unalotaka kulifanya katika maisha yako.
4.
Inachukua dakika moja tu, kumwambia mtu aliyekata tamaa kuwa ni lazima
atafanikiwa.
5.
Inachukua dakika moja tu, kusema mwenyewe kuwa basi nimeshindwa kwa kile
ninachokifanya au nitaendelea kung’ang’ania mpaka nipate matokeo
ninayoyahitaji.
6.
Inachukua dakika moja tu, kumwonyesha upendo mtu yule ambaye anajihisi mpweke.
7.
Inachukua dakika moja tu, kuamua kuwa wewe ndiye kiongozi pekee wa maisha yako.
8.
Inachukua dakika moja tu, kuamua kuishi
maisha ya kuwaumiza wengine au kuwa msaada kwao.
9.
Inachukua dakika moja tu, kuamua kuwa utabadilika na kuwa na tabia za mafanikio
au utaendelea na maisha yako uliyonayo sasa.
10.
Inachukua dakika moja tu, kujikubali kuwa wewe ni mshindi na hakuna kitu
kinachoshindikana kwako na kwa uamuzi huo ni lazima ufanikiwe.
Kitu
cha kujiuliza hapa, je unaitumia vipi dakika uliyonayo ili uweze kukufanikisha
kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji? Kumbuka dakika moja tu inaweza
kukufanikisha au kukufanya ukashindwa kwenye maisha yako kutokana na kile unachokiamua
ndani ya dakika hiyo.
Watu
wengi wameharibu maisha yao kutokana na maamuzi madogo madogo wanayoyafanya kwa
dakika hiyo moja. Kwa mfano kama umefanya maamuzi mabaya kwa dakika sitini,
tafsiri yake ni kwamba umeharibu maisha yako mara sitini. Kuwa makini na dakika
yako moja na itumie vizuri ikufanikishe.
Nakutakia
kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 24, 2015
Faida 7 Za kufanya Mazoezi Ya mwili.
Kuwa
na afya bora ni msingi wa mafanikio yote. Hata uwe na mipango na malengo mazuri
vipi lakini kama afya yako ni mbovu huwezi kuyafikia mafanikio hayo
unayoyataka. Unapokuwa na afya bora inakuwa inakupa nguvu ya kuishi maisha bora
wakati wote na kufanya mambo mengi bila kuteteleka.
Kama
ambavyo waswahili wanasema ‘mwili haujengwi kwa matofali’ ndivyo hivyo afya hii
tunayaoizungumzia haiji kwa bahati mbaya tu. Mara nyingi vyakula tunavyokula na
aina ya maisha tunayoyaishi karibu kila siku ndiyo inayotuamulia afya zetu
ziweje kwa sasa na baadae
Kama
unaishi maisha ya kulakula hovyo tu bila utaratibu kamwe usitegemee ikawa
rahisi kujenga afya bora ni lazima itakusumbua. Vilevile hata kama hujihusishi
na mazoezi nayo pia itakuwa ni tatizo kwa afya yako. Ili ufanikiwe ni muhimu
kutambua kitu cha kwanza kukilinda ni afya kuliko kitu chochote kile.
Kwa
hiyo utakuja kuona kuwa chakula bora chenye virutubisho vyote muhimu, ni kitu
cha lazima na msingi sana kwa afya zetu. Lakini mbali vyakula hivyo pia tunaona
hata mazoezi yanahusika pia katika kutupa afya zetu kwa kiasi kikubwa kuliko
wengi tunavyofikiri.
Wengi
huwa tunaona mazoezi ya mwili yanafanyika lakini huwa hatujui yanafanya kazi gani
hasa kwenye hii miili yetu. Mara nyingi zipo faida nyingi za kufanya mazoezi
ambazo siyo rahisi kuzitambua ikiwa hujafanya uchunguzi hata kidogo. Faida hizo
ni kama hizi zifuatazo:-
1. Mazoezi ya mwili husaidia kulirekebisha
shinikizo la damu.
2.
Mazoezi ya mwili huiruhusu damu nyingi zaidi kuzifikia sehemu zote za mwili na
kuifanya mikono na miguu ipate joto.
3.
Mazoezi ya mwili yanaondoa mambo yote mawili. Yaani mkazo wa mwili na mfadhaiko
wa moyo, na kukusiadia wewe kujisikia vizuri zaidi katika maisha yako. Mazoezi
ya mwili kwa kawaida ni tiba bora kabisa ya wasiwasi na msongo (stress).
4.
Mazoezi ya mwili hutupatia nguvu ya umeme kwa ajili ya ubongo wetu pamoja na
seli za neva. Yanaongeza afya kwa kuuamsha mfumo wa kinga mwilini (immune system).
Mwili unapowekwa katika hali ya afya kwa kufanya mazoezi yanayofaa. Ubongo
unakuwa na uwezo wa kufikiri kwa ubunifu na ufanisi zaidi.
5. Yanaweza kukusaidia kuiweka vizuri rangi ya uso wako na kukuweka katika hali nzuri kabisa kimwili.
6. Mazoezi ya mwili hukufanya uwe na nguvu nyingi zaidi, hivyo kuchelewesha kupatwa na uchovu kimwili na kimawazo
7. Yanausaidia ubongo wako kutengeneza dawa inayokupa wewe hali ya kujisikia vizuri na kukuongezea uwezo wa kustahimili maumivu.
5. Yanaweza kukusaidia kuiweka vizuri rangi ya uso wako na kukuweka katika hali nzuri kabisa kimwili.
6. Mazoezi ya mwili hukufanya uwe na nguvu nyingi zaidi, hivyo kuchelewesha kupatwa na uchovu kimwili na kimawazo
7. Yanausaidia ubongo wako kutengeneza dawa inayokupa wewe hali ya kujisikia vizuri na kukuongezea uwezo wa kustahimili maumivu.
Endapo
wewe ulikuwa hufanyi mazoezi, basi anza taratibu (polepole) na kuongeza nguvu
yake hatua kwa hatua upatapo uwezo wa kustahimili.
Nakutakia
kila la kheri katika maendeleo ya afya na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 23, 2015
Kama Unakimbia Kitu Hiki, Huwezi Kufanikiwa.
Kwa
hakika ‘Hakuna kisichowezekana chini ya
jua’ ikiwa nia hiyo ya kufanikiwa unayo kweli kutoka moyoni mwako. Kila
kitu unachokihitaji katika maisha yako kinapatikana ikiwa utaamua kufanya kwa
kazi kwa bidii. Haijalishi hali au rasilimali ulizonazo lakini kama wewe ni mtu
wa kufanya kazi kwa bidii zote huku ukiwa na mipango na malengo imara ni lazima ufanikiwe.
Watu
wote wenye mafanikio makubwa duniani
kote ni wachapakazi. Mafanikio yao yote ni matokeo ya kile walichokifanyia kazi
kwa muda mrefu bila kuchoka. Na pengine kazi hizo walizokuwa wakizifanya
ziliwachosha, kuwakatisha tamaa lakini kutokana na uvumilivu wao walivumilia na
kuendelea kujishughulisha mpaka malengo yao yakatimia.
Nakumbuka
katika maisha yake Daktari Ronald Rose kama ambavyo tuliwahi kuandika wakati fulani
katika mtandao huu, alifanya kazi kwa bidii sana ili kukamilisha ugunduzi wake
wa dawa ya malaria. Mbaya zaidi mazingira aliyokuwa akifanyia kazi hayakumpa
ushirikiano wowote lakini aliweka juhudi
mpaka dawa ya malaria ilipatikana bila kuchoka.
Hiyo
yote inatuonyesha uvumilivu na kufanya kazi kwa bidii ni vitu ambavyo
havikwepeki ili kufikia mafanikio makubwa. Ikiwa nia yako ni kutafuta mafanikio
ya kweli ni lazima ujue kazi inahitajika tena ya ubora wa juu na wala sio ‘hadithi’ za hapa na pale.
Achana na habari za sterehe zisizo na msingi kwako. Jitume ili kufikia uhuru wa kifedha,
vinginevyo utaendelea kuwa na maisha magumu mpaka mwisho wako.
Tatizo
kubwa la watanzania tulio wengi ni kukwepa majukumu ya kufanya kazi kwa bidii.
Kama unafikiri natania jaribu kuangalia hata
wale wote waliokaribu na wewe, utagundua
ni wengi wenye uvivu fulani fulani hivi hata kwenye kazi zao. Kazi zinakuwa
zinafanyika ila kwa kujivuta sana hali ambayo hupelekea majukumu mengi kukwama.
Ili
uweze kufanikiwa na kufikia viwango vya juu vya mafanikio kitu kikubwa ambacho
hutakiwi kukwepa ni kufanya kazi kwa bidii. Kama kwenye maisha yako hufanyi kazi kwa
bidii, sahau kuhusu mafanikio. Jaribu kuchunguza wale wote wanaofanikiwa sana
katika jamii yako ni watu wa aina gani? Utakuja kugundua ni wale wote wanaojituma
kila siku bila kuchoka katika kazi zao.
Kama
kanuni au maisha yako hivi kwa nini unataka kujidanganya na kuamua kutafuta
urahisi unaojua wewe? Kumbuka, kama unakimbia kitu hiki kwa namna moja au
nyingine huwezi kufanikiwa. Kila kitu ili uweze kukipata kina gharama yake. Na gharama
mojawapo ya mafanikio hadi uweze kuyafikia ni kujitoa na kufanya kazi kwa bidii.
Najua
kila mmoja wetu ana nia ya kufanikiwa katika mambo yake iwe katika biashara au
maeneo mengine. Lakini mafanikio hayo hayawezi kuja kama ndoto tu. Yatapatikana
kwa kufanya kitu kimoja tu ambacho ni kufanya kazi kwa bidii. Hapo ndipo ilipo
siri ya kufikia mafanikio makubwa na hakuna muujiza katika hilo.
Kama
wahenga walivyosema ‘kazi ni msingi wa
maendeleo’ hakuna ubishi katika hilo. Penda kile unachokifanya, weka juhudi
na nguvu zako zote bila kuchoka na mafanikio yatakuja upande wako. Haijalishi mazingira
uliyopo ni magumu kiasi gani lakini kitu cha muhimu kwako ni kujituma tu mpaka
uone hatma ya mafanikio yako.
Kwa
makala nyingine nzuri hakikisha unaendelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO
kujifunza zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 22, 2015
Jinsi Unavyoweza Kuwavuta Watu Unaokutana Nao.
Kwa
nguvu zake Mungu naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza kupitia DIRA YAMAFANIKIO ili kuboresha maisha yako. Leo napenda nianze makala hii kwa
kukuuliza swali hili, ni kwa nini baadhi ya watu, wakikutana na mtu kwa mara ya
kwanza tu, mtu huyo waliyekutana naye ‘anaboreka’ haraka? Na ni kwa nini
wengine, wanapokelewa kirahisi na watu wapya wanaokutana nao maishani?
Najua,
unajua kuna sababu nyingi. Lakini ningependa nikutajie moja tu, ili iweze kukusaidia
kukabiliana na ‘kuwaboa’ watu wengine. Na tumia neno ‘kuboa’ kwa sababu ni neno
ambalo limezoeleka kimatumizi kwa sasa, likiwa na maana ya kumfanya mtu asiwe
na haja ya kukusikiliza au kuwepo kwako hukera, wewe ukiwa ndiyo chanzo.
Kama
umekutana na mtu kwa mara ya kwanza, usizungumze sana kuhusu wewe,
usijizungumzie kwa kujisifu na kujipandisha sana. Ingawa haina maana kwamba
usijishushe. Usitake kuonesha kwamba wewe ndiye wewe.
Watu
wasiojitosha, huwa wanakawaida ya kujisifu sana, wanataka kuwavuta
wanaozungumza nao wawaone wa maana sana, huzungumza kwa muda mwingi wao tu,
hujisifu na kujikweza. Ni mara chache sana huwaacha wengine waseme.
Hebe
fikiria, hujamjua mtu, unasema kama kinanda kuhusu mambo yako, unadhani
atakuchukulia vipi? Ni lazima utamkera tu, badala ya kumfurahisha, kama
unavyofikiria. Ni lazima utaanza kuwa na wasiwasi nawe.
Jambo
la awali unalotakiwa kulifanya unapokutana na mtu mgeni, ambaye hujawahi
kukutana naye, iwe kibiashara, kimapenzi au kwa nasibu tu, inabidi uwe
msikilizaji tu kuliko kuwa msemaji.
Kuna
watu ambao wanatatizo la kutaka kusikilizwa wao tu, amablo chimbuko lake ni
kushindwa kwao kupata watu waliowajali walipokuwa wadogo.
Kama
nawe ni mmojawapo, inabidi uwe mwepesi kujikumbusha kwamba, una tatizo la
kutaka kusikilizwa wewe tu. Kujikumbusha au kukumbuka, kutakusaidia kuamua
kumsikiliza mwingine badala ya wewe kusema.
Siku
zote wanaopenda kusikiliza badala ya kusema, hao ndiyo mara nyingi huwa
wanawavutia watu, siyo wale wanaopenda kusema sana. Wengi hawalijui sana jambo
hili.
Ni
vizuri unapokutana na mtu mgeni, ukasema kidogo uhusu wewe, yaani yale mambo ya
msingi tu yanayokuhusu. Sema tu yale ambayo ni ya lazima au muhimu. Usiwe
kasuku kwanza.
Halafu,
soma kama huyo mtu ambaye humjui, ndiyo kwanza mnakutana, anavutwa na
mazungumzo gani? Unaweza ukaanza kubwata siasa wakati hataki kusikia kabisa
mambo yanayohusiana na siasa zako hizo. Unaweza ukaanza kubwata kuhusu vifo,
wakati pengine wiki iliyopita tu kapoteza mkewe au mumewe ama mtu wake wa
karibu kabisa.
Ukijua
mtu au watu wa fulani ambao ndiyo kwanza unakutana nao wanafurahia kuungumzia
mambo gani, hutawakera. Kwako itakuwa rahisi pia kuwasikiliza, kwani huenda
watakuwa na mengi, kwani wanazungumza yale wanayoyapenda na pengine wanajua
zaidi.
Unapokutana
na mtu mgeni popote na mazingira yakakulazimisha muwasiliane, siyo vibaya
ukaanza kwa kujitambuisha kwa kujitaja jina.
Hii
humjengea mtu huyo mwingine kukuamini na kuhisi ukaribu na urafiki. Onesha kwamba, mtu huyo mgeni anapozungumza
unafurahia mazungumzo yake. Unaweza kutabasamu, kumtazama bila kukodolea macho
na kutikisa kichwa mara kwa mara.
Hata
kama ikitokea mtu huyo anaongea upuuzi, ni vema kujenga uhusiano wa karibu na
mtu huyo. Wacha mgeni aseme zaidi ili umjue zaidi kuliko wewe anavyokujua.
Kumjua
kwako zaidi kutakusaidia kujua uzungumze vipi naye na kwa sababu zipi. Lakini,
usijaribu kuwa mtu ambaye siyo wewe. Kuwa wewe kwa kujikubali, bila
kujipandisha wala kujishusha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 21, 2015
Siri Nzito Katika Kufikia Mafanikio Makubwa.
Katika
maisha kila mtu hupenda kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa. Lakini pamoja
na umuhimu huo ni wapo ambao hujikuta wakifanya yale yasiyotakiwa kufanywa ili
kufikia mafanikio hayo. Mafanikio mazuri ni lazima yaanze na malengo. Bila kujiwekea
malengo yatakayokuongoza kwenye mafanikio inakuwa ni kama kazi bure.
Katika
mfano mzuri wakukueleza hili na ukanielewa vizuri ningependa leo nikusimulie
kisa kimoja cha ndege Tai. Ndege huyu ni moja kati ya ndege aliyefanikiwa kuwa
na uwezo mkubwa wa kuruka juu zaidi kuliko ndege wengine wote. Siku moja mfugaji mmoja katika pitipita zake alibahatika
kupata yai la Tai. Alipofika nyumbani
aliamua kuliweka yai lile kwenye mayai ya kuku ili litotolewe.
Ulipita
muda wa siku ishirini na moja malengo ya mkulima yule yaliweza kufanikiwa pale
yai lile lilipototolewa pamoja na mayai mengine ya kuku. Siku zote utambulisho
wa kitu au mtu ni jamii aishiyo. Kuku wale pamoja na tai yule waliweza kuishi
pamoja na hata kujita wote wana tabia za aina moja zinazofanana.
Siku
moja sasa kuku alikuwa akitafuta chakula kwa ajili ya vifaranga wake. Tai yule ambaye alikuwa pamoja na kuku alimuona tai mkubwa akiwa
angani na akamuuliza kuku yule ni ndege gani mbona yuko juu sana kuliko sisi?
Kuku alimjibu na kusema yule ni tai ndege aliyebarikiwa sana kuliko ndege
mwingine.
Tai
mdogo hakushia hapo aliendelea kumhoji kuku kwa hiyo sisi hatuwezi kuruka na
kuwa kama yeye? Kuku alimjibu ni kweli
hatuwezi sisi ni kuku hatuna uwezo huo. Kwa kuwa tai mdogo alishindwa
kujitambua yeye ni nani aliweza kukata tamaa na kuamini kabisa ni kweli hawezi
kufanana naye.
Tai
yule aliendelea kuishi maisha yaleyale akiwa na kuku hadi siku ya mwisho
alijikuta akiwa amekufa bila kutimiza malengo yake. Kitu kikubwa kilichomfanya
hadi afe na hali hiyo ya kutokuweza kuruka ni kutokana na yeye kuamini
asingeweza kuleta mabadiliko ya kuruka kumbe uwezo huo alikuwa nao tena mkubwa
wa kufanya hivyo ingawa yeye hakujua.
Ni mambo gani ya kuweza kujifunza
kupitia simulizi hii?
1.
Kama unataka kufanya mambo makubwa katika maisha yako, jifunze kuamini fikra
zako na kuwa wewe kama wewe. Ukisikiliza sauti nyingi za nje zitakuzuia kufika
kule unakotaka kufika. Kwa mfano kama tai yule mdogo angejiamini angeweza
kuruka lakini kwa bahati mbaya alikufa huku na uwezo wote akiwa nao.
Kilichomkwamisha ni sauti ya kuku. Angalia hata hapo ulipo usije ukakwamishwa
na kuku, wewe ni tai.
2.
Kila wakati ni lazima kujiandaa na kujifunza kwa ajili ya mafanikio yako. Kama
usipojiandaa na kujifunza utakufa na mambo mengi bila ya kuyatumia.
3.
Upo umuhimu wa kuachana na mambo ya zamani yanayotushikilia na kutukwamisha.
Acha kuaminishwa tena na mtu eti kuwa huwezi wakati uwezo huo unao tena mkubwa
sana.
4.
Watu wengi wanajikuta wakifa na kwenda makuburini bila kutimiza malengo yao
makubwa waliyojiwekea kutokana na kutokuelewa uwezo ulio ndani mwao. Wapo
waliokufa wakiwa na vipaji vikubwa vya mziki ndani yao, wengine walikufa wakiwa
na vipaji vya mpira na wengine hata vya uandishi lakini kwa bahati mbaya
hawakuweza kuvitumia vyote hivyo, kama tu ilivyokuwa kwa tai.
5.
Tulizaliwe ili tushinde katika maisha na siyo tushindwe. Acha kujiona mnyonge
katika dunia hii, kumbuka wewe ni mshindi na siyo mtu wa kushuindwa kama
unavyojiona.
Yapo
mengi ya kujifunza kupitia simulizi hiyo, lakini nimekushirikisha kwa sehemu
ili kujifunza pamoja. Tafakari juu ya maisha yako na chukua hatua kubwa ya
kutumia vipaji ulivyonavyo ndani mwako na kukufanikisha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Sep 18, 2015
Siri 6 Za Kuishi Maisha Yenye Afya Bora.
Habari
za siku rafiki na mpenzi msomaji wa
mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu umzima wa afya na
unaendelea kujifunza ili kuboresha maisha yako. Karibu tena katika siku nyingine
ambapo tunapata fursa ya kujadili mambo ya kimafanikio kama ilivyo kawaida
yetu.
Katika
makala yetu ya leo tutaangalia kuhusu afya kama sehemu muhimu sana kwa
mafanikio yoyote yale. Bila shaka utakubaliana nami kuwa kama afya yako ni
mbovu huwezi kufanikiwa hata iweje. Mafanikio yote unayoyatafuta yanahitaji uwe
na afya njema ili kuyafikia, vinginevyo utakwama.
Ikumbukwe
kuwa hakuna mtu anayependa kuumwa au afya yake kuwa mbovu hata kidogo. Kila mtu
anahitaji afya yake iwe bora tena hata siku zote ikiwezekana ili kuishi maisha
ya furaha. Lakini ubora huo wa afya tunaoutaka hauji hivihivi tu huwa zipo
kanuni au siri za kufanya ili kuweza kujijengea afya bora zaidi.
Hapa
zipo siri sita za kufuata endapo wewe kweli unataka kuishi maisha yenye afya na
yenye manufaa mengi zaidi.
1. Fanya Mazoezi ya mwili kila siku.
Mazoezi
ya mwili ni ya muhimu sana kwa afya yetu na yanafaida nyingi kwetu. Unapofanya
mazoezi hiyo inakuwa inakusaidia kuupa mwili afya kutokana na ukweli kwamba
yanapunguza magonjwa mengi kama ya msongo wa mawazo na shinikizo la damu. Hivyo
unapofanya mazoezi hata kama ni kidogo unakuwa upo katika hali nzuri kiafya
tofauti na yule ambaye hafanyi kabisa.
2. Pata muda wa kupumzika
Baada
ya kazi zetu tunazozifanya, mwili huu ni lazima upumzike ili upate kujitengeneza
upya wenyewe. Yatupasa kuwa na muda wa burudani na wa kupumzika ili kupunguza
msongo utokanao na kazi pamoja na majukumu ya kifamilia. Bila kuwa na muda wa
kutosha kupumzika mara nyingi watu wanakuwa na wasiwasi, mfadhaiko na hasira
kali. Hivyo ni lazima kutenga muda huu
ili kujijengea afya bora.
3. Kula chakula bora.
Ili
kujihakikishia usalama wa hili epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi. Kama
unazidisha vyakula hivi vyenye mafuta hali hiyo inaweza ikawa hatari kwa afya
yako. Vyakula hivi vinaweza vikawa nyama au vinginevyo. Hakikiha unajipatia
vyakula vyenye virutubisho muhimu vya mwili, lakini siyo lazima viwe vya mafuta.
Kwa kujijengea tabia hiyo mwili wako kwa namna yoyote ile ni lazima utakuwa na
afya bora.
4. Epuka Vitu Vinavyokuletea
Madhara.
Vitu hivi inaweza ikawa ni pamoja na matumizi mbaya
ya pombe hususani pombe kali au uvutaji wa sigara wa kupitiliza. Unapokuwa
unafanya mambo kama hayo tambua tu moja kwa moja yatakuharibia afya yako. Kitu
cha msingi hapo ni kuhakikisha unaachana na tabia hiyo ili kujijengea afya bora
na endelevu kwako.
5.
Kunywa maji safi na ya kutosha.
Tunapozungumzia afya safi huwezi kulikwepa hili la
kunywa maji safi. Unalazimika kunywa maji safi na ya kutosha ili kuipa akili
yako nguvu ya kufanya kazi kwa ufanisi. Unapokunywa maji mengi yanakuwa
yanasaidia ubongo wako kufanya kazi vizuri kwa sababu yanakuwa yanaiongezea
akili yako oksijeni kwa hali ya juu kabisa.
6.
Dumisha usafi.
Usafi ni suala la muhimu sana katika kuboresha afya
zetu. Usafi huu unaweza ukaanzia kwenye miili yetu, mavazi na hata pia katika
mazingira yetu. Tunapoimarisha usafi katika maeneo yote hayo inakuwa ni rahisi
kuweza kukabiliana na magonjwa mbalimbali ambayo yangeweza kutushambulia.
Kumbuka, kuwa
na afya bora ni msingi mkubwa wa mafanikio kwa binadamu. Hivyo ni lazima kwetu
kudumisha afya bora siku zetu ili kujihakikishia hata usalama wa maisha yetu
kwa kiasi kikubwa.
Nakutakia kila la kheri katika maendeleo ya afya yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au
changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa
ushauri na msaada wa haraka.
Sep 17, 2015
Mambo 7 Yakukusaidia Kutunza Muda Wako Vizuri.
Matumizi
mazuri ya muda ni moja kati ya changamoto kubwa sana inayotukabili wengi wetu.
Mara nyingi imekuwa ikitokea kwa wengi wetu karibu kila siku, kujikuta tuna mambo
mengi ya kufanya ukilinganisha na muda tulionao. Kutokana na mambo hayo kuwa mengi,
mipango yetu mingi pia hujikuta imekwama na kushindwa kuendelea kutokana na ukosefu
wa muda.
Lakini
hata hivyo, pamoja na changamoto zote hizo za ukosefu wa muda, kwa wengine bado
hubaki kuwa ni watu wa kupoteza muda katika maisha yao. Nikiwa na maana kuwa,
wanakuwa ni watu ambao hawajali sana kupoteza muda wao na pia hata wanakuwa wanawapotezea
wengine muda hivyohivyo. Najua umeshawahi kuwaona watu wa namna hii katika
maisha yako wasiojali thamani ya muda.
Hawa
ni watu ambao huishi maisha yasiyo na mafanikio sana kutokana na kupoteza muda
mwingi sana katika maisha yao. Kitu cha muhimu hapa kujua ni kuwa muda ni kitu
cha thamani sana kuliko kitu chochote duniani.
Mafanikio yote yanategemea muda. Unapopoteza muda wako ni sawa na kupoteza
mafanikio yako. Sasa jiulize kama wewe unapoteza muda unategemea nini katika
maisha yako?
Ili
uweze kufanikiwa na kuwa tajiri ni lazima kujifunza kutumia muda wako vizuri
tena sana. Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watumiaji wazuri wa muda wao
kuliko unavyofikiri. Kinachowatofautisha wao na wewe ni matumizi ya muda tu na
sio kitu kingine. Hiyo yote inaonyesha siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye muda.
Kitu kingine cha kujiuliza tena je,
unataka kutunza muda wako na kujijengea mafanikio ya kudumu? Kama jibu ni NDIYO.
Yafuatayo Ni Mambo 7 Yakukusaidia
Kutunza Muda Wako Vizuri.
1. Weka vipaumbele vya kila siku.
Ili
uweze kuepuka muingiliano wa mambo ni lazima kujifunza kuweka vipaumbele vya
kila siku. Andika mambo ya lazima ambayo unatakiwa uyafanye kwa siku hiyo
husika bila kuacha kitu. Hilo litakusaidia kutopoteza hovyo muda wako ulionao
kwa sababu kila kitu kitakuwa kwenye ratiba yake na muda wa kukifanya.
2. Jiwekee malengo.
Kama
utakuwa unajiwekea malengo hiyo itakuwa ni silaha ya kukuwezesha kutumia muda
wako vizuri pia. Kwa sababu utakuwa unajua kabisa baada ya muda fulani unatakiwa
uwe umetekeleza kitu hiki ama kile. Wengi wanaopoteza muda mara nyingi ni watu
ambao hawana malengo hata yale ya siku moja tu. Na kwa sababu hiyo kwao muda
kupotea ni kitu ambacho hakikwepeki.
3. Fanya mambo machache kwa uhakika.
Ni
rahisi sana kwako kupoteza muda kama utajikuta unataka kafanya mambo mengi kwa
wakati mmoja. Hii ni kwa sababu utashika hiki mara kile na kujikuta hakuna
ulichokifanya zaidi ya kurukaruka. Ili kufanikiwa jifunze kufanya mambo
machache kwanza ikiwezekana jambo moja tu. Hiyo itakupa ufanisi wa kutunza muda
wako vizuri sana.
4. Weka kumbukumbu ya muda wako.
Ili
uweze kujua muda wako unautumiaje, ni vizuri kujiwekea kumbukumbu ya muda wako
jinsi unavyoutumia. Unaweza ukaona ni kitu kama cha kijinga lakini ikifika siku
kitakusaidia kujua tathmini ya wapi hasa unapopoteza muda wako mwingi ili kama
ikiwezekana ujirekebishe. Kwa kujiwekea kumbukumbu ya muda wako uwe na uhakika
utaweza kumiliki na kuutawala muda wako vizuri sana kwa mafanikio.
5. Kuwa makini na mambo
yanayokupotezea muda.
Kuna
mambo ambayo wengi wetu huwa yanatupotezea muda bila sababu. Jiulize ni kitu
gani ambacho kinakupotezea muda sana. Je, ni mitandao ya kijamii, simu, mpira
au ni kitu gani? Ukishajua kitu kinachokupotezea muda sana, tafuta njia nzuri
namna ya kupunguza matumizi hayo. Acha kupoteza muda wako hovyo kwa kitu
ambacho hakikupi faida ya moja kwa moja, badala yake linda na tunza sana muda
wako kwani hapo ndipo mafanikio yako yalipo.
6. Jifunze kusema HAPANA.
Wengi
huwa wanajikuta ni watu wa kupoteza muda wao pengine kutokana na kukubali vitu
vingi bila kujiuliza kwa nini walikubali. Kabla hujasema ndiyo kwa jambo lolote
la makubaliano jiulize linawezekana? Kama hutajifunza kusemaHAPANA hii itakufanya
uzidi kupoteza muda wako mwingi wa thamani siku hadi siku bila ya wewe kujua. Kama
huelewi kitu ni bora ukasema HAPANA kuliko ukafanya na ukaacha, hiyo itakuwa ni
kupoteza muda.
7. Wape wengine majukumu.
Kama
pengine kuna jambo ambalo unataka kulifanya wewe, lakini ukagundua wapo watu
ambao wanaweza wa kakusaidia katika jambo hilo ni vizuri ukawapa wakafanya.
Hiyo itakusaidia kufanya majukumu mengine zaidi na isitoshe utakuwa umeokoa
muda wako mwingi. Acha kung’ang’ania kufanya mambo yote wewe, wape na wengine
wakusaidie majukumu hayo ili kuokoa muda wako.
Kumbuka,
muda ni kitu cha thamani sana ambapo ukijenga tabia ya kuutumia vizuri utakuwezesha
kufikia mafanikio makubwa yanajitokeza katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika matumizi bora ya muda wako na
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)