Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, September 23, 2015

Kama Unakimbia Kitu Hiki, Huwezi Kufanikiwa.

No comments :
Kwa hakika ‘Hakuna kisichowezekana chini ya jua’ ikiwa nia hiyo ya kufanikiwa unayo kweli kutoka moyoni mwako. Kila kitu unachokihitaji katika maisha yako kinapatikana ikiwa utaamua kufanya kwa kazi kwa bidii. Haijalishi hali au rasilimali ulizonazo lakini kama wewe ni mtu wa kufanya kazi kwa bidii zote huku ukiwa na mipango na malengo imara  ni lazima ufanikiwe.
Watu  wote wenye mafanikio makubwa duniani kote ni wachapakazi. Mafanikio yao yote ni matokeo ya kile walichokifanyia kazi kwa muda mrefu bila kuchoka. Na pengine kazi hizo walizokuwa wakizifanya ziliwachosha, kuwakatisha tamaa lakini kutokana na uvumilivu wao walivumilia na kuendelea kujishughulisha mpaka malengo yao yakatimia.
Nakumbuka katika maisha yake Daktari Ronald Rose kama ambavyo tuliwahi kuandika wakati fulani katika mtandao huu, alifanya kazi kwa bidii sana ili kukamilisha ugunduzi wake wa dawa ya malaria. Mbaya zaidi mazingira aliyokuwa akifanyia kazi hayakumpa ushirikiano wowote lakini aliweka  juhudi mpaka dawa ya malaria ilipatikana bila kuchoka.
Hiyo yote inatuonyesha uvumilivu na kufanya kazi kwa bidii ni vitu ambavyo havikwepeki ili kufikia mafanikio makubwa. Ikiwa nia yako ni kutafuta mafanikio ya kweli ni lazima ujue kazi inahitajika tena ya ubora wa juu  na wala sio ‘hadithi’  za hapa na pale. Achana na habari za sterehe zisizo na msingi kwako.  Jitume ili kufikia uhuru wa kifedha, vinginevyo utaendelea kuwa na maisha magumu mpaka mwisho wako.

Tatizo kubwa la watanzania tulio wengi ni kukwepa majukumu ya kufanya kazi kwa bidii. Kama unafikiri natania jaribu kuangalia  hata wale wote waliokaribu na wewe,  utagundua ni wengi wenye uvivu fulani fulani hivi hata kwenye kazi zao. Kazi zinakuwa zinafanyika ila kwa kujivuta sana hali ambayo hupelekea majukumu mengi kukwama.
Ili uweze kufanikiwa na kufikia viwango vya juu vya mafanikio kitu kikubwa ambacho hutakiwi kukwepa ni kufanya kazi kwa bidii.  Kama kwenye maisha yako hufanyi kazi kwa bidii, sahau kuhusu mafanikio. Jaribu kuchunguza wale wote wanaofanikiwa sana katika jamii yako ni watu wa aina gani? Utakuja kugundua ni wale wote wanaojituma kila siku bila kuchoka katika kazi zao.
Kama kanuni au maisha yako hivi kwa nini unataka kujidanganya na kuamua kutafuta urahisi unaojua wewe? Kumbuka, kama unakimbia kitu hiki kwa namna moja au nyingine huwezi kufanikiwa. Kila kitu ili uweze kukipata kina gharama yake. Na gharama mojawapo ya mafanikio hadi uweze kuyafikia ni kujitoa na kufanya kazi kwa bidii.
Najua kila mmoja wetu ana nia ya kufanikiwa katika mambo yake iwe katika biashara au maeneo mengine. Lakini mafanikio hayo hayawezi kuja kama ndoto tu. Yatapatikana kwa kufanya kitu kimoja tu ambacho ni kufanya kazi kwa bidii. Hapo ndipo ilipo siri ya kufikia mafanikio makubwa na hakuna muujiza katika hilo.
Kama wahenga walivyosema ‘kazi ni msingi wa maendeleo’ hakuna ubishi katika hilo. Penda kile unachokifanya, weka juhudi na nguvu zako zote bila kuchoka na mafanikio yatakuja upande wako. Haijalishi mazingira uliyopo ni magumu kiasi gani lakini kitu cha muhimu kwako ni kujituma tu mpaka uone hatma ya mafanikio yako.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unaendelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
 Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.  

No comments :

Post a Comment