Sep 21, 2015
Siri Nzito Katika Kufikia Mafanikio Makubwa.
Katika
maisha kila mtu hupenda kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa. Lakini pamoja
na umuhimu huo ni wapo ambao hujikuta wakifanya yale yasiyotakiwa kufanywa ili
kufikia mafanikio hayo. Mafanikio mazuri ni lazima yaanze na malengo. Bila kujiwekea
malengo yatakayokuongoza kwenye mafanikio inakuwa ni kama kazi bure.
Katika
mfano mzuri wakukueleza hili na ukanielewa vizuri ningependa leo nikusimulie
kisa kimoja cha ndege Tai. Ndege huyu ni moja kati ya ndege aliyefanikiwa kuwa
na uwezo mkubwa wa kuruka juu zaidi kuliko ndege wengine wote. Siku moja mfugaji mmoja katika pitipita zake alibahatika
kupata yai la Tai. Alipofika nyumbani
aliamua kuliweka yai lile kwenye mayai ya kuku ili litotolewe.
Ulipita
muda wa siku ishirini na moja malengo ya mkulima yule yaliweza kufanikiwa pale
yai lile lilipototolewa pamoja na mayai mengine ya kuku. Siku zote utambulisho
wa kitu au mtu ni jamii aishiyo. Kuku wale pamoja na tai yule waliweza kuishi
pamoja na hata kujita wote wana tabia za aina moja zinazofanana.
Siku
moja sasa kuku alikuwa akitafuta chakula kwa ajili ya vifaranga wake. Tai yule ambaye alikuwa pamoja na kuku alimuona tai mkubwa akiwa
angani na akamuuliza kuku yule ni ndege gani mbona yuko juu sana kuliko sisi?
Kuku alimjibu na kusema yule ni tai ndege aliyebarikiwa sana kuliko ndege
mwingine.
Tai
mdogo hakushia hapo aliendelea kumhoji kuku kwa hiyo sisi hatuwezi kuruka na
kuwa kama yeye? Kuku alimjibu ni kweli
hatuwezi sisi ni kuku hatuna uwezo huo. Kwa kuwa tai mdogo alishindwa
kujitambua yeye ni nani aliweza kukata tamaa na kuamini kabisa ni kweli hawezi
kufanana naye.
Tai
yule aliendelea kuishi maisha yaleyale akiwa na kuku hadi siku ya mwisho
alijikuta akiwa amekufa bila kutimiza malengo yake. Kitu kikubwa kilichomfanya
hadi afe na hali hiyo ya kutokuweza kuruka ni kutokana na yeye kuamini
asingeweza kuleta mabadiliko ya kuruka kumbe uwezo huo alikuwa nao tena mkubwa
wa kufanya hivyo ingawa yeye hakujua.
Ni mambo gani ya kuweza kujifunza
kupitia simulizi hii?
1.
Kama unataka kufanya mambo makubwa katika maisha yako, jifunze kuamini fikra
zako na kuwa wewe kama wewe. Ukisikiliza sauti nyingi za nje zitakuzuia kufika
kule unakotaka kufika. Kwa mfano kama tai yule mdogo angejiamini angeweza
kuruka lakini kwa bahati mbaya alikufa huku na uwezo wote akiwa nao.
Kilichomkwamisha ni sauti ya kuku. Angalia hata hapo ulipo usije ukakwamishwa
na kuku, wewe ni tai.
2.
Kila wakati ni lazima kujiandaa na kujifunza kwa ajili ya mafanikio yako. Kama
usipojiandaa na kujifunza utakufa na mambo mengi bila ya kuyatumia.
3.
Upo umuhimu wa kuachana na mambo ya zamani yanayotushikilia na kutukwamisha.
Acha kuaminishwa tena na mtu eti kuwa huwezi wakati uwezo huo unao tena mkubwa
sana.
4.
Watu wengi wanajikuta wakifa na kwenda makuburini bila kutimiza malengo yao
makubwa waliyojiwekea kutokana na kutokuelewa uwezo ulio ndani mwao. Wapo
waliokufa wakiwa na vipaji vikubwa vya mziki ndani yao, wengine walikufa wakiwa
na vipaji vya mpira na wengine hata vya uandishi lakini kwa bahati mbaya
hawakuweza kuvitumia vyote hivyo, kama tu ilivyokuwa kwa tai.
5.
Tulizaliwe ili tushinde katika maisha na siyo tushindwe. Acha kujiona mnyonge
katika dunia hii, kumbuka wewe ni mshindi na siyo mtu wa kushuindwa kama
unavyojiona.
Yapo
mengi ya kujifunza kupitia simulizi hiyo, lakini nimekushirikisha kwa sehemu
ili kujifunza pamoja. Tafakari juu ya maisha yako na chukua hatua kubwa ya
kutumia vipaji ulivyonavyo ndani mwako na kukufanikisha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia
mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035
kwa ushauri na msaada wa haraka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.